Katika malezi ya mtoto, upendo ni jambo la kwanza, upendo hujumuisha kumuonya pale anapokosea, na kumpongeza pale anapofanya vizuri. Upendo huu unalenga kumjenga mtoto kihisia na kisaikolojia na utachangia kazi ya malezi kuwa rahisi.
Ukaribu wako na mtoto utamsaidia mtoto kuwa huru kwako na kuwasiliana na wewe muda wowote anapohitaji msaada wako kwani upendo hujenga uaminifu wa mtoto kwa mzazi, na hupelekea misingi mizuri ya uadilifu na heshima.
Sisi wazazi, au walezi, ndiyo wajenzi wakuu wa tabia ya mtoto, kwani mtoto hujifunza mambo yanayofaa, au yasiyofaa, kutoka kwa wale wanaomzunguka. Mtoto huangalia na hujifunza kutoka kwetu namna ya kuishi na kuzungumza na watu, namna ya kukabiliana na kutatua changamoto.
Hivyo basi, ni jukumu letu kuwa mfano mzuri wa kuigwa. Siku zote tutambue kuwa sisi ndiyo walimu wa kwanza wa watoto wetu.
Katika malezi kuna kuzingatia mtindo maalum wa malezi. Hii inagusa zaidi katika mazingira ambayo mtoto anaweza kukua, kujitambua na kujengewa mfumo mzuri wa tabia na maadili yanayokubalika kwa jamii nzima.
SOMA ZAIDI: Fahamu Sehemu Watoto Wanaweza Kutoa Taarifa Kuhusu Vitendo vya Ukatili
Mara nyingi inakuwa ngumu kumlea mtoto awe na tabia fulani kwa sababu anapokua na kujumuika na wengine hujifunza vitu tofauti, vibaya au vizuri, kutoka kwao.
Hivyo, kazi yetu ni kuhakikisha mtoto anakuwa na mfumo maalum wa maisha na malezi utakaomsaidia kujitambua na kujisimamia na kukabiliana na changamoto anazokutana nanzo nje ya mfumo wa familia.
Siku zote tujaribu kumsikiliza na kumuelewa mtoto hisia zake, mawazo yake, juhudi zake yeye kama mtoto, kumsifu na kumpongeza akifanya vizuri.
Watoto wanaopongezwa na kusikilizwa kwa makini hujijengea tabia ya kujiamini na uthubutu wa kufanya mambo mbalimbali na asilimia kubwa hufanya vizuri zaidi katika maisha ya kawaida na hata katika masomo yao.
Tunapaswa pia kuwashirikisha watoto katika malezi. Hii inamaanisha kuhakikisha mtoto anashiriki kikamilifu katika maamuzi ya kifamilia na hasa mambo yanayogusa maslahi yake binafsi, ikiwemo kumpatia majukumu madogomadogo ya kila siku.
SOMA ZAIDI: Dondoo Hizi Zitakusaidia Mzazi Kumlinda Mtoto Kipindi Hiki cha Mvua
Hii humpa mtoto ufahamu wa kuwa yupo katika familia inayomkubali na kumtegemea, humpa mtoto nafasi ya kujiamini na kushiriki katika mambo mbalimbali ya jamii na kifamilia, humfanya achukue majukumu katika familia na pia kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Tufahamu kuwa kila umri katika makuzi ya mtoto una changamoto zake kwa mtoto mwenyewe na hata kwa mzazi. Kila hatua ya umri mtoto apitiayo kuna kitu kipya cha kujifunza na kuwafundisha Watoto wetu, kuimarisha uwezo wao wa kutatua matatizo au changamoto zinazowakabili.
Safari ya malezi ni ndefu na yenye furaha pale tutakapochukua kila siku kama zawadi ya kuwa na muda na watoto wetu.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.