The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hatimaye ACT-Wazalendo Wanatoka Mafichoni?

Kitendo cha viongozi wa juu kufika katika maeneo mbalimbali kinatoa motisha na kukuza ari miongoni mwa wananchi katika maeneo hayo kuendelea na mapambano ya kujenga chama na kusimamia maslahi yao

subscribe to our newsletter!

Licha ya kwamba chama cha ACT Wazalendo kinatambulika kama chama cha tatu kwa ukubwa na chama cha pili cha upinzani, bado chama hicho, hususani katika upande wa Tanzania Bara, kimeendelea kujitafuta kwa tochi na kupata changamoto ya kujipata kwa uhakika.

Katika miaka yake kumi, tangu kuanzishwa, chama cha ACT Wazalendo kimekuwa kikihaha kukimbizana, kushindana, na hata kujilinganisha na vyama vikuu nchini – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimejikuta kikilazimika kutaka kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.

ACT Wazalendo inajinasibu kama chama cha upinzani na wakati huohuo kinahudumu na kujiendesha kama “Serikali.” Wakati huohuo ACT inajitambulisha kama chama makini, chama cha masuala na hoja, na kwa wakati huohuo kimekuwa chama cha misala na vihoja – hususani mitandaoni. Vivyo hivyo, ACT inajinadi kama chama cha umma, huku ikitenda zaidi kama chama cha majukwaa na matamko ya kisera.

Pamoja na jitihada zote, rasmi na zisizo rasmi, za kujitambulisha kwa uchanya katika siasa na jamii, ACT inaandamwa na wingu na zimwi la utambulisho hasi. Kwa kiasi kikubwa, chama hicho kimekuwa kinaelezwa na kutambuliwa kama tawi au kitengo cha nje cha chama tawala, yaani kimekuwa kikitambuliwa kama “CCM B,” na hoja hii imekuwa ikivaliwa njuga zaidi na wanachama na wafuasi wa CHADEMA.

Isivyo bahati, mienendo ya chama hicho, hususan ile inayohusisha baadhi ya viongozi na wanachama wake, imekuwa ni kujinyenyekeza, kujipendekeza na kujihusisha na chama tawala na hususani Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala. 

Kwa kipindi kirefu, ACT inaonekana kujitenga na kujiepusha kuwa “wakali” dhidi ya Serikali na hususani kwa Rais; hivyo kutokana na mienendo na maamuzi hayo ya chama, ni dhahiri na rahisi mtu kuwa na mtazamo hasi dhidi ya chama hicho.

Mizizi katika umma

Binafsi, hoja ya ukosoaji dhidi ya ACT ninayojifungamanisha nayo asilimia zote ni chama hicho kutokufanya jitihada madhubuti za kujikita na kuweka mizizi kwa umma. Wakati chama hicho kimekuwa kikipambana kupata utambulisho wa jumla wa kitaifa; njia kuu ambayo imekuwa ikiitumia ni kupitia matamko ya kichama, hususani kupitia Baraza Kivuli la Chama.

SOMA ZAIDI: Kwenye Hili la SUK, ACT-Wazalendo Wamekalia Kuti Kavu

Licha ya kwamba viongozi wa chama wamekuwa wakieleza umuhimu wa Baraza Kivuli, kwamba kutokana na uchanga wa chama na “kutekwa” kwa demokrasia ya uchaguzi katika uchaguzi wa 2020, Baraza Kivuli la chama linalenga kuifuatilia Serikali na vivyo hivyo kuhakikisha na kuhamasisha uwajibikaji kwa watendaji wake. 

Pia, Baraza hilo linakusudia kujenga uzoefu kwa wanachama wake, wengi wao wakiwa ni vijana, katika kujihusisha na shughuli za kisiasa, kichama na kiserikali.

Hakika hizi sababu tatu zina maana na tija kisiasa na kitaasisi. Changamoto, hata hivyo, kwa chama hicho ni kwamba Baraza hilo, kama lilivyo Baraza halisi la Mawaziri la CCM, limebaki kuwa ni chombo cha watu wachache, waliopo “mjini,” waliojitenga na wasiokuwa na mahusiano hai na umma. 

Hali hii, hivyo basi, inalifanya Baraza hilo kutokuwa na tija na maana kwa umma na linakifanya chama hicho kubaki kuwa mafichoni na mbali ya macho na fikra ya wananchi.

Ziara za chama

Wakati Baraza kivuli likiendelea kubaki kivulini, chama hicho, hata hivyo, kimeamua kutoka kivulini na kuingia rasmi na kwa miguu miwili juani. Chama hicho kimeamua kuyavulia maji ya siasa na kuyaoga kwa kuamua kuingia kwenye duara na kuicheza ngoma mtaani. Au, kwa lugha nyingine, kama asemavyo Katibu Mkuu wa ACT Ado Shaibu, chama sasa kiko field.

Kwa miezi mitatu sasa, chama hicho kimekuwa kikifanya ziara za kichama zilizogawanywa katika makundi manne. Ziara hizi za chama ni tofauti na ziara “binafsi” za viongozi. 

SOMA ZAIDI: Je, Viatu vya Zitto Kabwe Vitamtosha Kiongozi Mpya wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu?

Wakati ziara binafsi za viongozi zina lengo kuu la kumtambulisha na kumjengea taswira njema kiongozi husika katika eneo lake analoliongoza, au analokusudia kuliongoza, ziara za chama, hata hivyo, ni ziara zenye lengo kuu la kujenga taswira njema ya chama.

Hatua hii ya kufanya ziara za chama nchi nzima ni hatua ya kupongezwa sana. Ziara hizi zinasaidia kuwakutanisha viongozi wakuu wa vyama na wananchi na wanachama wao, na ndio maana tunaona katika ziara zao, kabla ya mkutano wa hadhara ambapo viongozi huwahutubia na kuwasikiliza wananchi, chama hicho kimekuwa na mikutano ya ndani ya chama, inayolenga kukiimarisha chama na wanachama.

Kitendo cha viongozi wa juu kufika katika maeneo mbalimbali kinatoa motisha na kukuza ari miongoni mwa wananchi, wanachama na viongozi katika maeneo hayo kuendelea na mapambano ya kujenga chama na kusimamia maslahi na masuala yao. 

Kitendo hiki kinaweka mizizi, kinajenga msingi na kutoa fursa kwa viongozi wa kanda, mikoa na maeneo husika kuendelea kujijenga binafsi na kukijenga chama.

Pamoja na kulenga kukiimarisha chama, na hata kuonesha utajiri wa kiuongozi wa chama nchi nzima, ziara hizi pia zinasaidia katika kukifanyia chama tathmini. Vivyo hivyo, kupitia ziara hizi, wananchi wanapata majukwaa ya kusema na kupaza sauti zao dhidi ya madhila yanayowakabili na yaliyofichwa, au kufunikwa, na watawala, na hata baadhi ya vyombo vya habari.

Mifano hai

Mifano hai ni vilio vya wakulima dhidi ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), ambapo mpango huo wa Serikali kuwanusuru wakulima kwa kununua mazao yao, mahindi hususani, umegeuka mpango wa kuwanyanyasa na kuwakandamiza wakulima. 

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Kwa Nini ACT-Wazalendo Tumeamua Kuwa na Ofisi?

Vivyo hivyo, kupitia ziara hizi, tumesikia kuhusu vilio vya wananchi juu ya ukiukwaji wa haki mkoani Tabora, wilayani Kaliua, katika kijiji cha Isawima, ambapo wananchi wamelia juu ya uonevu mkubwa unaofanywa na askari wa hifadhi na Serikali.

Kutokana na mazingira na mifumo yetu ya kidemokrasia, vyama vya siasa vina nafasi kubwa sana katika kukuza na kuimarisha demokrasia. Vyama hivi vinatoa fursa na majukwaa kwa wananchi kusema shida zao, lakini pia vinatoa nafasi ya vyama, kama wawakilishi wa wananchi, kuisimamia na kuhakikisha uwajibikaji wa Serikali.

Kitendo cha ACT Wazalendo kutoa fursa kwa wananchi kuzungumza wakati wa mikutano yao ni jambo jema sana na la kheri. Jambo hili linatoa nafasi ya wananchi kutema nyongo zao.

Vivyo hivyo, linatoa si tu malalamiko dhahiri kwa Serikali, bali pia linakipa chama jukumu hadharani kabisa ya kufuatilia malalamiko hayo. Na kupitia kufuatilia na kusimamia malalamiko hayo ndipo hapo chama kinatarajiwa kujenga uhalali na mahusiano imara na umma.

Ni matumaini yangu kwamba Baraza Kivuli la Chama litapata fursa ya kujitathmini na kujinoa kupitia, na kutokana na, ziara hizi. Ni wakati sahihi kwa Baraza hilo kushiriki kikamilifu katika ziara hizo za chama na hivyo kufanya utaratibu wa kufanya ziara za kisekta kwa nyakati tofauti tofauti, ili kulipa Baraza hilo uhalali na mahusiano na umma.

Wanachama milioni 10

Pamoja na wananchi kupaza sauti zao, viongozi kusikiliza kero za wananchi na viongozi kuzungumza na hata kutoa elimu ya kisiasa na kiraia jukwaani, ili kuing’oa CCM, vyama vya siasa havihitaji tu kuwa na wafuasi, wapenzi na umati mkubwa wa kusikiliza mikutano yao. Vyama vya siasa, kwa umuhimu mkubwa, vinahitaji kuwa na wanachama ambao watajifungamanisha vilivyo na chama chao.

SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: ACT-Wazalendo Yapendekeza Njia Nne Kudhibiti Ubadhirifu Serikalini

Kutokana na mtazamo huu, ni dhahiri hii ndio sababu chama hiki cha ACT kimeanzisha kampeni ya kusajili wanachama milioni kumi ndani ya miezi kumi. Pamoja na kwamba idadi ya wanachama milioni kumi ni lengo kubwa mno, lakini zoezi zima la kupata na kusajili wanachama ni zoezi la muhimu sana ili kupambana na CCM. 

Katika zama hizi, CCM wakiendelea kuonesha hadharani jeuri na kiburi chao cha kisiasa kwamba iwe jua iwe mvua wataendelea kubaki kuwa chama tawala, vyama vya upinzani vinahitaji wanachama ili kupambana na jeuri na kiburi hicho cha chama tawala.

Hata hivyo, ni matumaini yangu kuwa chama hicho kimejidhatiti katika kuendelea kujenga uwezo kwa wanachama wake wapya na wa zamani, ili kuwa na wanachama imara na kupambana na hila zinazooneshwa dhahiri na wanachama na viongozi wa CCM. 

Ni matumaini yangu pia kwamba wanachama hawa, ambao ndio injini na askari miguu wa chama, pia watakuwa hai kiutendaji katika kujenga chama na kuhakikisha kufikiwa kwa kauli mbiu ya chama hicho, Taifa la Wote; Kwa Maslahi ya Wote.
Jasper “Kido” Sabuni ni mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kijamii. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia kidojasper@gmail.com au X kama @JasperKido. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts