Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na serikali imefafanua kuwa hitilafu katika baadhi ya njia za kusafirisha na kuzalisha umeme zilisababisha mitambo kujizima mnamo Juni 27, 2026, ili kujihami na uharibifu ambao ungeweza kutokea baada ya mifumo ya kidigitali kuona viashiria vya hatari kwa mitambo.
Hali hiyo ndio iliyopelekea umeme kukatika nchi nzima kuanzia majira ya saa kumi na mbili jioni na kurudi saa sita usiku.
Akizungumza wakati alipotembelea kituo cha Ubungo, ambapo ndio ofisi kuu ya kuendesha gridi ya taifa, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, ameeleza kuwa Shirika hilo linaendelea kufuatilia maeneo yaliyosababisha tatizo hilo kutokea.
“Kilichotokea jana, kuna maeneo yetu matatu yalipata shida,kuna njia zetu tatu za kusafirisha umeme na kituo chetu kimoja cha kuzalisha umeme kilipata hitilafu kwa bahati mbaya ikaleta hitilafu iliyosababisha gridi yetu kutoka,” alifanua Twange.
“Hii mifumo pia imewekewa zana za kujilinda. Kwa hiyo wakati fulani yanaweza yakatokea mambo yanayosababisha miondombinu yenyewe iweze kujilinda ili isiweze kuharibika pia,” aliongeza.
Hata hivyo Twange ameeleza kuwa jambo hilo limetokea bahati mbaya na sio jambo linaloweza kutokea mara kwa mara.
“Ni matokeo ambayo hayatokei mara kwa mara na tuna mifumo mingi sana ya udhibiti. Lakini hii ni mitambo iko [inaweza kumbana na changamoto] wakati fulani,” alieleza zaidi.
Twange amefafanua kuwa tayari timu ya mafundi wa TANESCO imesafiri kwenda katika maeneo yaliyosababisha hitilafu na katika vituo vya kuzalisha umeme ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.
Pia, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndenjembi ametoa agizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kuunda timu ya wataalamu itakayohusisha TANESCO, watendaji wa Wizara, na kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ili kujifunza kilichotokea na kuhakikisha hakitokei tena.
“Kikubwa ni kujifunza kutokana na yale yaliyotokea jana ili tuchukue hatua za haraka ili yasiweze yakajitokeza tena kwa maana nchi kukosa umeme kwa wakati mmoja,” alieleza Ndenjembi.
Ndenjembi amefafanua kuwa Wizara hiyo itapokea ripoti ya awali kutoka TANESCO kesho Juni 29, 2026, hata hivyo wanategemea taarifa zaidi baada ya timu hiyo kulichunguza suala hilo.
“Lakini jingine ambalo tumewataka sasa ni kuhakikisha kwamba network yetu ya grid ya taifa inakuwa ina namna ya kukata pale load inapozidi ubavu mmoja na ikataka kutoka basi isiondoe mikoa yote kwa wakati mmoja,” alitoa rai hiyo kwa viongozi wa TANESCO waliomabatana naye.
TANESCO kwa upande wake imeomba radhi kwa watumiaji wa umeme juu ya usumbufu uliojitokeza na kueleza kuwa shirika hilo linaendelea kuboresha miundombinu ya gridi ya taifa.