Ulimwenguni kote, madai na safari ya haki imekuwa ni safari ya mapambano. Kutokana na hili, haishangazi kwamba Nelson Mandela, mwanamapinduzi na Rais wa kwanza wa haki wa Afrika Kusini, alisisitiza, “Ni safari ndefu kuelekea uhuru.” Katika safari hii tunahitaji silaha na mbinu za aina zote – zinazoonekana na zisizoonekana.
Kama sehemu ya mapambano ya haki, hata kama tukichukizwa vipi, hatuwezi kuzipuuza mahakama kama ulingo mwingine wa kupambania haki. Wakati wa utawala wa makaburu nchini Afrika Kusini, na vivyo hivyo, wakati wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani, mahakama zilitumika kama ulingo wa kupambania haki, licha ya mahakama hizo na sheria za wakati huo kutokuwa upande wa Waafrika wa Afrika Kusini na watu weusi wa Marekani.
Nchini Tanzania, kwa sehemu kubwa ya historia ya nchi yetu, mahakama zilitumika na zilikuwa ni chombo kikubwa katika kukuza haki na demokrasia, chini ya dhana ya “harakati za kimahakama,” au judicial activism kwa kimombo.
Miaka ya karibuni, hata hivyo, taratibu tumeshuhudia mahakama zimekuwa zinapoteza imani na matumaini yake kwa sehemu kubwa ya umma wa Tanzania. Licha ya unyeti wake, mhimili huu umepokea ukosoaji mkubwa kutoka kwa wasomi, wananchi na wadau wa haki na demokrasia.
Leo hii, ni tathmini yangu kwamba, mahakama zimefifishwa meno yake, hususani na sheria za hovyo na mfumo mzima wa kiutawala. Hali hii ndiyo imenikumbusha kuhusu uzoefu na historia ya ukoloni na ubaguzi, ambapo mahakama zilikuwa na meno ya kuwauma zaidi watu weusi na Waafrika, kuliko kuwauma wadhalimu wazungu.
SOMA ZAIDI: Dorothy Semu: Kwa nini ACT-Wazalendo Tumeandaa Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa?
Kama nilivyoeleza hapo awali, Waafrika na watu weusi walipambana ndani na nje ya mahakama; na mageuzi na mabadiliko yalipatikana ndani na nje ya mahakama. Hivyo, leo hii, sisi kama ACT Wazalendo, tukionesha kuumizwa na kuchukizwa na mwenendo mzima wa uchaguzi, wakati tukiendeleza mapambano yetu kwengineko na kwa namna mbalimbali, tumeamua pia kuelekeza mapambano yetu ya kudai haki katika ulingo wa mahakama.
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, tumeshuhudia wagombea wetu nchi nzima wakienguliwa pasipo sababu za msingi; tumeshuhudia mawakala wetu wakikataliwa kuhudumu kama mawakala; na watu wetu waliojiandikisha majina kunyimwa haki na fursa ya kupiga kura, huku watu ambao hawajajiandikisha na wasiokuwa na vigezo vya kupiga kura, hususani watoto, wanafunzi wa shule, wameruhusiwa kupiga kura.
Tumeshuhudia kura kuibwa mchana kweupe; watu wetu kushinda lakini matokeo kutangazwa kivingine; kukosekana kwa uwiano katika kura zilizopigwa; na wagombea wetu kadhaa majina yao kukosekana au kutokuwepo kwenye karatasi za kupiga kura.
Haya, miongoni mwa mambo mengine mengi, yamejitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji. Ukiukwaji huu wa haki umewanyima wananchi kuchagua viongozi wao wa kweli kwenye ngazi ya msingi kabisa.
Viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji ndiyo kimsingi viongozi wanaoshughulika moja kwa moja na ustawi na maendeleo ya wananchi. Kunyimwa au kuporwa haki ya msingi ya kuchagua viongozi wa kweli na wanaowataka, kuna wanyima wananchi haki ya dhati ya kustawi na kuendelea.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Kwa Nini ACT-Wazalendo Tumeamua Kuwa na Ofisi?
Baada ya uchaguzi, kilio cha wanachama na wananchi wetu vijijini na mitaani ilikuwa ni sisi kama chama kuchukua hatua. Wananchi wamesisitiza kwamba wamechoshwa na uchafu na uporaji na dhulmati katika ardhi; wananchi wametueleza kwamba tunapaswa kukomesha huduma mbovu za kijamii na utawala wa mabavu; wananchi mitaani na vijijini baada ya uchaguzi wametukumbusha kauli mbiu yetu ya “Uwajibikaji na Uadilifu.”
Nasi kama ACT Wazalendo tumeamua kuwajibika kwa wananchi wetu kwa kwenda Mahakamani kudai haki. Tumeamua kuingia mahakamani kupingana na vitendo visivyo vya kiadilifu vya Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi. Tumeamua kwenda mahakamani kupambana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi. Tumeamua kwenda mahakamani kuishinda dhulma ya dola na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Tunatambua kadhia na ulakini wote uliopo katika sheria na katika vyombo vya kusimamia sheria na haki, na tunatambua changamoto za watu waliopo na kuviongoza vyombo hivi; lakini sisi ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba, kwetu sisi, mahakama ni ulingo wa mapambano, nasi tunaenda kupambana, na kimsingi tunaenda kushinda.
Nikikopa msemo aliousisitiza mwanazuoni Haroub Othman kwenye kitabu chake Yes, In My Lifetime, nasi tunasema, tutakuwa wa mwisho kubwaga manyanga kwenye kutetea na kuulinda. Kadiri ambavyo tutaendelea kuwa hai, hicho ni kitu ambacho kamwe, katu, hakitakaa kitokee!
Shangwe Ayo ni Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama cha ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ayoshangwe123@icloud.com au X kama @ayo_shangwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.