The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Siku ya Wanawake Duniani Itukumbushe Kuwafundisha Watoto Thamani ya Usawa na Haki

Dunia inayowapa wasichana nafasi sawa huanza kwa wavulana na wanaume wanaoelewa maana ya usawa. Kuwalea wavulana wanaoheshimu na kuwawezesha wasichana ni hatua muhimu ya kuvunja mifumo ya ukandamizaji wa kijinsia.

subscribe to our newsletter!

Kila tarehe 8 Machi, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, siku ya kusherehekea mafanikio ya wanawake na kusukuma mbele harakati za usawa wa kijinsia. 

Ingawa mabadiliko makubwa yanafanyika kitaifa na kimataifa, mabadiliko ya kweli huanzia nyumbani. Kama wazazi, tunao wajibu mkubwa wa kuwalea watoto wetu kwa misingi ya usawa na haki. Je, tunawezaje kutumia Siku ya Wanawake kuwafundisha watoto wetu thamani ya usawa na haki? Hebu tujadili.

Dunia inayowapa wasichana nafasi sawa huanza kwa wavulana na wanaume wanaoelewa maana ya usawa. Kuwalea wavulana wanaoheshimu na kuwawezesha wasichana ni hatua muhimu ya kuvunja mifumo ya ukandamizaji wa kijinsia.

Kuwafundisha huruma na uelewa wa hisia. Mara nyingi, jamii huwataka wavulana kuwa ‘wagumu,’ huku wasichana wakihimizwa kuwa wapole na wadhaifu. Tunapaswa kuwafundisha watoto wetu wote kuwa upole, heshima, na kuelewa hisia ni matendo ya utu na uungwana, si udhaifu.

Tuwe mfano wa kuigwa nyumbani, watoto hujifunza zaidi kwa kutazama tunavyotenda kuliko tunavyosema. Wakiwashuhudia baba na mama wakiheshimiana, kushirikiana katika majukumu ya nyumbani, kuhurumiana na kuthamini maoni baina yao, watajifunza kuwa hilo ndilo jambo sahihi na uataratibu wa maisha ya watu waungwana.

SOMA ZAIDI: Fahamu Jinsi Unavyoweza Kuelewa Lugha ya Upendo ya Watoto Wako

Kuanzia michezo wanayocheza, taaluma wanazozitamani, hadi matarajio ya maisha yao, tunapaswa kuvunja dhana potofu kwamba mambo yana ujinsia, kwamba ni ya wavulana tu au wasichana tu.

Uwiano wa kijinsia huanza pia kwa kuwafanya watoto wa kike na wa kiume kuona mifano ya wanawake waliokuwa na uthubutu na wakafanikiwa. Watoto wanaposhuhudia wanawake wakiongoza, wanajifunza kuwa uongozi, ujasiri, na uthubutu si mambo ya kiume tu.

Historia ina wanawake wengi waliopigania mabadiliko makubwa mithili ya Malala Yousafzai hadi Wangari Maathai, na nchini kwetu kuna mifano mikubwa ya wanawake walioshika ngazi za juu za uongozi tukianza na Raisi wetu Mama Samia Suluhu Hassan, Tulia Akson, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Asha Rose Migiro aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mama Gertrude Mongella aliyekuwa raisi wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika n.k.

Kusoma historia zao, vitabu vyao au kutazama filamu zinazowaonesha kunaweza kuwa njia bora ya kuwajengea dhana na ari ya usawa wa kijinsia.

Pia, tunapaswa kuwaeleza watoto wetu kuhusu mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali kama sayansi, siasa, michezo, na biashara. Wasichana wataona kuwa kila ndoto yao inawezekana, huku wavulana wakijifunza kuthamini na kutambua mafanikio ya wanawake.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuzungumza na Watoto Wetu Kuhusu Suala la Mahusiano?

Walimu, madaktari, viongozi wa jamii, kila siku, kuna wanawake wanaoleta mabadiliko. Tunapaswa kuwahimiza watoto wetu kuwaheshimu na kujifunza kutoka kwao.

Mbinu

Tunawezaje kulea watoto wa kike wenye ujasiri na kujithamini? Wasichana wanaojiamini huweza kupigania haki zao na kufanikisha malengo yao bila woga. Tunaweza kuwasaidia kufikia hilo kwa kusifia juhudi, sio tu muonekano wao. Ingawa ni vyema kuwasifia mabinti zetu kuwa wazuri, ni muhimu zaidi kuwapongeza kwa akili, ubunifu, na juhudi zao katika kazi wanazofanya.

Pia, wasichana wanapaswa kupewa nafasi ya kufanya maamuzi nyumbani, kushiriki katika nafasi za uongozi shuleni, na kushiriki shughuli zinazojenga ujasiri wao. Tunapaswa kuwafundisha wasichana kuwa sauti zao zina thamani. Wawe na ujasiri wa kusema wanachohisi, kutetea haki zao, na kupinga unyanyasaji au ubaguzi wa aina yoyote.

Siku ya Wanawake ni mwito wa kuchukua hatua za kuunda mustakabali wa haki na usawa. Tunapowafundisha watoto wetu thamani ya usawa, hatufanyi dunia kuwa bora kwa wanawake tu. Tunafanya dunia iwe bora kwa kila mtu. 

Tunatoa wito kwa wanawake ambao wamebeba jukumu la malezi kwa watoto wa jinsia zote kubadili mtazamo wao juu ya malezi yenye kuhimiza jinsia moja kuwa na fikra za upambanaji na kujituma na kuwa na malezi yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia katika fursa na mafanikio.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwalinda Watoto Wetu Mtandaoni?

Pia, jamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuunda mitazamo juu ya usawa wa kijinsia, hivyo wadau wote kuanzia ngazi ya familia hadi taifa tuelimishe watoto juu ya usawa wa kijinsia ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii. 

Siku hii ya wanawake, tuchukue hatua ya kulea kizazi kitakachokuwa na uthubutu wa kusimama, kusema, na kuongoza kwa wema. Maana mabadiliko tunayoyataka, yanaanzia nyumbani.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×