The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Hili, Serikali Imeheshimu AFCON 2027

Kwa kutenga fedha zaidi kwa ajili ya uandaaji wa michuano hiyo, Serikali imeonesha utayari na umakini kama moja wa waandaaji wa mashindano hayo muhimu ya soka.

subscribe to our newsletter!

Wiki hii Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambayo yamefikia Shilingi bilioni 285.3, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wizara hiyo kupangiwa kutumia fedha nyingi zinazofikia ongezeko la asilimia 700.

Na sehemu kubwa ya fedha hizo itakwenda kwenye miradi ya maendeleo, tofauti na miaka ya nyuma ambayo mgao wa eneo hilo ulikuwa haufiki hata robo ya matumizi kama yale ya mishahara.

Hii ni hatua kubwa kwa Serikali kuona umuhimu wa michezo na kupangia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya maendeleo, hasa kipindi hiki ambacho nchi inajiandaa kuwa mmoja wa wenyeji wa fainali za mpira wa miguu za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2027. Nchi nyingine zitakazoandaa fainali hizo ni majirani Kenya na Uganda.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa fainali hizo kubwa kuliko zote katika soka barani Afrika kufanyika katika nchi waanzilishi wa Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA) na mara ya kwanza tangu nchi kutoka ukanda huu, Ethiopia, iandae fainali hizo miaka 50 iliyopita.

Hata hivyo, haitakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa mashindano makubwa kwa kuwa mwaka 2020 nchi hiyo iliandaa fainali kama hizo kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17, jambo lililochangia pia kurahisisha kupewa uenyeji japo ni wa pamoja na majirani zetu.

Utayari wa Serikali

Hata hivyo, fainali za U-17 hazikuambatana na utayari wa Serikali kuwekeza fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya michezo, ya usafirishaji na mawasiliano. Hata barabara inayokwenda Uwanja wa Azam, ambao ulitumika kwa fainali hizo, haikufanyiwa marekebisho yanayolingana na hadhi ya mashindano makubwa.

SOMA ZAIDI: Ni Muda Makocha Wazawa Tanzania Waanze Kufanya Kazi Kisasa

Lakini safari hii, utashi wa kisiasa umeonekana katika kujiandaa kwa fainali hizo kubwa.

Katika maombi yaliyowasilishwa na nchi hizi tatu, maarufu kama Pamoja Bid, kila nchi iliahidi kuwa na viwanja vitatu na hivyo, kwa mara ya kwanza, fainali hizo za mataifa ya Afrika zitatumia viwanja tisa.

Tanzania itatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, New Amaan, ambao umeboreshwa na uwanja mpya unaojenga mkoani Arusha utakaoitwa Samia Suluhu.

Na tayari mkandarasi yuko eneo la kazi akiendelea na shughuli za ujenzi baada ya mkataba kusainiwa na sasa fedha kutengwa katika jitihada za kuhakikisha unakamilika kabla ya mwaka 2025 kuisha, kuepusha kadhia ya kupokonywa uenyeji ambao utachafua taswira ya nchi.

Pamoja na faida za kiuchumi na kijamii, fainali hizo zitasaidia sana kuongeza ari na ushiriki kwenye michezo, achilia mbali mchezo wa mpira wa miguu ambao utanufaika moja kwa moja kutokana na fainali hizo kuchezwa hapa nchini.

Michezo kama ya riadha, ambayo kwa nadra imekuwa haifanyiki, sasa imeongezewa wigo kutokana na ukweli kwamba eneo la kaskazini mwa nchi na kati ndiko wanakotoka wanariadha wakubwa wa mbio za masafa ya kati na marathoni. 

SOMA ZAIDI: Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania

Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Singida na Dodoma imekuwa ikizalisha wanariadha wakubwa nchini, lakini imekuwa haina viwanja vinavyofikia viwango vya kimataifa.

Lakini sasa wananchi wa maeneo hayo wamesogezewa uwanja ambao utawawezesha kupima viwango vyao na kuviboresha ili baadaye tupate wanariadha wa mbio za masafa ya kati na mafupi ambao kwa sasa wamepotea na kubakia wa marathoni.

Hatua muhimu

Pamoja na Serikali kupanga kiasi hicho kikubwa cha fedha, hatua ya pili na muhimu ni uachiaji wa hizo fedha ili mipango iende kama ilivyopangwa. 

Ingawa simaanishi iwe hivyo, nchini Kenya, Rais William Ruto amelihusisha jeshi katika usimamizi wa ujenzi wa Uwanja wa Talanta, akitaka lihakikishe kila kitu kinakwenda kama ilivyopangwa na kukagua kila wiki.

Si lazima Tanzania iige Kenya ilivyofanya, lakini inaonyesha ni kiasi gani Ruto hataki kurudia makosa kama yaliyofanyika miaka ya 1980 wakati nchi hizo ilipopewa uenyeji wa Michezo ya Afrika, lakini ikanyang’anywa katika dakika za mwisho kutokana na kutokamilisha ujenzi wa Uwanja wa Kasarani. 

SOMA ZAIDI: CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco

Hiyo ni hatua inayoonyesha utashi wa dhati wa kuhakikisha miundombinu hiyo ya michezo inajengwa kwa wakati na ubora unaostahili.

Sisi pia tunahitaji mbinu yetu ya kuhakikisha mambo yanakwenda badala ya kutumia staili iliyozagaa hivi sasa ya kwenda eneo la ujenzi na kuanza kumhoji mkandarasi maswali mbele ya kamera ambayo wakati mwingine yanafichua udhaifu wa Serikali katika kutekeleza mradi.

Usimamizi mzuri

Ni muhimu tukawa na usimamizi mzuri unaoendana na utoaji wa fedha kwa mujibu wa mkataba ili kuondokana na kadhia za kukimbizana dakika za mwisho na pengine hata kupoteza haki ya kuandaa fainali hizo.

Pamoja na utayari huo, ni muhimu pia kwa wadau wengine kuanza maandalizi mapema, hasa ya timu tunayotazamia kuwa ndiyo itashiriki michuano hiyo. Ni vema kwa nchi kutafuta kocha na benchi la ufundi linaloaminika kwa ajili ya fainali hizo.

Hivi sasa klabu zinajenga kisayansi mabenchi yao ya ufundi yanayohusisha wataalamu tofauti. Ni muhimu pia kwa Shirikisho la Soka (TFF) kuona hilo na kuanza kujenga benchi la ufundi la AFCON 2027 linalohusisha wataalamu waliobobea watakaowezesha kuandaa timu imara yenye uwezo wa kupambana katika fainali hizo.

SOMA ZAIDI: Tutapataje Mabondia Bora Bila Ngumi za Ridhaa?

Mambo ya uswahiba na undugu, au mazoea, hayafai yaendelee kwenye benchi la ufundi. Kama Serikali imeonyesha kuheshimu fainali za Mataifa ya Afrika za 2027, basi na mamlaka za soka zionyeshe umakini ili tusifanikiwe katika kuandaa peke yake, bali na uwanjani pia.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts