Shamrashamra za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya zinaendelea sehemu mbalimbali duniani. Ndugu, jamaa na marafiki wanajumuika kwa furaha wakibadilishana mawazo na kujipumzisha. Ni wakati muhimu kwa wanafamilia. Wanafunzi ambao muda mrefu huwa wanakua shuleni wamerejea nyumbani. Wazazi ambao muda mrefu huutumia kazini wanapumzika nyumbani. Familia, kama nguzo muhimu ya ujenzi wa taifa, zinakutanishwa pamoja na kufurahi.
Kwa bahati mbaya, hali haipo hivi kwa mamia ya watumishi wa halmashauri zetu hapa nchini. Wao wameambiwa wasiende likizo ya mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka mpaka wakamilishe ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo vitatumiwa na wanafunzi wanaotarajia kuanza Kidato cha Kwanza mwakani, 2021. Si vyumba vya madarasa tu, wameambiwa pia wahakikishe na madawati yanapatikana. Wameambiwa wafanye kazi usiku na mchana na mpaka ikifika Februari 28, 2021, kazi hiyo iwe imekamilika.
Agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni na Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Wakuu wa Mikoa limesema: “Kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na utengenezaji wa madawati lazima ifanyike usiku na mchana kwa vyanzo vyenu [halmashauri] na vyanzo vyovyote vile. Na kwenye hili hao wasaidizi wenu [Wakuu wa Mikoa] hakuna atakayeenda likizo ya Krismasi wala Mwaka Mpya. Hiyo sikukuu wataitumia palepale kazini na hawatasafiri kwenda kuwasalimia wazee. Msitoe ruhusa hiyo mpaka kazi hii iwe imekamilika.” Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha kuwa, maafisa elimu na idara yote ya elimu, wahandisi, watu wa manunuzi katika halmashauri, hakuna atakayeruhusiwa kwenda likizo huku akitaka wasambae wilaya nzima chini ya usimamizi wa wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kukamilisha ujenzi wa madarasa.
Raisi Magufuli apigia msumari agizo la Majaliwa
Agizo la Waziri Mkuu limeungwa mkono na Rais John Magufuli ambaye katika salamu zake za sikukuu za mwisho wa mwaka, alizozitoa Disemba 24, 2020 amesisitiza kuwa ‘wembe ni uleule’ kwa watumishi wa halmashauri waliozuiwa kwenda likizo. Raisi Magufuli alisema: “Nawatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya. Wale mtakaosafiri kwenda kuwaona ndugu zenu, rukhsa kwa sababu mna wajibu wa kuziona familia zenu. Siku tatu, nne, tano ukikimbia kwenda nyumbani [nje ya kituo cha kazi] kumuona mama yako au babu yako si vibaya. Kweli si vibaya kufika nyumbani na kusalimu, isipokua kwa wale waliozuliwa kwenda likizo na Waziri Mkuu. Nafikiri ni wakurugenzi na watu wengine ambao wanatakiwa kuwajibika kuhakikisha shule zitakapofunguliwa pawepo madarasa.”
Ni ukweli usiopingika kuwa kuna tatizo kubwa la uhaba wa vyumba vya madarasa. Na tatizo hili halijawahi kuisha kwa miongo kadhaa sasa. Kila wakati unapokaribia mwaka mpya wa masomo kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi basi hekaheka za matamko ya ujenzi wa madarasa zinaanza. Hata Disemba mwaka 2019 tulishuhudia Waziri Mkuu Majaliwa Kassim akitoa tamko la kuwataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha vyumba vya madarasa vinajengwa haraka ili mwaka 2020 ukianza, wanafunzi waliofaulu darasa la saba waweze kwenda shule.
Tarehe 5 Disemba, 2019, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo naye alitoa taarifa ya msisitizo kuwa zaidi ya wanafunzi 58,699 waliofaulu darasa la saba walikua hawajui hatma yao ya kujiunga na sekondari kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Jafo akasema zaidi ya mikoa 13 ina tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa ikiongozwa na mkoa wa Kigoma ambao wanafunzi zaidi ya 12,000 walikua wanasubiria ujenzi wa vyumba vya madarasa ufanikiwe ndipo wajue kama wataenda sekondari au la.
Kwa mwaka huu, taarifa bado ni ileile. Uhaba wa vyumba vya madarasa. Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Waziri Jafo wiki iliyopita, inaonesha kuwa ni mikoa tisa tu kati ya 26 ndiyo imeweza kupangia shule wanafunzi wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza. Katika hali hii, zaidi ya wanafunzi 74,166 waliofaulu hatma yao ya kuanza kidato cha kwanza itategemea na kasi ya ujenzi wa madarasa unaofanywa na watumishi wa umma waliozuiwa kwenda likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya. Mkoa kama Dar es Salaam zaidi ya wanafunzi 14,926 waliofaulu hawajapangiwa shule.
Jitihada za zimamoto
Kinachonishangaza si watumishi wa halmashauri kunyimwa kwenda likizo. Nastaajabu, ni vipi tatizo lileile linalojitokeza kila mwaka linaendelea kufanyiwa majiribio ya utatuzi kwa njia za dharura? Ni kwa nini kila mwaka tunasubiri mpaka Disemba na Januari ndipo tuanze ujenzi wa madarasa usiku na mchana ili ikifika Machi ndiyo wanafunzi wetu waanze masomo? Wale wataalamu wa TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Serikali za Mikoa na Halmashauri wameshindwa kabisa kubuni mkakati wa kutatua tatizo hii?
Kama wanafunzi wanafaulu na wanakaa nyumbani miezi miwili wakisubiri madarasa yakamilike kujengwa ndiyo waende shule, tuna uhakika gani kuwa huko shuleni wanapoenda watakuta mazingira rafiki ya kujifunza masomo yote kwa ukamilifu? Nani anao uhakika wa asilimia 100 kuwa wanafunzi hawa elfu sabini na nne wanaosubiri madarasa yajengwe Januari na Februari wakifika shule hawatakuta upungufu wa walimu, upungufu wa matundu ya vyoo, upungufu wa vitabu, upungufu wa maabara au upungufu wa mabweni? Nani anao uhakika kuwa watumishi hawa tuliowanyima likizo za sikukuu ili wajenge madarasa watajenga kwa viwango vya ubora vinavyokubalika na utakuwepo muda wa kutosha wa kuhakiki ubora wa majengo hayo kwa kulinganisha na thamani ya fedha iliyotumika (value for money)? Tuna uhakika hawatachota ‘hela ya sikukuu’ kutoka katika fedha za umma?
Najihoji maswali haya kwasababu tumewahi kuona shule zikijengwa kwa kutumia mbao zilizooza badala ya mpya. Tumeshuhudia majengo yakitoa nyufa katika hatua ya ujenzi wa msingi tu na baadaye ujenzi wote kusimamishwa. Tumeona waziri akikuta ujenzi ukifanyika kwa kutumia udongo badala ya mchanga. Leo sisi tukiwa likizo ya sikukuu, watumishi wetu wanaendelea kujenga majengo ‘mputamputa’ huku wamenuna. Na tunategemea wajenge kwa ubora kabisa. Na kwa kuwa jambo hili linajitokeza mara kwa mara si ajabu mwakani tena tukawazuia watumishi kwenda likizo ili wajenge madarasa na kuchonga madawati usiku na mchana.
Kupanga ni kuchagua
Kama kweli tunataka watoto wetu waende shule kusoma na si kuyaona madarasa tu, ni wakati muafaka sasa viongozi wetu waweke mipango madhubuti kwa kuzingatia sera ya elimu tuliyonayo ili kuondoa tatizo ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa njia zilizo sahihi. Kila mwaka Bunge linaketi na kupitisha Bajeti ya nchi. Halmashauri zote pia zinaketi kupitisha bajeti zao. Ni wazi kuwa ujenzi huu wa madarasa unaofanyika kwa dharura hautazingatia matakwa ya bajeti.
Watumishi hawa wanaenda ‘kuchota’ fedha yoyote ya vyanzo vya halmashauri ili wajenge madarasa. Hawatajali kuwa baada ya kuchota fedha hiyo, kuna tatizo lingine lililotakiwa kutatuliwa litaibuka. Hatuwezi kupanga mipango ya maendeleo ya nchi tena katika eneo nyeti kama elimu kwa hali ya dharura kila mwaka. Nina uhakika wataalamu wetu wa elimu na wale wa takwimu serikalini hawashindwi kufanya makadirio ya idadi ya wanafunzi wanaotarajia kuingia kidato cha kwanza kila mwaka.
Wasikilizwe, watoe makadirio na mipango ya ujenzi ianze mapema bila kusubiri mwisho wa mwaka. Ujenzi ufanyike mchana kweupe kwa usimamizi mzuri. Wala hakuna sababu ya ujenzi huo kufanyika mpaka usiku wa manane kwa kutumia mwanga wa koroboi na taa za chemli.
Kupanga ni kuchagua na kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa. Tusizuie likizo za mwisho wa mwaka kwa watumishi wa umma. Rais Magufuli ameshasema wengine wanazitumia likizo za mwisho wa mwaka kwenda kutambika. Tutakuja kuichokoza mizimu ya mababu bure ambayo mingine ni mizimu ya mvua kisha itunyime mvua mwaka mzima na ukame utawale!
Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa wote!
Charles William ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni charleswilly93@gmail.com au Twitter kupitia @2charlesWilliam. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi maoni na msimamo wa The Chanzo Initiative.