Dar es Salaam. Hatimaye jana Januari 5, 2024, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, alijitokeza hadharani na kutangaza kuwa atawania nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaofanyika Januari 21, 2025.
Kitendo cha Heche kuchukua fomu na kutangaza kuwa atamuunga mkono mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti, Tundu Lissu, kimeendelea kuufanya uchaguzi huo uwe na mvuto mkubwa, na huenda upinzani ukawa mkali zaidi kwa Ezekiel Wenje, anayegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara pia, akimuunga mkono Freeman Mbowe, anayegombea Uenyekiti.
Mpaka anatangaza uamuzi wa kugombea nafasi hiyo, Heche amekuwa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA tangu mwaka 2011, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), amekuwa diwani wa kata ya Tarime Mjini pia amewahi kuwa mbunge wa Tarime Vijijini, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.
“Nimeamua kuchukua fomu baada ya kutafakari, na wanachama wengi kuzungumza na mimi kugombea Umakamu Mwenyekiti,” alisema Heche wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza.
“Ninataka tuongoze chama hiki kuelekea malengo ya uanzishwaji wake. Malengo ya kushinda uchaguzi, kuiondoa CCM madarakani, na kutumia rasilimali za nchi yetu kwa ajili ya mabadiliko ya watu wetu.”
“Tunataka tuchukue chama hiki, kiende kishike dola, kitengeneze madini yetu, dhahabu yetu ichimbwe na vijana wetu watajirike na waishi maisha mazuri. Tuwape watu wetu matibabu bora, inawezekana.”
SOMA ZAIDI: Kinachoendelea CHADEMA ni Matokeo ya Mkinzano wa Kitabaka Ulioshindwa Kutatuliwa Tangu Kuanzishwa Kwake
Kwa upande wake Ezekiel Wenje amewahi kuwa Mjumbe wa Jimbo la Nyamagana kwa tiketi ya CHADEMA katika kipindi cha 2010 hadi 2015. Lakini pia Wenje ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, ambaye mwaka 2020 alijitosa ubunge katika jimbo la Rorya ambapo alijikuta ni mkimbizi wa kisiasa baada ya kuhofia hali ya usalama wake kutokana hali ya mbaya ya usalama kwa wanasiasa wa upinzani baada ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa utafiti ambao The Chanzo imeufanya kutokana na taarifa za kwenye mitandao ya kijamii, kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho mpaka sasa waliojitokeza kuchukua fomu ya kuwania ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, Mwenyekiti anayetetea nafasi hiyo, Freeman Mbowe na makada wa chama hicho Odero Charles Odero na Romanus Mapunda.
Hata hivyo, kwenye nafasi hii ushindani mkali upo baina ya Mbowe na Lissu, mafahari wawili ambao duru zinaonesha kuwa mmoja wao ndiyo ataibuka kidedea.
BAVICHA
Hili ni Baraza la Vijana wa CHADEMA, chombo ambacho kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kwenye mapambano ya kupigania agenda mbalimbali za chama chao ikiwemo ya Katiba Mpya, pamoja na masuala mengine yanazozigusa jamii za Kitanzania. Kwa kipindi hiki kinachomalizika baraza hili likuwa chini ya Mwenyekiti wake John Pambalu.
Deogratius Mahinyila ni moja wa vijana waliojitokeza kutaka kurithi mikoba ya Pambalu. Mahinyila ni kada wa CHADEMA aliyewahi kuwa mfungwa wa kisiasa kwenye uchaguzi wa 2020 baada ya kushiriki uchaguzi kwenye nafasi ya diwani, huko Dodoma.
Mwaka 2021 aliapishwa kuwa Wakili baada ya kutoka gerezani, tangu hapo Mahinyila amekuwa kwenye jopo la Kurugenzi ya Sheria ya CHADEMA. Kwa nyakati zote amekuwa mstari wa mbele kushiriki shughuli za chama chake hicho.
SOMA ZAIDI: CHADEMA Kuelekea 2025: Mivutano Hii Itaiacha Salama?
Wengine waliojitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti BAVICHA ni Masoud Mambo, kijana aliyewahi kuwa kiongozi wa CHADEMA wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya CHADEMA(CHASO), tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2019/20. Mambo pia amekuwa mwanaharakati wa masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii tangu alipohitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pamoja na Shija Shibeshi, kada wa CHADEMA ambaye amejinasibu kuwa endapo atachaguliwa atalifanya baraza hilo liwe lenye ushirikishwaji wa kazi wa pamoja kati ya vijana wa ndani ya chama na nje ya chama. Shija amewahi kuwa mgombea wa ubunge kupitia CHADEMA katika jimbo la Misungwi mwaka 2020. Kabla ya hapo aliwahi kuwa kiongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya CHADEMA(CHASO) katika kipindi cha mwaka 2018/19.
Walijitokeza kugombea kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti BAVICHA ni pamoja na; Nice Sumari, Katibu wa (BAVICHA) jimbo la Kibamba, ambaye ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo ili akipata nafasi afanye kazi ya kuwakumbusha vijana juu ya wajibu wao wa kisiasa na kushiriki kulikomboa taifa.
Wengine wanaogombea kwenye nafasi hiyo ni Necto Kitiga, pamoja na Juma Mohammed Ng’itu, kada wa CHADEMA kutoka kanda ya kusini ambaye amejinasibu kutengeneza baraza litakalowafanya vijana wapate moyo wakupambania nchi na chama chao.
Kwenye nafasi ya Katibu Mkuu BAVICHA aliyejitokeza ni Sheila Mchamba na Benjamin Ntele, na kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu BAVICHA aliyejitokeza ni Revlin Mbugi.
BAWACHA
Hili ni Baraza la Wanawake wa CHADEMA ambalo nalo limekuwa mstari wa mbele kupigania masuala mbalimbali yanayozigusa jamii za Kitanzania. Uongozi unaomaliza muda wake kwenye baraza hili ulikuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti wake, Sharifa Suleiman.
SOMA ZAIDI: Maandamano ya Septemba 23 ya CHADEMA na Mustakabali wa Siasa za Tanzania
Sharifa ameibuka tena na hivi sasa ametangaza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Susan Kiwanga, kada wa CHADEMA ambaye amewahi kuwa mbunge wa jimbo la Mlimba, huko Morogoro, naye ameibuka na kutia nia ya kuwa Mwenyekiti wa BAWACHA.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Wananchi la CHADEMA na mgombea ubunge wa jimbo la Ulanga mwaka 2020, Bi Celestine Simba naye ametia nia katika kinyang’anyaro hiko.
Kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti BAWACHA, Moza Ally, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA taifa anayemaliza muda wake amejitokeza kuwania nafasi hiyo. Anategemewa kuchuana na Elizabeth Mwakimomo.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa BAWACHA, Catherine Ruge, ambaye alikuwa ameikalia nafasi hiyo hadi sasa ametia nia ya kuitetea tena, lakini pia Ester Daffi na Pamela Maasay aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, wamejitokeza kuwania nafasi hiyo, huko Glory Tausi yeye akiwania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu.
BAZECHA
Hili ni Baraza la Wazee wa CHADEMA ambalo nalo limekuwa mstari wa mbele kupigania masuala mbalimbali ya wazee na jamii nzima za Kitanzania kwa ujumla. Kwa kipindi cha miaka mitano inayomalizika baraza hili lilikuwa chini ya Hashim Juma Issa.
Waliojitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti ni John David Mwambigija maarufu kama Mzee wa Upako ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa CHADEMA mkoani Mbeya na mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CHADEMA jimbo la Rungwe mwaka 2015.
Wengine ni Suzan Lyimo, Spika wa Bunge la Wananchi la CHADEMA na mbunge wa muda mrefu wa zamani wa viti maalumu, na kada Hungo Kimaryo. Kwa upande wa Katibu Mkuu amejitokeza Casmir Mabina, kada wa CHADEMA aliyewahi kuwa mratibu wa CHADEMA kanda ya Pwani.
Wajumbe wa Kamati Kuu
Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA mkutano mkuu wa chama hiko huchagua wajumbe wa Kamati Kuu watakaotoka katika makundi ya upande wa Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika). Ambapo katika hayo makundi wajumbe watapatikana kwenye makundi madogo yenye lengo la kuleta ujumuishaji yaani, walemavu, wanawake na kundi mchanganyiko.
SOMA ZAIDI: Kamata Kamata ya Wanachama na Viongozi wa CHADEMA Yaendelea. Lissu, Mnyika na Sugu Wakamatwa
Waliochukua fomu ni pamoja na Naftal Daniel ambaye ni kada wa muda mrefu wa chama hiko aliyewahi kuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Kwela mwaka 2015 na 2020 kwa tiketi ya CHADEMA. Naftal pia amewahi kuwa Afisa Utawala wa makao makuu ya BAVICHA chini ya Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu Deogratius Munisi.
John Pambalu, huyu ni Mwenyekiti wa BAVICHA anayemaliza muda wake na aliwahi kuwa diwani wa kata ya Butimba, Mwanza kipindi cha 2015 hadi 2020. Pambalu ambaye alianguka katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kanda ya CHADEMA ya Victoria ameamua kujitosa katika ngazi ya taifa.
Twaha Mwaipaya, Katibu wa Hamasa wa BAVICHA anayemaliza muda wake naye amejitosa katika kinyang’anyiro hiko. Twaha amekuwa kada mashuhuri ndani ya CHADEMA na mwaka 2020 alijikuta kama mfungwa wa kisiasa baada ya kuwekwa mahabusu pasipo kushitakiwa kwa zaidi ya miezi mitatu.
Dorcas Fransis mwanachama wa CHADEMA ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa vuguvugu la wanawake ndani ya BAVICHA maarufu kama BAVICHA queens naye amejitosa katika kinyang’nyiro hiki.
Patrick Ole Sosopi, kada huyu wa CHADEMA amewahi kuwa kaimu Mwenyekiti wa BAVICHA taifa na mgombea ubunge wa jimbo la Isimani kwa tiketi ya CHADEMA mwaka 2015. Sosopi pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA ambaye anamaliza muda wake.
Wengine waliochukua fomu ni Grace Kiwelu, Sina Said Manzi, Pasquina Ferdinand Lucas, William Mungai, Jenerali Kaduma, Frank Mwakajoka, Wakili Michael Mwangasa na Sina Said Manzi.