The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Taarifa ya Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Uliofanyika Tarehe 27 Novemba, 2024

Wananchi waliopiga kura siku ya tarehe 27 Novemba, 2024 ni 26,963,182 sawa na asilimia 86.36 ya wananchi waliokuwa na sifa ya kupiga kura.

subscribe to our newsletter!

Taarifa hii imetolewa  Novemba 28, 2024, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mohamed Mchengerwa, kutoka katika ofisi zake zilizopo Jijini Dodoma. Unaweza kupakua taarifa hii hapa, au endelea kuisoma.

Ndugu Wanahabari, nimewaita ili kupitia kwenu kuwapa Watanzania taarifa ya matokeo ya uchaguzi wa Viongozi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa uliofanyika jana tarehe 27 Novemba, 2024. Uchaguzi huo ulikuwa na lengo la kuwachagua viongozi ambao ni Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vitongoji, wajumbe wa halmashauri za Vijiji na kamati za mitaa watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2029.

Maandalizi ya Uchaguzi:

Ndugu Wanahabari, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288 zinaelekeza kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kila baada ya miaka mitano (5). Kwa mwaka 2024 Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa NA Vitongoji, wajumbe wa Halmashauri ya Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa umefanyika tarehe 27 Novemba, 2024. Katika Uchaguzi uliofanyika mwaka huu nafasi zilizogombewa ni Mwenyekiti wa Kijiji nafasi 12,280, Mwenyekiti wa Mtaa nafasi 4,264, Mwenyekiti wa Kitongoji nafasi 63,886, Wajumbe wa Serikali ya Kijiji nafasi 230,834 na wajumbe wa Kamati ya Mtaa nafasi 21,320.

Uchaguzi huu umefanyika mara baada ya kukamilika kwa maandalizi ya awali ikiwemo uandaaji wa Kanuni zilizotumika kuongoza zoezi la uchaguzi. Kanuni hizi ziliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau wote wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wengine.

Uandikishaji wa wapiga Kura:

Ndugu Wanahabari, kama mnavyokumbuka, zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lilifanyika kuanzia tarehe 11 mpaka 20 Oktoba, 2024 ambapo jumla ya wapiga kura 31,282,331 walijiandikisha. Kati yao, wanawake walikuwa 16,045,559 na wanaume walikuwa 15,236,772. Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 12 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573 na 574 na Kanuni ya 11 ya Tangazo la Serikali Na. 572 kulikuwa na muda wa wananchi kuweka pingamizi kwa wananchi waliojiandikisha. Baada ya kushughulikia pingamizi wapiga kura waliohakikiwa kwa ajili ya kupiga kura walikuwa 31,255,303. Pingamizi za uandikishaji zilitokana na sababu mbalimbali ikiwemo wananchi kutokuwa wakazi wa maeneo husika na wengine kujiandikisha kwenye maeneo wanayofanya shughuli zao za kiuchumi badala ya maeneo yao ya makazi. Aidha, wananchi waliopiga kura siku ya tarehe 27 Novemba, 2024 ni 26,963,182 sawa na asilimia 86.36 ya wananchi waliokuwa na sifa ya kupiga kura.

Uteuzi wa Wagombea:

Ndugu Wanahabari, mtakumbuka kwamba, tarehe 26 Oktoba, 2024 mpaka tarehe 1 Novemba, 2024 lilifanyika zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa kila chama kwa ajili ya maombi ya uteuzi wa wagombea wa nafasi za uongozi za Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Mtaa, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa.

Baada ya zoezi hilo jumla ya wagombea walioteuliwa baada ya mchakato wa rufani kwa kila nafasi kwa vyama vyote 19 vyenye usajili kamili ni kama ifuatavyo; Mwenyekiti wa Kijiji 18,340: Mwenyekiti wa Mtaa 7,545: Mwenyekiti wa Kitongoji 85,522: Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko) 160,371: Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) 108,166: Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi Mchanganyiko) 18,552 na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) 11,762.

Kampeni za Uchaguzi:

Ndugu Wanahabari, Kampeni za uchaguzi zilifanyika kwa muda wa siku 7 kuanzia tarehe 20 hadi 26 Novemba, 2024 kwa kuzingatia Kanuni na Miongozo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kampeni zilifanyika kwa amani na utulivu kwa kipindi chote cha kampeni kwenye maeneo mengi. Kampeni hizo ziliratibiwa kwa kuzingatia ratiba zilizoandaliwa na kuridhiwa na vyama vyote katika maeneo husika. Nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendesha kampeni za kistaarabu.

Matokeo ya Uchaguzi:

Ndugu Wanahabari, baada ya kukamilika kwa zoezi la kampeni, jana tarehe 27 Novemba, 2024 wananchi walitumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano. Hivyo, naomba nitumie nafasi hii kuujulisha umma wa Watanzania kuhusu matokeo ya uchaguzi huo kwa mujibu wa nafasi zilizogombewa kama ifuatavyo:-

i) Nafasi za Mwenyekiti wa Kijiji:

Ndugu Wanahabari, maeneo yaliyofanya uchaguzi terehe 27 Novemba, 2024 kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji ni 12,271 kati ya nafasi 12,280 zilizopaswa kufanya uchaguzi. Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 12,150 sawa na asilimia 99.01, CHADEMA imeshinda nafasi 97 sawa na asilimia 0.79, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 11 sawa na asilimia 0.09, CUF imeshinda nafasi 10 sawa na asilimia 0.08, NCCR Mageuzi imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01, UMD imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01. Aidha, vijiji 9 havikufanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo vya wagombea baada ya uteuzi.

ii) Nafasi za Mwenyekiti wa Mtaa:

    Ndugu Wanahabari, maeneo yaliyofanya uchaguzi terehe 27 Novemba, 2024 kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa ni 4,264 kati ya nafasi 4,264 zilizopaswa kufanya uchaguzi.

    Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 4,213 sawa na asilimia 98.83, CHADEMA imeshinda nafasi 36 sawa na asilimia 0.84, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 9 sawa na asilimia 0.21, CUF imeshinda nafasi 4 sawa na asilimia 0.09 na CHAUMA imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.02. Aidha, katika mtaa mmoja wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga hakupatikana mshindi kwa sababu kura za wagombea wawili zilifungana.

    iii) Nafasi za Mwenyekiti wa Kitongoji:

    Ndugu Wanahabari, maeneo yaliyofanya uchaguzi terehe 27 Novemba, 2024 kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji ni 63,849 kati ya nafasi 63,886 zilizopaswa kufanya uchaguzi. Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 62,728 sawa na asilimia 98.26, CHADEMA imeshinda nafasi 853 sawa na asilimia 1.34, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 150 sawa na asilimia 0.23, CUF imeshinda nafasi 78 sawa na asilimia 0.12, NCCR -Mageuzi imeshinda nafasi 10 sawa na asilimia 0.02, UDP imeshinda nafasi 6 sawa na asilimia 0.01, UMD imeshinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.003 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.002.

    Aidha, vitongoji 37 havikufanya uchaguzi tarehe 27 Novemba, 2024. Kati ya hivyo, vitongoji 8 havikufanya uchaguzi kwa kuwa wagombea wake walifariki baada ya zoezi la uteuzi. Wagombea hao walitoka katika Halmashauri za wilaya za Kilwa (2), Nanyumbu (1), Itilima (1), Ikungi (1), Manyoni (1), Uyui (1) na Mbarali (1). Aidha, vitongoji 29 havikufanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali. Vitongoji 12 vitarudia uchaguzi kwa kuwa matokeo ya wagombea yalifungana. Vilevile, vitongoji 9 vitarudia uchaguzi kutokana na wagombea pekee kutopata kura za kutosheleza.

    iv) Nafasi za Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji

    Ndugu Wanahabari, matokeo ya nafasi za Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji ni kama ifuatavyo, CCM imeshinda nafasi 229,075 sawa na asilimia 99.31, CHADEMA imeshinda nafasi 1,222 sawa na asilimia 0.53, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 232 sawa na asilimia 0.1, CUF imeshinda nafasi 105 sawa na asilimia 0.05, NCCR – Mageuzi imeshinda nafasi 16 sawa na asilimia 0.01, Demokrasia Makini imeshinda nafasi 3 sawa na asilimia 0.001, NLD imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.0004 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.0004.

    v)  Nafasi za Wajumbe wa Kamati ya Mtaa:

    Ndugu Wanahabari, matokeo ya nafasi za Wajumbe wa Kamati ya Mtaa ni kama ifuatavyo, CCM imeshinda nafasi 21,148 sawa na asilimia 99.30, CHADEMA imeshinda nafasi 101 sawa na asilimia 0.47, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 29 sawa na asilimia 0.14, CUF imeshinda nafasi 16 sawa na asilimia 0.08, NCCR – Mageuzi imeshinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.01, CCK imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.005 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.005.

    Ndugu Wanahabari, maeneo ambayo hayakufanya uchaguzi yatapaswa kuzingatia Kanuni ya 21 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573 na 574 na Kanuni ya 20 ya Tangazo la Serikali Na. 572 ili maeneo hayo yaweze kufanya uchaguzi na kupata viongozi wao. Kanuni hizo zinaelekeza endapo baada ya uteuzi kufanyika, mgombea wa nafasi husika atafariki, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ataahirisha uchaguzi wa nafasi husika na Chama cha Siasa kilichotoa mgombea aliyefariki kinaweza kuwasilisha jina la mwombaji mwingine ndani ya siku arobaini tangu kuahirishwa kwa uchaguzi ili hatua za uteuzi wa mwombaji huyo zifanyike.

    Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573 na 574 na Kanuni ya 36 ya Tangazo la Serikali Na. 572 endapo siku ya kupiga kura kutatokea jambo lolote litakalozuia upigaji kura kuendelea kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ataahirisha upigaji kura hadi siku inayofuata au siku nyingine anayoona inafaa ambayo haitazidi siku saba tangu siku uchaguzi ulipoahirishwa.

    Hivyo, ninawaelekeza Wasimamizi wa Uchaguzi kuzingatia Kanuni hizo katika maeneo yote ambayo hayakufanya uchaguzi siku ya tarehe 27 Novemba, 2024 kutokana na sababu mbalimbali.

    Ndugu Wanahabari, nitumie nafasi hii kuwashukuru vyama vingine ambavyo vilishiriki vizuri kwa kunadi sera zao lakini havikuweza kufanikiwa kupata nafasi katika Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa. Niendelee kuwasihi kuwa ukuaji wa demokrasia ni mchakato hivyo, waendelee kuwa wamoja na kushiriki katika chaguzi zijazo.

    Ndugu Wanahabari, naomba nihitimishe taarifa yangu kwa kutoa shukrani za dhati kwa viongozi wakuu wote, vyombo vya ulinzi na usalama, vyama vya siasa, vyombo vya habari, taasisi za dini, viongozi wa kimila, asasi za kiraia, wasanii, watumishi wa umma na sekta binafsi na wananchi wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa tunathamini na kutambua mchango wao.

    Kipekee, napenda kuvishukuru vyama vyote 19 vya siasa vyenye usajli kamili ambavyo vimeonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa wa kudumisha demokrasia nchini kwa kushiriki kikamilifu mchakato mzima wa uchaguzi huu kuanzia kwenye maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi, kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi, kushiriki kampeni na kugombea nafasi hizo.

    Nitumie fursa hii kuvitambua vyama hivyo ambavyo ni CCM, CUF CHADEMA, UMD, NCCR Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, ADA-TADEA, TLP, UDP, Demokrasia Makini, DP, SAU, AAFP, CCK, ADC, CHAUMA na ACT- Wazalendo,

    Vilevile, natoa shukrani zangu za dhati kwa Wagombea wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa kiwango kikubwa wameonyesha uzalendo mkubwa wa kuchukua fomu, kunadi sera za vyama vyao, kushiriki nafasi mbalimbali za uchaguzi na wengine kuibuka washindi siku ya jana yaani tarehe 27 Novemba, 2024. Niwakumbushe kuwa mwisho wa uchaguzi huu ni mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi ujao hivyo waendelee kujiimarisha ili kushiriki chaguzi zijazo kwa ufanisi zaidi.

    Ndugu Wanahabari, niwashukuru viongozi wote wa Serikali kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali kwa ushiriki wao katika mchakato wa uchaguzi huu. Nishukuru na kuwapongeza viongozi wenzangu na watumishi wote wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata, Vijiji na Mitaa pamoja na vitongoji vyote nchini kwa ushiriki wao katika kufanikisha uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa Mwaka, 2024.

    Ndugu Wanahabari, niwashukuru Wananchi wote walioshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka, 2024. Wananchi wengi walijitokeza kujiandikisha, kugombea nafasi mbalimbali na kupiga kura kwa amani na utulivu. Huu ndio utamaduni wa watanzania na tunu tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu.

    Ndugu Wanahabari, kwa kuhitimisha napenda niwapongeze wagombea wote walioshinda kwenye nafasi zote za uongozi za Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Mtaa, Mwenyekiti wa Kitongoji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa. Aidha, niwatakie utekelezaji mwema wa majukumu yao kwa kuzingatia utawala wa sheria katika kuwahudumia watanzania wote bila ubaguzi. Nichukue fursa hii kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Viongozi wateule wanaapishwa ndani ya siku 14 baada ya siku ya uchaguzi na kupewa mafunzo kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa vitendea kazi muhimu.

    Ndugu wanahabari, sasa nitamke rasmi kuwa, pazia la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka, 2024 limefungwa.

    Digital Freedom and Innovation Day
    The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

    Register to secure your spot

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *

    Related Posts