Uongozi bora wa mwenyekiti wa kijiji ni rasilimali muhimu sana ya kuchochea maendeleo kijijini kwa sababu yeye ndiye mwakilishi wa wanakijiji katika Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), ngazi ambayo ndipo vipaumbele vya bajeti ya halmashauri na taifa vinaanzia kupangwa.
Lakini kwa sasa, idadi ya wanawake wenyeviti wa vijiji ni ndogo sana hapa nchini Tanzania, na hivyo kuashiria kwamba nchi yetu inaendelea kuwa maskini, hasa vijijini, kutokana na kukosekana kwa juhudi za kuhakikisha wanawake wengi zaidi wenye sifa za kutoa uongozi bora vijijini wanapata fursa hizo sawa na wanaume.
Kwa mfano, wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, yenye kata 25 na vijiji 125, ni kijiji kimoja tu cha Mwanambaya, kilichopo katika kata ya Mipeko, ndicho ambacho mwenyekiti wake ni mwanamke ambaye anaitwa Leila Chamlumo.
Chamlumo amekuwa kiongozi wa kupigiwa mfano kwa utumishi wake uliotukuka kwa wananchi wa kijiji hicho na wilaya ya Mkuranga kwa ujumla. Wananchi, pamoja na wadau wengine wa maendeleo waliowahi kufika Mwanambaya, wanalithibitisha hili.
“Chamlumo ametoa uongozi ambao umeleta maendeleo ya wananchi katika nyanja mbalimbali kwenye kijiji chake maana anajituma sana na ni mwadilifu,” Prisca Ngwechemi, Mkurugenzi Mtendaji wa Himiza Developemnt Organisation, shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi za maendeleo ya wananchi wilayani Mkuranga, aliniambia.
Katika mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi wa makala hii, Chamlumo ametaja baadhi ya mambo makubwa ya maendeleo ya wananchi ambayo ameyasimamia na yakatekelezwa kwa ukamilifu na ufanisi kupitia nafasi yake kama mjumbe wa WDC ni pamoja na kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, kuhakikisha kwamba kodi za wananchi zinatumika kikamilifu kuleta maendeleo ya wananchi.
SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Mikakati Imara Kuongeza Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi
Amesema, kwa mfano, alipoingia kwenye uongozi katika kijiji chake cha Mwanambaya, zahanati ya kijiji hicho ilikuwa imechakaa kiasi kwamba paa lilikuwa linavuja, akisema: “Mvua ikinyesha, daktari alilazimika kuondoka kwenye kiti chake na kwenda kujibanza eneo lingine.”
Chamlumo amesema hata hivyo alisimamia kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa mapato ya kijiji chake na kwa muda mfupi kijiji kikafanikiwa kukusanya Shilingi 5,000,000 kwa ajili ya kukarabati zahanati hiyo.
Pia, amesema alizungumza na kampuni ya Songas ambayo ilichangia Shilingi 20,000,000 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Shilingi 3,000,000 kabla ya yeye mwenyewe kupeleka ajenda hiyo kwenye kikao cha WDC ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga nayo ilitoa Shilingi 5,000,000 ambapo, kwa pamoja, fedha hizo zilitumika kukarabati zahanati na kujenga wodi ya wajawazito.
Mafanikio
“Nilipoanza kazi, zahanati ya kijiji chetu, chenye vitongoji saba, ilikuwa na kitanda kimoja tu kwa ajili ya wajawazito, lakini leo tuna wodi ya wajawazito na vitanda vya kutosha,” anasema Chamlumo. “Vilevile, tayari tumeshajenga jengo la makazi ya daktari na manesi na wanakaa hapahapa kijijini kwetu kuwahudumia wagonjwa mchana na usiku.”
Kuhusu elimu, uongozi wa Chamlumo umeweza kukusanya fedha kutoka mapato ya kijiji na kwa sasa, tofauti na miaka ya nyuma ambapo kijiji cha Mwanambaya kilikuwa na shule moja tu ya msingi, wamejenga kwa fedha zao wenyewe zinazotokana na mapato ya kijiji shule mbili zaidi za msingi ambazo zitaanza kuchukua wanafunzi wakati wowote kuanzia sasa, na tayari wameshanunua madawati 200 kwa ajili ya shule hizo zilizojengwa katika vitongoji vya Mizugu na Mivule.
“Hizi shule zitawapunguzia wanafunzi umbufu wa kutembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani kwao,” anasema Chamlumo, akiongeza kwamba kijiji cha Mwanambaya kina vitongoji saba ambavyo ni Kiloweko, Madodo, Mizungu, Mamangwa, Kibeneke, Mabatini na Mivule.
SOMA ZAIDI: TGNP Yataka Wanahabari Kuchochea Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi
Aidha, Chamlumo anasema kazi kubwa nyingine ambayo amehakikisha mapato ya fedha za kijiji kutokana na vyanzo mbalimbali zimewezesha ni pamoja na kujenga ofisi kila kitongoji katika vitongozi vyote saba ili viongozi wa vitongozi hivyo waweze kufuatilia kwa karibu na kutatua matatizo ya wananchi na kuweka kumbukumbu za utendaji wao.
Kadhalika, anasema alipochaguliwa Mwenyekiti kwa mara ya kwanza mwaka 2006 akaumti ya kijiji ilikuwa na Shilingi 20,000 tu, lakini leo akaunti ya kijiji chake ina mamilioni kadhaa ya fedha.
“Kwa kweli ninamshukuru Mungu maana ninaamini ni kwa sababu ya utendaji wangu ndiyo wananchi wa kijiji chetu wameendelea kunichagua tangu mwaka 2006 kwa miaka 15 sasa,” anasema kiongozi huyo. “Ila nataka niwaombe kuanzia sasa nisogee mbele kwenye uongozi wa juu zaidi, kwenye Kata, nishughulikie Kata nzima ipige hatua ya maendeleo kama hiki kijiji chetu.”
Hali isiyoridhisha
Ingawa Chamlumo ni mmoja wa wanawake ambao wametoa mfano wa uongozi bora katika ngazi ya kijiji, takwimu zinaonyesha idadi ya wanawake wenyeviti wa kijiji ni ndogo mno hapa nchini na kama juhudi hazitafanywa na wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia yanayotetea haki za wanawake, vyombo vya habari na wanahabari na taasisi za dini, huenda uchaguzi ujao idadi ya wanawake wenyeviti wa Serikali za vijiji ikaendelea kuwa ndogo.
Swali kuu la kujiuliza ni: Je, uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu wa 2024 utaongeza idadi ya wanawake wenyeviti wa vijiji, hasa kwa kuzingatia kuwa viongozi hao ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya vijiji?
Takwimu zinaonyesha kwamba katika ngazi ya kitongozi, ambayo ndiyo ya chini kabisa katika utawala wa nchi yetu, idadi ya wanawake katika ngazi hiyo ni mdogo sana. Nchi yetu ina vitongoji 62,612, ambapo, kwa mujibu wa takwimu kutoka Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2019, ni wanawake 4,171 tu ndiyo walioshinda nafasi za uenyekiti wa vitongoji, sawa na asilimia 6.7.
SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?
Kwa upande wa mijini, ingetarajiwa kwamba wananchi wangeweza kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya demokrasia na hivyo idadi ya wanawake wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uwe ni mkubwa, lakini hali halisi ya ushiriki wa wanawake kwenye uongozi wa utawala wa mitaa mijini bado ni duni sana.
Takwimu zinaonyesha kwamba wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaawa mwaka 2019, nchi ilikuwa na mitaa 4,171, ambapo wanawake waliochaguliwa kuwa wenyeviti wa mitaa walikuwa ni 528 tu nchi nzima, sawa na asilimia 12.6.
Hali ya uongozi wa wanawake ni mbaya zaidi vijijini. Nchi nzima ina vijiji 11,915, ambapo wenyeviti wa vijiji wanawake ni 246 tu, sawa na asilimia 2.1.
Tafsiri ya idadi hii ndogo sana ya wanawake wenyeviti wa vitongoji, mitaa na vijiji ni kwamba maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika ngazi za chini wanakoishi wananchi wengi bado ni changamoto kubwa sana hapa nchini na ndiyo sababu mamilioni ya wananchi wa taifa hili ni mafukara na wanaishi maisha yasiyo na furaha.
Taarifa ya dunia kuhusu hali ya furaha kwa wananchi kwa mwaka 2024 inaonesha kwamba Tanzania imeshika namba 131, wakati mwaka jana, 2023, ilikuwa nchi ya 129. Hii inaashiria kwamba hali ya wananchi wa Tanzania kutokuwa na furaha mwaka 2024 imepungua ikilinganishwa na mwaka 2023.
Sababu zatajwa
Je, nini chanzo cha kuwa na idadi ndogo ya wanawake viongozi kwenye ngazi za chini?
Mtaalamu wa masuala ya siasa na uongozi, Dk Victoria Lihiru, anasema moja ya tatizo ni mfumo wa uchaguzi ambao umewapangia wanawake viti maalumu, hivyo wanawake wenyewe, na wanaume kutoka vyama vyote vya siasa, wamekuwa wakidhani nafasi za wanawake ni kwenye viti maalumu wakati utaratibu huo ulipaswa kuwa kuwa ni wa mpito.
Jambo lingine ni kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi ambayo itawezesha kila mtu mwenye sifa za uongozi, bila kujali ni mwanaume au ni mwanamke, au chama chake cha siasa, kuweza kugombea nafasi ya uongozi na kushinda au kushindwa kwa haki.
Hoja hii ni muhimu kwa sababu, “Waziri wa TAMISEMI, ambaye ni mwanasiasa na mwenye upande wa chama, ndiye mwenye kauli ya mwisho kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, huyu hataweza kutenda haki kwa mgombea ambaye si wa chama chake,” anasema William Maduhu, Afisa Uchechemuzi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Vilevile, vyombo vya habari, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, au NGOs, ni taasisi ambazo hazifanyi juhudi kubwa kuelimisha na kuhamasisha jamii na wanawake wenye uwezo wa uongozi wajiunge kwenye vyama vya siasa na wagombee nafasi za uongozi katika Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kuweza kutoa uongozi wa kubadilisha maisha duni ya wananchi.
Hatua stahiki
Je, nini kinapaswa kufanyika kutatua changamoto hizi? Jambo la kwanza ni kwa Serikali kuhakikisha inapeleka Bungeni haraka Mswada wa Sheria ambayo itawezesha uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongozi usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili wagombea wa vyama vyote, wanawake na wanaume, watendewe haki, maana kifungu cha 10(1c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi iliyopitishwa mwnzoni mwa mwaka huu ndivyo kinavyoelekeza.
Wizara ya TAMISEMI itoe, mapema iwezekanavyo, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa mwaka huu 2024 na kuhakikisha kanuni hizo na vipengele vyake vinatangazwa kwenye vyombo vingi vya habari ili wananchi wafahamu kanuni hizo na wagombea waweze kujiandaa kikamilifu.
Vyama vyote vya siasa viandae idadi sawia ya wanawake na wanaume wenye sifa na uwezo wa kuwa viongozi bora wa vijiji, mitaa na vitongoji na kuhakikisha wanawake hao wanagombea nafasi hizo.
SOMA ZAIDI: Mwanahamisi Singano: Mfumo Dume Huwabeba Wanaoutetea na Kuwaadhibu Wanaotaka Kuubomoa
Mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na vyama vya siasa watumie mikutano na vyombo vya habari kuhamasisha wanawake na wanaume wa rika mbalimbali, waadilifu na wenye sifa za uongozi, wajitokeze kugombea nafasi za uongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji, na pia kuwaelimisha kuhusu kanuni za uchaguzi huo kwa mwaka huu ili uchaguzi huo uipatie nchi yetu viongozi bora wanaume na wanawake katika nafasi hizo.
Mungu ibariki Tanzania!
Dk Ananilea Nkya ni mwanahabari na mwanaharakati wa jinsia na haki za binadamu. Ana Shahada ya Uzamifu kuhusu namna vyombo vya habari Tanzania vinaripoti masuala ya maendeleo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ananilea_nkya@yahoo.com na @AnanileaN kwenye mtandao wa X.