The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, ‘English Mediums’ za Serikali Zinakinzana na Sera ya Elimu Bila Ada?

Serikali yasema hapana, ikidai kwamba wazazi hawalazimiki kuwapeleka watoto huko kama shule nyingine zipo.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameiambia The Chanzo kuwa mpango wa Serikali wa kuanzisha shule zake za msingi zinazofundisha kwa lugha ya Kiingereza unalenga kuwapa wazazi machaguo sahihi ambayo watayamudu katika kuamua hatma ya elimu ya watoto wao. 

Aidha, kiongozi huyo ameeleza kuwa mpango huo unakuja na lengo la kuboresha ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kwa sababu wamebaini kuna udhaifu mkubwa kwa wanafunzi kwenye kutumia lugha hiyo baada ya kumaliza elimu ya msingi. 

Profesa Mkenda aliyabainisha hayo Aprili 13, 2024, katika ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam, kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika kabla ya hafla utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

“[Tunataka] kuwa na machaguo ambayo watu wanaweza wakamudu,” alidokeza Mkenda kwenye mahojiano hayo. “Kwa sababu unazungumzia shule za Serikali [za Kiingereza], lakini na kuna shule za binafsi pia.”

“Suala kubwa ni hili, tunaboresha ufundishaji wa lugha,” aliendelea kuzungumza. “Mimi nimesoma mpaka darasa la saba masomo yote kwa Kiswahili isipokuwa Kiingereza. Sasa udhaifu ambao tumeuona ni jinsi ambavyo tunafundisha lugha, kama unamfundisha mtu Kiingereza sasa hivi mpaka darasa la saba lakini hawezi kukimudu ni kwamba kuna udhaifu mkubwa wa namna tunavyofundisha.” 

SOMA ZAIDI: Mkenda: Vyuo Vikuu Vinahitaji Kweli Mijadala, Lakini Siyo ya Kiharakati Pekee

Profesa Mkenda ameeleza kuwa mpango huo wa kuboresha ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kupitia kuanzisha shule za ‘English Medium’ unakwenda sambamba na kuboresha shule za msingi zinazotumia lugha ya Kiswahili kufundishia kwa kuboresha ufundishaji wa somo la Kiingereza. 

Mkenda alisema hiyo itamfanya mzazi awe na machaguo matatu ya kumpeleka mtoto kwenye shule ya Kiingereza ya Serikali, shule ya Kiingereza ya binafsi pamoja na shule ya Serikali ya Kiswahili ambayo ufundishaji wa somo la Kiingereza utakuwa umeboreshwa.  

“Tumeliweka hilo kwenye mitaala mipya,” Profesa Mkenda, ambaye ni Mbunge wa Rombo (Chama cha Mapinduzi – CCM), anasisitiza. “Kwanza sasa hivi Kiingereza kinaanza tangia darasa la kwanza halafu tunafundisha Kiingereza kama lugha ya pili wakati tulikuwa tunafundisha kwa ujumla kanuni za msingi zaidi kuliko mawasiliano na vitu kama vile.”

“Na tunaendelea kujifunza namna ya kuhakikisha kwamba huyu [mwanafunzi] akimaliza darasa la saba kweli aweze kumudu Kiingereza.” 

Mpango wa Serikali kuwa na shule zake za Kiingereza ambazo zimekuwa zikishamiri kwa kiasi kikubwa katika siku za hivi karibuni umekuwa ukipingwa vikali na wadau mbalimbali wa masuala ya elimu hapa nchini, kwa kile wanachodai kuwa ni una lengo la kutengeneza matabaka kwenye elimu ya umma. 

SOMA ZAIDI: Serikali Yatetea Uamuzi wa Kuanzisha Tahasusi za Masomo ya Dini

Wadau hao wamekuwa wakiishinikiza Serikali kuziacha shule za Kiingereza ziendelee kuendeshwa na watu binafsi kama ilivyokuwa awali na yenyewe ijikite kwenye kuboresha shule zake za Kiswahili ambazo zipo na zinaendeshwa kwa mujibu wa sera ya elimu. 

Utafiti wa The Chanzo umebaini kwamba mpaka kufikia Aprili 2023, kulikuwa na shule za Kiingereza za Serikali 42 ambazo zinaendeshwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Baadhi ya shule hizo zinapatikana Geita, Manyara, Ruvuma, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma na Kilimanjaro.

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imebainika kuwa ni moja wapo ya halmashauri ambayo idadi ya shule za mtindo huo imekua kwa kiasi kikubwa ndani ya muda mfupi. Mwaka 2021 halmashauri hiyo ilikuwa na shule hiyo moja tu lakini hadi kufikia Januari mwaka huu ilikuwa na shule hizo 10. 

Alipoulizwa kama je, ni haki kwa wanafunzi waliosoma kwa lugha mbili tofauti wakati walipokuwa shule ya msingi na kisha kukutanishwa katika darasa moja la kidato cha kwanza, Profesa Mkenda alieleza kuwa ili kuweka usawa, Serikali itaendelea kuboresha shule zake za Kiswahili ili kuondoa matabaka ambayo ayanaweza kujitokeza sekondari. 

SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi

“Ni kweli kuna suala kubwa sana la haki, na kwenye elimu, pengine kuliko maeneo mengine yote, suala la haki ni muhimu [kwani] lipo kwenye moyo kabisa wa utoaji wa elimu kwa haki,” alieleza Mkenda.

“Mtoto aliyezaliwa katika kaya maskini apate fursa sawa na yule ambaye anatoka kaya tajiri [lakini] hatujafika huko, pengine itachukua miaka chungu nzima kufika huko, lakini siku zote lazima kuna suala hilo la kufanya.

“Sasa, kazi ambayo inafanyika ni kuongeza uwekezaji katika shule za umma na kuhakikisha kwamba tunaongeza ubora kadri tunavyokwenda. Kama tukifundisha Kiingereza vizuri kama mitaala yetu inavyokwenda [itakuwa] huwezi kumaliza darasa la sita [mwaka 2027] utoke pale ushindwe kuzungumza Kiingereza,” Profesa Mkenda anafafanua.  

Kwa sasa Serikali imekuwa ikiendesha elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita bila wazazi kuchangia ada kwa kiasi chochote. Hata hivyo, kwenye shule hizi za Serikali za Kiingereza wazazi wamekuwa wakitakiwa kuchangia kiasi cha Shilingi 400,000 ambacho hulipwa kila mwaka. 

Profesa Mkenda amedai kuwa utaratibu huo wa kulipa ada haumuathiri mzazi yoyote ambaye yupo karibu na shule hiyo na hakuna shule nyingine ya Serikali ya Kiswahili, kwani atakubaliwa kumpeleka mtoto wake hapo na hatalazimishwa kulia ada. 

“Mara nyingi ni wazazi wenyewe wote kwa umoja wao [wanakuwa] wamekubaliana, wamehimizana, wamekubaliana kwamba tunataka hii [shule] iwe ‘English Medium’ na tunachangia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata walimu wa ziada,” alisema Mkenda.

“Msingi mkubwa ni lazima kuwe na chaguzi kwa mzazi ambaye hataki kuchangia,” aliongeza kiongozi huyo. “Kama shule ndiyo hiyo pekee iliyopo kwenye eneo lile, hakuna shule ya karibu, hakuna chaguo lingine kwa mzazi la kumpeleka mtoto shule, hatuwezi kukataa mtoto asiende shule kwa sababu hajalipa [ada].”

Modesta Mwambene ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mbeya. Anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com. Habari imehaririwa na Lukelo Francis.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *