The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kivulini Talks: Dunia Pasua Kichwa na Hali ya Sasa ya Tanzania, Tutatoboa?

Wapo wanaokiita kipindi hiki kuwa ni cha mpito, huku wengine wakikiona kama mwanzo wa zama mpya.

subscribe to our newsletter!

Wapo wanaokiita kipindi hiki kuwa ni cha mpito, huku wengine wakikiona kama mwanzo wa zama mpya. Sheria za kimataifa zinageuzwa kuwa mapendekezo tu na chombo cha wenye nguvu; mabavu yanachukua nafasi ya mazungumzo na diplomasia, huku wengi wakiuona Umoja wa Mataifa ukivunjwa vunjwa siku baada ya siku. Katika kipindi hiki cha Kivulini Talks, jopo la wachambuzi wa sera na diplomasia linachambua  hali ya sasa ya dunia kwa mtazamo wa Kitanzania.

Mjadala huu wa Kivulini Talks uliwashirikisha Dastan Kweka, mchambuzi na mtafiti; Diana Kamara, mtafiti na mwandishi; Festo Mulinda, mchambuzi anayejikita katika diplomasia na siasa; Buberwa Kaiza, mtaalamu wa sera; na mchambuzi wa The Chanzo, Tony Alfred K. Mjadala uliendeshwa na Khalifa Said.

Unaweza kuendelea kusoma au kuangalia kipindi kizima.

Khalifa Said: U hali gani mtazamaji wa The Chanzo? Tunakukaribisha tena kwenye mfululizo wa vipindi ambavyo tumekuwa tunafanya hapa The Chanzo vya Kivulini Talks. Na leo tupo hapa tena na wenzetu hawa ambao tunaenda kujadili suala zima la Tanzania katika mabadiliko ya kidunia: tunaenda vipi, tunafanya nini kuona namna ambavyo tunaweza kujiandaa kukabiliana na vitu ambavyo vitaenda kutokea huko mbele, au ambavyo tayari vinatokea hivi sasa. Mimi naitwa Khalifa Said, ambaye nitakuwa nakuendeshea mazungumzo haya, na kwa niaba ya wenzangu walioko nyuma ya kamera tunakukaribisha sana.

Jamani, karibuni sana. Shukrani. Labda nianze na utangulizi kidogo halafu tufungue mjadala kama ambavyo nilizungumza kabla hatujaanza kurekodi. Sasa hivi dunia inashuhudia mabadiliko makubwa sana kwenye nyanja mbalimbali: akili unde, au wengine wanasema akili bandia; mabadiliko ya tabia ya nchi; migogoro ya kivita Mashariki ya Kati, lakini vilevile vita vya ndani ya nchi kama tunavyoshuhudia Sudani na maeneo mengine mengi katika dunia. Ni haki kuuliza: sisi kama nchi tunajipanga vipi kukabiliana na athari ambazo zitakuwa zinatokana na mambo haya yote yanayotokea?

Kwa hiyo niko hapa na watu ambao wanafuatilia kwa karibu haya masuala kwa kusoma, kwa kutafiti na kwa kuchunguza, na tutataka kupata mtazamo wao: wanaionaje dunia, na sisi kama nchi tunajipanga vipi? Kwa hiyo swali langu la kwanza labda kwenu nyote: kama mtafupisha hali ya dunia kama mnavyoiona nyinyi sasa hivi, mngeielezea vipi? Dunia unaiona vipi kama ilivyo hivi sasa kulingana na kila kitu ambacho kinatokea? Labda tunaweza tukaanza kwako, Festo.

Festo Mulinda: Nakushukuru sana.

Hali ya dunia ilivyo sasa

Khalifa Said: Diana, we unaionaje dunia? Unaweza kufupisha vipi unavyoiangalia?

Diana Kamara: Kwa upande mmoja, utawala wa kiimla na matumizi ya mabavu, yaani ndio yako waziwazi. Sisi wenyewe hapa tuna mifano yetu Tanzania. Lakini vita ya Marekani na Umoja wa Ulaya, inavyoangalia suala la Iran, tishio la uvamizi wa Iran inatokea wakati tunaona upande mmoja, upande huo huo pia, ndio Marekani inaweza tu kwenda kumchukua Rais ndani ya nchi yake, ikamrudisha, ikampeleka Marekani ili impeleke Mahakamani.

Kwa upande mwingine, kutokana na kilichotokea Gaza na vita vya Palestina, kumezuka duniani mshikamano kupitia mitandao ya kijamii. Kwa hiyo zile harakati zimetusaidia kuona kwamba bado kuna matumaini. Na kutokana na hilo, kweli upande moja tuko vibaya zaidi kwa sababu mabavu yanaendelea, na ile kusaka rasilimali bila kificho, yaani kunaendelea kwa hali ya juu. Lakini upande mwingine tunaona, hasa baada ya kilichotokea Gaza, watu wanavyoweza kutafutana, kutafuta habari, kujulishana, kuona yanayoendelea, kupinga na kuendelea kujenga solidarities kwa nje ya mataifa yetu.

Kwa hiyo upande mmoja ni mbaya sana, lakini upande mwingine ni mzuri sana. Kuna matumaini kwa sababu tunaweza sasa, kupitia mitandao ya kijamii, hata kama bado inatukandamiza, kuvuka siasa ndogo ndogo za ndani ya mataifa yetu na kuangalia kilichoko mbele yetu sisi kama binadamu kwa ujumla.

Khalifa Said: Kaka Buberwa, unaiona vipi dunia?

Buberwa Kaiza: Asante sana. Mimi ninavyoona dunia ni kwamba dunia, tangu tumeanza kuijua, ukiangalia upande wa sayansi, ukiangalia upande wa mifumo ya utawala na siasa, dunia imekuwa ikibadilika kila baada ya muda fulani, na haijawahi kusimama. Kwa hiyo ukiangalia mti wa mabadiliko wa dunia, utaona kila baada ya muda fulani, inaweza ikawa baada ya miaka mia moja, dunia inabadilika. Pengine swali kuu linaloweza kuulizwa ni juu ya: dunia inapobadilika, anayebadilisha nani? Na iwapo Afrika, na sisi Tanzania, pengine tuna nafasi katika dunia inayobadilika kuwa sehemu ya kusukuma mabadiliko hayo.

Utakumbuka kwa mfano, takribani miaka mia moja na kama hamsini hivi, mia na thelathini na arubaini, utaona tuliingia kwenye ukoloni kuanzia elfu moja, kuanzia 1884, na ukoloni huo ukatoa mwelekeo kabisa wa Afrika tofauti na ilivyokuwa wakati ule. Tukapata watawala wapya, wakatutengenezea mataifa, wakatuwekea mipaka, tukatajiwa mataifa yetu. Kabla ya hawajaja wakoloni, [Tanganyika] haikuwepo. Wao ndio walisema, “[Tanganyika] tunayoitaka ndio hii,” wakawaonyeshe Tanzania; “Kenya tunayotaka ndiyo hii,” na hiyo ndiyo leo tunayo mpaka leo.

Lakini baadaye, kwa sababu mawasiliano yalikuwa siyo makubwa ya dunia kama tunavyoweza kufikiria, ikatokea mkanganyiko mwingine. Ni katika mkanganyiko huu tukaona Umoja wa Mataifa unaanzishwa baada ya vita kuu ya pili ya dunia; baada ya… ulianzishwa mwaka baada ya vita ya kwanza kushindikana. Lakini vilevile tukawa na matumaini na Umoja wa Mataifa, lakini sisi kama Afrika hatukuwa sehemu; tulikuwa ni wapokeaji tu. Lakini sasa kinachotokea, tunaona vilevile kwamba nyufa zimekuwa kubwa kwenye Umoja wa Mataifa.

Dastan Kweka: Ninavyoangalia mimi, nafikiri dunia iko katika kipindi cha mpito, na nafikiri ni mpito kutoka kwenye dunia ambayo kwa muda mrefu imekuwa chini ya mustakabali wa mataifa ya Magharibi; ndiyo yaliyokuwa yanatawala kwa kiwango kikubwa. Na sasa tunaona kwa upande mwingine wa dunia, especially Asia, kuna mataifa yenye nguvu yanaibuka, kwa mfano China, India. Na sio tu China na India, lakini kuna mengine; hata ukiangalia mataifa kama Malaysia, Philippines, ukiangalia Vietnam kwa mfano.

Na tunaelekea kwenye dunia ambayo kwa kiasi kikubwa mataifa ya Magharibi yanalazimika kukabiliana na mazingira ambayo ushawishi wake umepungua. Na nafikiri kwa kiasi kikubwa hiyo hali ndiyo hasa unaiona ikileta shida duniani kwa sasa. Tumefikia kwenye hatua ambayo Marekani, kwa mfano, inaona kama inafanya mambo yake kwenye mazingira ambayo siyo ya haki; nafikiri unaweza ukasema siyo fair, siyo? Lakini kwa miaka mingi wao ndiyo walikuwa wametengeneza sheria na miongozo na kila kitu. Kwa hiki kipindi cha mpito, hasa ndicho kinacholeta shida.

Na nafikiri suala kubwa ambalo Mr. Buberwa pia amegusia ni kwamba hii hali tunaweza kuitafsiri kwa namna gani? Mi nafikiri, kwa haraka haraka, nafikiri tumewahi kuwa hapa kabla: ile miaka ya hamsini, sitini, kipindi nchi yetu inapata uhuru, tulikuwa hapo, sio? Tulikuwa hapo kwa sababu ni kipindi ambacho kilikuwa ni cha vita baridi. Sasa hivi unaweza ukaita ni kama vita baridi, lakini hatujafika kwenye hatua hiyo kwa ujumla, lakini tunaelekea huko.

Na nafikiri haya mazingira tunaweza tukajifunza pia, tukasema hivi: tulivyokuwa pale, tulikuwa na fikra gani ambazo zilikuwa zinatusaidia? Nafikiri cha kwanza ilikuwa ni kuhusu suala la umoja, kama Afrika, siyo, na kama nchi zinazoendelea, kwamba ni lazima tushikamane kwa sababu huu ni wakati ambao wenye nguvu wanagombania nafasi kwenye meza ya maamuzi. Sisi tunatakiwa tufanye nini? Lazima tuje pamoja, tuungane kama Waafrika, kama nchi zinazoendelea. Nafikiri naweza nikaelezea hivyo.

Khalifa Said: Tutakuja kwenye namna ambavyo tunaweza ku-engage na hii hali, lakini mpe Tony mic. Tony, wewe summary yako ya dunia iko vipi?

Tony Alfred K: Naweza nikasema ni kipindi cha utungu; kuna kitu kipya kinazaliwa. Kwa hiyo kutakuwa kuna maumivu makubwa, ila kuna jambo jipya linazaliwa. Lakini pia kuna contradiction kama ni bado ni miaka ya watu au ya watawala wa mabavu. Unajua, kuna wakati wa wafalme, Majenerali; every time inakuwa hivyo. Kwa hiyo kuna hiyo. Kwa hiyo unaona sehemu nyingi wanaibuka wababe, wanachukua, wanahodhi mamlaka ya watu, wanatumikisha watu. Kwa hiyo nikiangalia hichi kipindi, bado nadhani ni… mimi nikiona ni cha mpito, lakini bado ni era ya watu. Kwa hiyo hawa wababe wataanguka, halafu watu bado wataendelea kuwepo, wanashikilia nguvu za madaraka.

Tanzania inaingiaje kwenye dunia mpya?

Khalifa Said: Labda nikibaki na wewe. So, tumejaribu kuielezea dunia kama ambavyo tunaiona sisi, lakini sisi tupo Tanzania, na Tanzania bila shaka itapaswa kuingia sio kwenye hiyo era mpya ambayo tumejaribu kuielezea hapa, au hiyo dunia mpya. Na nilikuwa nataka nikuulize: unaona Tanzania tukiingia vipi kwenye hiyo dunia? So nilikuwa najaribu tu kuwaza: tunaingia from the position of strength, vulnerability, or illusion? Kwa mtazamo wako wewe, how do we enter hiyo new era ambayo ipo, it looms large? Kwa hiyo tuseme tupo, tayari tumeshaingia.

Tony Alfred K: Nadhani tunaingia kwenye hali fulani ya udhaifu mkubwa.

Khalifa Said: Tukiwa dhaifu, yaani?

Tony Alfred K: Eeh. Udhaifu wa kwanza kwenye kipindi cha confusion, au cha mchanganyiko, ni kwamba ni kipindi ambacho unahitaji uwe na watu wako wameungana sana. Amezungumzia miaka ya sitini: moja ya nguvu kubwa ilikuwa inawapa nguvu kubwa viongozi wakati ule ni kwamba walikuwa na taifa lililoungana, lakini pia taifa linaloamini viongozi wao wana nia njema na wao. Sasa kwa sasa hivi tumegawanyika, lakini pia hakuna nia ya kuunganisha watu. Kwa hivyo ni udhaifu mkubwa ambao hata uwe na nani nyuma yako… sababu saa hivi tunaona mataifa madogo yanajishikiza kwa mataifa makubwa. Kama watu wako hawajaungana, wamegawanyika, hauwezi kuhimili vishindo; utakuwa ni nchi ambayo inatumiwa. Kwa hiyo hicho ni cha kwanza.

Lakini kitu cha pili, nadhani bado hatuja… hatujatoka kwenye… Tulivyotoka kwenye uhuru tulikuwa tunafahamu taswira ya Tanzania kwenye dunia ni nini: kwamba Tanzania ilikuwa inaamini binadamu wote ni sawa, binadamu wanatakiwa kuwa huru, na ilipigania hivyo. Kwa sasa hivi Tanzania ni kama hatuamini chochote. Sijui tunaamini nini; hata mi mwenyewe nashindwa kuelewa tunaamini nini. Kwa hiyo hiyo pia ni changamoto ambayo pia inakupa…

Lakini pia tuna fursa. Fursa ambayo tunayo sasa ni kwamba tuna rasilimali fulani ambazo zinatupa fursa. Kwa mfano, tuna madini mkakati, lakini pia tuko katikati ya nchi ambazo zimetuzunguka ambazo zina attention kubwa ya dunia, kama Congo. Kwa hiyo ukilinganisha, kwa mfano, Tanzania na Congo, Tanzania pia sisi tuna madini mkakati, tuna madini mkakati ambayo unaona mataifa makubwa yanayapigania; namaanisha Marekani, China, Ulaya.

Lakini ukiangalia Tanzania, kwa mfano Kanda ya Ziwa: Kanda ya Ziwa kuna Wachina wanajaribu kuchukua, yaani ni wawekezaji kwa namna moja. Lakini Kanda ya Ziwa, ukija huku Kagera, Wamarekani wanafungua mgodi mkubwa wa mkakati wa madini mkakati. Ukija kwenye reli, sasa hivi tuna reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA inaconnect, inaunganisha Tanzania na Zambia kwa ajili ya madini mkakati. Hapa tunazungumzia kwa level ya dunia.

Lakini hapo hapo una Ziwa Tanganyika saa hivi linaunganisha Tanzania; kuna namna ambavyo tumeliboresha, madini mkakati kutoka Congo yanakuwa yanapita kwa urahisi. Hizi ni njia ambazo hasa Wachina wanategemea. Lakini hapo hapo sasa ukiangalia reli ambayo tunajenga, hii ya katikati, SGR, inaweza ikaunganishwa mpaka Burundi, lakini pia mpaka huku Kagera inaweza ikawa inatumika, ambapo huku ni ambapo tunasema kuna interest za kama Wamarekani, West kwa ujumla. Kwa hiyo Tanzania tuna namna ambavyo bado tunaweza… tuko kwenye position, tunaweza tukashirikiana na haya mataifa yote makubwa na sisi kuwa na nafasi kubwa.

Khalifa Said: Tutakuja hapo, kwa sababu kwanza nilitaka tu tuone hiyo level ya preparedness. Labda pengine nije kwako Festo, kwa sababu nadhani ni swali la haki, so it’s a fair question, kuuliza kwamba kuna haya mabadiliko makubwa yanatokea katika ngazi ya kidunia. Tukiangalia sisi hapa, policy wise, strategy wise, kama nchi, unaona kuna level yoyote ya kujiandaa? Kuna intervention ambazo tunazifanya kama nchi ambazo unaweza ukasema zinatuandaa kushiriki meaningfully kwenye hiyo dunia mpya inayojijenga saa hizi?

Festo Mulinda: Kwa miaka kama kumi hivi iliyopita, Tanzania imekuwa ikijiweka katika mazingira ya, niseme, ya kuvizia: kuvizia wapi tushike kwa wakati huu. Hatuna dira inayoeleweka. Aliwahi kuuliza mtu mmoja kutoka mataifa haya mengine yaliyoendelea; alinishtukiza tu sehemu, akaniuliza, “Kwani nyie mpango wenu huwa ni nini? Yaani mnataka kuwa nchi ya namna gani katika miaka ishirini?” Aliniambia generations, vizazi; kizazi kimoja huwa ni miaka ishirini. “Kwa hiyo kwa miaka ishirini ijayo, we unahisi nchi yako inataka kuwaje?”

Sikuwa na majibu, kwa sababu nimepitia katika vipindi ambavyo nimepitia kampeni nyingi: Tanzania ya kijani, Tanzania ya viwanda; kila mtu anakuja na jambo lake. Na kwa kweli kisera hatujajiandaa. Unaweza ukasikia hii Dira ya 2050 imetangazwa, ina publicity ni kubwa, lakini kwa maana ya sera, kwa maana ya maandalizi ya kimfumo, bado hiyo dira yenyewe haina uhakika wa kufikiwa.

Na niseme tu kabisa kwamba nina uhakika 2030 hatuwezi kuwa na uchumi wa dola trilioni 1 kama hatubadiliki kimfumo, hatubadiliki kwa namna ya kujipanga kama taifa. Kwa hiyo hakuna mpango kwa kisera wala wa kimfumo ambao mimi naona nchi imejiandaa kuendana na mazingira ya sasa na kuvuka kipindi ambacho ndugu yangu hapa ameita cha mpito cha kimataifa.

Khalifa Said: Sawa sawa. Labda kaka Buberwa, kwa mtazamo wako wewe unadhani… ni kwa sababu pale mwanzo tulizungumza kiujumla jumla, lakini kwa mfano tukijaribu kuwa specific kidogo: unaona mabadiliko gani specific yanayoweza kutokea kwenye dunia na yakawa na athari kubwa sana kwa Tanzania na watu wake?

Buberwa Kaiza: Asante. Kwa maoni yangu, na kwa pengine kusimamia yale ambayo ninakuwa nakutana nayo kwa maana ya maandishi mbalimbali, ninakubaliana anayosema kwamba tuko nyuma sana na hakuna maandalizi mahususi ya kitaifa, ila tuna miitikio. Kuna miitikio ya suala hili; tunafanya kwa sababu tumeitikia jambo fulani, lakini sio kwamba tumepanga. Kama tunapanga, basi kuna utaratibu wake.

Kwa mfano, ukichukua kundi la wakulima wadogo, ukachukua kundi la wafugaji wadogo, ukachukua kundi la wavuvi wadogo, ukachukua kundi la wachimba madini wadogo, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwa muda huu ni 92% ya Watanzania. Lakini ukienda ukifanya utafiti, pengine ukaangalia maamuzi ya Bunge kwa miaka yote — sasa hivi ni Bunge la kumi na tatu kama sikosei — ukaangalia maamuzi ya Bunge kwa miaka yote, ukaenda kwenye halmashauri ukaangalia maamuzi ya halmashauri, halafu ukatathmini kujua ni kwa namna gani Tanzania imekuwa ikijiandaa, au kuna muda gani ilipanga kuhakikisha kwamba wakulima, au makundi manne niliyoyazungumza, ndio wazalishaji wakuu katika kuhakikisha kwamba Tanzania inatoka hapa ilipo, kwa mfano.

Kwa sababu bila watu walio wengi kuzalisha, wakazalisha malighafi, wakazalisha chakula, wakafikia soko… Saa hizi kuna internet; unaweza internet ikawa kijijini, kijiji ikajua kwamba tunatakiwa, ama “hapa kwenye kijiji chetu tuna uwezo wa kuzalisha nini.” Watu wakulima wote pale, wako labda laki mbili au laki moja, wakajua wanaweza kuzalisha nini wakati, wakasema kwamba, “Tunazalisha; baada ya miezi sita tunahitaji mtu wa kuja kununua mazao yetu haya,” na wakazalisha, wakapata namna ambayo itakuwa. Lakini yote hayo lazima serikali ijue, iwe na mpango huu kwamba tunahitaji wakulima wazalishe ili taifa liweze kutoka mahali lilipo.

Na tunahitaji, kwa mfano, wachimba madini wadogo. Kwa ripoti ya TEITI — nadhani tunafahamu TEITI, kamati ya kutazama namna ya madini yanavyoleta mapato — ripoti ya mwaka 2023 inasema kwamba 45% ya mapato ya serikali kutokana na madini yalitoka kwa wachimbaji wadogo. Asilimia 45; asilimia 55 ndiyo ulitoka kwa wachimbaji wakubwa, ambao siyo makampuni ya Tanzania. Na sheria tuliyo nayo inawasaidia wale wachimbaji wakubwa, si wachimbaji wadogo.

Kwa hiyo unachokiona hapa ni kwamba wale walioleta pesa zote zile serikali ikachukua, lakini hawana namna yoyote kisera, kisheria kuwawezesha, kwamba hawa ndio wazalishaji wetu kimkakati. Kwa hiyo ukiangalia wao wakulima, ukaangalia wao wafugaji, ukaangalia wavuvi wadogo, ukaangalia wakulima wadogo, wavuvi wadogo: samaki tunaokula, nyama tunaotumia, chakula tunachokula, vyote ni kama bahati; bahati tu imejitokeza.

Kwa hiyo katika mazingira ninaweza sema kwamba hatujafanya maandalizi, kwa sababu ukiwacha hii kundi la watu asilimia 92, ukaliacha nje kwenye mipango, mambo yako ya dira wakaandika wasomi, wakaandika, wakamaliza, haina maana yoyote. Lazima uangalie kwenye Bunge, ukute kwamba mambo yanayohusiana na wakulima ndiyo yanayojadiliwa.

Na kwa mfano, mfano mmoja tu haraka haraka: una watu wanaitwa wataalamu wa kilimo, wanakaa ngazi ya halmashauri, Ofisi ya DED, Mkurugenzi wa Halmashauri. Kama hakuna pesa ya posho, pesa ya mafuta ya pikipiki ya kwenda kwenye kijiji fulani kwa ajili ya huduma za ugani, hawawezi kwenda mpaka kuwe na bajeti ya posho aende. Lakini unajiuliza: kama hawa wanaohudumia wakulima, kwa nini wasikae vijijini kule? Kwa hiyo serikali isiwapeleke kule, wakapanga huko nyumba, serikali ikalipa mshahara? Halafu, lakini, wakulima vilevile wawe na mipango ya kufanya kazi.

Kwa hivyo point ninayosema hapa ni kwamba pengine ninachokiona — namalizia point yangu — pengine ninachokiona ya kwamba tunataka tufikiri upya, tudesign upya kimsingi. Hata hiyo kinachoitwa Dira ya miaka ishirini na tano inayokuja, hamsini hamsini, inatakiwa vilevile ipitiwe upya, ireflect ukweli wa mambo; sio kuangalia viwanda ambavyo vitajengwa, ambavyo kimsingi ni extension ya masoko ya wanaozalisha viwandani kwao kule, kuja hapa we ukanunua vile walivyozalisha. Sio… haituwezeshi watu wanaozalisha hapa kupeleka mali zao zikauzwe huko nje ya dunia. Kwa hiyo hiyo ni maoni yangu sasa. Asante.

Khalifa Said: Sasa Kweka, kwanza kuna hilo swali ambalo nimemuuliza kaka Buberwa, kwamba unaona mabadiliko gani katika ngazi ya dunia yanayoweza kutokea na yakawa na athari kubwa sana kwetu hapa. Hilo nitapenda ugusie kidogo. Lakini vilevile swali jingine ni kwamba mtu si anaweza akasema kwamba hatuitendei haki serikali tukisema kwamba hatujajiandaa, kwa sababu serikali itakwambia, “Sisi tuna dira, tuna sera, kuna sijui… tulibadilisha kidogo sera yetu ya mambo ya nje kuweka diplomasia ya kiuchumi.” From the position ya serikali, inaweza ikasema, “Sisi tunafanya tunachoweza kuhakikisha kwamba tunaiposition nchi kulingana na mabadiliko ambayo yatatokea ya kidunia,” si ndio? Kwa mtazamo wako?

Dastan Kweka: Naam. Nafikiri, nikirudi pale nilipoanzia, kwamba dunia iko kwenye kipindi cha mpito, na nafikiri athari mojawapo kubwa katika hiki kipindi cha mpito ni kwamba sheria za kimataifa zinapuuzwa kwa kiwango kikubwa sana. Na kwenye dunia ambayo wakubwa wanapuuza hizi sheria wanavyotaka — huku tulikotoka walikuwa wanapuuza, ila kwa aibu kidogo, ila saa hivi na aibu ile inapotea — ni hatari kwa mataifa madogo kama ya kwetu haya, na mengine ya Afrika, na nchi zinazoendelea.

Na nafikiri hiyo ndiyo athari ya kwanza kubwa kabisa: kwamba kama wana… unaona Mrusi anavyoivamia, kwa mfano, Ukraine; unaangalia namna gani Israeli ni taifa dogo, lakini anachokifanya Gaza kwa msaada wa nchi za Magharibi ni kitu ambacho hakikubaliki. Kwa hiyo nafikiri kumomonyoka kwa msimamo dhidi ya sheria za kimataifa ni tatizo moja kubwa ambalo nafikiri kwa huku kwetu unaona.

Lakini pia athari ziko kiuchumi kwa namna ambayo ni mahususi kabisa. Nafikiri wenzangu wamezungumza hapa kuhusu suala la madini, kwa mfano, na rasilimali, siyo? Kwa kiasi kikubwa, kwa sababu ule mfumo wa kisheria wa kimataifa unaporomoka, hata namna ambavyo nchi zinajihusisha na uchumaji wa rasilimali kwenye nchi zinazoendelea nayo inakuwa ni ya kihuni fulani hivi, kwa sababu angalau kulikuwa na aibu, lakini uhuni unakuwa mkubwa sana. Na nafikiri Congo na maeneo mengine… ingawa hizi nchi nazo moja moja zitakuwa zinajitahidi kupata mikataba ambayo ni ya haki, lakini kulikuwa na framework, kulikuwa na makubaliano ya kimataifa ambayo kwa kiasi fulani yalikuwa yanajaribu kuzipa sauti nchi ambazo ni ndogo. Sasa nafikiri ningesema hayo ni mojawapo ya madhara ambayo tunayaona, mbali na masuala mengine.

Sasa tukija kwa hapa kwetu, kwamba je, tumejipanga? Nafikiri kuna masuala kama… kuna namna kama mbili tatu za kuangalia. La kwanza ni uelewa wa kawaida wa sera ya mambo ya ndani; ni kwamba [sera] ya mambo ya nje ni kwamba ni mwendelezo wa sera ya mambo ya ndani, siyo? Sasa nafikiri hapa ndani kuna baadhi ya maneno ambao tuna clarity, uelewa wa pamoja wa nini tunataka. Kwa mfano, ni muhimu kukuza uchumi wetu, kwa sababu bila kukuza uchumi inakuwa ni ngumu kupambana na umaskini. Hilo nafikiri tunakubaliana.

Lakini kuna suala lingine la msingi sana ambalo linahusiana na haki za watu. Na nafikiri Tony aliligusia hapa kwamba binadamu hataki tu kula na sehemu ya kulala na mavazi; binadamu pia anataka uhuru, anataka heshima yake ithaminiwe, sio, ile dignity, utu wa mtu, sio? Na ndiyo maana nafikiri ukiangalia hata kwenye maandiko ya TANU, yalikuwa yanaweka sana msisitizo kwenye utu wa mtu, kwa sababu sio tu chakula na mavazi na sehemu ya kulala; ni pamoja na utu wa mtu. Na nafikiri hilo ni eneo ambalo linahitaji msisitizo, kwa sababu tumeshaona linatugawa sasa hivi, na linatugawa kwa namna ambayo inaweza ikatufanya tukashindwa kukabiliana na hiki kipindi cha mpito.

Lakini nafikiri la pili ni kuhusu suala la utaifa. Nafikiri limezungumzwa pia hapa utaifa: kwamba mimi ni Mzanzibari, sijui mimi ni Mtanzania Bara, kwa mfano; wengine wanasema Mtanganyika, wengine Mzanzibara; kila mtu anasema la kwake. Lakini nafikiri kimsingi utaifa ni jambo la msingi, lakini utaifa wa namna gani, si ndiyo? Sisi tulishasema ni Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaweza kuwa tuna differences zingine, tunaweza tukazifanyia kazi, lakini tuna utaifa wa aina fulani.

Lakini pia naomba nimalizie. Nilitaka kusema pia kulikuwa na utaifa mpana zaidi ya mataifa moja moja, ambayo ilikuwa ni Pan-Africanism, ni Umajumuhi wa Afrika. Nafikiri viongozi waliotangulia, kina Mwalimu na wengine, walikuwa wanajua kwamba ukiwa na hili taifa dogo la Kenya, Uganda na nchi zingine, usipokuwa na utaifa mkubwa zaidi, haya mataifa madogo madogo yatatufanya turudi kwenye utaifa wa chini zaidi yake, ambao ndio huu tunasema: mimi wa Bara, mimi Wazanzibar, labda mimi sijui ni Mmanyema, mimi sijui ni wa wapi.

Kwa hiyo lazima uwe na utaifa ambao ni mkubwa zaidi ya hivi vitaifa vyetu tulivyo navyo. Na nilisema mwanzo kwamba hii ni mbinu ya msingi: tukiungana kwenye level ya bara, tutaondokana na huu utaifa mdogo mdogo tulionao. Ndivyo ninavyoliona mimi, sawa. Sitasema kwamba hatujajipanga; tumejipanga, kwa sababu tuna sera, tuna clarity kuhusu nini tunataka, ila tuna vitu vinatugawa, ambacho tusipofanyia kazi haraka itatutoa barabarani.

Tunapaswa kujibu vipi mabadiliko haya?

Khalifa Said: Moja kati ya mabadiliko makubwa sana ambayo yanatokea sasa hivi duniani, na ambayo athari zake tayari zimekuwa dhahiri, ni nchi ambazo zilikuwa mstari wa mbele kwenye kutoa misaada, kwa mfano ya maendeleo, ku-look inward, tunasema kujiangalia wao wenyewe. Nchi hizi nyingi ni za Ulaya, Western Europe na Nordic countries, na tunaona kwenye namna ambavyo hilo linajidhihirisha ni hizi nchi kutoka kwenye hicho kinachoitwa development cooperation na kuhamia kwenye biashara. Tunaziona nchi kama Sweden, na nchi nyingine nyingi zinafuata. Lakini bila shaka suala zima la kudhibiti masuala ya uhamiaji: nchi nyingi sasa hivi zinajiangalia zenyewe kwanza kabla kuangalia nchi zingine.

Na nilikuwa nataka niwaulize, na kila mtu pengine apate kushiriki kwenye hilo: kwenye haya mabadiliko, sisi kama nchi tunapaswa tu-react vipi? Kwa mfano, tulimsikia Rais mwenyewe kabisa alisema — nadhani alikuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa, nadhani kule Zanzibar — akasema kwamba hakuna pesa. Na hakuna pesa kwa sababu mbalimbali, lakini moja kati ya sababu ni hizo za wale long-standing partners wa Tanzania wana-withdraw development aid, na wanasema sasa hivi tufanye biashara. Strategically, sisi kama nchi, inabidi ijazwe nini? Ungependa kukiona kikitokea ambacho pengine sasa hivi, pengine kwenye utekelezaji, pengine kwenye… ukasema kwamba hapa sasa hivi tunaona tunajipanga vizuri kukabiliana na haya mabadiliko?

Tony Alfred K: Nadhani kwanza msingi: kwa nini tunazungumzia sera ya mambo ya nje kwa ujumla yake? Nadhani kwa enzi na enzi kuna vitu vitatu: fanaka, prosperity, kwamba unataka nchi yako ifanikiwe; usalama, kwamba unavyoshirikiana na watu wengine unataka kuna namna ulinde usalama wako; lakini cha tatu ni kuna values, ubinadamu: ukiona wengine wanateseka, unawasaidia.

Kwa hiyo ukiangalia kwenye hii misingi, na tukirudi… kwa hiyo kitu cha kwanza kwanza, mimi nataka tubadilishe, au natamani tubadilishe mtazamo. Kwa mfano, sasa hivi tunaona Marekani wameweka zuio, Watanzania hawawezi kupata visa kwenda. Nadhani ni sawa. Yaani kwa nini? Yaani kwani kuna shida gani? Hiyo ni sera Wamarekani. Yaani una nchi yako; kuna shida gani? Hiyo ya kwanza, naanzia hapo.

Lakini cha pili, sasa, shida ninayopata ni kwamba dunia yote inafunga milango. Kote kila mtu anafunga milango yake, lakini hapa nchini kwetu tuna matatizo, watu wanakimbia nchi. Kwa hiyo sasa hii inafanya mambo yanakuwa magumu sana. Zamani, unakumbuka, kwa Tanzania tulikuwa tunasema wale wanaokimbizwa na walowezi, “Karibuni Tanzania.” Yaani tulikuwa tunahakikishia dunia na Afrika… actually dunia: kuna watu walikuwa wanatoka Jamaica, Marekani, wanakimbilia Tanzania; mpaka leo wapo. Kuna watu wanatoka nchi zote za Afrika.

Sasa hivi watu wanakimbia Tanzania, wanaenda huko nje. Kwa hiyo ni changamoto ya kwanza. Kwa hiyo inabidi tukubali kwamba dunia inafunga milango; tuhakikishe nchi yetu inafanya kazi kwa kila mtu. Yaani haiwezekani watu wanakimbia kwa kutekwa, wanakimbia kwa kufungwa kwa kesi za uongo. Yaani huo wote ni udhaifu kwenye hii dunia ambayo itafanya nchi inakuwa ngumu.

Lakini kitu cha pili, nadhani uliona hivi karibuni kulikuwa kuna changamoto ya viza za China; imekuwa ni issue kubwa, na ni issue kubwa kwa sababu tunaitegemea China kweli kweli. Sasa imagine una changamoto ya visa za China. Of course China walisema kwamba… watu walikuwa wanaamini ilikuwa ni kama retaliation, kwamba China walifanya hivyo baada ya ile sheria ya kuletwa, ile ya kazi fulani hazitakiwi kufanywa na wageni, ambao sehemu kubwa iliathiri raia wa China ambao walikuwa wanafanya kazi hizo. Kwa hiyo… lakini pia wengine walikuwa wanaamini China walifanya hivyo kwa sababu ya kuhakikisha wafanyabiashara wake ambao wameshika masoko, masoko ya jumla hapa, waendelee kuyashikilia; ni kama kuwasaidia zaidi. Watu ndiyo walikuwa wanaamini hivyo, ila China ilisema siyo kweli. Kwa hiyo kuna…

Khalifa Said: Walisema lini?

Tony Alfred K: Ni kama, nadhani, wiki tatu. Ilitoa taarifa ikasema changamoto ya visa imetatuliwa, na sasa hivi watu wanasema imetatuliwa, lakini ilisema kwamba hivyo vitu sio kweli. Ingawa nina mashaka; binafsi nina mashaka kama ni hivyo. Naamini kwamba kulikuwa kuna… kuna namna… unafahamu China ni nchi ya efficiency, efficient duniani kwenye kila kitu. Sasa kwa visa tu za Tanzania, ni visa kidogo sana, somehow imekuwa na mkanganyiko; lazima ikuachie maswali.

Sasa imagine, tafakari: katika hiki kipindi, una Marekani imetuzuia kabisa kwenda kwake, halafu una China nayo… kuna namna hii inatuzungumzia sisi, sera yetu ya mambo ya nje. Kuheshimika kwetu kama nchi kume-shake. Yaani watu hata hawakumbuki Tanzania iko wapi. Yaani hiyo ni… kwa hiyo inabidi tutafute namna ya kurudisha heshima yetu duniani.

Na unarudisha heshima kwa kufanya mambo ambayo watu wakiangalia… watu walikuwa wakiangalia wanaona kwamba ile ni nchi inajiheshimu, ile ni nchi inapambana na watu wake wapate haki, ile ni nchi… kwa mfano ukienda kwenye mambo ya rushwa, yaani kwamba ni nchi, kukitokea skendo za rushwa, inapambana, inadeal nazo. Sasa tuna mambo mengi ambayo yanafanya tusiheshimike. Kwa hiyo inabidi turudishe heshima yetu.

Kwa hiyo cha kwanza nilichokujibu: usalama, ili niwape wenzangu. Lakini cha pili, kwa mimi ninavyoona: heshima ya nchi, na hiyo inaanzia kwenye sera ya mambo ya nje, lakini sheria zetu. Hauwezekani ukawa na sheria ambazo mtu akiangalia anaona hizi ni sheria za kama… eeh, hata uki… banditry, unafahamu? Yaani sheria ambazo hata, maseme, kuna sehemu ambapo majambazi wanaongoza, nao wanaweza kuzitumia hivyo hivyo; yaani sheria katili. Unakamata watu, unawafungia. Yaani watu wanashangaa tu: yaani kijana anakamatwa, anasema anataka kuchoma vituo vya polisi nchi nzima. Sasa haya ni mambo ambayo yanatushushia standing yetu kama nchi.

Kwa hiyo kuna namna inabidi tujitafute; tumepoteza nafsi, ile roho ya taifa. Na hapo, unajua, mara nyingi, kwa mfano, viongozi wakisikia vitu vinavyozungumzia kuhusu nchi, wanajiunganisha na nchi. Tanzania itakuwa miaka elfu moja ijayo, naamini, natumaini; viongozi watapita. Kwa hiyo kuna vitu inabidi tuviangalie kwa mfumo huo: kwamba tunarudishaje heshima yetu kama nchi ambayo imepotea. Asante.

Khalifa Said: Festo, halafu Kweka. Swali hilo hilo: tunapaswa ku-respond vipi kwenye haya mabadiliko ambayo nimegusia hapo, nchi nyingi za Ulaya ambazo zilikuwa ni wadau wetu wakubwa kwenye maendeleo zinasema sasa hivi, “Sisi pia tuna mambo yetu huku; inabidi tujiangalizie sisi wenyewe”? How should we strategically respond kwenye hiyo, kama nchi?

Festo Mulinda: Asante. Na nafikiri niongezee kwa mifano miwili ya Bwana Tony hapo, ya mataifa mengine kutufungia milango; si Marekani tu na China. Mwezi uliyopita tu, viza za kwenda Japani zilikuwa shilingi elfu hamsini na mbili; wameongeza, saa hivi ni laki mbili na nusu, mara tano. Hawasemi sababu, lakini wametuongezea tupungue kwenda, kwa namna moja au nyingine.

Sasa mimi, kwa kweli, huwa naamini sana… kuna Professor mmoja wa psychology anaitwa Jordan Peterson, Canada, Clinical Psychologist. Anasema, Bwana Khalifa hapa akitaka kunishauri mimi niache pombe, kwa mfano, kama chumbani kwake anakoishi vitu havijapangiliwa vizuri, hajasafisha akapanga vitabu hapa, kikombe pale, kukawa smart, asiniambie chochote kuhusu ulevi wangu. “Clean your room first.” Kama huwezi kusafisha chumba chako, huna uhalali wowote wa kuona ulevi wangu.

Sasa taifa letu lina changamoto sana ya identity: tunavyojichukulia, tulivyojichukulia zamani na tulivyo sasa, tumebadilika sana. Hapa ndani imani imepotea. Tunatakiwa kujenga imani kwanza kati ya wananchi na serikali yao; kuwe na muunganiko. Tukisema tunaonewa nje, tunakataliwa huku, tujipange hapa, wananchi waamini. Saa hivi hilo jambo hakuna.

Tunaangalia kinachotokea Iran — achana na propaganda zozote — lakini bado kuna asilimia kubwa ya imani ya wananchi na serikali yao; wanakubaliana kwamba, “Tunavamiwa kwa sababu ambazo si kweli za kutuokoa sisi; ni kwa sababu ya interest za mataifa yanayotuvamia.” Sisi hapa hatuko level hiyo. Serikali imekaa peke yake, wananchi wamekaa peke yao.

Nitatoa mfano mmoja. Kuna miradi midogo midogo inatolewanga na serikali ya Japan, wanaita Grassroots Human Security Development Projects; midogo tu, milioni mia mbili, mia tatu: kujenga shule, kujenga vyoo, madarasa mawili, kuweka mabomba ya maji shuleni. Hiyo, kwa kweli, kama taifa hatuhitaji; hatuhitaji katika taifa ambalo linanunua magari mapya, very expensive, kutoka nchi hiyo hiyo ambayo tunaiomba itujengee vyoo kwa milioni mia moja. Gari moja linaweza kujenga vyoo vingapi nchi hii?

Kwa hiyo tumeshindwa kusafisha chumba chetu hapa, na hatuwezi kwa kweli kuwa na uhalali wa kuzungumzia mpango wa nje. Hatuaminiki nje; tumeshindwa kushughulikia mambo yetu ya ndani. Kwa hiyo mimi naamini tuanzie ndani, tusafishe nyumba yetu, halafu tutaeleweka.

Khalifa Said: Kwako wewe, kaka Buberwa.

Buberwa Kaiza: Asante sana. Mimi ninaamini kwamba, kama nilivyosema awali, hatujaanza kwa maana ya mipango. Yeah, lakini kwenye hii nakuja katika hilo… hiyo, kwa maana ya mipango, kwa maana ya sera, kwa kuandaa watu, kwa maana ya mitaji, na kwa maana ya kuijua dunia ikoje. Kwa hiyo tunachoweza kufanya sasa hivi, moja, ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania mwenye uwezo wa kuzalisha anazalisha kile ambacho anaweza akazalisha. Kwa hiyo serikali inaweka support.

Ninajua kabisa kuna kaya nyingi, kama nilivyotoa mfano ya haya makundi manne, ambazo zina uwezo wa kuzalisha potentially pengine dola elfu thelathini, arubaini kwa mwaka, kama GDP wanasema, per capita; wana uwezo huo. Maana yake wana ardhi, wana nguvu kazi. Hawana choice kwamba wazalishe mazao gani. Mazao yaliyopo saa hizi ni yale yaliyoanzishwa na mkoloni; utasikia tunalima pamba, tunalima kahawa, tunalima korosho, hayo tu. Huoni kwamba hawajibidishi kuzalisha pilipili, hawajibishi kuzalisha mazao mengine ambayo ya muda mfupi, ambayo yana export value, yanaweza yakauzwa nje ya nchi, maadamu mnafikia huko yanakotakiwa.

Sasa katika mazingira hayo, tumebaki tunasubiri hayo mahusiano ya kidiplomasia, ya diplomasia ya uchumi, maana yake kule nje wanataka nini, zaidi ya kwamba sisi kujua kwamba tunaweza tukazalisha nini tukawapelekea. Kwa hiyo nadhani kikubwa zaidi hapa ni sera za nchi zetu kutuwekeza, kuhakikisha kwamba kila mtu anazalisha, halafu kila mtu akizalisha wawe na uwezo wa kujisimamia, kwa maana msaada wa masoko, internet, miundombinu, mabarabara kule vijijini, watu kupata uelewa.

Yote yakawepo kule, wataalamu wakawa kule vijijini, watu wakajua kwamba Tanzania iliko, position saa hizi, ni tunazalisha sote kwa ajili ya ku-supply dunia, ili wakati tunapokea misaada, pengine tusipokee tena misaada ya kupewa, na sisi tuwe na uwezo wa kujitegemea, kwa sababu tuna uwezo huo. Nadhani hiyo mentality, hiyo kufikirika hiyo, ikitoka, nchi itatoka mahali ilikogota. Vinginevyo pengine inakuwa ni vigumu sana. Kule wanashindwa kuleta msaada kwa sawa, hawana, na si tunayopekee kutegemea msaada ambao hautatokea, na tuna uwezo wa kuzalisha ambao hatuutumii. Nadhani hapo ndiyo tatizo lililopo; tunatakiwa tubadilishe.

Khalifa Said: Diana, vipi kuhusiana na wadau wengine, actors wengine? Kwa sababu serikali ni sehemu tu ya taifa, si ndio? Kuna vyuo vikuu, kuna vyama vya wafanyakazi, kuna jumuiya za wananchi wenyewe, vyombo vya habari. Ukiangalia vyenyewe vinavyofanya mambo yake, inakupa picha kwamba sisi tunajiposition vizuri kulingana na mabadiliko ya kidunia ambayo yanatokea, na mengine ambayo yanakuja? And of course pia kuna hilo swali ambalo liligusia, kwamba kuna upande mbaya lakini vilevile kuna upande mzuri, kwa mfano wa mshikamano, wa matumaini. Hilo pia unaliona kwenye namna ambavyo sisi kama Tanzania, sisi kama wadau mbalimbali hapa Tanzania, tunafanya shughuli zetu kulingana na yale mambo yanayotokea duniani?

Diana Kamara: Wadau mbalimbali nao wana… nao ni taasisi zinaundwa kulingana na fikira zilizopo, na fikira zinazotawala ni za kiliberari. Kwa hiyo tunafikiria haki, uhuru, uwakilishi, Bunge, uwajibikaji. Kwa upande moja ni jambo zuri kwamba sekta binafsi, vikundi mbalimbali, kila mtu anajaribu kuangalia mambo haya yazingatiwe katika kuelekea… kwa sababu, kama aliyosema mzee Buberwa, yaani tunaangalia mbele: tunataka tufikie wapi? Kwa sababu mabadiliko ni constant; ni lazima tubadilike. Lakini tunapokuwa tumetawaliwa na fikira za kiliberali, tunafikiria tu mambo yanahusu uchaguzi na uongozi; tunasahau mambo ambayo bado yangehitaji mshikamano, mambo ambayo bado yangehitaji harakati.

Mfano mdogo tu ambao mimi nafikiria mara zote ni nishati ya upishi nyumbani. Ni kitu ambacho NGOs, CSO zingekuwa zinakiongelea; ni kitu ambacho serikali ingekiongelea, ili sisi na sisi tuwe self-conscious kama Watanzania kwamba tunahitaji ku-transform. Hakuna sababu katika nchi ambayo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme — hatujaweza kufikia uwezo wetu wa kuzalisha umeme — lakini hatuna sababu ya kutokuzalisha umeme mwingi wa kutosha wa kutumia pia majumbani. Hakuna sababu bado tunatumia mkaa na kuni; hata hapa Dar es Salaam kuna watu bado wanapikia kuni, kwa sababu hakuna mkakati wa… hakuna hiyo vision.

Serikali itakuambia inao mkakati wa kuwa na matumizi ya nishati safi, lakini we umewahi kuona tangazo? Umewahi kuona kampeni? Umewahi kuona ikifanyika mitaani? Na sisi wenyewe, unajua, hivi tu viko connected: tulichoona kimetokea Nepal kinaweza kutukuta sisi, na kinatukuta kwa namna ndogo ndogo. Tunavyoendelea kukata miti ndiyo tunavyozidi kuhatarisha nini? Mazingira na sisi wenyewe. Ikitokea El Niño, eneo ambalo limekatwa miti, wale watu wataathirika zaidi kuliko watu wa ambapo eneo bado lina miti. Lakini badala yake wanaenda kukamatwa wanaokata miti na wanaochoma mikaa. Kwa nini serikali isiweke mkakati wa kudumu wa nishati ya kupikia? Mfano, inapunguza bei, inaondoa baadhi ya kodi kwenye gesi na kwenye umeme.

Kwa hiyo utayari… hatuna utayari, kwa sababu hata hizi sekta binafsi na other actors, wote tuko kwenye moment ya liberali nje ya nyumbani, tukiwaza representation na nini, lakini zile siasa ambazo zinatuathiri sisi kweli kweli kama tu sekta… I mean, siyo? Tunaweza tukabishania uchaguzi, lakini tutabishana kwamba tunatakiwa kupika na kula majumbani?

Tunapokuwa hatuna mkakati thabiti after sixty years, wote ndio sera watasema nayo, lakini mimi sera ambayo inatekelezwa ni kila kitu unachokiona kwamba serikali imeingia mfukoni, Waziri ameliongelea, Mbunge ameliongelea, pale diwani wetu amekuja ameliongelea, ama serikali za mtaa; kitu kinatekelezwa. Kwa hiyo ile tu inatosha kunionyesha kwamba tumeandaliwa ili… yaani wametuweka katika mazingira magumu sana, kwa sababu chochote kikitokea, hivi tu El Niño zinapokuja, yaani we are set for failure.

Khalifa Said: Kweka.

Dastan Kweka: Naam. Unafikiri… tunaishi kwenye dunia ambayo kwa kiasi kikubwa, na imekuwa hivyo kwa miaka mingi tangu hii idea ya taifa, kwa maana ya state, iwepo duniani, taifa ndilo lina jukumu la kulinda haki za watu wake, sio? Na kwenye dunia ambayo mfumo wa kimataifa uko kwenye kipindi cha mpito, na sheria za kimataifa zimeporomoka kwa kiasi kikubwa, ni hatari kwa mataifa moja moja kuyumba. Kwa hiyo sisi hapa — nafikiri wenzangu wamesema, na nilisema mwanzo — kwamba kuna nyufa na tumeshatikiswa. Kwa hiyo lazima tuimarishe taifa, kwa sababu tukubaliane kwamba taifa letu likiyumba, sisi mmoja mmoja humu ndani hali yetu itakuwa ni mbaya. Kwa hiyo lazima tuimarishe taifa.

Halafu nafikiria pili, tuweke nguvu kwenye uzalishaji, na hasa kwenye lengo la kujitegemea katika mazingira tuliyonayo. Na ndiyo maana niligusia mwanzo kwamba tuliwahi kuwa mahali kwenye miaka ya sitini na sabini; tulikuwa na misingi fulani. Umuhimu wa kujitegemea ni mkubwa kwa sababu nchi zilizoendelea pia moja moja utaifa wao umeyumba. Ndiyo maana, kwa mfano, unaona idadi ya watu kwenye hizo nchi inapungua, kwa maana ya nchi ambao wanajiita wazawa wenyewe inapungua; wanategemea sana watu kutoka nje wawasaidie, hata kwenye huduma tu za kuangalia wazee, kwa mfano, na huduma za msingi za hospitalini na maeneo mengine.

Kwa hiyo lazima sisi pia tuangalie hilo eneo kwa kiasi kikubwa, la kuimarisha utaifa. Na nilitaka kusema la pili: tuweke nguvu kwenye kuhakikisha tunazalisha kwa lengo la kujitegemea. Sasa kujitegemea ni kwamba, kwa maana alikuwa self-reliant, na sio necessarily ile wanaita autarky; siyo lazima. Uendelee kushirikiana na wenzio, lakini kwa lengo la kujitegemea.

Nafikiri nilitaka kusema la tatu, ambalo ni la msingi; nafikiri amegusia pale Bwana Mulinda: ni kwamba lazima tuangalie pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho. Kwa mfano, tunaishi Dar es Salaam. Sasa hivi mimi kila siku nikipita hapa mjini nakumbushwa ni namna gani nilivyo maskini, kwa sababu pengo ni kubwa sana kati ya wenye nacho na wasio nacho, kwa maana ya watu wanavyomiliki, kuanzia kwa mfano magari ya kifahari, majumba, na maisha tu ya anasa.

Unaona kabisa huku tunakoelekea watu hawawezi tu kukaa kimya; kuna mahali tutafika. Hili pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho litaharibu utulivu tulionao, kwa sababu watu watakataa hii hali. Na tuliwahi kuwa na msimamo thabiti kuhusu usawa katika taifa; nafikiri tumeshatoka hapo. Sasa hivi tumeweka zaidi nguvu kwenye kukuza uchumi; tumesahau kwamba pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho ni tishio kubwa sana.

Maslahi ya kitaifa yasiyo na mjadala

Khalifa Said: Labda swali jingine ambalo nataka niwaulize ni kwamba — na hili pia linahusiana na mabadiliko makubwa yaliyotokea — pale Bwana Festo alitupa nadharia ile ya bwana fulani yule ambaye nimemsahau jina, lakini kuna Marekani kama superpower anataka abaki pale; China… China anasema yeye hataki kuwa superpower, lakini hiyo ni debate ya siku nyingine. Lakini kumekuwa kuna mjadala sasa Tanzania: Tanzania i-look West au i-look East? Ijikumbatie kwa watu wa Magharibi, au ijikumbatie kwa watu wa Mashariki? Na tunaona hapa, kwa mfano, Rais akiwa ameenda China, akienda Urusi, kunakuwapo na mjadala kidogo kwamba pengine ni Tanzania ina-pivot kutoka kwenye…

Lakini swali langu ninalotaka kuwauliza nyinyi ni kwamba, haijalishi Tanzania inaamua kushirikiana na nani — kwa sababu kwanza hiyo ni sovereign power ya Tanzania yenyewe kuamua inataka kushirikiana na nani — lakini haijalishi Tanzania inataka kushirikiana na nani, ni maslahi gani makubwa ya kitaifa yawe hayana mjadala? Kwamba haijalishi kama watakwenda Marekani, watakwenda Umoja wa Ulaya, watakwenda China, lakini these national interests lazima ziwe protected kwa gharama yoyote ile, haijalishi Tanzania tunashirikiana na nani. Labda Diana, unatabasamu.

Diana Kamara: Unajua, wakati wa Magufuli, alipoamua kushirikiana na Waisraeli, akasema, “Sisi hatufungamani na upande wowote,” lakini kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni upotoshaji. Maana ya kutokufungamana na upande wowote ni kwamba Magharibi na Mashariki tutashirikiana nao, mradi tunalinda masilahi yetu. Tofauti ya kutokufungamana na upande wowote na sasa hivi kushikilia chochote ni kwamba, tulipokuwa hatufungamani na upande wowote, tulikuwa tuna… kweli hatuna uwezo wa kumzuia Marekani asiendeleze vita na Vietnam, lakini haimaanishi hatutaongea. Tutasema, “Tunalaani vita vya Marekani juu ya Vietnam.” Tutalaani mambo ya Marekani Amerika ya Kusini.

Sasa hivi tunaposhikilia lolote, tunaona nchi hizi hizi: Umoja wa Ulaya unavyoitikia jambo la Iran, unavyoitikia suala la wahamiaji; tunaona Marekani inavyofanya Amerika ya Kusini, kitu ambacho ni cha ajabu, kuwatoa madaktari wa Cuba, Honduras, Jamaica, wapi, nchi zote ambazo hazina sekta ya afya ya umma ambayo inaweza kuhimili vitu tu vya kawaida, yaani vya sekta ya afya. Tunawaangalia wale, halafu tunataka bado waendelee kutupenda na kutuweka karibu nao.

Walikuwa wanatuweka karibu kwa sababu tulikuwa tunalinda masilahi yao, makampuni ya uchimbaji. Hatuwasemi wala hatuwanyooshei vidole kuhusu mambo wanayoyafanya. Hatuwezi hata kutoa tamko sisi kama nchi: uvamizi unaoendelea waziwazi, kukamatwa kwa viongozi wa nchi nyingine. Ile tu kiasi cha kwamba sisi tunataka wao waendelee kutupenda na kutuweka karibu, inacompromise masilahi yetu.

Kwa hiyo sera tunayojipa ya kimataifa na uso tunaojipa unaonyesha kwamba masilahi ya dola ni masilahi ya kujilinda wenyewe. Ndio maana hata swali la… suala la msaada, lazima dola litetereke. Wananchi wao wamezoea; wavuvi, wakulima hawapangi bei za bidhaa; watakachopewa ndio watakachopewa. Kwa hiyo sisi tumezoea; dola ndio litatetereka, sio sisi wananchi.

Khalifa Said: Kaka Buberwa, swali langu ni lile lile: haijalishi Tanzania inaamua kushirikiana na nani, ni maslahi gani ya kitaifa lazima iyalinde, kwamba haya hakuna mjadala, lazima tuyapiganie, iwe ni wanaenda Marekani, wanaenda Umoja wa Ulaya, wanaenda China, au wanaenda popote?

Buberwa Kaiza: Asante, Khalifa. Pengine niweke angalizo kidogo: Tanzania ipi? Mahali… Tanzania ziko mbili. Kuna Tanzania ya watawala, halafu kuna Tanzania ya raia wa kawaida. Kwa hiyo jambo la kuangalia pale ni watawala na raia wote wanakutana kwenye Tanzania kwa maana ya masilahi, kwa maana ya maamuzi, kwa maana ya sera, kwa maana ya kusikilia, ku-respond, yaani wa uwajibikaji, kwa maana ya mifumo yoyote, wala kwa maana ya taasisi, kwa maana ya zile feelings ambazo katika mataifa mengine raia wa kawaida akitoa kelele yoyote inapokelewa haraka, kwa sababu ile ile gap, pengo kati ya watawala na watu wa kawaida, ambao ni raia, basically ambao ni jamhuri, inakuwa ni ndogo sana.

Pengine hiyo tu kabla sijaenda kushauri hoja yenyewe: pengine kuna haja basi sera zetu kwanza kuhakikisha kwamba tunapunguza hilo pengo. Kwa mfano polisi: ukienda polisi mpaka leo, ukitokea ukaenda pale CRO, utaulizwa kabila lako; mwanaume au mwanamke. Anakuona we ni mwanaume, anakuuliza mwanaume, mwanamke. Point tunayosema hapa ni kwamba haya yote yalitoka wakati wa mkoloni, na mkoloni tunajua alikuwa anataka nini.

Haya, kwa hii, tukianza, hatua ya msingi kabisa ni kuondoa yale mabaki aliyoacha mkoloni, yale ya kimfumo, ya kimuundo, ya kitaasisi, ya kifikra, ya kimtazamo. Tukishaondoa hayo, sasa tunaikuta Tanzania ambayo sasa tunaifikiria tu, inakuwa ni theoretically, inakuja saa.

Swali lako: hiyo Tanzania, hiyo sasa, masilahi yetu katika Tanzania namna hiyo ni yapi? Ni utu; ameshazungumza hapa: Tanzania ambayo ina utu. Utu utaupataje? Lazima kila raia anayeweza akazalisha anaingia kwenye mainstream ya production ya nchi; anajulikana kwamba hata akipungua kidogo, najua kitu kimepungua; akiongezeka, unajua uko na increment; inaonekana kwa kila raia. Akiweza kuzalisha, na uzalishaji ule ukaunganishwa na uzalishaji wa dunia, maana yake tutaweza kuwa na Tanzania ya ambao serikali inaizungumzia; ndio itakuwa Tanzania watu wengine wa kawaida. Hiyo ni moja.

Lakini la pili, la utu: tukitaka kwenye utu tunaingia kwenye afya. Watu raia ambao wana afya bora, maana yake ni kwamba wanaweza wakazalisha, wanaweza wakasimama, wanaweza wakainfluence mambo. Maana yake ni nini? Sisi hapa, ukienda — na sijui kama nitapata muda kutoa mfano mmoja, lakini ngoja niende haraka haraka tu — ukienda hospitali hivi ukasema, “Nimeota ninaumwa,” hakuna atakayekusikiliza, kwa sababu sisi sera yetu afya ni kuwezesha mtu asife. Usife, maana yake unaumwa tayari, umepata ajali.

Lakini kama ukiwa na mambo ya kwamba, “Sina uhakika, kwa sababu kila siku naota hivi vibaya; nataka nipate msaada wa kitabibu,” pengine siyo tabibu wa kiafya, public health, niwezeshwe kujua namna ya… pengine nalala vibaya, pengine ni chakula, pengine mazingira anayozunguka. Kwa hiyo ninachokisema hapa ni kwamba mfumo wetu wa afya, maana yake, unatakiwa ubadilishwe vilevile, uwe wa kujali afya za watu badala ya kujali wagonjwa. Kwa hiyo unakuja kuugua pengine accidentally.

Lakini mfumo tulionao sasa hivi tunawekeza zaidi kwenye madawa, tunawekeza zaidi kwenye majengo ya hospitali, na tunaambiwa tumefika mbali sana kwa sababu kuna majengo yamejengwa kiasi kadhaa. Kimsingi unazungumza na wagonjwa. Kwa hiyo pengine niache wenzangu wengine waendelee, lakini pointi ni kwamba lazima tubadilishe mifumo ya kisera na mtazamo. Lakini hatua ya kwanza kabisa: turejeshe uhusiano wa raia na watawala uwe eneo moja, lakini tuanze kuona masuala kama ya afya, masuala ya uzalishaji na masuala mengine.

Muda kama huu mwakani

Khalifa Said: Ndugu zangu, mimi nawashukuru sana. Nataka kuwauliza swali jingine, moja tu la mwisho, halafu twende kufunga. Kwa ufupi sana, sote tutajibu. Lakini tumezungumza mambo mengi hapa, tumejadili vitu vingi, na nilikuwa nataka kuwauliza: unikamilishie sentensi. Unakumbuka lile zoezi tunafanya shule ya msingi? Kwamba: “Muda kama huu mwakani, Tanzania itakuwa ipo kwenye nafasi nzuri ya kuendana na mabadiliko yanayotokea kwenye dunia endapo kama hiki kitatokea, endapo hiki kitafanyika.”

Kwa hiyo kwa haraka haraka tu, kwa sentensi fupi, uniambie kwamba, kwa mtazamo wako wewe, kwa imani yako, kwa matumaini yako, kwamba kipindi kama hiki mwakani Tanzania itakuwa ipo kwenye nafasi nzuri ya kukabiliana au kushiriki kwenye mabadiliko ya kidunia endapo kama hiki kitafanyika, halafu uniambie hicho ni kipi kwa mtazamo wako. Tukaanza na Festo.

Festo Mulinda: Asante. Tanzania mwaka kesho majira kama haya: tukiweza kutengeneza imani kati ya wananchi na serikali, tukaweka mifumo ya uwajibikaji — kwa sababu huo ndio ugomvi mkubwa tulio nao sasa — ikawekwa sawa, kama ni kuandika katiba mpya, au kuweka sera ambazo zinamfunga mtawala kutokuweza kutoa maamuzi kwa niaba ya wananchi bila kuwashirikisha, tutakuwa tunaelekea kwenye dira nzuri. Asante.

Khalifa Said: Shukrani sana. Diana.

Diana Kamara: Wakati kama huu mwakani, wakati kama huu mwakani, Tanzania inaweza kujiandaa na mabadiliko yanayotokea duniani endapo tutaweka nia ya dhati ya kujenga sekta ya umma, kwa sababu sekta ya umma ndiyo itaweza kumkomboa mwananchi, kuliko kuweka juhudi na mikakati katika kujenga urasimu na sekta binafsi.

Khalifa Said: Shukrani. Kaka Buberwa.

Buberwa Kaiza: Asante sana. Hilo swali, jibu lake linahitaji mkakati wa muda mfupi. Hayo tulikuwa tunazungumza ni maneno mazuri, ni fikira nzuri, lakini tangu uchaguzi mkuu mwaka jana, Oktoba 29, Tanzania haijakuwa salama; haijakuwa kama ilivyokuwa zamani. Kuna mgawanyiko mkubwa, kuna kuwindana, kuna watu wanatekwa, kuna watu wanapelekwa Mahakamani, kuna kupelekwa polisi, kuna hali ambayo kimsingi haijengi taifa ambalo liko solid, limekaa pamoja.

Kwa hiyo tunao mgogoro; tunao wajibu kama taifa wa kuhakikisha kwamba mipango, utaratibu, sera za kuweka taifa pamoja kuondokana na mgogoro uliopo, watawala wakawa kama wakasikiliza wananchi, na wananchi wakakubaliana na watawala, halafu tatizo lililopo hili la mgogoro uliotokana na uchaguzi likaisha. Nadhani tukifika wakati ile mwaka kesho muda kama huu, nitakuwa taifa inaweza ikaanza kufikiria sasa kwani yale ambayo tulikuwa tunajadili.

Khalifa Said: Kweka.

Dastan Kweka: Asante. Nafikiri na mimi nitaungana na wenzangu kwamba tuimarishe umoja na mshikamano katika taifa. Hilo jambo ni muhimu sana kwa sababu ya hali inayotokea duniani; inabidi uwe na taifa imara. Na nafikiri cha pili, tuimarishe mshikamano na ushirikiano na mataifa mengine ya Afrika, kwa sababu mwisho wa siku sisi ni Waafrika, na tumewahi kuwa na mtazamo wa namna hiyo. Turudi kwenye misingi, tujikite hapo. Asante.

Tony Alfred K: Na naomba pia nichangie kwenye lile la value. Mimi nadhani tunachotakiwa kufanya ni kuifanya Tanzania iwe salama kwa kila mtu; kwa hiyo kila mtu ataweza kuchangia. Lakini kuna ile nilikuwa na… nasubiri nichangie; naomba nichangie hapo, lile la values. Of course, zamani tulikuwa tunasema tunu zetu ambazo tunaziangalia, ambazo tutaziangalia kwenye kila mahusiano, ni utu, kwamba binadamu wote ni sawa, lakini pia Uafrika, umajumuhi wa Afrika.

Na nilitaka nizungumzie kwenye… umajumuhi wa Afrika, Pan-Africanism. Changamoto ambayo tunayo sasa hivi: viongozi wetu wa Afrika wanaungana, ila sio kuendeleza maslahi ya watu; ni kutukandamiza watu. Kwa hiyo una viongozi wanashirikiana kwenye kuteka watu, kwenye kukimbiza watu kwenye nchi zao. Yaani ndio hivyo; ndio umajumuhi ulioibuka. Kwa hiyo sasa, kama Tanzania, moja ya tunu yetu ni kuendeleza Pan-Africanism. Labda tu-redefine; inabidi turudi kwenye msingi wa Pan-Africanism, kwamba Waafrika nao ni binadamu wanaopenda uhuru na vitu.

Lakini cha pili, kuna mjadala mkubwa sana unaendelea duniani, mjadala kuhusu values. Kwamba watu wanasema kuna wale walikuwa wanafuatilia kuhusu tunu zile, kwamba nchi nyingine inaweza ikajali: kwa mfano, we nchi yako ukianza kunyonga watu, nchi nyingine inasema, “Bwana, si tuna… hatukubali we unyonge watu; tunakataa.” Au ukianza kunyang’anya mali za watu, nchi nyingine inaweza kuingilia.

Sasa dunia sasa hivi inajadili kwamba, kama sisi maslahi yetu tunapata — kama sisi, tuseme nchi yetu, tunapata kwenye hicho kitu, kwenye hiyo nchi, kama ni biashara, nini — je, kuna umuhimu wa nchi kujali values? Kwa hiyo dunia, kwa mfano West, saa hivi ndio big debate: je, wajali kuhusu hizi tunu? Na unafahamu hii West walikuwa wanapush sana hii demokrasia, nini.

Sasa mimi nadhani moja ya kitu ambacho tuangalie, hasa kutokea Tanzania: duniani hakujawahi kuwa na ombwe. Kwa mfano, sasa hivi nchi zote zikaamua kutokufuata… useme kwamba kila mtu anafuata masilahi yake. Tuseme watu wakiwa nchini nyingine, watu wakiwa wananyongwa, we unanyamaza as long as watoto wako wako salama; majirani zako wakiwa wanafanya wakimbizi, we unanyamaza.

Sasa kitakachotokea, serikali zote za dunia zikiamua kunyamaza na kuwa kujali masilahi yake, ni kwamba kutakuwa kuna ombwe, ambalo, kwa sababu dunia haina ombwe, kitu kitajaza, na kinaweza kikawa dini; sana sana kinakuwa dini. Mimi naamini inaweza ikawa dini, au ideolojia fulani ambayo itakuwa tofauti. Kwa hiyo kama mataifa ya dunia yanataka kuamua kwenye hilo swali, inabidi yaangalie kwamba ombwe haiwezi kuwepo.

Lakini kingine, turudi nyuma tuangalie mfano Tanzania kuhusu value. Yaani kwa miaka mingi Tanzania ilikuwa ni nchi maskini, lakini imepambana kwenye nchi nyingine. Sijui unasikia Seychelles wameenda; tuliweka mpaka majeshi Seychelles kusimamia nchi; Uganda, Mozambique. The first, nineteen sixty-four, ile wakati jeshi linaundwa, mission ya kwanza, hata bado hawajaelewa, walienda Mozambique kupigana, kuwapigania watu wa Mozambique wawe huru.

Sasa ukirudi kwa Tanzania, ni kwamba kuna value. Tanzania haikuwa tajiri kiasi hicho, lakini iliweza kujaza ombwe ambalo lilikuwepo la kujali values. Kwa hiyo nadhani tu nchi nyingine zinaweza zikaiga kwenye huo mfano wa Tanzania. Asante.

Khalifa Said: Sawasawa. Ndugu zangu, mimi nawashukuru sana kwa maoni na tafakuri zenu, na natumai pia mtazamaji umefaidika na kufurahia michango ambayo wachangiaji hapa walikuwa wanaitoa. Nadhani kama kuna kitu kimoja kikubwa mimi binafsi ambacho naweza ikawa nimekichukua kutoka kwenye michango yote ambayo ndugu zetu hapa wameitoa, ni umuhimu wa sisi kama nchi kusema kweli, kutuliza kichwa chetu na kusafisha mambo yetu hapa ndani, na kuwa wamoja, kuwa na mshikamano, na kutokuanza ku-deal na vitu vidogo vidogo, kwa sababu bila hivyo maana yake uwezo wetu wa ku-respond kwenye mabadiliko makubwa ya kidunia utakuwa mdogo sana.

Lakini wewe pia unaweza kuwa na maoni kuhusiana na maswali ambayo tumeyauliza hapa na hoja ambazo zimeibuliwa hapa, na unaweza kutuandikia kwenye comment section au kutuandikia kwenye namba zetu ambazo utakuwa unaziona hapa zikipita, na email address zetu.

Mpaka hapa ndio tumefikia tamati ya mazungumzo ambayo tulikuwa tunayafanya hapa na ndugu zetu hawa kuhusiana na nafasi ya Tanzania kwenye mabadiliko makubwa ya kidunia yanayotokea hivi sasa. Mimi ambaye nilikuwa nakuendeshea mazungumzo haya ni Khalifa Said, na kwa niaba ya wenzangu walioko nyuma ya kamera, Joseph Kirati, Ambrose Dawai na Frank Mtoro, mpaka muda mwingine, kwaherini.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×