Dar es Salaam- Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Tundu Lissu, imeendelea leo Agosti 21, 2026, ambapo Mahakama chini ya jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru,James Karayemaha and Ferdinand Kiwonde, imeamua kuwa Tundu Lissu ana kesi ya kujibu.
Akianza kusoma uamuzi wa Mahakama majira ya saa tatu na dakika hamsini na saba asubuhi na kumaliza majira ya saa nne na dakika 20 asubuhi. Jaji Ndunguru alianza kwa kusoma mwenendo wa kesi, kwa kuanza kusoma mashtaka, pamoja na kueleza kuwa mshtakiwa alikana mashitaka. Pia Jaji Nduguru aliwataja mashahidi wote 17 walioweza kutoa ushahidi kwa upande wa mashitaka na kisha kuingia kwenye misingi ya uamuzi wao.
Jaji Nduguru alieleza kuwa kanuni walizozitumia kufikia uamuzi wao ni pamoja na ile inayoeleza kuwa mshtakiwa atakuwa ana kesi ya kujibu endapo kama ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ukibaki bila kujibiwa unatosheleza au utaweza kumtia mshtakiwa hatiani.
Mahakama ilifafanua zaidi kwa kueleza kanuni nyingine kuwa kesi ilipo sasa, kinachohitajika ni kuonesha endapo upande wa mashtaka kwa ushahidi wao wamejenga kesi ambayo itapelekea mshtakiwa apate nafasi ya kujibu au kujitetea. Mahakama ilieleza zaidi kuwa katika wakati huu Mahakama haiangaalii au haiendi kiundani kuangalia uzito wa ushahidi au kuaminika kwa ushahidi bali Mahakama inaangalia uhusiano uliyopo kati ya ushahidi uliotolewa na shtaka lililopo na jinsi mshtakiwa anavyohusishwa na shtaka hilo.
“Hivyo basi kwa kuwa Mahakama haiendi kwa kiwango hicho na kama nilivyosema ushahidi wote unamzunguza mshtakiwa na maneno ambayo yako kwenye hati ya mashtaka,” alieleza Jaji Ndunguru.
“Basi Mahakama hii inaona kwa mujibu wa kifungu cha 312 [cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jiani. Mahakama hii inaona kwamba kuna kesi iliyojengwa kwamba kuna kesi imekuwa ‘established’ sio kuthibitishwa, ‘established’ dhidi ya mshtakiwa, na hivi basi Mahakama hii inasema kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu ili apate nafasi ya kujitetea au kutoa ushahidi wake dhidi ya ushahidi ambao umeletwa na upande wa mashtaka,” alifafanua zaidi.
Baada ya kusoma maamuzi hayo Mahakama alimweleza mshtakiwa haki zake katika kesi hii ikiwa ni pamoja na kujitetea, au kama akikaa kimya Mahakama itaruhusu upande wa mashtaka uongee kitu kutokana na maamuzi ya mshtakiwa kukaa kimya. Tundu Lissu alieleza kuwa atajitetea na kuendelea kutaja mashahidi wake.
Unaweza kufuatilia chini sehemu ya wasilisho la Jaji Dunstan Ndunguru, wakati akisoma uamuzi wa kesi hii.
Jaji Dunstan Ndunguru: ….Pande zote mbili kwa maana ya mshtakiwa pamoja na upande wa mashtaka walionesha nia ya kuleta hoja kuhusiana na endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Mahakama ilikubaliana na hoja hiyo ya pande zote mbili ya nia ya kuleta hoja ya endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la na hivi basi kutokana na hoja zilizotolewa na mshtakiwa na upande wa mashtaka ndio sababu ya uamuzi huu.
Na hivi basi katika kuleta hoja za endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, mshtakiwa alikuwa wa kwanza kutoa hoja zake akikanusha au akieleza kwamba upande wa mashtaka wameshindwa kabisa kujenga kesi kwa maana ya ku-establish kesi ya awali ambayo ingemtaka sasa yeye kuleta utetezi wake.
Na hivi basi katika hoja zake mshtakiwa aliielekeza Mahakama kwenye kanuni mbalimbali zilizokwisha kuzungumzwa na maamuzi mbalimbali ya mahakama ya rufani yakizingatia pale ambapo Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi wa endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au endapo kuna kesi ya kujibu. Aliirejesha Mahakama hii katika maamuzi mbalimbali, ukianza na shauri la Ramanlal Trambaklal Bhatt v. R [1957] E.A katika ukurasa wa 334 and 335, lakini pia aliirejesha Mhakama katika shauri la Murimi v Republic [1967] EA 542 hasa katika ukurasa wa 544, ambapo amesema shauri hili liliadopt au liliasili zile kanuni ambazo zilishawekwa kwenye shauri hilo.
Hata wakati upande wa Mashtaka wakijibu hoja kuhusiana na kanuni zinazotakiwa kutumika au muongozo uliokwishawekwa na mamuzi ya Mahakama mbalimbali kwa kuzingatia mashauri niliyoyataja hapo juu. Upande wa mashtaka pia walikubaliana pia hizo ndio kanuni zilizowekwa na ndizo zinazozingatiwa pale ambapo Mahakama inakutana na mazingira ya kuamua endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Na hivi basi kwa sababu ni kanuni za kisheria na zinawekwa na Mahakama za juu, pia Mahakama hii inaunga mkono kanuni hizo na kwamba kimsingi ndizo kanuni zinazotumika na kwamba Mahakama inapokutana na mazingira endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu kanuni hizo lazima zizingatiwe. Kimsingi kanuni hiyo inaeleza kwamba Mahakama pale inapotaka kutoa uamuzi mshtakiwa ana kesi ya kujibu lazima ijielekeze kwenye hoja ya msingi endapo ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka utabaki bila kujibiwa na mshtakiwa kama Ushahidi huo unatosheleza au utaweza kumtia mshtakiwa hatiani.
Sio lazima upande wa mashtaka ulete wingi wa mashahidi isipokuwa Mahakama iangalie ushahidi ule uliotolewa na upande wa mashtaka endapo hautajibiwa au endapo mshtakiwa hatapewa nafasi ya kutoa utetezi wake, je ushahidi huo unatosha kumtia mshtakiwa hatiani. Hiyo ndio kanuni ya msingi.
Lakini pia Mahakama hii pamoja na maamuzi hayo ilizingatia na ilijielekeza kwenye muongozo uliotolewa katika shauri la DPP Dhidi ya Morgan Marinyi na wenzake criminal appeal namba 133 ya 2023. Ambayo kimsingi uamuzi wa shauri hili ulienda mbele kidogo katika maamuzi ya shauri lile la Bhatt la Afrika Mashariki. Na hivi Mahakama ikaeleza kwamba katika hatua ya Mahakama kutoa uamuzi endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au lah, kinachotakiwa kuangalia endapo ushahidi uliotolewa unalenga au unaelekeza au unaonyesha kosa alilofanya mshtakiwa lina mahusiano na kosa ambalo mshtakiwa ameshtakiwa nalo, na kama sio kosa hilo kama ushahidi huo unaweza uka-establish au ukajenga hata kosa dogo linalofanana kimsingi kutoka kwenye same genus na kosa ambalo mshtakiwa anashtakiwa nalo.
Lakini pia Mahakama ilijielekeza pia kwenye shauri la DDP dhidi ya Philipo Ntonda, Criminal Appeal No 217-2020 inapatikana pia kwenye Tanzlii,ambapo Mahakama ya rufani ilienda mbele zaidi na kueleza pale ambapo Mahakama inaamua au inatoa uamuzi endapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la. Mahakama hiyo haitakiwi kujikita au kwenda kwa undani kwenye kuchambua ushahidi au kwenye kuchambua uzito na kuaminika kwa ushahidi uliotolewa kwamba Mahakama haitakiwi kuelekea huko.
Cha msingi inatakiwa iangalie connection iliyopo kati ya ushahidi uliotolewa na shtaka lililopo na jinsi mshtakiwa anavyohusishwa na shtaka hilo. Niseme tu kimsingi kwamba Mahakama hii kwa kusoma kanuni hizo ambazo nimezieleza pamoja na maamuzi ambayo ya kushawishi ambayo pia mshtakiwa aliyacite kutoka kwenye mashauri ya nchi jirani kama shauri la Antony Njeru dhidi ya Jamhuri shauri la mwaka 2006 kutoka Kenya. Lakini pia shauri la Jamhuri dhidi ya Bernard *Wangu Yankubu kutoka Kenya, lakini pia shauri la jamhuri dhidi ya James Nyagina na wenzake.
Lakini pia mshtakiwa katika hoja zake aliieleza Mahakama kwamba anaona kwamba upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha shtaka hilo kwa sababu wameshindwa kuthibitisha viini vile vitatu vya msingi vya shauri la treason au uhaini kama ambavyo imeelezwa na kifungu cha 39 (d) na kama ambavyo pia imefafanuliwa katika shauri la Gray Mattaka na wenzake lakini pia imeappear katika shauri la Gandhi na wenzake.
Na kwamba element au hivyo viini kwa sababu viko kwa mujibu wa sheria na sheria ndiyo iliyotengeneza kosa, upande wa mashtaka pia hawakuwa na tofauti kuhusiana na viini hivyo ambapo kimsingi vinatoka kwenye mashauri haya niliyoyataja Gray Likungu Mattaka pamoja na Hatibu. Imeeleza viini ya shtaka la uhaini na kwamba kiini cha kwanza ni kwamba ni lazima mshtakiwa awe ni Mtii wa Jamhuri ya Muungano lakini pia kwamba kiini cha pili lazima mshtakiwa awe ametengeneza nia ya kufanya kosa au tendo la uhaini lakini kiini cha tatu endapo mshtakiwa ametekeleza au amemanifest nia hiyo au amefanya nia hiyo kwa kufanya publication au overt act au kitendo. Hivyo basi kama nilivyosema mshtakiwa alieleza Mahakama kwamba upande wa mshtaka wameshindwa kuthibitisha viini hivyo, upande wa mashtaka walieleza kuwa kutokana na mashahidi hao 17 waliowaita walieleza kuwa wanaamini viini hivyo vitatu vimeweza kujengwa.
Na kimsingi kutokana na hoja za pande zote mbili kiini cha kwanza kwamba mshtakiwa anatakiwa kuwa mtii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kiini ambacho kilikuwa hakibishaniwi. Hivyo basi viini vilivyokuwa vinabishaniwa ni hivyo viwili endapo mshtakiwa alitengeneza nia ya kufanya kosa hilo la uhaini. Lakini kiini cha tatu ambacho ni endapo alidhihirisha nia hiyo kwa matendo au kwa kufanya publication. Hivyo basi kutokana na hoja zote mbili, Mahakama hii baada ya kupitia hati ya mashtaka pamoja na ushahidi ulioletwa na upande wa mshataka lakini pamoja na kanuni za kisheria ambazo zimesemwa au zimejadiliwa na pande zote mbili ambazo kimsingi kanuni hizo ni kanuni za jumla na pande zote mbili zilikubaliana na kanuni hizo.
Hoja iliyopo mbele ya Mahakama hii ni endapo Mahakama hii inaona kwamba upande wa mashtaka wame-establish, sio kuthibitisha, neno linalotumika ni ku-establish, kesi dhidi ya mshtakiwa. kwa maneno mengine ni kwamba endapo upande wa mashtaka kwa Ushahidi wao wamejenga kesi ambayo itapelekea mshtakiwa apate nafasi ya kujibu au kujitetea.
Mahakama hii kwa ufupi ilipitia ushahidi na hivi basi kwa kutambua kwamba hakujawa na ubishi na haikuwa hoja ya kwamba maneno hayo ambayo yako kwenye hati ya mashtaka yalitamkwa na mshtakiwa na kwamba yalitamkwa mbele ya viongozi wa chama na wafuasi pamoja na umma kwa ujumla kupitia vyombo vya habari na kwamba mashahidi waliotoa ushahidi kila mmoja alijaribu kumkutanisha mshtakiwa kwa maneno hayo na kosa ambalo mshtakiwa anashtakiwa nalo, na hivi basi kwa kuzingatia hayo yote ambayo nimeyasema kwamba ushahidi uliotolewa unamzungumza mshtakiwa dhidi ya maneno yaliyozungumzwa na pia ukiangalia ushahidi uliotolewa na shahidi wa mwisho ambaye ni P anaeleza kwamba alikuwepo siku ya huo mkutano na akaeleza baadhi ya maneno ambayo yalizungumzwa na kueleza kuwa maneno hayo yalitolewa na mshtakiwa yeye akiwepo na akaeleza kwamba yalitolewa mbele ya watu wengine pia.
Hivyo basi kutokana na ushahidi huo na kama mwanzoni nilivyosema kwamba katika hatua hii Mahakama haiangaalii au haiendi kiundani kuangalia uzito wa ushahidi au kuaminika kwa ushahidi. Uzito wa ushahidi au kuaminika kwa ushahidi ni pale ambapo upande wa pili pia unakuwa na nafasi au unapewa nafasi ya kujitetea ndipo sasa kuaminika kwa ushahidi wa shahidi unaweza ukafanyiwa assessment, katika hatua hii Mahakama haiendi kwa kiwango hicho.
Hivyo basi kwa kuwa Mahakama haiendi kwa kiwango hicho na kama nilivyosema ushahidi wote unamzunguza mshtakiwa na maneno ambayo yako kwenye hati ya mashtaka basi Mahakama hii inaona kwa mujibu wa kifungu cha 312 cha Kanuni ya Adhabu Mahakama hii inaona kwamba kuna kesi iliyojengwa kwamba kuna kesi imekuwa established sio kuthibitishwa, established dhidi ya mshtakiwa, na hivi basi Mahakama hii inasema kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu ili apate nafasi ya kujitetea au kutoa ushahidi wake dhidi ya ushahidi ambao umeletwa na upande wa mashtaka.
Mshtakiwa ana haki ya kujulishwa haki yake ya kutoa utetezi wake au kutoa ushahidi wake yeye mwenyewe lakini haki ya pili mshtakiwa ana haki ya kuita mashahidi wake baada ya yeye kutoa ushahidi wake. Lakini pia kifungu cha 312 kifungu kidogo cha tatu bado kimetoa nafasi ya mshtakiwa kama ataamua kukaa kimya kwa maana ya kutotoa utetezi wake kwamba Mahakama italazimika kutoa adverse inference.
Na hivi basi Mahakama hii inasema baada ya kumpa haki hiyo kama ataamua kufanya hivyo kifungu hicho cha 312 kinasema kama mshatakiwa ata-opt kukaa kimya basi Mahakama itawapa pia upande wa mashtaka kutoa comment zao kutokana na mshtakiwa kutotaka kutoa ushahidi. Kwa hiyo Mahakama inamueleza mshtakiwa haki zake zote ambazo ziko kwa mujibu wa kifungu cha 312. Mshtakiwa atapewa nafasi ya kusema chochote kuhusiana na hizo haki zake ambazo nimeshamuelekeza kwa mujibu wa Kifungu cha 312 kifungu kidogo cha pili.
Tundu Lissu: Waheshimiwa Majaji baada ya kusikiliza uamuzi wa Mahakama ninaomba kujulisha Mahakama kwamba ndio nitajitetea. Nitajitetea mimi mwenyewe kama shahidi, shahidi wa kwanza na vile vile Waheshimiwa Majaji nitaita mashahidi wafuatao nitaomba Mahakama iwapelekee summons (Wito).