Mijadala mingi baada ya mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba kushindwa kuchezwa, imeangalia kanuni kutaka kujua nani alikosea na nani ana haki kutokana na kitendo cha Simba kuamua kutopeleka timu uwanjani, Yanga kuweka msimamo kuwa mechi ifanyike na Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo wakati mashabiki washaingia uwanjani.
Kabla ya mechi hiyo ya Machi 8, 2025, Simba ilitoa taarifa jioni ya Machi 7 kueleza kuwa timu yao imezuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi mepesi kama kanuni zinavyotaka, na hivyo kutangaza kutocheza mechi hiyo hadi waliohusika watakapochukuliwa hatua. Barua hiyo haikueleza imesimamia kanuni gani kuamua kutopeleka timu uwanjani, wala kanuni ambayo inalazimisha hatua zichukuliwe kwanza ndipo mechi ichezwe.
Hata hivyo, taarifa ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ilieleza kuwa Simba haikutoa taarifa popote kuwa itakwenda uwanjani muda huo kwa ajili ya mazoezi mepesi. Hata hivyo, ikaeleza kuwa kuna mambo ya kufanyia kazi kabla ya kuchukua hatua, na hivyo imeahirisha mchezo hadi siku itakayotangazwa.
Taarifa zaidi zinasema kuwa basi la wachezaji liliruhusiwa kuingia uwanjani, lakini lililobeba watu ambao si wachezaji lilizuiwa na ndio kisa cha Simba kususa na kuondoka uwanjani bila ya kufanya mazoezi.
Kanuni
Katika mazingira hayo unaona kabisa kuwa kila upande unajua kanuni zinasemaje na kwa makusudi kila upande ukaamua kufanya uamuzi, ukijua kuwa kasoro nyingine zote zitatuliwa kisiasa zaidi kwenye vikao vya juu ambavyo hata Shirikisho la Soka (TFF) na TPLB hawana nguvu.
SOMA ZAIDI: CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?
Katika mazingira hayo ni kupoteza muda kuzungumzia kanuni kwa lengo la kujua ni upande gani ulikuwa halali kuanzia Yanga, Simba, TPLB na TFF. Wote walijua nini wanafanya na mwenye haki hapo atalazimika kufuata maamuzi ya vikao vya juu ambavyo hata wasimamizi wa mpira hawana nguvu, isitoshe hao wenye mamlaka ndio wataomba wasaidiwe na vikao hivyo.
Pande zote tatu zinapima upepo unaelekea wapi kabla ya kufanya uamuzi wa kuridhishana wa kucheza mechi hiyo iliyoahirishwa licha ya Yanga kusema bayana kuwa haitacheza hata iwe nini.
Lakini pia upepo utategemea matokeo ya mechi zinazofuata za timu hizo ambazo kwa kiasi fulani zinaweza kutoa taswira ya bingwa wa 2024/25, Yanga ikiwania kutwaa ubingwa kwa mwaka wa nne mfululizo na Simba ikataka kuurejesha.
Yaani, kama Yanga akiendelea na tofauti ya pointi alizonazo dhidi ya Simba na watani hao wakapoteza angalau pointi nyingine tatu, suala la mechi kupangwa upya halitakuwa na tatizo tena.
Lakini iwapo Yanga hatafanya vizuri katika mechi hizo kabla ya ile itakayopangwa upya, kuna uwezekano mkubwa akaendelea kung’ang’ania apewe ushindi katika mechi iliyoahirishwa. Na msimamo huo utafika mbali.
SOMA ZAIDI: Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti
Hali hiyo pia itakuwa kwa Simba. Iwapo atafanya vizuri mechi zoinazofuata kabla ya mechi itakayopangwa upya, huku Yanga ikiboronga kiasi cha kufikisha tofauti ya pointi angalau nne, Simba haitahangaika na matokeo ya mechi hiyo na itaweza kuiruhusu TPLB iiipe Yanga ushindi ikijua hautaisaidia.
Hali itakuwa mbaya kama matokeo ya mechi hizo hayatatoa picha halisi ya ubingwa. Hapo ndipo TFF italazimika kutumia watu maarufu na wanasiasa kuhakikisha mechi hiyo inachezwa ili kuondoa kadhia ya kufikishana mbali.
Na hali itakuwa mbaya zaidi iwapo Simba itashikilia msimamo wake kuwa haitacheza mechi yoyote ya ligi hadi waliohusika watakapochukuliwa hatua. Hapo msimu utaweza kuwa umeisha.
Madhara
Kwa ujumla, haya ndio madhara ambayo nimekuwa nikiyazungumzia siku zote kuhusu uhuru wa chombo kinachoitwa Bodi ya Ligi (TPLB). Wakati tulipokianzisha tulitaka shughuli zote za uendeshaji wa ligi, utafutaji udhamini, kuajiri wafanyakazi, usimamizi wa fedha na mambo mengine yote.
SOMA ZAIDI: Uwakilishi wa Wazanzibari Unahitajika Uongozi wa Michezo Kitaifa
Ufanyaji wa maamuzi uzingatie kanuni na usimamiwe na klabu kwa utaratibu uliowekwa ambao hazitaruhusu klabu moja kupata upendeleo wakati nia ya kila moja ni kuwa bingwa.
Klabu zenyewe zingeweza kutengeneza utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila moja inatendewa haki kulingana na stahiki zake, na hivyo kuwafanya watendaji, ambao ni menejimenti inayoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, ijisikie kuwajibika zaidi kwa klabu kuliko kwa TFF.
Yaani, klabu ndio wanakuwa wanahisa wanaoichagua bodi ambayo inamuajiri CEO na maofisa wakurugenzi wake, na hivyo kuwa na timu kamili inayoweza kufanya kila jambo bila ya kuingiliwa. Haiwezekani mwenyekiti wa TPLB ashiriki katika vikao vya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (au kamati ya saa 72), halafu pia ndiye aje aendeshe vikao vya bodi.
Anatakiwa awe mbali na uendeshaji na aongoze vikao vya bodi ambavyo vitasikiliza na kujadili taarifa ya utekelezaji ya CEO na baadaye kwenda kuwajibika kwa wanahisa ambao ni klabu. Mwenyekiti wa TPLB akishahusika katika uendeshaji, anawezaje kumuwajibisha CEO?
Hata uenyekiti wa bodi hautakiwi uwe wa kugombea na kuushika kwa miaka minne kama ilivyo sasa, bali kwa viongozi wa klabu au wenyeviti kubadilishana nafasi hiyo kwa zamu kama wanavyofanya wengine kwa sababu tayari CEO anakuwa na timu kamili ya wataalamu wanaoweza kufanya kila kitu kama masuala ya utawala, ufundi, rasilimali watu, masoko na mawasiliano, kama taasisi iliyokamilika.
SOMA ZAIDI: Jamii Haina Budi Kumlinda Ladack Chassambi
Lakini, kwa mfumo uliopo sasa, baadhi ya waajiriwa wanatoka TFF ambao walifuta utaratibu uliokuwa umeanzishwa wa kuajiri wafanyakazi wa ngazi za juu kwa kutumia kampuni binafsi za rasilimali watu.
Badala yake, wengi wanaajiriwa kutokana na utashi wa mtu mmoja, au genge la watu, na hivyo ufanisi hutegemeana na maelekezo na si uwezo.
Taasisi kubwa
Kwa hiyo, TPLB ilitarajiwa kuwa taasisi kubwa yenye uwezo wa kupata fedha nyingi, lakini imebakia kuwa taasisi ndogo ambayo mamlaka yake mengi yapo TFF na hivyo haiwezi kufanya maamuzi yake ikiwa huru kama ilivyoshughulikia sakata la Simba na Yanga.
Kama Simba ilivyotangaza kutokwenda uwanjani, kanuni haziangaliwi TPLB ilivyofanya katika taarifa ya awali kuwa mechi itachezwa kama ilivyopangwa na waliohusika wataadhibiwa. Bali siasa inatumika kama ilivyokuwa katika taarifa ya pili ya kuahirisha mchezo.
SOMA ZAIDI: Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka
Siasa ziliingizwa kwamba Simba ni timu kubwa na ni moja ya taswira za nchi katika soka, hivyo ikisimamia msimamo wake, kanuni zinataka ishushwe daraja.
Siasa hizo ndio zitasababisha kutafutwe mbinu za kunusuru hali hiyo na matokeo yake uamuzi wa kuahirisha mechi ukafanywa kwa makusudi kabisa, huku wanaofanya hivyo wakijua kuwa hawasimamii kipengele chochote cha kanuni. Hapo unajadili vipi uhalali wa timu moja kufanya uamuzi fulani?
Kuokoa jahazi
Kwa hiyo, nilipoona ile taarifa ya TPLB ya kuahirisha mechi na kusoma kilichomo, nilijua ulikuwa ni mpango uleule wa mwaka juzi wa kuokoa jahazi badala ya kusimamia kanuni ili kuilinda ligi na mchezo wa mpira wa miguu.
Kwa hiyo, kuahirisha mechi ulikuwa ni uamuzi wa kuikinga Simba na adhabu ya kushushwa daraja kwa kuwa sababu za kutokwenda zinabadilika kuwa mamlaka zilishaahirisha mchezo na si msimamo usio wa kikanuni.
Ndivyo ilivyokuwa miaka miwili iliyopita wakati Yanga ilipopinga uamuzi wa TPLB wa kubadili muda wa kuanza mechi ndani ya saa 24 wakati kanuni inataka uamuzi huo ufanywe saa 24 kabla ya muda wa mechi. Yanga ilisema ingepeleka timu uwanjani saa 10:00 kama muda uliopangwa awali, na Simba ikasema itapeleka timu saa 11:00 jioni.
SOMA ZAIDI: Uraia kwa Viungo Watatu wa Singida Big Stars Haukidhi Maslahi Yoyote ya Kisoka au Kitaifa. Ubatilishwe
Kati ya saa 10:00 na saa 11:00 TPLB ikatoa taarifa ya kuahirisha mechi na haikutuma waamuzi saa 10:00 wala saa 11:00 ili isiwepo timu ambayo ilistahili kupewa ushindi kutokjana na moja kutofika uwanjani.
Hii ni sinema nyingine iliyochezwa na TPLB kwa kuzingatia siasa za soka na si kanuni zinazolinda mchezo. Kwa hiyo, ni kupoteza muda kujadili kanuni wakati wanaotakiwa kuziheshimu na kuzitumia, hawataki kuziheshimu wala kuzifuata.
Muundo mpya
Maana yake ni nini? Maana yake kunahitajika muundo mpya kabisa wa uendeshaji Ligi Kuu na mamlaka huru ya chombo kinachosimamia ambayo hayataingiliwa na mtu yeyote mwingine wa nje, isipokuwa klabu zenyewe na hivyo kuwajibishana kwa mujibu wa kanuni na taratibu ambazo zitajiwekea.
Hii ya kuweka chombo juu yao, ndiyo inayosababisha klabu ithubutu kusema itasusia kwa sababu yuko wa kumsusia, yaani TFF na Bodi ya Ligi, ambazo haziwajibiki kwa wanahisa wa Ligi Kuu ambao ni klabu.
Kwa hiyo, nguvu kubwa ya mijadala ingeelekezwa kwenye mamlaka ya TPLB badala ya kanuni ambazo inaonekana zinatengenezwa ili zivunjwe, linapofikia suala la Yanga na Simba.
Kama wadhamini wanaotumbukiza fedha nyingi, wamiliki wa haki za matangazo kama Azam Media ambao wametoa taarifa ya kusikitia uozo uliotokea, mashabiki ambao wamesafiri umbali mrefu, wafanyabiashara na wengine wengi walio kwenye mfumo wa kiuchumi na kijamii unaotengenezwa na mpira wa miguu.
Tukijali hao wote tutajiwekea kanuni ambazo zitawajali na kuulinda mchezo, tutakuwa na mfumo mzuri wa uendeshaji utakaojali wadau wote, tutakuwa na muundo wa chombo kinachowajibika kwa wadau wengi zaidi na tutatengeneza mfumo wa haki ambao hautatazama sura za Yanga wala Simba.
Mpira wetu unahitaji uwajinbikaji zaidi kwa wadau mbalimbali.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.