Baada ya kumalizika kwa fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Qatar, kiongozi mmoja wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) alinukuliwa akisifu unazi wa mashabiki wa nchi hiyo ya Asia Magharibi.
Ofisa huyo alisema takriban asilimia 40 ya mashabiki waliokuwa uwanjani kushuhudia mchezo wa nusu fainali kati ya Morocco na Ufaransa walikuwa ni Wamorocco, na hivyo akasema haitakuwa ajabu kwa taifa hilo la Kiarabu kupewa nafasi ya kuandaa fainali hizo.
Na kweli, haikuwa ajabu kwa Fifa kuipa Morocco haki za kuandaa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030 pamoja na Hispania na Ureno, ikiwa ni mara ya kwanza kwa shirikisho hilo kuzipa nchi tatu uenyeji wa pamoja.
Kwa hiyo, mbali na kuwa na miundombinu bora kama viwanja na hoteli, ushabiki una nafasi kubwa katika kuamua masuala kama hayo ya uenyeji wa miashindano makubwa.
Kwa sasa, Tanzania inajiandaa kwa fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, maarufu kama CHAN 2025, zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuzipa nchi tatu uenyeji wa mashindano hayo makubwa yanayoshirikisha timu za taifa zenye wachezaji wanaosakata soka ndani ya bara la Afrika.
SOMA ZAIDI: Kwa Kamwe, Ali: Soka Sasa ni Biashara
Ushabiki wa mpira nchini Kenya na Uganda umeshuka, hasa kutokana na timu zenye upinzani wa jadi za Express na Sports Club Villa (Uganda) na AFCL Leopards na Gor Mahia (Kenya) kupoteza nguvu zao.
Ushabiki wa soka
Lakini kudumu kwa Simba na Yanga katika kupigania ubingwa wa nchi kumewezesha klabu hizo kuendelea kuwa na mashabiki lukuki nchi nzima. Lakini hawa si mashabiki wa mpira wa miguu, ni mashabiki wa Simba na Yanga tu.
Kwa mantiki hiyo, hata timu ya taifa inapocheza, hufanyika juhudi kubwa ya kuhamasisha watu waende uwanjani kuishangilia na mara kadhaa Rais Samia Suluhu Hassan hununua tiketi zote za mzunguko ili kuwezesha mashabiki kujaa uwanjani.
Mashabiki kama hawa wanahitaji kampeni kubwa ya hamasa ili wajitokeze viwanjani kwa wingi wakati fainali za CHAN zitakapofanyika nchini kuanzia Februari 1 hadi Februari 28.
Ukizingatia kuwa fainali za CHAN hazihusishi wachezaji nyota wanaosakata soka barani Ulaya kama vile akina Ashraf Yakini, Victor Osimhen, Mohamed Sallah na Victor Onana, ni nadra sana mashabiki wanazi kujitokeza uwanjani hadi sifa zitakapotamalaki za wachezaji wanaong’ara.
SOMA ZAIDI: Wageni Hawakuzi Soka la Tanzania, Wanalitangaza
Hivyo, kuwaambia watu wajitokeza kuangalia fainali kama hizo ni kitu ambacho kinahitaji ubunifu mkubwa na mbinu za kiufundi.
Tayari Serikali ilishatangaza kamati ya maandalizi ya mashindano hayo na yale ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) yatakayoandaliwa kwa pamoja tena na nchi hizo tatu za ukanda wa Afrika Mashariki.
Hakuna hamasa
Tukiwa tumesaliwa na takriban mwezi mmoja kabla ya kuanza fainali hizo, hakuna hamasa kubwa inayoonekana ya kuwaandaa mashabiki na nchi kwa ujumla. Hatuoni hata kama fursa inayoendana na kuandaa fainali hizo kiuchumi, kibiashara na kijamii inatumiwa vizuri wakati huu wa kuelekea fainali hizo.
Hatuoni mabango yanayowaandaa watu kwa fainali hizo, na hivyo hata kampuni za kibiashara hazijitokezi kujihusisha na fainali hizo za CHAN 2025 ambazo zitakuwa kama mtihani wa uwezo wetu katika kuandaa mashindano makubwa kabla ya mwaka 2027 kufika.
Ni vigumu kwa CAF kutupokonya uenyeji wa AFCON 2027 kwa kutoandaa vizuri CHAN 2025, lakini tutakuwa tumetia doa taswira ya nchi na kulifanya shirikisho hilo kufikiria mara mbili kila tatizo litakapotokea kabla ya kuandaa fainali zijazo.
SOMA ZAIDI: Wanaohoji Rangi ya Njano Yanga Wako Sahihi. Viongozi Wawasikilize
Ni muhimu kwa waliopewa dhamana ya kuandaa fainali za CHAN 2025 kujitokeza sasa na kuangalia jitihada gani zifanyike kujenga hamasa na kuuandaa umma ili fainali zitakapofika zikute taifa liko tayari.
Unazi huu wa Simba na Yanga ukigeuzwa kuwa wa mpira wa miguu, unaweza kulipa taifa letu sifa kubwa barani Afrika na duniani kama itabidi.
Zile jitihada za kuwatumia akina Ali Kamwe na Ahmed Ali kuhamasisha mashabiki kujitokeza kuiangalia Taifa Stars ziongezwe nguvu na kupanuliwa zaidi, huku watu wa masoko wakiziuza fainali hizo kiufundi ili kuzipa thamani itakayovuta kampuni kuangalia fursa zinazoambatana na mashindano hayo makubwa.
Uzalendo
Vyombo vya habari pia havina budi kuweka mbele uzalendo kwa kuanza kuzungumzia fainali hizo za kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kwa kuibua mijadala kama ya viwango vya bei za tiketi, nyota wanaotarajiwa kung’aa, ubora wa timu na mambo mengine.
Kama kuna sehemu taifa limepata fursa ya kuchukua pointi, basi ni kuanzia fainali za CHAN 2025 ambazo zitatupa picha kubwa ya fainali za AFCON, kabla ya kuanza kufikiria mashindano mengine makubwa ya Afrika, kama AFCON ya wanawake na mechi za Super Cup.
SOMA ZAIDI: Lini Tutamsikia Toni Kroos wa Tanzania?
Mechi kama za Super Cup ni za kibiashara sana na zinapelekwa katika nchi ambazo zina mashabiki wanazi ambao hata kama timu zao hazishiriki, hujitokeza uwanjani kushuhudia nyota wa bara lao, au hata nyota wanaotamba dunia, ndio maana Hispania ilipeleka Super Cup yake Marekani.
Tunahitaji aina hii ya ushabiki wakati wa CHAN 2025 na AFCON 2027.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.