The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji

Yusuf Manji aliwaachia wafadhili na watu wenye nia ya dhati ya kuzisaidia klabu za wananchi.

subscribe to our newsletter!

Kwa sasa mashabiki wa Yanga wako kwenye majonzi ya kumpoteza mmoja wa viongozi wao na mfadhili mkubwa kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo katika miaka ya karibuni,Yusuf Manji. 

Manji alifariki wiki iliyopita akiwa nchini Marekani ambako inaonekana aligeuza kuwa makao yake baada ya kukwaruzana na viongozi wa kisiasa na kujikuta akihaha kuendesha biashara zake.

Manji amefariki akiwa mbali na klabu hiyo kutokana na kujiweka kando baada ya kupata misukosuko hiyo ya kibiashara iliyosababisha wakati fulani akae gerezani, huku baadhi ya mali zake zikitaifishwa.

Pamoja na Serikali ya awamu ya sita kurekebisha mazingira ya kibiashara na kumtuliza, bado Manji hakutaka kurejea kwenye mpira wa miguu, ingawa alishiriki mkutano mmoja mkuu wa Yanga kuwahakikishia wanachama kwamba bado yuko nao.

Mfanyabiashara huyo alifanya mengi yaliyoipaisha Yanga katika mashindano ya ndani na barani Afrika, na wakati fulani nusura ifanye maajabu ya kuiondoa Al Ahly ya Misri kama si kukosa penati.

SOMA ZAIDI: Lini Tutapunguza Kukimbilia Wachezaji wa Kigeni?

Lakini lililo kubwa ni lile la kuamua kuingia mwenyewe kwenye uongozi badala ya mbinu zinazotumiwa na wafanyabiashara wengi za kuwatumia watu kushika uongozi.

Baada ya watu aliokuwa anawatanguliza kukumbana na misukosuko mbele ya wanachama na hivyo kuongoza klabu kwa shida, au wakati mwingine kushindwa katika uchaguzi, Manji aliamua kujitosa mwenyewe kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, akigombea uenyekiti.

Na kwa bahati nzuri alifanikiwa na akashinda uchaguzi huo na huo ukawa mwanzo wa mafanikio ya klabu ya Yanga ndani ya nchi. Alisajili wachezaji wengi nyota kama Donald Ngoma, Amis Tambwe, Haruna Niyonzinma, Vicent Boussoue ma Thaban Kamusoko.

Yanga ilitawala soka la Tanzania kwa takribani misimu mitano hadi mfanyabiashara huyo alipoachana nayo na Yanga kuingia kwenye misukosuko ya kiuchumi iliyoifikisha hatua ya kutembeza bakuli.

Nachotaka mkione hapa ni ile hatua ya Yusuf Manji kuamua kugombea uenyekiti ili asisumbuke kutumia watu na kulazimika kusema uongo mwingi kutetea kila kitu ambacho wanachama wanaona hakiko sawa.

SOMA ZAIDI: Hivi Wachezaji Wazawa Hawazidai Klabu Zinazowaacha?

Hii ni tofauti na hali ilivyo kwenye klabu ya Simba, ambako Mohammed Dewji anasumbuka kupata uhalali wa kumiliki klabu, huku sheria na kanuni za umiliki wa klabu zinazomilikiwa na wanachama zikimzuia kufikia malengo yake.

Suala la mabadiliko ya muundo wa uongozi, uendeshaji na umiliki wa klabu bado halijawa sawa na hata muundo unaotumiwa sasa wa kuwa na bodi ya wakurugenzi, bado haujawa halali kutokana na sheria na kanuni zinazoongoza suala hilo.

Sikushangaa wakatika CPA Masoud Issa alipotoka na tuhuma dhidi ya vitendo vya mwekezaji huyo kuwa anataka fedha anazotoa zijumlishwe na kuhesabiwa kama mtaji wa Shilingi bilioni 20 alizotakiwa kuwekeza.

Ni dhahiri kuwa msimamo wa CPA Masoud unaweza kuwa ndiyo msimamo wa mwenyekiti wake, Murtaza Mangungu, ambaye amekuwa akilaumiwa kwa klabu hiyo kutofanya vizuri bila ya wanachama na mashabiki kujua ni kwa kiwango gani anahusishwa katika uendeshaji wa shughuli za klabu na nguvu zake kwenye bodi.

Pamoja na kwamba klabu ndiyo inayomiliki zaidi ya asilimia 50 za hisa za klabu, Mangungu ni mjumbe wa kawaida kwenye bodi ya wakurugenzi, wakati Dewji, ambaye anatakiwa kuwa mmoja wa wawekezaji, ndiye mwenye sauti kubwa na anayeteua mwenyekiti!

SOMA ZAIDI: Tujipe Muda Kabla ya Kuanza Kuitumia V.A.R

Hoja kubwa iliyopo ni kwamba upande unaotakiwa uwe na hisa nyingi ni chombo kinaitwa Simba Sports Club Company Limited na si Simba Sports Club ambayo ilifanyiwa tathmini ya mali zake na kupata thamani iliyomtaka Dewji atoe kiwango hicho cha fedha.

Kwa jinsi hali inavyokwenda na ikifikia Simba ikakosa tena mafanikio ndani ya nchi, si ajabu baadhi ya wanachama wakaamua kulivalia njuga suala hilo na kuthubutu hata kwenda mahakamani kwa kuwa masuala kuhusu umiliki hayazuiwi na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

Ni ukweli ulio wazi kuwa kufanya mabadiliko ya umiliki kwa klabu ambayo ilianzishwa na inamilikiwa na wanachama ni kitu kigumu sana, hasa wanapogundua kuwa mabadiliko hayo yanawaondolewa sauti yao katika uendeshaji wa klabu.

Inawezekana kabisa kuwa ugumu huo ndiyo unaifanya Yanga ipige hatua taratibu badala ya kukimbilia kuimilikisha klabu kwa wawekezaji, halafu baada ya miaka miwili watu wawili wanaenda mahakamani na chombo hicho cha haki kuamua kubatilisha mchakato mzima.

Haya ndiyo mambo ambayo Manji aliamua kuachana nayo. Kwa kuwa alikuwa na nia ya dhati ya kuipa Yanga mafanikio bila ya kutumbukiza maslahi yake binafsi, aliamua kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi ili awe kiongozi kamili asiyebughudhiwa na wanachama kwa hoja yoyote ile ya kikatiba.

SOMA ZAIDI: Simba Inahitaji Kutathmini Safari Yake ya Mabadiliko

Akawa mwenyekiti mwenye mamlaka kamili asiyehitaji mizengwe wala hila katika kutekeleza kile alichodhani kitaisaidia Yanga na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa.

Pengine hii ndiyo njia ambayo Mohammed Dewji angeifuata ili aachane na lawama ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara kuhusu fedha anazotoa kwa ajili ya usajili kutotumiwa vizuri na viongozi ambao hawezi kuwaadhibu.

Yusuf Manji aliwaachia wafadhili na watu wenye nia ya dhati ya kuzisaidia klabu za wananchi, mfano mzuri ambao utawafanya wasiingie kwenye migogoro ya kikatiba na wenye klabu zao.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts