The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fahamu Sehemu Watoto Wanaweza Kutoa Taarifa Kuhusu Vitendo vya Ukatili

subscribe to our newsletter!

Watoto wana haki ya kulindwa. Kulindwa huko kunahusu kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa katika kila hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa. 

Mathalani, mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizoendana na umri wake na zilizohatarishi kwa afya na ustawi wao; kudhulumiwa mali, hasa kwa watoto yatima; kutupwa au kutelekezwa na wazazi; utoaji mimba wa makusudi; adhabu kali zenye kupelekea athari za kimwili, kiakili, kisaikolojia a kijamii; vitendo vya kingono; ndoa za kulazimishwa na za umri mdogo; ukeketaji; kuonewa, na kadhalika. 

Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania pia inasisitiza juu ya ulinzi dhidi ya matendo yote maovu yakiyotajwa hapo juu.

Hivi karibuni, kumekuwa na taarifa nyingi za matukio yanayohusu watoto kufanyiwa ukatili na udhalilishaji uliotajwa hapo juu. Lakini je, ni sehemu zipi watoto wanaweza kutoa taarifa za matukio haya?

Kama wazazi na walezi, inatupasa kuhakikisha kuwa tumetengeneza mazingira ambayo watoto wetu wanaweza kutueleza kila kitu kinachowasibu. 

SOMA ZAIDI: Dondoo Hizi Zitakusaidia Mzazi Kumlinda Mtoto Kipindi Hiki cha Mvua

Lakini pia, tunapaswa kuwaeleza na kuwaelimisha watoto kwamba kuna watu na sehemu ambazo wanaweza kutoa taarifa ikiwa wao, rafiki yao, au mwanafunzi mwenzao amefanyiwa ukatili, au udhalilishaji na hawawezi kueleza. 

Sehemu ya kwanza inaweza kuwa shuleni. Kama tunavyofahamu, waalimu hufanya mambo mengi mbali na kufundisha. Wana wajibu wa kuwalinda watoto maana wao ndiyo walezi wa watoto wetu wakiwa mbali na nyumbani. Tuwafundishe kwamba wanaweza kuzungumza na mwalimu wao ikiwa wanahitaji msaada.

Sehemu nyingine inaweza kuwa Huduma ya Simu kwa Mtoto namba 116. Hii ni huduma ya simu isiyo na malipo iliyopo kwa ajili ya watoto na watu wazima kutoa taarifa na kuomba msaada pale ambapo watoto wamefanyiwa ukatili au haki zao zinapokiukwa.

Sehemu nyingine ni maafisa ustawi wa jamii ambao kwa mujibu wa sheria wana wajibu wa kuwalinda watoto, hivyo tujitahidi kuwafahamisha watoto wanaweza kuzungumza nao ili wapate msaada. Maafisa hawa mara nyingi wanapatikana kwenye ofisi za kata, wilaya, mkoa, hospitalini, makao makuu ya wizara na vituo vya mkono kwa mkono.

Kuna vituo vya ‘Mkono kwa Mkono’ pia ambavyo mtoto aliyefanyiwa ukatili, au udhalilishaji, hasa wa kingono, anaweza kwenda kupata msaada wa haraka kutoka kwa afisa ustawi wa jamii, polisi, na daktari kwa wakati mmoja. Watoa huduma hawa wote hushirikiana kuwasaidia na kuwalinda watoto na kuhakikisha wanapata huduma za kisaikolojia, kitabibu na za kisheria.

SOMA ZAIDI: Mzazi, Hakuna Ushahidi Kwamba Viboko Vinasaidia Katika Malezi ya Mtoto Wako

Bila kusahau, kuna Madawati ya Jinsia na Watoto ya Polisi ambayo yapo kwa ajili ya kumsaidia mtu yeyote aliyefanyiwa ukatili au udhalilishaji, bila ubaguzi. 

Mara nyingi wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa wa ukatili na udhalilishaji, hivyo watu wengi hufikiria kwamba madawati haya yanatakiwa kuwasaidia wanawake na watoto tu. 

Lakini Madawati ya Jinsia na Watoto yanatakiwa kumsaidia mtu yeyote aliyefanyiwa ukatili, au udhalilishaji, awe mwanamume au mwanamke; kijana au mzee.

Watoto wakifahamu hizi sehemu na kuzitumia vyema wanaweza kujilinda na kuwalinda wenzao dhidi ya vitendo vya ukatili.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *