The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mama Samia Kuna Haya Mengine Kwa Vijana

 Fao la kujitoa na vigezo visivyo na uhalisia ili kuweza kupata mikopo kutoka halmashauri ni miiba kwa ustawi wa vijana.

subscribe to our newsletter!

Mama Samia Suluhu Hassan, kwanza pole na hongera kwa majukumu ya kulitumikia taifa letu tukufu la Tanzania, kama kijana wako wa Tanzania nina maoni yangu kadhaa ningependa kukupatia kuhusu kutusaidia sisi vijana wako, mengi mazuri yalisemwa na uliyasema pale Mwanza, naomba nami niongezee kidogo kwa kifupi kwenye ambacho tayari kimesemwa.

Jambo la kwanza ambalo ningependa kuliwasilisha kwako Mheshimiwa Rais linahusu fao la kujitoa. Mama, kutokana na kuwa na uhaba wa ajira serikalini, vijana wengi wanafanya kazi za mikataba ya muda mfupi mfupi kwenye taasisi binafsi au mashirika ili kuendesha maisha. Hivyo, mikataba ikiisha wanateseka kupata stahiki zao zote kutoka mifuko ya hifadhi za jamii na hivyo kupelekea kuishi kwa tabu huku pesa zao walizotolea jasho zikiwa zimehifadhiwa.

Fedha hizi mama zikiwa zinatoka zote kwa mara moja kwa vijana wanaomaliza mikataba yao sehemu wanazofanyia kazi zitawasaidia sana kuendesha miradi yao au kufungua biashara zao ambazo zitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wengine na kuongeza kodi kwa taifa tofauti na zikiendelea kukaa hadi wafike umri wa kustaafu. Tunaomba jambo hili liangaliwe kwa jicho la huruma sana.

Mikopo ya halmashauri

Jambo jengine linahusiana na asilimia nne ya fedha za halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa vijana. Mama, mfumo uliopo sasa hivi ni kwamba kikundi ili kiweze kukidhi vigezo cha kupata mkopo ni lazima kiwe na watu kuanzia watano na kuendelea. Sasa changamoto inayokuja hapa ni kwamba pesa inayotolewa ni ndogo sana ambayo haiendani na uwiano wa idadi ya watu kwenye kikundi. Nitatoa mfano. Kikundi cha watu 12 wanapewa mkopo wa shilingi milioni tano. Tukiwa wakweli, pesa hii ni ndogo sana kuweza kusaidia vijana husika. Matokeo yake ni kwamba vijana wanagawana hiyo pesa na kutumia kujikimu na hivyo kushindwa kurejesha.

Mama, ikikupendeza, iangaliwe namna idadi ya wana kikundi ipungue hadi watu wawili au hata mtu mmoja ambae atakuwa na wazo zuri ambalo linatekelezeka ambalo akipewa pesa atafanya mradi na kuajiri wengine au halmashauri kusimamia hatua zote za awali za hilo wazo la huyo kijana na kumkabidhi kila kitu yeye aanze tu.

Mama, ushauri wangu mwengine ni kwamba ile robo ya faida itokanayo na miradi inayoendeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ipelekwe Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili kusaidia kama sio kupunguza tatizo la vijana wanaotaka kupata elimu ya juu  kukosa mikopo. Naamini kabisa kwamba tukichukua hii robo ya faida tukaiongeza kwenye pesa inayotokana na bajeti ya Serikali tutasaidia sehemu kubwa sana.

Kuna haja pia ya HESLB kuunda kitengo kitakachokuwa kinahusika na kusaidia kiuchumi wanufaika wake waliomaliza chuo. Kwa sasa HESLB haipati pesa nyingi kwa sababu mdeni wake akiishamaliza chuo anamtelekeza na hamjali tena wala hajui yuko wapi na atalipa vipi. Hiki kitengo kisaidie kutambua wahitimu wenye mawazo bora na wanaohitaji msaada wa kifedha kutekeleza miradi yao ili bodi au idara nyengine yoyote ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo waone namna bora za kuwasaidia.

Madawati ya vijana

Hoja nyengine inahusu umuhimu wa kuundwa kwa madawati ya kushughulikia masuala ya vijana na kuendeleza vijana kwenye miradi au makampuni yao. Hapa ningependa kuzungumzia mchango unaoweza kufanywa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) pamoja na halmashauri zetu.

Mama, BRELA wao wanasajili kampuni zote hivyo wanajua kampuni zote zinazoundwa nchini, dawati la vijana likiwepo litakuwa linaangalia kampuni/biashara zote zilizofunguliwa na vijana zinaendeleaje, changamoto zao ni zipi na wapi zinahitaji msaada. Dawati hili likiwepo BRELA litasaidia kuokoa kampuni nyingi za vijana ambazo zinafunguliwa na kufa pengine tu kwa kukosa uangalizi na ushauri.

Sido, kwa upande wao, wakiwa na dawati la vijana watakuwa wanafuatilia ukuaji na ufanyaji kazi wa viwanda vyote vidogo vidogo vilivyoanzishwa na vijana. Hii pia itasaidia mno hivi viwanda vya vijana kuwa imara na kuongeza munkali ya kazi. Kwa upande wa halmashauri zetu, hawa ndio wanatoa vibali kwenye maeneo yao endapo dawati la vijana likiwepo litakuwa linaangalia vibali vyote vilivyotolewa kwa vijana kama biashara zao zinafanyika, changamoto zao na wapi wamekwama hii itasaidia sana kuamsha vijana na kujituma.

Hamis Abeid ni mtaalamu wa masuala ya masoko anayefuatilia kwa karibu ustawi wa vijana Tanzania anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni hamisabeid@yahoo.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupitia @hamisabeid. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *