The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

 Kutana na Kijana Aliyepania Kuleta Mapinduzi ya Kiteknolojia Tanzania

Ni mwanzilishi mwenza wa MITz Group, kampuni iliyokuja na MITz Kits, vifaa vya maabara vinavyolenga kuboresha uelewa wa masomo ya sayansi.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Wilson Richard Mabala ni mwanzilishi mwenza wa MITz Group ambapo, kwa kushirikiana na mwenzake Kelvin Paul, amedhamiria kuleta mapinduzi kwenye namna elimu ya Tanzania inatumia teknolojia zilizopo kuboresha ufaulu kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati au STEM kama masomo hayo yanavyojulikana kwa kimombo.

Ambacho Mabala na wenzake katika MITz Group wanafanya kimsingi ni kutengeneza vifaa vya kufanyia majaribio ya kisayansi ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kuboresha uelewa wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Tuliona kuna changamoto kwenye jamii, kwamba tunajifunza mara nyingi darasani, hususan kwa masomo ya sayansi, lakini tunajifunza zaidi nadharia,” Mabala aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano hivi karibuni.

“Kwa hiyo, tukawa tumefikiria kwamba kwa nini tusitengeneze namna ya mtoto anapokuwa anajifunza darasani haya masomo ya sayansi aweze kuyaunganisha na mazingira ambayo yanamzunguka, yaani asiwe anakariri zaidi bali aweze kuelewa,” aliongeza mwanateknolojia huyo.

SOMA ZAIDI: Mdau Apendekeza Haya Kuchochea Ufaulu Masomo ya Sayansi Tanzania

Ndipo ilipofika mwaka 2017 MITz Group ilipokuja na MITz Kits, kusanyiko la vifaa kadhaa vya maabara ambavyo vinaweza kutumika katika majaribio ya somo la Fizikia kuanzia Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne.

“Tulianza tukatengeneza mfano wa kwanza, ilikuwa ni kubwa kidogo tofauti na hizi za sasa,” Mabala alieleza. “Tukaitengeneza ile, tukafanya mkutano na walimu tukishirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa [wa Mwanza], na matokeo ya vikao hivyo ndiyo tukatengeneza hii ya sasa.”

MITz Group wanatumia teknolojia ya kuchapisha kwa kutumia 3D na PCD, ambazo ni teknolojia inayotumika kuchapisha kitu kama kilivyo.

“Unaweza kuchapisha kwa kutumia nyenzo kama ni chuma au plastiki, yoyote unayoitaka,” alieleza Mabala. “Sisi tunatumia nyenzo ya plastiki ambayo inaweza kutumika tena ikiharibika, yaani ni rafiki kwa mazingira.’’

“PCD ni zile sakiti kama unaziona kwenye redio, inaonekana mchoro kama ramani ramani hivi,” anaongeza kijana huyo. “Sisi tunatengeneza sakiti halafu tunazichapisha.”

SOMA ZAIDI: Wadau Wazitabiria Mema ‘Startups’ za Kitanzania 2023

Mpaka sasa, MITz Group wameweza kutengeneza aina nane za vifaa ambavyo vinatumika katika shule za msingi na sekondari katika majaribio mbalimbali ya somo la Fizikia.

“Tuna vifaa kwa ajili ya shule za msingi ambayo ina majaribio zaidi ya 10 mtoto anaweza akafanya mule,” anaeleza Mabala. “Na kama mwalimu pia akitumia anaweza akafanya pia majaribio yake mengine. Lakini pia tuna vifaa kwa ajili ya shule za sekondari.”

“Kwa sasa mtoto wa darasa la nne anapojifunza soketi rahisi, kama ametumia kifaa cha MITz Kits, tayari anakuwa ameshakutana na vifaa ambavyo amezoea kuviona kwenye michoro ya vitabu,” anafafanua mwanateknolojia huyo.

Faida ya vifaa hivyo ni kwamba mtoto hasubiri muda wa kwenda maabara kwa ajili ya kufanya majaribio ili aweze kujifunza bali ana uwezo wa kufanya majaribio yake popote pale atakapokuwa.

“Mtoto ana uwezo wa kufanya majaribio yake tofauti tofauti akiwa nyumbani, akiwa darasani au akiwa sehemu yoyote ile,” Mabala anafafanua. “Tumetengeneza maabara ambayo ina bebeka.”

“Kuna programu zetu ambazo tunafanya, mtoto anaweza kuyatumia maarifa aliyoyapata akatengeneza vitu mbalimbali,” Mabala anasema. “Kwa mfano, kwa kutumia sakiti rahisi watoto wanatengeneza tochi kwa kutumia maboksi ambayo yanapatikana tu kwenye mazingira yake ya kawaida.”

Kupitia MITz Kits pia, watoto wa shule za msingi na sekondari wameweza kubuni vifaa mbalimbali kama gari linalotumia ‘motor’ na ‘sensor,’ tochi ya umeme, roboti na vifaa vingine mbalimbali.

SOMA ZAIDI: Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti

“Kwa hiyo, tunamjenga mtoto aweze kuwa na mawazo ya ubunifu na kuweza kutumia rasilimali ambazo zinamzunguka kuweza kutatua changamoto mbalimbali,” anasema Mabala.

“Kwa kufanya hivyo, tunaona tutapata kizazi ambacho baadae kitakuwa na uwezo wa kutatua changamoto katika jamii yake pasina kusubiri msaada kutoka nje,” aliongeza.

Mabala anawasihi wasimamizi wa shule kuruhusu matumizi ya vifaa vya MITz Group kwenye shule zao.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba licha ya kwamba walimu wameonesha kuvutiwa na vifaa hivyo, wasimamizi wa shule, wakiwemo wakuu wa shule, wamekuwa wazito kuruhusu matumizi yao.

Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *