Dar es Salaam-Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 04, 2026, Wakili Kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, William Maduhu, ameeleza kuwa amefungua maombi rasmi Mahakama Kuu ya kutaka Davidlevi Kindikwa, afikishwe Mahakamani au kauchiwa huru.
Hii ni baada ya Kindikwa kushikiliwa kwa zaidi ya siku 40, ikiwemo siku kadhaa ambazo hakuna mtu yeyote aliyekuwa akifahamu alipo, au waliomchukua.
“Ndugu Kindikwa almaarufu kama kijana mzalendo alikamatwa na Jeshi la Polisi au na watu ambao waliojitambulisha kuwa ni Jeshi la polisi tarehe 25 ya mwezi wa sita mwaka huu wa 2026 akiwa eneo la Kerege CCM Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani,” anafafanua Wakili Maduhu William.
Wakili Maduhu anafafanua Kindikwa aliendelea kuhamishwa katika vituo mbalimbali.
“Baada ya kundi hilo kumvamia ndugu Kindikwa au kijana mzalendo na kutokomea naye kusikojulikana mpaka ilipofika tarehe 27 mwezi wa sita 2026, ndipo alipobaini kwamba yuko Kibaha mkoa wa Pwani na alikaa hapo kwa takribani siku tatu.”
Baadhi ya vituo vya Polisi alivyoendelea kupelekwa ni pamoja na:
-Juni 27 mpaka Julai 09, 2026, aliwekwa katika kituo cha Oysterbay, Kindondoni
-Julai 09 mpaka Julai 12, 2026, alipelekwa kituo cha Central, Dar es Salaam
-Julai 12, 2026 mpaka Agosti 03, 2026, alirudishwa kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam.
“Kindikwa au kijana mzalendo amekuwa chini ya mikono ya jeshi la polisi kwa takribani siku 40 sasa bila kupewa haki yake ya dhamana au kufikishwa mahakamani,” anaeleza zaidi wakili Maduhu William.