Kwa Waislamu, mtu akienda Hijja Makka au kumzuru Mtume Muhammad Madina, halafu akafia na kuzikwa huko anatabiriwa kuwa amepata mwisho mwema. Wengi wenye imani thabiti juu ya uwepo wa maisha ya baada ya kifo, kila waendapo Hijja, hutamani wafie huko. Mara mbili nimeenda Makka na Madina kwa ibada za Hijja na Umra, sikupata bahati hiyo (au bahati mbaya) hiyo. Silalamiki kwa sababu walau wanangu hawakubaki yatima.
Kama ambavyo unaweza kupoteza uhai katika tukio la kidini, unaweza pia kufariki katika hafla ya kiserikali au kiinchi. Tofauti na Mwenyezi Mungu, Serikali haiwezi kukupa pepo. Lakini angalau inaweza kukupa heshima na kutambua kujitoa kwako kwa uzalendo wako. Heshima na kutambuliwa, mawili hayo, kwa uchache ndiyo waliyostahili kufanyiwa wale watu 45 waliokufa na wengine 37 waliojeruhiwa pale Uwanja wa Uhuru siku ya Jumamosi, Machi 20, 2021, kwenye shughuli ya kumuaga Rais wa awamu ya tano, hayati John Pombe Magufuli. Ukiniuliza mimi, mpaka sasa, watu wale 45, hawakupata heshima ile waliyostahili.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kilichochangia vifo hivyo ni msongamano wa watu, ambao baadhi walifikia hatua ya kuruka geti kwa lengo la kwenda kuaga mwili wa Magufuli. Kutokana na wingi wa watu waliojitokeza na kukosekana kwa taratibu muafaka za kuwadhibiti waombolezaji, baadhi yao walijikuta wakikanyagana na wengine kupoteza fahamu.
Watu wale 45 walistahili heshima kwanza kwa sababu ya thamani ya uhai wao, pili, kwa sababu ya wingi wao (vifo 45 katika tukio moja) na tatu kutokana na mazingira ya vifo vyao – ambapo walijitokeza kwa sababu ya tukio la kitaifa. Kinyume na matarajio hayo, Watanzania wenzetu wale 45, wakiwemo watano wa familia moja, walizikwa bila kutambuliwa au kupewa heshima na uzito uliotarajiwa.
Vifo vyao na namna vilivyochukuliwa kimzaha vinanikumbusha wasichana vigoli waliokuwa wakifukiwa kaburini enzi za utawala wa kichifu kule kwetu uyaoni ili wakampakate Sultani aliyefariki. Maisha ya vigoli wale hayakuwa na thamani, kiasi unaweza kudhani walikuwa ni nyongeza tu katika mchakato wa Mwenyezi Mungu wa uumbaji baada ya kuumba wanadamu halisi, yaani hao machifu!
Kwa kiasi fulani namlaumu rais wangu, Samia Suluhu Hassan aliyepaswa kuonesha uongozi katika kujali maisha ya watu waliofariki wakati wakiomboleza. Nilitegemea tamko rasmi la rais la kuwapa pole wafiwa na kuwatambua waliokufa kwa kuguswa na msiba!
Nilitegemea Rais Samia angetembelea walau familia chache za wafiwa na kuwapa mkono wa pole. Nilitegemea zaidi kumuona akienda kuiona familia iliyopoteza watu sita, wakiwemo watoto wanne. Katika familia hiyo, bwana Dennis Mtuwa Kimara, Dar es Salaam, alipoteza mke na watoto wawili, msichana wa kazi na watoto wengine wawili wa ndugu zake. Unaweza kuhisi maumivu ya familia hii? Bila shaka ndugu wangefarijika sana iwapo wangepewa pole kutoka Ikulu.
Nilitegemea mwaliko wa wawakilishi wa wafiwa Ikulu au popote pale kwa ajili ya dua ya kitaifa kutoka kwa masheikh, maaskofu na wachungaji kuombea roho za marehemu. Nilitegemea mazungumzo ya fidia. Nilitegemea mengi lakini sikuyaona yakitokea.
Nionavyo, mwenye shughuli ile ya maombolezo alikuwa ni rais. Ni yeye aliyetangaza msiba. Ni yeye aliyeandaa kusanyiko la kuaga. Watu wameumia katika mkusanyiko aliouitisha. Je, isingekuwa jambo la kiungwana kuuungana na wafiwa na majeruhi kuonesha masikitiko yake?
Wapo wanaodai kuwajibishwa kwa wahusika. Sishawishi hilo kwa sababu ya asili ya tukio lenyewe na namna lilivyotokea. Hakika, haikutegemewa watu wangekuwa wengi kiasi kile. Hata hivyo, ni muhimu uchunguzi ufanyike ili walau kung’amua udhaifu ili makosa kama yale yasitokee tena siku za usoni na kugharimu maisha ya watu. Mamlaka zisipochukua hatua kama hizi inafanya thamani ya maisha ionekane ndogo sana Afrika.
Kwangu, hii ni fursa iliyopotea kwa Rais Samia, fursa ya kuonesha uongozi, kujali, huruma, kuguswa kwa wananchi wake. Uzuri ni kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hajachelewa sana. Linatengenezeka.
Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia 0735420780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.