The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Siku ya Pili ya Kesi ya Kikatiba ya Lissu Juu ya Haki ya Faragha na Mawakili: Ahoji Utaratibu wa Wafungwa Waliohukumiwa Kifo Kutumika Dhidi Yake

Katika dodoso na Mawakili wake Lissu amehoji juu ya utaratibu wa wafungwa waliohukumiwa kifo kutumika dhidi yake, huku akitaja nyaraka mbalimbali kutofikishwa kwake au kuzuiwa

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam-Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, umeendelea kuwa jukwaa la mjadala kuhusu mipaka ya haki za mawakili William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo na mazingira ya mawasiliano kati yao na mteja wao Tundu Lissu, huku mawakili hawa wakiwasilisha ushahidi katika kesi ya kikatiba inayopinga madai ya kunyimwa faragha wanapomtembelea gerezani.

Katika siku ya pili ya usikilizwaji wa shauri hilo, Julai 21, 2026, jopo la majaji watatu Amir Mruma, Dkt. Angelo Rumisha na Dkt. Evaristo Longopa liliendelea kusikiliza ushahidi kutoka kwa waleta maombi, huku Tundu Lissu akiwa miongoni mwa wajibu maombi katika shauri hilo waliododosa mashahidi.

Tofauti na siku ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi hiyo Julai 20, 2026, ambapo Wakili William Maduhu aliwasilisha ushahidi wake na kudodoswa na upande wa utetezi pamoja na wakili wa Serikali, leo mashahidi wawili wengine, Nashon Nkung na Paul Kisabo, wameendelea kueleza mazingira waliyodai kukutana nayo walipokuwa wakimtembelea Tundu Lissu katika Gereza la Ukonga.

Katika ushahidi wake siku ya kwanza, Maduhu alionekana akitokwa machozi mahakamani baada ya kueleza madai kuwa alinyimwa fursa ya kuzungumza na Lissu kutokana na changamoto yake ya ngozi (ualbino). Alidai kuwa miongoni mwa mawakili watatu wa Lissu, yeye ndiye aliyepata nafasi chache zaidi za kumuona mteja wao, huku akieleza kuwa kulikuwa na nyakati ambapo aliambatana na mawakili wenzake ambao waliruhusiwa kumuona Lissu lakini yeye hakuruhusiwa.

Katika mwendelezo wa ushahidi huo, mjadala wa leo umejikita kwenye mazingira ya mawasiliano kati ya mawakili hao na Lissu gerezani. Mashahidi hao walieleza madai kuhusu uwepo wa askari magereza katika maeneo ya mazungumzo pamoja na kuwepo kwa kamera za usalama (CCTV) ndani ya chumba walichokuwa wakikutana na mteja wao, wakidai kuwa hali hiyo iliathiri faragha ya mawasiliano ya wakili na mteja.

Lissu alionekana akiwa mchangamfu huku aina yake mpya ya nywele ya kama rasta ikionekana kumea alianza kwa kumuuliza maswali Wakili wake Paul Kisabo.

Lissu : Nitakuuliza maswali kuanzia Juni 16, 2025  hadi November 15.

Tarehe 16 mwezi wa sita pale Kisutu Nililalamika kuhusu mawasiliano yangu na mawakili wangu?

Wakili Kisabo: Ni kweli na ukasema umetuondoa kazini.

Lissu: Baada ya hapo utaratibu wa mawasiliano ulibadilika?

Wakili Kisabo: Ni kweli

Lissu: Utaratibu ulibadilika na tukawa tunazungumza kwenye admission office.

Wakili Kisabo: Ndio na walikuwa wanatusikiliza

Lissu: Kwenye kiti cha wakili anachokaa pale admission kuna askari  anaandika. Na wengine wengi wanaandika humo ndani na kuna mwingine wa sheria na mwingine wa usalama.

Wakili Kisabo: ni kweli kabisa.

Lissu: Na kule kwenye kile chumba cha awali tunachoongea na simu ni kweli wanakusimamia na kukusikia unachoongea kwenye hiyo simu?

Wakili Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Kuna CCTV camera hapo kwenye kale ka Chumba?

Lissu: Je unapozungumza na mteja wako kuna usiri wowote?

Wakili Kisabo: Hakuna usiri maana wanakusikiliza na kutusimamia kwa kila kitu.  

Lissu aliendelea kumdodosa Wakili Kisabo ambapo alimhoji zaidi juu ya utaratibu wa wafungwa waliohukumiwa kifo kutumika dhidi yake, ambapo aligusia juu ya kanuni ya 33(1)(a) ya Kanuni za Magereza. Kanuni inayotaka mfungwa wa kifo kusimamiwa mara zote na Askari wawili usiku na mchana, kupewa eneo maalum la kuongea na ndugu, jamaa pamoja na mawakili. Huku kanuni ikitaka mfungwa aliyehukumiwa kifo kila anapotembelewa lazima kuwepo na maofisa wawili wanaotakiwa kusikiliza kila kitu.

Lissu: Baada ya 15/11/2025 utaratibu ukabadilika kutoka admission office kwenda kwa Naibu Mkuu wa Gereza, ofisi ambayo yupo pia mtu wa usalama wa gereza?

Wakili Kisabo: ilikuwa hivyo.

Lissu: Ofisi ya Mkuu wa Magereza tumekutana mara ngapi ukazungumza na mimi?

Wakili Kisabo: Zaidi ya mara tatu.

Lissu: Tulipofanya kwa mkuu wa gereza tulikuwa peke yetu?

Wakili Kisabo: Alikuwepo Mkuu wa Gereza, Walinzi wako na maaskari wengine wanajaaa mle.

Lissu: Ni kweli hujawahi kupima ukubwa wa ofisi ya Mkuu wa Gereza?

Wakili Kisabo: sijawahi kupima.

Lissu: Je sasa kuna uwezekano wa kusikia au kutosikia tunachoongea?

Wakili Kisabo: Lazima watusikie. Wametusikia mara zote.

Lissu: Kwanini unasema wanatusikia.

Wakili Kisabo: Kwanza wako karibu na sisi chumba ni kidogo. Kuna muda tukicheka wanacheka na kuna muda tukisikitika na wao wanasikitika. Maana yake wanatufuatilia.

Lissu: Tuzungumze mabadilishano ya nyaraka, Ni kweli mmeniletea nyaraka mbalimbali kuhusu kesi inayonikabili Mahakama kuu.

Wakili Kisabo: Ni kweli lakini kabla hatujakupa wanazichukua na kuzisoma.

Lissu: Na hadi unapoondoka huwa bado wako nazo wao?

Wakili Kisabo: Ni sahihi

Lissu: Ni kweli mara nyingi nimewalalamikia kuwa sipati hizo nyaraka mara nyingine?

Wakili Kisabo: Mara nyingi sana umelalamika hata ile hotuba ya Jaji Chande kuhusu ripoti ya uchunguzi wa matukio ya oktoba 29 hujapata hadi leo.

Lissu: Unafahamu kama mawakili wa serikali walisema Mahakamani wanataka kuongeza ushahidi kuniunganisha na matukio ya oktoba 29

Wakili Kisabo: Ni kweli na nyaraka ile nilikuletea ujiandae na utetezi.

Lissu: Ni kweli mwezi uliopita uliniletea nyaraka kutoka umoja wa mataifa ikisema niachiwe kwa kesi hii.

Wakili Kisabo: Ni sahihi nilikuletea lakini admission officer aliichukua akaisoma na kuwapa wengine na baada ya hapo wakasema hatuwezi kuruhusu umpatie Tundu Lissu hii nyaraka.

Nyaraka ya Umoja wa Mataifa inayotajwa ni ile ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotambuliwa rasmi katika kikao kilichofanyika Novemba 10 mpaka Novemba 14, 2025, ambapo walieleza kushikiliwa kwa Tundu Lissu hakufuati sheria.  Nyaraka hiyo ilionesha kusikitishwa juu ya hoja kuwa haki za Lissu kuonana na mawakili kwa faragha zimekuwa hazifuatwi.

“Madai kuwa vikao vya Lissu na Mawakili hufanyika mbele ya maofisa wa magereza, na kupitia simu ambayo inawezekana kuwa inafuatiliwa, na kuwa nyaraka zote zinasomwa na maofisa wa magereza ni uvunjwaji mkubwa wa haki ya faragha na Mawakili. Hoja ya ujumla ya serikali kuwa ufuatiliaji ni kwa ajili ya sababu za kiusalama hazitoi majibu juu ya hitaji kuwa mawasiliano kati ya mawakili na mteja yanatakiwa kuwa na faragha,” ilieleza taarifa hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza Mahakamani, Wakili Kisabo alieleza nyaraka zingine ambazo alishindwa kupatia Lissu ni pamoja na zinazohusu Jumuiya ya Madola (Commonwealth), ikiwemo tamko lililohusishwa na wito wa Lissu kuachiwa ndani ya siku 30.

Wakili Nkung, ambaye ni mmoja wa waleta maombi, alidai kuwa wakati wa mazungumzo yao na Lissu kulikuwa na zaidi ya askari zaidi ya wanne katika eneo hilo, huku akieleza pia kuwa walipokea maelekezo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa gereza kuhusu mambo yaliyokuwa yanaweza au yasiyoruhusiwa kujadiliwa wakati wa mawasiliano yao.  Kwamba hawapasi kuzungumza mambo ya siasa hasa kesi  ya mgawanyo wa mali za chama iliyopo mahakamani.

Shauri hilo la kikatiba namba 7300/2026 limefunguliwa na mawakili William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo, wakidai kuwa hatua za mamlaka ya Gereza la Ukonga zimewaathiri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria na haki yao ya mawasiliano ya siri na mteja wao.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Jenerali wa Magereza, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Chama cha Mawakili na Tundu Lissu ambaye ameunganishwa katika shauri hilo ili kueleza nafasi yake kuhusu madai yanayowasilishwa.

Akimdodosa Wakili wa Lissu, Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola alihoji kama malalamiko yaliyoletwa Mahakamani yaliwahi kuwasilishwa katika ngazi za juu za magereza.

Wakili wa Serikali Kalokola: ulioneshwa maoni mbalimbali ya Mkuu wa Gereza?

Wakili Kisabo: Niliona.

Wakili Kalokola: Kila anayeona anasikia.

Wakili Kisabo: Inategemea na mazingira.

Wakili Kalokola: umewahi kuwapima masikio maaskari magereza wa Ukonga ukajua wamesikia au hawajasikia?

Wakili Kisabo: Watu nikifika naongea nao wananijibu. Ukisema hawasikii tena labda uwe na tatizo lako wewe.

Wakili  Kalokola : Sasa mawasiliano ya simu kwenye chumba chenye vioo na ukasema kuna uwezekano wa kusikilizwa.

Wakili Kisabo: Yanasikilizwa.

Wakili  Kalokola: Ulitaja kifaa kinachorekodi.

Wakili Kisabo: Sikijui, lakini simu yenyewe inarekodi. Sasa unataka kifaa gani kingine.

Wakili Kalokola: Unafahamu kwenye gereza la ukonga na magereza mengine kuna mtu anaitwa Principal Officer ambae yuko juu ya wakuu wa magereza?

Wakili Kisabo: Hawanihusu kama wakili mimi.

Wakili Kalokola: Ulienda au hukuenda kupeleka malalamiko kwa askari magereza wa juu?

Wakili Kisabo: Nimeshajibu hilo swali.

Wakili Kalokola: Mahakama hii ina uwezo wa kutekeleza maamuzi ya working group ya UN? Na uamuzi wa Jaji Mkwizu. Inaweza kutekeleza?

Kisabo: Kwanini isiweze. Kama jambo ni la kisheria. Lazima litekelezwe.

Lissu amekuwa mahabusu katika Gereza la Ukonga tangu Aprili 10, 2025, akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Katika hatua mbalimbali za kesi hiyo, amewahi kueleza mahakamani kuwa yeye na mawakili wake wamekuwa wakikumbana na changamoto katika kupata mazingira ya mawasiliano ya faragha.

Mahakama inatarajia kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo Julai 22, 2026, ambapo shahidi kutoka upande wa Serikali anayewakilisha wajibu maombi namba moja, mbili na tatu anatarajiwa kuwasilisha ushahidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×