Kijiji cha Mdimni, kilichopo Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, kinapatikana umbali wa kilomita 110 kutoka jijini Dar es Salaam. Shughuli kubwa za kiuchumi za wanakijiji cha Mdimni ni uvuvi na kilimo cha mazao ya korosho, mpunga na mahindi. Hata hivyo, shughuli hizi zimeathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi na kufanya maisha ya wanakijiji hawa kuwa magumu kila siku.
Kiini cha matatizo ya wanakijiji wa Mdimni, kilichoanzishwa mwaka 1971, ni kuongezeka kwa kina cha Bahari ya Hindi iliyopo kaskazini mwa kijiji hicho, hali iliyopelekea bahari hiyo kujaa matope na kuzidi kwa kasi ya upepo wa bahari hali inayosabisha samaki kupungua katika eneo hilo.
“Kutokana na kina cha maji kuongezeka baharini samaki wamekimbia na hivyo wamekuwa adimu,” Latifa Mbonde, 55, aliyedumu katika shughuli ya uvuvi kwa miaka 16 anasimulia wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo iliyotembelea kijijini hapo.
Latifa, mama wa watoto watano, aliingia kwenye uvuvi mwaka 2009 baada ya shamba lake lenye ukubwa wa eka 10 alilokuwa analima mpunga kuvamiwa na maji ya bahari na kuifanya ardhi hiyo kutofaa tena kwa shughuli za kilimo.
“Kwa siku ninapata samaki kidogo ambao nikiuza hunipatia wastani wa Sh5,000 tofauti na zamani ambapo nilikuwa napata samaki hadi wa Sh70,000. Kwa kweli maisha yamekuwa magumu kwani uvuvi ndio chanzo pekee cha pesa ninachokitegemea kwa sasa,” anasema Latifa kwa unyonge.
Wakati ipo kijijini Mdimni, ambacho takwimu kutoka Serikali ya Mtaa zinaonesha kuwa kina wakazi 1,332 ambao kati ya hao wavuvi ni 400 na kaya masikini ni 90, The Chanzo ilikutana na Omar Kilumbi aliyeanza shughuli za uvuvi tangu mwaka 1985. Kilumbi alikuwa ndiyo kwanza ametoka baharini na The Chanzo ilitaka kufahamu kama kumekuwa na mafanikio yoyote kwenye siku yake hiyo.
“Mambo yamekuwa tofauti na nilivyotegemea,” anasema Kilumbi, 60, akiwa ameketi nje ya nyumba yake. “Samaki hakuna, tunaambiwa ni athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hivi sasa fedha ninayopata kutokana na kuuza samaki ni ndogo sana, haiwezi hata kutosheleza mahitaji ya familia yangu. Hii ni kwa sababu hakuna biashara ya samaki inayofanyika na bado naendelea kutumia mtumbwi wa asili ambao hauwezi kwenda kwenye maji mengi au kina kirefu kuvua samaki.”
Kabla hali haijabadilika, Kilumbi alikuwa anavua ndoo tatu za samaki aina ya mtepa, odwe, dagaa aina ya koti na njo kwa kutumia mtumbwi wa asili na alikuwa na uwezo wa kupata Sh20,000 hadi Sh50,000 kwa siku. Lakini sasa hivi anavua robo beseni ya samaki na akiuza anapata Sh5000.
Utumiaji wa vifaa duni
Utafiti wa The Chanzo umebaini kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea kuongezeka kwa kina cha bahari zinaongezwa kasi na utumiaji wa vifaa duni kama mitumbwi anayoilalamikia Kilumbi kwa sababu inawazuia wavuvi wengi kwenda kwenye maji ya kina kirefu ambako ndiko samaki waliko.
Utumiaji wa mitumbwi pia si salama kwa maisha ya wavuvi kwani huwafanya wavuvi wakutwe na dhoruba kadhaa nyakati za usiku wakiwa wanavua na kusababisha kuzama kwa mitumbwi hiyo na hivyo kupelekea hata baadhi ya wavuvi kupoteza maisha.
“Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha maji baharini, vimbunga, upepo mkali, mawimbi ya bahari yameleta madhara makubwa katika kijiji cha Mdimni,” Kilumbi anaisimulia The Chanzo. “Mpaka sasa jumla ya wavuvi watano wameishafariki kwa sababu ya kwenda kuvua samaki katika maji mengi kwa kutumia mitumbwi ya asili.”
Hali hii imezaa athari jengine kubwa kwa kijiji cha Mdimni nayo ni kuondokewa na nguvu kazi yake baada ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi kuhama kijiji hicho na kuhamia sehemu nyengine, huku wakiacha kabisa shughuli za uvuvi na kutafuta kazi zingine ikiwemo kufanya kazi kwenye makampuni ya ujenzi.
Miongoni mwa watu hawa ni Ramadhani Saidi, mkazi wa Kijiji cha Mdimni aliyehamia eneo la Kisemvule kufanya shughuli za vibarua wa kulima mashamba ya watu, shughuli anayosema inamuingizia kipato cha kati ya Sh5000 na Sh 20,000 kulingana na ukubwa wa shamba.
“Nimehamia huku [Kisemvule] mwaka 2014 baada ya maisha kuwa magumu hapo kijijini [Mdimni],” Saidi anaieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu kwa njia ya simu. “Tangu maeneo yetu kuvamiwa na maji ya bahari maisha yamekuwa magumu. Hatukuwa na maeneo ya kulima. Samaki nao wamekuwa adimu kuvua. Nimeona nihamie huku na familia yangu tuangalie upepo.”
Adam Ulanga ni Mwenyekiti wa kijiji cha Mdimni ambaye anakiri kwamba kwa sasa wavuvi katika kijiji hicho wanaishi kwa shida huku hali zao za maisha zikiwa duni sana kiasi ya kwamba wengi wameacha shughuli za uvuvi na kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine ili wapate fedha za kulisha familia zao.
Kutokana na changamoto hiyo, Ulanga na Serikali yake wameanza kuwahamasisha wavuvi katika kijiji hicho kujiunga katika vikundi au vyama ili waweze kupata mikopo au vifaa vya kisasa vya uvuvi kutoka serikalini au kwa wadau wengine ili waweze kuendelea na shughuli zao za uvuvi.
“Mpaka sasa jumla ya wavuvi 120 wakiwemo wanawake na wanaume tayari wamejiunga katika kikundi kinachoitwa ‘Tangu Asili’ kulingana na kazi wanazozifanya,” Ulanga anaieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake.
“Vitu wanavyohitaji hivi sasa kutoka serikalini na wadau wengine ni kupata mafunzo jinsi ya kuanzisha vyama vya ushirika au kuweka na kukopa, jinsi ya kuviendesha, elimu ya ujasiriamali, vifaa vya kisasa vya uvuvi hata kwa mkopo ili waweze kubadilisha maisha yao na pia wanufaike na biashara ya uvuvi.”
Vijiji vingi vipo hatarini
Wadau wa masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi wanakubaliana kwamba tatizo linaloikumba kijiji cha Mdimni ni tatizo linalovikabili vijiji vingi vinavyopaka na mwambao wa Bahari ya Hindi nchini Tanzania.
Moja kati ya njia inayopendekezwa na wataalamu wa mazingira na tabia nchi ya kukabiliana na athari hizi ni kuzuia bahari isivamie maeneo ya makazi ya watu na mashamba yao na hivyo upandaji miti umetajwa kuwa ni njia bora ya kufanikisha hilo.
Hii ndiyo kazi inayofanywa katika kijiji cha Mdimni na shirika lisilo la kiserekali la Tanzania Cleanup and Conservation Initiative (TCCI) ambalo limeanzisha kampeni ya kutoa elimu kwa wanakijiji kuhusu upandaji wa mikoko, athari za mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa TCCI Salum Kingungo ameiambia The Chanzo kwamba lengo kuu la kampeni hiyo ni kusaidia wananchi kupanda mikoko ufukweni ili kupunguza kasi ya mawimbi ya bahari ambayo hivi sasa yameanza kuleta madhara kwa wananchi kwa kubomoa nyumba zao na kuathiri sehemu walizokuwa wakifanya shughuli za kilimo.
“Hivi sasa tupo katika hatua ya kupeleka maombi kwa uongozi wa shule ili kusaidia wanafunzi kujua umuhimu wa mikoko na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa sababu wananchi katika kijiji hiki wanakata sana miti ya mikoko,” anasema Kingungo. “Wakati wa utekelezaji wa kampeni hii tutaanzisha kitalu cha miche ya mikoko ambayo itakuwa inatolewa bure kwa wanafunzi na wazazi wao bure ili watu wakapande ufukweni na mpaka sasa wapo kwenye mchakato wa maandalizi ya elimu.”
Serikali kuingilia kati
The Chanzo ilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga kutaka kujua endapo kama anafahamu kadhia hiyo inayowakumba wanakijiji wa Mdimni ambapo alisema kwamba hafahamu lakini akiahidi kwenda kuwatembelea ili kuona namna Serikali inaweza kuwasaidia wananchi hao.
“Nilikuwa sifahamu kama wana tatizo hili,” Sanga aliileza The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu. “Sikujua kama wamefikia hatua hata ya kukosa chakula kulisha familia zao. Nitakwenda niongee nao ili kuona jinsi gani tunaweza kutatua changamoto waliyonayo katika eneo lao.”
Naye Meneja wa Maeneo Maalum Yaliyoathirika na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Fredrick Mulinga anasikitika kutokufahamu matatizo hayo yanayokikabili kijiji cha Mdimni na kwamba kama wangepata taarifa hizo mapema wangeijumuisha kwenye taratibu za kutafutia fungu la pesa za kufanyia kazi majanga hayo.
“Tumeingia mkataba na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi (UNFCC), mfuko wao wa kusaidia kuhimili mabadiliko ya tabia nchi — Adaptation Fund — huwa tunapokea pesa kwa ajili ya kusaidia maeneo yalioathirika.“ anasema na kuongeza: “Tutalifanyia kazi, tutakwenda kutembelea eneo hilo kisha tuone jinsi ya kulisaidia. Ipo mifuko mingi inayosaidia majanga hayo kama vile Green Climate Fund. Tunaweza kufanya kitu.”
Jenifer Gilla ni mwandishi wa kujitegemea wa habari za kijamii, wanawake na vijana anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: jenifergilla2@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.