Katika jamii nyingi, hususan zile za Kiafrika, watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazozuia uwezo wao wa kufikia ndoto zao.
Licha ya juhudi za wazazi na jamii kutoa nafasi sawa kwa watoto wa kike na wa kiume, bado kuna mwanya mkubwa wa usawa wa kijinsia. Leo, tunazungumzia changamoto hizi na jinsi ya kumuwezesha mtoto wa kike kujiamini, kujithamini na kuwa na uwezo unaohitajika kufikia ndoto zake.
Changamoto zinazowakabili watoto wa kike ni pamoja na kukutana na vikwazo vingi vinavyowafanya watamani kuwa na upendeleo sawa na wavulana. Sababu wanazitoa ni pamoja na kuthaminiwa kidogo katika jamii.
Wasichana wanaeleza kuwa mwanamke hathaminiwi kama mwanaume na kuona kama jamii inaona kama kuna stahiki hapaswi kuzipata mtoto wa kike. Wanaona baba, wajomba, na kaka wakipiga wake zao kwa makosa madogo.
Wasichana wanakumbana na vitisho na udhalilishaji kutoka kwa wavulana, wakihisi kuwa mwili wao ni chanzo cha matatizo.
SOMA ZAIDI: Dondoo Muhimu za Kuzingatia Katika Safari ya Malezi
Wanawake wanaeleza jinsi mama zao wanavyotukanwa na kupigwa wakati wa kujifungua, wakihofia kuwa hata wao watakutana na unyanyasaji huo.
Wasichana wanapata nafasi chache za kusoma na kufikia ndoto zao ikilinganishwa na wavulana.
Ili kusaidia watoto wa kike kujiamini na kuthaminiwa na kupata uwezo thabiti, hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa, ikiwepo kutoa kipaumbele kuhusu elimu.
Elimu ni nyenzo muhimu kwa mtoto wa kike. Walimu wanatakiwa kuhakikisha usawa katika masomo, kuwahamasisha wasichana kupenda elimu na kuwapa moyo katika masomo yao. Hii itawafanya wajione wana haki, fursa na stahiki sawa na watoto wa kiume.
Mtoto wa kike anatakiwa kufahamu kuwa yeye ni sehemu muhimu ya jamii na si jukumu lake tu kuzaa. Katika maeneo kama kanda ya ziwa, ambapo wanawake hawakupata fursa ya elimu na walitarajiwa tu kuolewa na kuzaa, elimu ya utambuzi ni muhimu ili kubadili mtazamo huu. Wanawake wanapaswa kutambua mchango wao wa kiuchumi na kijamii.
SOMA ZAIDI: Fahamu Sehemu Watoto Wanaweza Kutoa Taarifa Kuhusu Vitendo vya Ukatili
Kingine ni kuendesha kampeni za kuondoa dhana potofu ambazo zinaweza kusaidia jamii kuondokana na fikra kwamba mtoto wa kike hana thamani sawa na mtoto wa kiume. Asasi kama FEMINA HIP, TAMWA, na TGNP zinaweza kutoa elimu juu ya thamani ya watoto wote na jinsi ya kuripoti unyanyasaji wa mtoto wa kike.
Kuna haja pia ya kupiga vita ajira za wasichana wa ndani kwa watoto wadogo. Sheria inayozuia ajira za watoto chini ya miaka 18 kufanya kazi za ndani na nyingine hatarishi inapaswa kufuatwa . Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 inatoa muongozo juu ya umri na kazi sahihi kwa watoto.
Tufahamu kuwa ili kuwasaidia watoto wa kike kujitambua na kufurahia kuwa mabinti, programu maalum za kuwajengea usawa, kujiamini, na kuheshimiana zinahitajika.
Programu hizi zinapaswa kushirikisha watoto wa kike na kiume ili kujenga msingi mzuri wa usawa wa kijinsia kutoka umri mdogo.
Wito wetu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ni kwamba tutumie nafasi tulizonazo nyumbani, shuleni, kazini, ama kokokote katika jamii, kuondoa changamoto zinazomkabili mtoto wa kike kutokana na ubaguzi wa kijinsia, ili kuwajengea watoto dhana chanya za usawa wa kijinsia wakiwa na umri mdogo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.