The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Lini Tutamsikia Toni Kroos wa Tanzania?

Labda kwa klabu chache kama Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, lakini klabu nyingine ni nadra kukuta wachezaji wengi wanadumu kwenye klabu moja kwa muda mrefu.

subscribe to our newsletter!

Nyota wa zamani wa Real Madrid, Toni Kroos, amefungua milango kwa klabu hiyo, akisema pamoja na kubanwa na shughuli zake kwa sasa, hawezi kusema hatakubali kurudi katika jiji hilo kufanya kazi atakayopewa.

Kroos, ambaye ni Mjerumani, alistaafu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuwa sehemu ya Madrid iliyotwaa karibu kila kombe ambalo mchezaji angetamani kulinyanyua katika maisha yake ya kusakata soka.

Kiungo huyo aliyetwaa Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani, ameeleza hisia zake kali kuhusu mahusiano yake ya karibu na Real Madrid, akionyesha jinsi klabu hiyo ilivyomlea na kumjengea mapenzi makubwa.

“Umuhimu wa Real Madrid utaendelea kuwa uleule kwangu. Ulikuwa wa muda mrefu, mzuri, wa mafanikio na pia uliofikia hatua ya upendo,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Bayern Munich.

“Nitaendelea kujisikia kuwa karibu na Real Madrid, hakuna shaka katika hilo. Na wakati wote nitaitetea Real Madrid, wakati wote nitakuwa upande wao. Hilo halitabadilika, uhusiano ni wa karibu sana.

SOMA ZAIDI: Prince Dube Anapitia Ugumu wa Mbappe

“Kujiweka hadharani katika mazingira ya Real Madrid ni kitu ambacho nitasema si muhimu kwangu kwa sasa. Kwa sasa nitasema hapana, bila kujali ni kwa kiasi gani niko karibu na klabu. Lakini sisemi kwamba katika maisha yangu yote sitafanya kitu na Real au kuwa na chochote cha kufanya na Real, sitasema haiwezi kutokea.”

“Kufanya jukumu gani, hilo litaonekana, labda nitajua baada ya miaka kadhaa kupita tangu nistaafu, katika mwelekeo gani, ningeweza kufikiria kitu au la. Lakini sisemi kwamba haiwezi kutokea wakati fulani ninawezakuonekana kwenye jukumu fulani pale Real.”

Mchezaji aliyeishiba klabu

Haya ni maneno ya mchezaji aliyeishiba klabu yake, akiuambia umma kuwa yuko tayari kurejea kuendelea kuitumikia katika jukumu atakalopewa.

Hii ni kuonyesha heshima kubwa kwa klabu yake kwa jinsi ilivyothamini mchango wake wakati wote alipoitumikia Real hadi ikatwaa ubingwa wa Hispania mara kadhaa, ikaandika historia ya kutwaa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo, Klabu Bingwa ya Dunia, Kombe la Mfalme na mashindano mengine.

Kwa maneno hayo, Kroos ni kama anawaambia aliowaacha kuwa Real inajua kuishi vyema na wachezaji ili mradi wakitekeleza majukumu yao vizuri na kuwa waaminifu hadi pale muda unapolazimisha kuachana na hiyo itamaanisha mahusiano yao na klabu hayataisha pale watakapoondoka.

SOMA ZAIDI: Mwamuzi Omary Mdoe Anastahili Adhabu Kali

Kroos anamaanisha yuko tayari kupokea majukumu kama ya mkurugenzi wa michezo, au wa soka, na kama amesomea ualimu wa mpira wa miguu basi aanze na timu za vijana na kwa kawaida nyota kama hao waliodumu muda mrefu hupewa hadhi ya ubalozi wa klabu.

Hii ni pamoja na kutumia nyota hao wa zamani kuwa mwakilishi katika shughuli za kijamii, kimichezo, vijana, programu za watoto ambao hujisikia vyema pale wanapohudhuria kliniki zinazoendeshwa na wachezaji nyota au wastaafu.

Wachezaji wastaafu wa Real Madrid walipokuja Tanzania walikuwa chini ya mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo, Luis Figo. Figo ndiye aliyekuwa akiongoza timu hiyo katika shughuli kadhaa za kijamii, kama vile mechi za hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha kusaidia jambo fulani katika jamii.

Jicho la Kitanzania

Namuangalia Toni Kroos kwa jicho la Kitanzania, nikiangazia jinsi klabu zetu zinavyoachana na wachezaji katika njia ambazo pengine baadhi hawana hamu na wanajutia kupitia klabu fulani, ingawa kijamii hujitambulisha kama wastaafu wa klabu fulani linapokuja suala la mechi za veteran.

Labda kwa klabu chache kama Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, lakini klabu nyingine ni nadra kukuta wachezaji wengi wanadumu kwenye klabu moja kwa muda mrefu. Kila mwaka viongozi wanajikita kutafuta wachezaji wapya hata kama mchezaji huyo anaenda klabu ambayo nafasi yake tayari kuna wachezaji watatu.

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Wapaze Sauti kwa Pamoja Dhidi ya Upangaji wa Ratiba Unaobadilikabadilika

Inakuwa kama viongozi hufanya maamuzi hayo wanakutana na wachezaji mitaani na baada ya mazungumzo kidogo ndipo huamua kuwasajili bila ya kuwafuatilia kwa muda mrefu kujua kama kiwango chake ni kama homa ya vipindi; leo iko kali, kesho imepoa.

Katika mazingira hayo, klabu inaweza kuwa na wachezaji wachache sana waliodumu kwa muda mrefu na kustahili hadhi ya ugwiji au lejendi, kiasi cha kufikia kiwango cha kutoa maneno kama ya Kroos kwa Real Madrid.

Mchezaji anayerudi kwa ajili ya kufanya kazi na klabu baada ya kustaafu ni yule aliyekuwa mnyenyekevu kwa viongozi waliopo wakati huo au anayerudi na vyeti kwa kuwa ameshasomea utaalamu au fani fulani au ambaye kiongozi aliyepo sasa alikuwa anamuhusudu na hivyo kumpatia jukumu.

Klabu zinahitaji kujenga utamaduni huu wa kuishi na wachezaji vizuri kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kuwezesha vipaji vyao vichangie mafanikio ya klabu na zionyeshe kutambua mchango huo.

Ni ajabu sana kwamba hawa wachezaji waliozihudumia klabu zao kwa nguvu zote wanalelewa na Shirikisho la Soka (TFF) baada ya kustaafu. Klabu hazijui zifanye nini nao, hazina programu za kijamii na kimichezo zinazoweza kufanywa na wachezaji wao wa zamani, na hazijui wastaafu wanaweza kufanya kazi gani za kibalozi. 

SOMA ZAIDI: Mashabiki Taifa Stars Watoke Wapi?

Toni Kroos aliziona hizo kazi ndiyo maana anasema yuko tayari kwa kazi yoyote muda utakapofika. Kwa klabu zetu, kuna kazi gani za kufanywa na akina Zamoyoni Mogella, Omary Hussein, Huseing Ngulungu, Muzamil Yassin au Kally Ongala?

Bila ya kuwa na programu nje ya zile dakika tisini, hatutasikia maneno kuntu kama ya Toni Kroos, maneno ambayo yanamaanisha klabu zina shughuli nyingi na tofauti za maendeleo.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts