The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kijana Asiye na Kipato ni Rahisi Kushawishiwa na Makundi Mabaya

Vijana wengi wanatoka katika kaya masikini, ambapo mpaka anamaliza masomo kuna gharama kubwa imelipwa na familia.

subscribe to our newsletter!

Idadi kubwa ya vijana hapa Tanzania wanamaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali za elimu kila mwaka. Taasisi za elimu, kuanzia Darasa la Saba, Kidato cha Nne, Kidato cha Sita, vyuo mbalimbali vya ufundi na Vyuo Vikuu vinazalisha idadi ya wahitimu kila msimu.

Takwimu kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kwa mfano, zinaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanafunzi wa ngazi ya Cheti mpaka Shahada ya Uzamivu katika taasisi za elimu ya juu nchini kutoka 213,829 kwa mwaka wa masomo 2017/18 mpaka kufika 314,643 kwa mwaka wa masomo 2022/23. 

Hii inatupa picha ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu hapa nchini kwetu, licha ya kwamba wachache wao wanakatiza masomo hayo. Wahitimu hao wanaondoka wakiwa na matumaini ya maisha bora kwa kupata ajira zenye tija.

Lakini hali halisi ikoje? Inawezekana wote tukawa na jibu la hili swali kwa sababu sisi ni sehemu ya jamii ambayo vijana hawa wapo. Huenda katika familia zetu, ama jamii zetu, tumeshuhudia vijana hawa wakihangaika kupata walau kibarua cha kujiingizia kipato. 

Si ajabu kukutana na wahitimu wa vidato na shahada mbalimbali wakiwa katika hekaheka hizi mitaani. Kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wa namna hii.

SOMA ZAIDI: Mama Samia Kuna Haya Mengine Kwa Vijana

Mara nyingi vijana wengi ni wale wanaotoka katika kaya masikini, ambapo mpaka wanamaliza masomo kunakuwa na gharama kubwa imelipwa na familia. Kutokana na hali hii, kijana anajikuta ana mzigo mkubwa wa matazamio ya wazazi, ndugu na jamaa nyuma yake. Hili huongeza sonona kwa kijana!

Athari za hali hii ni vijana kujikuta wanajiingiza kwenye vitendo vibaya ili mradi tu maisha yaende wakati akipambana. Lakini wapo wachache wanaoamua kuweka elimu zao pembeni na kufanya kazi ambazo zinaonekana hazina staha. 

Suluhu ni nini?

Kwa mfano, niliwahi kumuona binti mmoja, mhitimu mmoja wa Chuo Kikuu, akiuza mahindi ya kuchoma barabarani. Hili ni jambo la huzuni. Lakini suluhisho la kudumu la hali hii inaweza kuwa ni nini? 

Moja ya suluhisho ni ile ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu, ikishirikiana na Shirika la Global Peace Foundation na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imekuja nayo, ya kuanzisha kituo kitakachohusika na kuratibu mipango ya kusaidia vijana. 

Kwenye vituo hivi, vijana wataweza kupata taarifa za fursa mbalimbali za biashara, ajira, masomo na mikopo na mengine mengi kupitia kituo hicho. 

SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu

Vituo hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Dumisha Amani kwa Maendeleo Endelevu unaosimamiwa na Shirika la Global Peace Foudation Tanzania kwa ushirikano na UNDP na Ofisi ya Waziri Mkuu. Mradi huo utakelezwa katika mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, ni moja ya wilaya zilizochaguliwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, kitakachojulikana kama Kituo Maalum cha Vijana (ICT Centre). 

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, aliwasihi vijana kuwa wasione aibu kuweka usomi pembeni na kutafuta njia mbadala za maisha, akisema maarifa peke yake hayatoshi, hususan katika mazingira yetu ya sasa, bali ujuzi. 

Kijana badala ya kukumbatia cheti cha shahada yake, anaweza kujifunza stadi maalumu ambazo zinahitajika mtaani kwa sasa kama ufundi magari, mapishi, ubunifu mashine, kilimo cha kisasa, uvuvi, nakadhalika, aliongeza kiongozi huyo.

Elimu ya ufundi

“Badala ya kutoa shahada zilizopitwa na wakati, tukazanie zaidi elimu ya ufundi,” Ngubiagai alisema, akisisitiza umuhimu wa kuufanyia mageuzi mfumo wa elimu ili uakisi mahitaji ya sasa. “China na nchi kadhaa zinazoendelea zimetoa mfano bora wa njia ya kusaidia makundi ya vijana.”

Filberto Sanga, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, ambaye wilaya yake pia imewekwa kwenye mpango wa kupatiwa kituo hicho, alitanabahisha kwamba kundi la vijana lina changamoto nyingi.

SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

“Kila kijana anatamani kupata maendeleo kwa kasi, wakati huo anashindana na wenzake bila kujali wenzake wanatumia mbinu gani kupata mafanikio. Na yeye anajikuta anatumia njia ambazo hazitakiwi ili afanikiwe haraka,” alisema Sanga.

“Hata akiambiwa ‘pale kuna madawa ya kulevya, kasafirishe kule utapata utajiri.’ Yeye yuko tayari! Akisikia pale kuna vitu vya kuiba, yeye anakwenda anaiba akitengemea atapata utajiri.

“Hata kwenye uvunjifu wa amani katika mataifa mbalimbali, sehemu kubwa wanaotumika ni makundi ya vijana. Hata hapa kwetu, wahalifu hulenga kutumia vijana,” aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya.

Vijana wasibwete

Mratibu wa Masuala ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Nassibu Richard Mwaifunga, aliongelea kwa undani fursa zinazotolewa na Serikali kusaidia vijana kujiinua kiuchumi, ikiwemo mikopo ya mtu mmoja mmoja, masomo ndani na nje ya nchi, na fursa za kusaidia vijana waliomaliza masomo kupata ujuzi kivitendo.

SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa

Mmoja wa vijana washiriki, Jane Songalele, kutoka Nyasa, aliwaasa vijana kwamba kama wamekosa ajira wasibweteke bali wajiongeze kwa kuangalia fursa ambazo zipo. 

“Ili kuweza kuwa na amani nchini, ni lazima tufanye kazi kwa bidii kujitafutia riziki,” alisema Songalele. “Tusiogope kuchukua mikopo bali tuone kuwa kama ni fursa. Kinachotakiwa ni uaminifu tu.”

Martha Nghambi ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Global Peace Foundation Tanzania.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *