The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mkenda: Vyuo Vikuu Vinahitaji Kweli Mijadala, Lakini Siyo ya Kiharakati Pekee

Mkenda: Vyuo Vikuu Vinahitaji Kweli Mijadala, Lakini Siyo ya Kiharakati Pekee

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amekubaliana na madai ya wanazuoni mbalimbali hapa nchini ya kuwa suala la mijadala kwenye vyuo vikuu limekufa, lakini ameipinga hoja ya kuwa Serikali imehusika katika mchakato huo.

Kwa mujibu wa Mkenda, moja ya sababu iliyopelekea mijadala kufa ni kasi ya Serikali ya kuongeza fursa za elimu ili kuendana na ubora unaotakiwa baada ya idadi ya wanafunzi waliokuwa wanahitaji kwenda vyuo vikuu kuongezeka.

Aidha, sababu nyingine ni mabadiliko yaliyofanywa kwenye mfumo wa elimu hapa nchini, akitolea mfano suala la kuanzishwa kwa utaratibu wa wanafunzi kusoma na kufanya mitihani kwa semista, tofauti na hapo awali wanafunzi walivyokuwa wakisoma na kufanya mitihani kila mwisho wa mwaka wa masomo.  

Profesa Mkenda anadai kuwa hali hiyo imepelekea wanafunzi kutumia muda wao mwingi kusoma kwa ajili ya kufanya mitihani na hivyo kukosa muda wa kujumuika na kufanya mijadala kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. 

“Serikali haizuii watu wasiwe na fikra tunduizi,” Profesa Mkenda aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika Aprili 13, 2024, katika ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam kabla ya kufanyika kwa hafla utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu. 

SOMA ZAIDI: Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha

“Maslahi ya dola ni kuwa na jamii iliyoelimika vizuri,” aliongeza, akijibu swali endapo kama kukosekana huko kwa mijadala vyuo vikuu ni sehemu ya mikakati ya makusudi ya Serikali. “Serikali ambayo isingependa watu waelimike sana isingepanua wigo wa elimu.” 

“Unapomfikisha kijana mpaka chuo kikuu, matumaini yake katika jamii ni makubwa sana,” aliongeza Mbunge huyo wa Rombo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). “Kwa vyovyote vile utakavyofikiria, kwa aina ya elimu inayotolewa, unatarajia anaporudi mtaani matumaini yake yapoje na maana yake kisiasa ni nini? Kama dola ingependa kweli kudhibiti ingezuia watu wengi wasiende vyuo vikuu.”

Malalamiko

Kauli hiyo ya waziri mwenye dhamana ya elimu Tanzania inakuja wakati ambapo watu kadhaa, wakiwemo wanazuoni mashuhuri, wamelalamikia kukosekana kwa mijadala vyuo vikuu, hali ambayo wamekuwa wakidai si nzuri kwa hatma ya Tanzania kama taifa.

Mmoja kati ya wadau ambao kwa kiasi kikubwa amekuwa akisononeshwa na hali hiyo ni mwandishi wa habari mkongwe hapa nchini, Jenerali Ulimwengu, ambaye, akitolea mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amekuwa akieleza kutoridhishwa na hali inayoendelea vyuo vikuu Tanzania.

“[UDSM ilikuwa] ni mahali ambapo akili yako inawekwa ndani ya ‘pressure cooker’ kwa muda wa miaka mitatu,” alisema Ulimwengu kwenye kipindi chake cha Jenerali Ulimwengu Exclusive on The Chanzo cha Januari 21, 2024.

SOMA ZAIDI: Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe

“Na kila wiki kuna majadiliano,” aliongeza Ulimwengu ambaye pia ni wakili. “Ukumbi wa Sanaa namba fulani wanakuja wapigania uhuru kutoka ANC kutoka FRELIMO, kutoka PAGC, kutoka wapi, Black Panthers kutoka Marekani wako hapo, hiyo ndiyo chuo kikuu. Chuo kikuu unaweka kama sekondari unawambia namna ya kufikiri hicho siyo chuo kikuu ni kidato cha kumi.”

Ulimwengu aliendelea kukosoa mfumo uliopo na kufikia hatua ya kusema kuwa UDSM imegeuka kuwa extended high school, kauli iliyozua mjadala mpana kwenye nyanja za kiuwanazuoni na kitaifa kwa ujumla.

Mtu mwingine ambaye amekuwa mstari wa mbele kwenye kukosoa hali hiyo ni Profesa Issa Shivji, gwiji la sheria barani Afrika, ambaye mara kwa mara amekuwa akisikitikia hali ya kutokuwepo kwa mijadala vyuo vikuu, akieleza wasiwasi wake kwamba taifa haliwezi kujengwa bila watu kujadili.

Akizungumza katika mdahalo wa kitaifa wa kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, uliofanyika Aprili 8, 2024, katika Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro, Shivji alieleza kuwa enzi za uhai wake kiongozi huyo alisisitiza wasomi kufanya na kuongoza mijadala kwa ajili ya maendeleo. 

Akinukuu moja kati ya kauli maarufu za Sokoine, Shivji alisema: “Hakuna mtu mwenye kauli ya mwisho juu ya mtazamo wa maendeleo. Muelekeo wa maendeleo sahihi na ule unaofaa katika mazingira ya nchi yanatokana na mijadala. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa mijadala.”

SOMA ZAIDI: Tuongee Kuhusu Shahada za Udaktari wa Heshima

“Kwa sababu mbalimbali katika miongo mitatu hivi mijadala imekufa, mijadala ya kitaifa, mijadala katika vyuo vikuu vyetu,” alisema Shivji baada ya kumaliza kunukuu. “Siwezi nikaangazia kwenye sababu zake lakini ukweli sijui kama leo Sokoine angefufuka angesema nini, labda angesusia kuja chuoni kabisa.”

Mijadala anuwai

Lakini kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Mkenda alionesha kukubaliana na tathmini za wale wanaokosoa kukosekana kwa mijadala vyuo vikuu, akikiri kwamba ni hali inayopaswa kurekebishwa.

Hata hivyo, Mkenda alitahadharisha kwamba mijadala haipaswi kuwa ya kisiasa na kiharakati tu, akihimiza uwepo wa mijadala anuwai kwani Tanzania inayo matatizo mengi ambayo yanahitaji kujadiliwa ili kutafuta suluhu zake. 

“Bado tunadhani kwamba, kumuelimisha mtu akaelewa, akawa na fikra tunduizi, tunafikiria kisiasa tu,”  anasema Mkenda kwenye mahojiano yake hayo na The Chanzo

“Hatufikirii elimu tiba, kwa mfano, na nadhani hiyo ndiyo changamoto nyingine vilevile,” aliongeza mhadhiri huyo wa zamani wa chuo kikuu. “Watu wanaposema hakuna mijadala ya kutosha, wanafikiria mijadala ya kisiasa tu, lakini vyuo vikuu ni sehemu za kuzalisha uelewa mpana zaidi.”

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com. Habari hii imehaririwa na Lukelo Francis.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *