The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Mhitimu wa NIT Alivyobadili Changamoto ya Taka Kuwa Fursa Wilayani Mafia

Abdul ni mwanzilishi na mwenyekiti wa kikundi cha Taka Dampo, ambacho kilianza kutokana na wazo alilolibeba tangu akiwa mwanafunzi wa chuo.

subscribe to our newsletter!

Kila siku katika Kisiwa cha Mafia, taka zinazozalishwa na kaya, biashara na hoteli zinahitaji kuondolewa ili kulinda mazingira na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea bila kuathiri mazingira ya kisiwa hicho.

Kwa Abdul Amran, kijana mwenye umri wa miaka 26 na mhitimu wa Shahada ya Lojistiki na Menejimenti ya Usafirishaji kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), changamoto hiyo haikuwa kero pekee, bali pia fursa ya kujiajiri.

Kisiwa cha Mafia, chenye urefu wa takribani kilomita 50 na upana wa kilomita 15, kina wakazi 66,180 na kaya 18,360, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kisiwa hicho ndicho kinachounda Wilaya ya Mafia katika Mkoa wa Pwani.

Mafia pia ni miongoni mwa maeneo ya Tanzania yenye shughuli za utalii wa baharini. Utalii huo unahusisha fukwe, ikolojia ya bahari, shughuli za kuzamia na kuogelea, pamoja na utazamaji wa viumbe wa baharini.

Katika mazingira hayo, usimamizi wa taka si suala la usafi pekee, bali pia ni sehemu ya kulinda mazingira yanayosaidia shughuli za kiuchumi na maisha ya wakazi wa kisiwa hicho.

Wazo lililoanza akiwa chuoni

Abdul ni mwanzilishi na mwenyekiti wa kikundi cha Taka Dampo, ambacho kilianza kutokana na wazo alilolibeba tangu akiwa mwanafunzi wa chuo.

Baadhi ya wanachama wa Kikundi cha Taka Dampo wakiendelea na zoezi la kuondoa na kusafirisha taka zilizokusanywa wakati wa usafi wa mazingira kisiwani Mafia.

Anasema kuanza kujihusisha na ukusanyaji taka akiwa kijana aliyesoma katika chuo kikuu hakukuwa jambo lililoeleweka kwa urahisi na baadhi ya watu katika jamii, akiwamo familia yake.

“Watu wanatamani wakikuona kama ni mtu uliyesoma wanataka wakuone unafanya kazi fulani ambazo zina majina makubwa, zile zilizozoeleka,” anaeleza Abdul. “Wakikuona unazoa taka ni kitu ambacho ni kigumu na kinakuwa kigumu kuelezeka.”

Kwa mujibu wa Abdul, wazo la kuanzisha mradi huo lilizaliwa Machi 2024, kabla ya shughuli rasmi za ukusanyaji taka kuanza Machi 11, 2026.

SOMA ZAIDI: Kijana Asiye na Kipato ni Rahisi Kushawishiwa na Makundi Mabaya

Anasema wazo hilo lilitokana na tathmini aliyofanya kuhusu changamoto ya ukusanyaji taka katika Wilaya ya Mafia, ambako Halmashauri haikuwa na ratiba rasmi ya ukusanyaji taka mitaani kama ilivyo katika baadhi ya miji iliyopiga hatua katika huduma hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Abdul aliona fursa ya kutumia taaluma yake na kuwashirikisha vijana katika kutoa huduma ya ukusanyaji taka, huku wakipata kipato.

Kutoka wazo hadi huduma rasmi

Ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa kuzingatia taratibu na sheria, kikundi cha Taka Dampo kilifuata utaratibu rasmi wa kupata vibali kutoka Serikali za Mitaa kabla ya kuanza kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya kisiwa.

“Kabla ya kuhudumia kata yoyote, ni lazima tufike katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata na Halmashauri za Vijiji kuomba kibali,” anaeleza Abdul. “Wanapojiridhisha kuwa tunakidhi vigezo na tuna ufanisi unaotakiwa, wanatupa idhini ya kuanza kazi.”

Kwa sasa, kikundi hicho kinahudumia takribani kaya 362, pamoja na biashara ndogo ndogo na hoteli katika Kata za Kilindoni na Kiegeani wilayani Mafia.

Taka zikiwa zimekusanywa na kupakizwa kwenye guta tayari kwa kusafirishwa kuelekea jalalani kuu baada ya kukusanywa na kutenganishwa.

Ukusanyaji wa taka hufanyika mara tatu kwa wiki kwa kutumia vyombo vya usafiri kama guta na toyo, kabla ya taka hizo kusafirishwa hadi jalala kuu la Halmashauri.

Mbali na kusaidia katika usafi wa mazingira, shughuli hiyo imekuwa chanzo cha kipato kwa vijana. Kikundi kina wanachama hai watano na pia hutumia vibarua katika kutekeleza baadhi ya majukumu ya ukusanyaji taka ambao nao hujipatia ujira.

Abdul anasema wana mpango wa kupanua shughuli zao na kutoa ajira kwa vijana wengine 15 katika siku zijazo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo waliyojiwekea.

Zaidi ya tani 100 za taka

Katika kipindi ambacho kikundi hicho kimekuwa kikifanya kazi, kimekusanya zaidi ya tani 100 za taka kutoka kwenye kaya, biashara na maeneo mengine.

Kwa Abdul, hatua hiyo si tu imechangia kupunguza taka zilizokuwa zikikusanyika majumbani bila kuwa na njia mbadala ya kuzifikisha katika maeneo rasmi ya utupaji, bali pia imewasaidia vijana kujipatia kipato kupitia huduma hiyo.

Hata hivyo, mchango wa Taka Dampo hauishii katika usafi wa mazingira pekee. Abdul anaeleza kuwa shughuli zao zimeanza pia kuchochea mabadiliko katika namna Halmashauri inavyoshughulikia suala la ukusanyaji taka.

Anasema baada ya takribani miaka miwili ya shughuli za ukusanyaji taka nyumba kwa nyumba, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imetangaza, kwa mara ya kwanza, zabuni rasmi ya ukusanyaji taka.

SOMA ZAIDI: Kutana na Kijana Aliyepania Kuleta Mapinduzi ya Kiteknolojia Tanzania

Kwa mtazamo wake, hatua hiyo inaonyesha kuwa changamoto iliyokuwa ikikabiliwa na jamii inaweza pia kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiutendaji na kisera.

Miundombinu bado ni changamoto

Pamoja na mafanikio hayo, Abdul anasema changamoto ya miundombinu ya udhibiti wa taka bado ni moja ya vikwazo vikubwa vinavyowakabili katika utekelezaji wa shughuli zao.

 “Kwa sababu kwa kiasi kikubwa, miundombinu yenyewe ya udhibiti wa taka bado haijawa imara,” anasema Abdul.

Anaeleza kuwa changamoto hiyo haiwakabili wao pekee, bali pia jamii kwa ujumla, ambayo inakabiliwa na uhaba wa miundombinu ya kudhibiti taka pamoja na uelewa mdogo kuhusu utenganishaji wa taka.

“Jamii inakabiliwa na miundombinu duni ya udhibiti wa taka pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu utenganishaji wa taka,” anaongeza.

Taka zilizokusanywa zikiwa zimefikishwa eneo la utekezaji zikiwa kwenye guta, tayari kushushwa na kuanza kwa zoezi la kuziteketeza kisiwani Mafia.

Kwa sababu hiyo, anasema Taka Dampo imekuwa ikifanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudhibiti na kutenganisha taka, huku ikihamasisha wakazi kushiriki katika juhudi za kuweka mazingira ya kisiwa katika hali ya usafi.

Kwa Abdul, usafi wa mazingira haupaswi kuonekana kama jukumu la kikundi chake pekee, bali ni jukumu linalohitaji ushirikiano kati ya jamii, Serikali na wadau wengine.

Ndoto ya miaka mitano ijayo

Akiangazia miaka mitano ijayo, Abdul anasema ana mpango wa kukuza Taka Dampo kutoka kikundi kinachotoa huduma ya ukusanyaji taka na kuwa kampuni inayotekeleza mfumo wa taka sifuri.

“Tunatamani kujenga mfumo kamili wa taka sifuri. Iwe ni kampuni ambayo inatekeleza mfumo rasmi wa ‘zero waste’ ambayo inatambulika kimataifa na kidunia,” anaeleza.

Ndoto yake, hata hivyo, haiishii katika kukuza biashara. Anataka kuona shughuli hizo zikiacha alama katika utunzaji wa mazingira ya Kisiwa cha Mafia na kupanua wigo wa huduma zao.

“[Tunahitaji] tuache ‘impact’ ya kweli, lakini pia tutanue  wigo wa huduma zetu,” anasema Abdul.

Kwa kijana huyo, taka ambazo hapo awali zilionekana kuwa mzigo kwa jamii zimegeuka kuwa chanzo cha ajira, kipato na fursa ya kushiriki katika kulinda mazingira ya Kisiwa cha Mafia.

Ibrahim Mgaza ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia ibrahimmgaza39@gmail.com.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×