The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mdau Apendekeza Haya Kuchochea Ufaulu Masomo ya Sayansi Tanzania

Asema hatua ya kwanza muhimu ni kuwa na walimu wanaoweza kufundisha masomo hayo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mwandishi wa vitabu vya masomo ya sayansi Ngaiza Lusima amesema ipo haja ya Serikali kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya sayansi, akisema hiyo ni hatua muhimu kwenye mchakato mzima wa kuongeza ufaulu wa masomo hayo nchini.

Lusima, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ngaiza Education Hub, shirika linalojikita kwenye kutoa ushauri kuhusu masomo ya sayansi, alitoa tathmini yake hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.

“Kama Serikali inataka iongeze mapenzi ya wanafunzi kwenye masomo ya sayansi ni lazima iwaongezee uwezo walimu wanaofundisha masomo ya sayansi ili waendane na mahitaji ya sasa,” Lusima alieleza kwenye mahojiano hayo. 

“Masomo ya sayansi yanahitaji walimu wenye uwezo kweli kweli. Kwamba, hata yeye mwalimu wakati anasoma hayo masomo awe alikuwa anayapenda na anayamudu.

“Lakini pia, Serikali haiwezi kukwepa wajibu wa kujenga miundombinu ya shule, ikiwemo maabara ili wanafunzi waweze kusoma kwa vitendo na kufanya majaribio. 

“Hii itasaidia kuwajengea wanafunzi ari ya kupenda masomo ya sayansi,” alisema Lusima kwenye mahojiano hayo.

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Maoni hayo ya mdau huyo yanakuja wakati ambao matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2022 yanaonesha kwamba ni asilimia 27.4 tu ya jumla ya wanafunzi 114,144 waliofanya mtihani wa somo la Fizikia ndiyo waliofaulu kwa kupata alama A, B na C.

Kwa somo la Biolojia, ni asilimia 36.54 tu ya wanafunzi 520,399 waliofanya mtihani wa somo hilo ndiyo waliopata alama A, B na C huku asilimia 68.21 ya wanafunzi 154,957 waliofanya mtihani wa somo la Kemia walipata alama A, B na C.

Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Lusima alieleza kwamba ni muhimu Tanzania ikawa na walimu wenye uelewa na umahiri wa masomo ya sayansi.

Kwa maoni yake, hiyo ni muhimu kwani wanafunzi wengi wa masomo ya sayansi wamekuwa wakiukwepa ualimu na kwenda kwenye kada za afya, uhandisi na nyenginezo ambazo zina maslahi bora zaidi.

SOMA ZAIDI: Mpaka Sasa Serikali ya Awamu Ya Sita Imefanya Nini Kwenye Elimu?

“Kama Serikali inaweza kutafuta namna nzuri ya koboresha maslahi ya walimu basi itawavutia hata wale wanafunzi ambao wana uwezo mkubwa kusoma ualimu wa masomo ya sayansi,” alisema mdau huyo. 

“Vilevile, ipo haja kwa Serikali kuwa bunifu na kubuni programu mbalimbali, au tuzo mbalimbali, ambazo zitawavutia wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi,” aliongeza Lusima.

Lusima aligusia umuhimu wa wanafunzi kuachana na kasumba kwamba masomo ya sayansi ni magumu, akisema kasumba hiyo huweka msingi wa wanafunzi hao kufanya vibaya kwenye masomo hayo.

Suala la ufaulu usioridhisha wa wanafunzi kwenye masomo ya sayansi nchini Tanzania limekuwa mada ya mijadala mingi ya wadau na tafiti nyingi za wasomi kwa miaka mingi.

Mijadala na tafiti hizo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikielekezwa kwenye kuchambua chanzo cha tatizo na kupendekeza baadhi ya afua muhimu za kuchukuliwa.

SOMA ZAIDI: Wadau Wasisitiza Utekelezaji wa Vitendo Mikakati Elimu Jumuishi

Akiwa kama sehemu ya wadau muhimu wanaolenga kuchochea mabadiliko kwenye eneo hilo, Lusima aliamua kuanza kuchapisha vitabu vya masomo ya sayansi kusaidia Tanzania isiachwe nyuma kwenye mapinduzi ya kisayansi yanayoendelea kuikumba dunia.

“Unakuta kwenye matokeo hata ya NECTA moja ya masomo ambayo wanafunzi wanafanya vibaya ni masomo ya sayansi siyo Kidato cha Pili, Nne wala cha Sita,” alisema Lusima kwenye mahojiano yake na The Chanzo

“Kwa hiyo, niliona kuna haja ya mimi mdau ambaye nina uelewa mzuri wa masomo ya sayansi nifanye kitu ambacho kitarahisisha kuelewa hayo masomo ya sayansi kupitia vitabu ninavyoandika,” aliongeza mdau huyo.

Lusima alianza kuandika kitabu cha Kemia ambacho alisema mapokezi yake yalikuwa ni mazuri na kwa sasa kinatumika kwenye shule zote za sekondari nchini Tanzania, akiamini kwamba kinaweza kuchochea mabadiliko yanayohitajika.

Hata hivyo, Lusima anasema kuna changamoto zinazohusiana na sekta ya uchapishaji nchini ambazo anadhani Serikali inapaswa kuzishughulikia.

“Changamoto ya kwanza kabisa ambayo ni kubwa ni watu kutoa vitabu vyangu feki,” alisema mwandishi huyo wa vitabu. “Kuna baadhi ya watu wanatengeneza vitabu ambavyo ni feki na kusambaza shuleni.” 

Lusima anasema kwamba zaidi ya asilimia 70 ya vitabu vyake ambavyo viko sokoni kwa sasa ni feki, hali inayomuumiza kwani anaingia gharama sana kwenye kuzalisha vitabu hivyo.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *