The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CHADEMA Kuelekea 2025: Mivutano Hii Itaiacha Salama?

Wafuatiliaji wa siasa wameonesha hofu yao kuwa kama CHADEMA ikipoteza kuaminika kwa wananchi, itakuwa vigumu kujipanga na kuongoza vuguvugu katika sera zake.

subscribe to our newsletter!

Hali ya mivutano ndani ya CHADEMA ni jambo ambalo kwa sasa halifichiki huku kukionekana pande mbili zinazotofautiana kimtazamo. Kwanza upande wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na upande wa pili Makamu Mwenyekiti wa chama kwa Tanzania bara Tundu Lissu.

Hali hii ya mvutano imekuwa wazi zaidi baada ya chama hicho kutoa tamko mnamo Novemba 14,2024, kukanusha kauli kadhaa zilizotolewa na Lissu akiongea na vyombo vya habari huko mkoani Singida.

Akiongea na vyombo vya habari mnamo Novemba 12 na 13, 2024, Lissu amezungumzia kuhusu rushwa, huku akieleza kuwa fedha chafu zimesambaa katika chaguzi za chama hicho.

Ukiacha suala la rushwa, mambo mengine yanayoonekana kuleta mvutano katika chama hicho ni pamoja na: nani atakayekuwa mgombea wa Urais mwaka 2025, lakini pia kutofautiana katika mbinu na mikakati ambayo chama hicho inapaswa itumie kuelekea kwenye uchaguzi.

Baada ya CHADEMA na CCM kuanza mazungumzo ya maridhiano, ndani ya CHADEMA kulikuwa na baadhi ya wanachama waliokuwa wakiona sio njia sahihi kwa chama hicho, huku Tundu Lissu akiwa mmoja ya wadau wakubwa waliokosoa maridhiano hayo.

Mwishoni mwa mwaka 2023, viongozi wakuu wa CHADEMA walikutana Machame, Kilimanjaro, nyumbani kwa Mwenyekiti Mbowe, huku wengi wakiona ilikua ni fursa ambapo mivutano iliyokuwa ikionekana ikitajwa kati ya viongozi wa chama hicho kuweza kumalizwa.

Baada ya kikao hicho, mabadilko yalianza kuonekana hasa katika uelekeo wa chama. Mnamo Januari 13,2024, CHADEMA ilitangaza mabadiliko katika sera zake na kuitisha maandamano kupinga miswada ya uchaguzi pamoja na ugumu wa maisha. Katika kikao hiki Mwenyekiti wa CHADEMA aliweza kugusia kuhusu hali ya umoja wao na sababu ya kubadili msimamo.

“Sisi ni kitu kimoja,” Mbowe alieleza kwenye mkutano huo. “Na wale wote waliofikiri chama hiki kina mgogoro watasubiri sana. Wote wanaofikiri kwamba kuna mpasuko CHADEMA haupo na hautakuwepo tutakilinda na kukihami chama hiki kwa gharama yeyote. Umoja wetu ni wa muhimu kuliko mtu yeyote mmoja mmoja.”

“Mimi nilikuwa mtetezi mkubwa wa maridhiano kwa sababu niliamini  maridhiano ni jambo la msingi katika nchi,” alieeleza zaidi Mbowe. “Hata wenzangu waliponitaka mapema mwenyekiti toka kwenye maridhiano mimi bado niliamini kuna nafasi ya maridhiano.  Ni lazima nikubaliane na wenzangu wote kwamba sasa ni lazima tuanze mapambano na tuwe tayari kwa chochote kitakachotokea”

Katika mkutano huo Mbowe alisisitiza kuwa kutofautiana kwa mawazo kati ya viongozi wa chama chao ni ishara ya demokrasia na sio migogoro.

“Sioni mnaonaje viongozi kuwa na mawazo tofauti yanayokizana eti ni mgogoro sio mgogoro ni kutofautiana kwa fikra na mnapotofautiana kwa fikra mnakaa mnayazungumza mnafanya maamuzi kwa kadiri muda unavyoruhusu,” alieleza Mbowe.

Suala hili la maridhiano limerudi upya katika mijadala ndani ya CHADEMA kufuatia kauli ya Lissu akiongea na vyombo vya habari mnamo Novemba 12, 2024.

“Tunahitaji kujipanga upya, katikati hapa tumedanganywa tukadanganyika,” alieleza Lissu akiongea na waandishi wa habari. Tumeletewa lugha laini ya uongo ya maridhiano, tukazungumzishwa kwa mwaka mzima, tukaacha hoja za msingi za Katiba mpya, mfumo mpya wa uchaguzi.”

Lissu alieleza zaidi kuwa chama chake kilidanganywa na ahadi za uwezekano wa uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo viongozi wake wangepewa nafasi mbalimbali, jambo ambalo CHADEMA imelipinga katika taarifa yake ya Novemba 14, 2024.

“CHADEMA haijawahi kuletewa hoja ya kugawana madaraka,haijawahi kujadili,kutoa au kupokea mapendekezo yeyote ya kitu kinachoitwa ‘Serikali  nusu mkate’,” inaleza taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa chama John Mrema. “Agenda ya Katiba Mpya na madai ya mifumo huru ya uchaguzi haijawahi kuachwa na chama wakati wote wa utekelezaji a program zake.”

Taarifa hiyo inaendelea: “Tunawataka wanachama wetu na viongozi wetu wa CHADEMA kuwekeza nguvu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kupuuza propaganda za kukigawa chama.”

Mgombea wa Urais 2025

Moja ya jambo linalonekana kuleta joto CHADEMA ni suala la nani atakayekuwa mgombea wa Urais CHADEMA ifikapo mwaka 2025. Baadhi ya wadau ndani ya CHADEMA wanaeleza kuwa baada ya Lissu kuona utofauti kati yake na viongozi wenzake unaongezeka, aliamua kutangaza nia yake ya kugombea Urais mnamo Julai 26,2024, kama njia ya kujihami.

Hii inakuja katika kipindi ambacho tayari kukiwa na fununu za malalamiko hasa juu ya mikutano yake kutowezeshwa ipasavyo kifedha ikilinganishwa na viongozi wenzake.

Pia wengi wana matarajio kuwa Mbowe naye atasimama kama mgombea wa Urais mwaka 2025.

Akiongea na The Chanzo, Dk.Azaveli Lwaitama, mtaalamu wa siasa, ambaye pia ni mzee mashuhuri ndani ya CHADEMA anaeleza kuwa kuna kukuza mambo hasa suala la mgombea wa Urais linapotajwa.

“Lissu aliulizwa swali kuhusu mipango yake mwaka 2025, na akajibu, hiyo ndiyo demokrasia,” Lwaitama ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Udhamini CHADEMA anaeleza. “Mwenyekiti hajaongea chochote kuhusu kugombea, na taratibu ni rahisi, yeyote anayetaka kugombea anachukua fomu.”

“Sielewi hii mivutano inayotajwa inatokea wapi,” aliongeza Lwaitama. “Hakuna mtu mwenye wasiwasi CHADEMA, kwa sababu chama hakina utaratibu wa kutoa fomu moja, fomu nyingi zinatolewa.”

“Kuna suala la wapambe ndani ya chama na watu wao, lakini mimi sioni kama ni mivutano; ila wapo wanaokuza mambo kuonesha kuna mivutano, ili kuleta hoja ya kuwa kuna mbadala, CCM; ila kuna mijadala ya kidemokrasia na mitazamo tofauti tu,” alifafanua zaidi.

Lwaitama alisisitiza mambo yote humalizikia katika vikao, jambo ambalo hakuna aliyegoma kuhudhudhuria. Jambo ambalo Mbunge wa zamani na Mwanasiasa mashuhuri wa CHADEMA, Suzanne Lyimo naye alilisisitiza alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu uwepo wa mivutano.

“CHADEMA ni chama kikubwa sana, hatuwezi kuwa na mitazamo sawa; ila haitakiwi iende nje ya chama; tukishamaliza uchaguzi, mkutano utafanyika; tutashikana mikono,” alifafanua Lyimo.

Utofauti kati ya Mbowe na Lissu ni moja ya jambo linaonesha ugumu katika maamuzi ya nani awe mgombea wa Urais CHADEMA. Mbowe anajulikana kama mwanamikakati hodari, mtulivu na mwenye kuzingatia kauli zake.

Upande wa pili Lissu anafahamika kwa kuongea mawazo yake bila kuficha, na hata kwa kutumia maneno magumu na makali. Lissu ameweza kuwa maarufu kwa vijana wengi kutokana na uwezo wake wa kuelezea mambo magumu ya kisheria na kisiasa kwa lugha inayomgusa mtu wa kawaida.

Viongozi wote wawili, Mbowe na Lissu wanaonekana kuwa mashujaa mbele ya wafuasi wa CHADEMA, hata hivyo, Mbowe anaonekana kumuongelea Rais Samia, anaeyetegemewa kusimama kwenye uchaguzi kwa upole zaidi ukilinganisha na Lissu.

“Kama Lissu akiwa mgombea wa CHADEMA, atatumia kampeni nzima kuwafanya CCM wabaki wakijitetea, hasa kwa maneno yake makali,” moja ya mtaalamu wa siasa na mshauri katika vyama vya upinzani aliimbia The Chanzo. “Hii itasumbua sana. Kwa CCM, kwa sasa itakuwa bora wakabiliane na Mbowe kwenye uchaguzi kuliko Lissu.”

Fedha chafu

Mnamo Mei 2024, Lissu akiwa Iringa alitoa tuhuma za rushwa ndani ya chaguzi za CHADEMA kwa mara ya kwanza. Lissu pia alikuja kueleza kuwa hata yeye alifikiwa na baadhi ya viongozi wenzake katika mazingira ya kumtaka apokee rushwa. Lissu alienda mbali zaidi kusema alitajiwa orodha ya viongozi wenzake waliopokea mgao wa rushwa ambazo anasema zinatoka chama tawala.

Hivi karibuni, Lissu alitoboa siri kuwa moja ya kiongozi mwandamizi wa CHADEMA alimpelekea ugeni nyumbani kwake mnamo Novemba 13,2023, kwa lengo la kutaka kumhonga. The Chanzo ina taarifa za uhakika kuwa kiongozi huyo wa CHADEMA aliyepeleka ugeni kwa Lissu ni mmoja wa viongozi wa Kanda za CHADEMA ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge.

The Chanzo ilimtumia ujumbe pamoja na kumpigia simu juu ya tuhuma hizi kiongozi huyo  hakujibu chochote.

“Ukifuatilia chaguzi zinazoendelea kuna hela nyingi sana,” Lissu alieleza akiongea na waandishi wa habari  Novemba 12,2024. “Ni za kwetu? Kama sio za kwetu ni za nani na kwa maslahi ya nani? Sasa tutakabiliana nazo namna gani? Jambo la kwanza kabisa ni kuzipigia kelele.”

“Sisi wanaCHADEMA tunajulikana kwa Watanzania, tulijenga chama chetu kwenye msingi imara wa kukemea rushwa, tukiacha kuzungumza habari ya rushwa ndani ya chama tutaacha kuzungumzia rushwa na ufisadi nje ya chama,” alisisitiza Lissu.

“Kwenye hilo mimi nitasimama, nitazungumza kupinga rushwa mahali popote ilipo na kwa sauti kubwa kabisa kwa sababu tusipofanya hivyo itatuangamiza, itatuangamizia chama,” aliendelea zaidi.

Katika taarifa yake CHADEMA imetoa wito kwa yeyote mwenye ushahidi wa uwepo wa rushwa awasilishe vielelezo ili chama kichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni za CHADEMA.

Wafuatiliaji wa siasa wameonesha hofu yao kuwa kama CHADEMA ikipoteza kuaminika kwa wananchi, itakuwa vigumu kujipanga na kuongoza vuguvugu katika sera zake.

Kuendelea kupungua kwa imani ya wananchi juu ya misimamo ya wanasiasa inaonekana kuwa moja ya sababu ya wananchi kuonesha muitikio mdogo hasa pale wanapohitajika kujitolea.

Kwa sasa, CHADEMA ndio chama pekee cha upinzani ambacho kimeweza kuendelea kuwa katika uwezo mkubwa wa kufanya siasa kwa zaidi ya miongo mitatu. Toka 2005, CHADEMA kimekuwa chama chenye ushawishi wa kipekee katika siasa za Tanzania na kuwa chama kikuu cha upinzani, muda ambao vyama vingine viliweza kupotea katika taswira ya siasa.

Hii inajumuisha vyama kama CUF ambacho kilishuka katika anga la siasa baada ya uchaguzi wa 2015 na NCCR Mageuzi ambayo ilikua katika kilele katika mzunguko mmoja pekee wa uchaguzi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts