The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe

Apigia chapuo Kiingereza kutumika kama lugha ya kufundishia, akisema ni muhimu kwa Watanzania kujifunza lugha nyingi za kigeni kadiri inavyowezekana.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chama cha Mapinduzi – CCM), Profesa Kitila Mkumbo, ameichambua Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, ambapo licha ya kuipongeza amebainisha maeneo ya kuboresha.

Mkumbo, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu nchini Tanzania, alitoa tathmini hiyo alipofanya mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika nyumbani kwake hivi karibuni, ambapo, pamoja na mambo mengine, aligusia kuhusu mjadala tata wa lugha ya kufundishia.

Hapa Profesa Mkumbo anaanza kwa kutoa maoni yake ya ujumla kuhusu rasimu hiyo:

Kitila Mkumbo: Moja, ni vizuri tukatambua-. Kwanza, nishukuru, kama nilivyosema awali, nashukuru sana kwa kuweza kunipa fursa hii ya kutoa maoni yangu kwenye jambo hili kubwa na la maana sana katika nchi yetu. Kwanza, hii ni sera ya tatu tangu nchi yetu ipate uhuru. 

Sera ya kwanza ni ya mwaka 1995. Na sera hii ya [mwaka] 1995 ilijaribu kurekebisha mfumo wa elimu wa kikoloni, na ndiyo yalikuwa maudhui yake makubwa, na pili ilikuwa ni kupanua elimu ya sekondari. Kabla ya hapo elimu ya sekondari ilikuwa finyu sana nchini Tanzania ambayo imetuhudumia. 

Na msingi wake ilikuwa ni taarifa ya, au ripoti ya tume maalum ya Rais, maarufu sana hapa Tanzania kama Tume ya Makweta, ndiyo iliyozaa Sera ya Elimu ya mwaka 1995. Ilifanya utafiti mkubwa kwenye mambo mengi sana hapa Tanzania, ndiyo itakutupa hiyo sera. Sera ambayo tumekaanayo kwa takribani miaka karibu 20. Tukaja tukaibadilisha sera ya elimu mwaka 2014.

Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ilikuwa na maudhui mengi lakini kubwa kuliko yote ilikuwa ni kuifanya elimu ya msingi, kwa maana elimu msingi, badala ya kuwa miaka saba iwe miaka 11. Kwa maana kwamba watoto wetu 2014 kuanzia mwaka 2021 ilikuwa wasiishie darasa la saba waende mpaka kidato cha nne. Hayo ndiyo yalikuwa madhui makubwa. Na ili kufanya vile, sera ya mwaka 2014 ikafuta ada ya kidato cha nne. 

Hayo ndiyo maudhui makubwa sana kwenye ya sera ya mwaka 2014 na pengine la tatu la maana ni kwamba ilipunguza miaka ya elimu ya msingi kutoka miaka saba kwenda miaka sita. Na ikapunguza umri wa kuanza shule, badala ya kuanza shule na miaka saba utaanza ukiwa na miaka sita. Kwa hiyo, huo ndiyo msingi wa sera ya mwaka 2014 mambo hayo mawili matatu makubwa. 

Tulivyokuwa tumekubaliana kipindi kile ilikuwa ni kwamba utekelezaji wake rasmi uwe umekamilika au umeanza ifikapo mwaka 2021. Ilikuwa inamaanisha kwamba ifikapo 2021 watoto wote wanaoingia shule ya msingi wangeenda moja kwa moja mpaka shule za sekondari, bila kikwazo. Na kulikuwa na mambo ambayo yaliwekwa. 

Bahati mbaya, ilivyofika mwaka 2021, hapakuwa na maandalizi ya maana yale ambayo yalikubaliwa. Kwa hivyo, ile sera kimsingi haijawahi kutekelezwa. Kwa hiyo, tukaendelea kuwa katika sera ya mwaka 1995 kwa maana ya kuendelea kubakia elimu ya msingi miaka saba. Kitu pekee ambacho kilitekelezwa ilikuwa ni kuondoa ada ya kidato cha nne. 

Kwa hiyo, hii sera ya tatu [ya elimu] kimsingi siyo mpya. Ndiyo maana pale imeandikwa marejeo, tuseme ‘revised’ ya sera ya 2014. Kwa hiyo, hii siyo sera mpya. Na kitu pekee ambacho kimebadilika ni kimoja tu. Sera imebakisha mambo yote ya 2014, imebadilisha jambo moja kubwa, au mawili. 

La kwanza, imeamua kuingiza elimu amali, mafunzo ya amali, ambapo tumekopa lugha kutoka Zanzibar. Kimsingi ni mafunzo ya elimu ya ufundi. Ndiyo imeingizwa [kwenye sera] kwamba elimu ya jumla inaenda sambamba na elimu ya mafunzo ya amali. 

La pili, imebeba yaleyale ya mwaka 2014, kwamba elimu yetu ya msingi itakwenda mpaka kidato cha nne badala ya kuishia elimu ya darasa la saba. Watoto wataanza shule wakiwa na [umri wa] miaka sita. 

Pengine kidogo ambacho kimebadilika ni kwamba ile sera ya mwaka [19]95 na 2014, elimu ya msingi, elimu msingi kwa maana ya ‘basic education’ ilihusisha pia elimu ya awali, ile miaka miwili ya elimu ya awali. Safari hii sera ilivyo, kama [Serikali] hawatakubaliana na maoni ya wadau, ni kwamba elimu ya awali haitakuwa sehemu ya lazima, [jambo] ambalo kidogo ni kurudi nyuma. 

Lakini huwezi kuijadili hii [rasimu ya sera] bila ya kuijadili mitaala mipya ambayo inaendana na sera hii. Kwa hiyo, kwenye mitaala mipya idadi ya masomo imepunguzwa sana. Zamani tulikuwa tunasoma masomo ya lazima masomo tisa. Sasa, kwa sera mpya, hayazidi masomo sita. 

Kwa hiyo, nadhani hayo ni mabadiliko makubwa. Imeingizwa somo la biashara kama somo la lazima. Lakini pia watoto watasoma somo la kilimo, kuakisi hali halisi ya taifa kwa sasa. Kwa hiyo, nadhani, kwa maana ya tathmini ya haraka, ni kwamba sera mpya imeboresha sana sera ya zamani na mitaala mipya, ikitekelezwa, itakuwa bora kuliko ya zamani.

The Chanzo: Na kuna hili pia la kwamba shule ya msingi sijui kama ni sasa itaishia darasa la sita. Nilikuwa nawaza kwa sababu Zanzibar, kwa sababu suala la shule ya msingi elimu ya msingi siyo suala la muungano, Zanzibar walikuja na hilo na wakatekeleza lakini, kama niko sahihi, walibadilisha tena wakarudi darasa la saba.

Kitila Mkumbo: Na walibadilisha kuwafuata [Tanzania] Bara, hapakuwa na sababu zozote za kisayansi. Walibadilisha kwa kuwafuata Bara. Na Bara nao wanakwenda darasa la sita. Itabidi waje huku tena. 

Lakini, hoja ya msingi ni kwamba hii miaka sita inatekelezeka tu kama tutakuwa na uwezo wa kupeleka watoto mpaka kidato cha nne. Kama hawaendi kidato cha nne itakuwa haina maana kwa sababu watoto watamaliza shule wakiwa bado wadogo mno. 

Utamtoa mtoto shule akiwa na [umri wa] miaka 14 ili afanye nini? Kwa hivyo, kama Serikali itakuwa haina uwezo wa kuweka miundombinu, kwa maana ya miundombinu tunayoifahamu ya vifaa na miundombinu kwa maana ya rasilimali watu, itabidi tuendelee na miaka saba. 

Hii sera inatekelezaka tu na ni ya maana kama [mtoto] atakwenda mpaka kidato cha nne. Tusipoenda haina maana yoyote kwa sababu tutawatoa watoto katika mfumo wa elimu wakiwa bado [ni] wadogo mno, wataenda kufanya nini [mtaani]?

The Chanzo: Sawa sawa. Labda pengine na hili ni suala ambalo wewe umelizungumza bungeni, suala la lugha ya kufundishia. Kwa sababu hii rasimu inasema kwamba lugha ya kufundishia kuanzia masomo ya sekondari itakuwa ni Kiingereza. Kiswahili kitatumika kwenye baadhi ya masomo na kwa shule ya msingi. Kuna mambo mengine hapo umezungumza kama shule itaomba kutumia lugha hii na hii. Na wewe umezungumza bungeni kuonesha kwamba unaunga mkono hilo jambo japo kwamba ulitoa pendekezo tuwe na walimu wengi wa Kiingereza. Mimi nilikuwa nataka kufahamu haya maoni ya Serikali na maoni yako kama mtalaam lakini pia kama mwakilishi wa wananchi, yanatokana na nini? Yaani je, Serikali kuna utafiti inautegemea kwenye kuja kwenye kufanya tamko kama hili la kisera kama hiyo, au wewe kama mbunge ambaye unazungumza kwamba ni jambo sahihi watoto wafundishwe kwa lugha ya Kiingereza. Haya maoni yenu yanatokana na nini?

Kitila Mkumbo: Yanatokana na mambo mengi. Kwanza twende kwenye msingi. Moja, lugha ni nyenzo muhimu sana ya kusaka na kusambaza maarifa, hilo halina ubishi. Pili, [ni] muhimu watoto na walimu watumie lugha ambayo wanaimudu. 

Lugha ambayo wanaitumia lazima waimudu ili waweze kuitumia katika kusaka [na] kutafuta maarifa na kuyasambaza kwa sababu ndiyo maana ya elimu. Elimu ni kusaka maarifa na kuyasambaza. Kwa hiyo, hili halina shaka. 

Jambo la tatu, Tanzania, sera yetu ya lugha kimsingi, kwa miaka mingi, tunasema lugha ya taifa ni Kiswahili [na] lugha rasmi Tanzania ni mbili, Kiswahili na Kiingereza na ndiyo imekuwa hivyo. Kwa hivyo, na tangu tuanze mfumo wetu wa elimu upo hivyo, tulianza na Kiingereza sisi mwaka 1950 mpaka 1960 tulikuwa tunatumia katika elimu yetu Kiingereza. 

Tukajakubadilisha 1967 baada ya ya Azimio la Arusha, ndiyo tukasema tutatumia Kiswahili kwenye elimu ya awali na elimu ya msingi [na] tutatumia Kiingereza kuanzia elimu ya sekondari na kwenda mbele. Kwa hivyo, kutumia Kiingereza siyo kitu kipya, kimekuwepo. Kwa hiyo, unajaribu kurekebisha nini, kuna tatizo? Ndiyo hoja ya msingi hapo. 

Je, kitu gani kimeharibika mpaka tuweze [kukirekebisha]? Kwa hiyo, moja, kwa upande wangu mimi, moja, sioni sababu ya kubadilisha kwa sababu inayotolewa ni moja tu kwamba watoto na walimu wa Kitanzania hawaimudu lugha ya Kiingereza. 

Na hoja yangu ni kwamba lugha ya Kiingereza, kama ilivyo Kiswahili, kama ilivyo Kinyiramba, kama ilivyo Kifaransa, unajifunza, huzaliwi nayo. Kwa hivyo, kama hawaimudu, wafundishwe ili waitumie. Hiyo ndiyo hoja yangu ya kwanza. 

Ya pili mimi naamini kwamba hapa Tanzania sisi tuna faida, [kwamba] tuna Kiswahili, tuna Kiingereza na lugha zingine, na lugha za kikabila. Kwa hiyo, tuione hii kama faida. Hatupaswi kuipoteza hiyo faida. 

Kwa hiyo, maarifa hapa Tanzania lazima yapatikane kwa lugha mbili, kwa kuanzia, Kiswahili na Kiingereza, maarifa yapatikane. Mpaka nimeenda, nimepiga hatua kwamba hata kitabu, kwa mfano, “Abbot,” kitabu maarufu katika Fizikia, kiwepo katika lugha ya Kiingereza [na] kiwepo katika lugha ya Kiswahili, kiasi kwamba mwanafunzi anaposoma akiona Kiingereza kinambabaisha, anafungua kwenye Kiswahili inasema nini? Akiona kwenye kiswahili Archimedes Principle haielewi, afungue kwa [Kiingereza] aione. Hii ni faida ambayo tunapaswa kuikumbatia, tuwe nayo.

The Chanzo: Lakini huo siyo muelekeo wa Serikali.

Kitila Mkumbo: Ndiyo naenda huko. Wenzetu Afrika Kusini wana lugha rasmi 11 za kutumika kwenye elimu na mwanafunzi anaruhusiwa kutumia yoyote. Hatua ambayo nimepiga nimesema lugha isiwe kikwazo. Kwa hiyo, hata nikitoa mtihani, siyo, mwanafunzi aseme, akitaka kujibu mtihani kwa Kiswahili apewe, akitaka kujibu mtihani kwa Kiingereza, apewe.

Kwa hiyo, mimi hoja yangu ni kwamba hatupaswi kuwawekea mipaka wanafunzi wa Tanzania kwamba eti lazima watumie Kiswahili tu, hapana. Eti lazima watumie Kiingereza tu. Hii ni kupoteza msingi ambao tunao, ambao ni wa faida ya kuwa na lugha mbili zote. 

Kwa hivyo, sera mpya imepiga hatua. Imesema, tutatumia Kiswahili kuanzia elimu ya awali na elimu ya msingi. Hata hivyo, shule ambayo inataka kutumia Kiingereza kuanzia mwanzo, inaruhusiwa kuomba na Kamishna wa Elimu atamruhusu. Kuanzia sekondari, utatumia Kiingereza kufundishia, mpaka chuo kikuu. 

Hata hivyo, kama kuna shule, ama kuna chuo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikiamua tunataka kutumia Kiswahili [kufundishia], kitaomba na kitaruhusiwa [kufanya hivyo]. Kwa hiyo, hiyo ni hatua kubwa sana. Ni mageuzi makubwa mno. Kwa hivyo, mimi nadhani hili tulichukue. 

La tatu ambalo nimesema ni lazima tukiri tuna udhaifu sisi wa ufundishaji wa lugha ya Kiingereza. Tuna changamoto ya mambo mawili. Tuna changamoto ya walimu na tuna changamoto ya mazingira. Walimu kwa maana kwamba walimu wetu wengi – hakuna shaka, kumeshafanyika utafiti – wana udhaifu wa lugha ya Kiingereza kwenye kuifundisha. 

Kwa hiyo, nikatoa ufumbuzi kwamba tunahitaji kwa muda fulani, tuna faida hapa ya uwepo wa Soko Huru la Afrika Mashariki ambalo linaruhusu, pamoja na mambo mengine, linaruhusu kubadilishana watumishi, mfanyakazi anaweza akatoka Kenya [na] na atanzania akaenda Kenya. Kwa hiyo, wenzetu Wakenya [na] Waganda wana uwafadhali kwenye lugha ya Kiingereza. Kwa hiyo, wana walimu wengi kuliko sisi. Waruhusiwe kuja kufundisha hapa. 

Huko [Uganda, Rais Yoweri] Museveni ameamua kuanza kufundisha somo la Kiswahili, atatoa wapi walimu wa Kiswahili? Watatoka Tanzania wakafundishe Kiswahili kule Uganda, wakafundishe kiswahili Rwanda. Kwa hiyo, tutumie faida ya hii hali. Miaka mitano mpaka kumi tutakuwa tumeshakuwa na walimu wa kutosha [wa Kiingereza]. 

La pili la mazingira. Hapa Tanzania tulikuwa na mazingira mazuri ya matumizi ya lugha, maana yake Kiswahili kinatumika na Kiingereza kinatumika. Hapa katikati sijui kitu gani kikatokea tukaanza kuzuia matumizi ya Kiingereza kwenye jamii. Kwa hiyo, tukaanza kuweka mipaka Kiingereza kisitumike, ukishafanya hivyo unaua lugha. 

Kama, kwa mfano, tulikuwa tuna hata kwenye vyuo vikuu tulikuwa tunaweza kutumia midahalo kwa Kiswahili kwa Kiingereza. Lakini siku hizi wanatumia zaidi Kiswahili. Hata barua ulikuwa unaweza ukaandika barua kwa Kiswahili [au] Kiingereza, unaamua inategemeana. Siku hizi ikaanza kupitishwa semina kwamba usitumie Kiingereza. 

Kwenye midahalo utakuta watu wamekaa wanazungumza wanawafanya Watanzania wote hawajui Kiingereza kwamba wanaende kutafsiriwa. Unakaa unatafsiri wakati tunafamu sisi watoto wa Kitanzania wanasoma Kiingereza kuanzia shule ya msingi moja kwa moja mpaka chuo kikuu, unamtafsiria nani?

Kwa hivyo, lazima mazingira ya lugha yawepo ili watu waweze kujifunza. Kwa hiyo, mimi hizo ndiyo hoja zangu za msingi. Kwa nini hii naiona kwamba hakuna sababu ya kubadilisha.

The Chanzo: Kitu kinachoshangaza miongoni mwa wadau, hata mimi mwenyewe binafsi, ni kwamba hii sera inasema kwamba – rasimu – inasema kwamba lugha ya kufundishia itakuwa ni Kiingereza, na umezungumza kwamba kama kuna shule, au taasisi, itataka kutumia Kiswahili ni rukhsa, sera imeruhusu. Lakini kinachoshangaza ni kwamba hii rasimu inasema kwamba tunatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia isipokuwa somo la Maadili na Historia ya Tanzania. Sasa huoni kama huo ni mkanganyiko?

Kitila Mkumbo: Nadhani Serikali inatakiwa itoe maelezo kwa nini. Lakini [kwa] fikra zangu nadhani ni uamuzi sahihi kwa sababu Historia ya Tanzania tutaenda kujifunza mambo ya Kitanzania, yanayohusu Tanzania. Mambo ambayo hatuhitaji kutafsiri kwenda kupeleka Kiingereza, tutaenda kujifunza huko sijui mababu zetu wapi huko Songea siyo?

Badala ya kuanza kupambana kutafsiri kutoka kwenye lugha ile ya kwao ya Kiswahili au sijui lugha gani kule Songea kupeleka Kiingereza hatuna sababu. Kwa hiyo, tusema ile mambo ya asili ya Kitanzania tusiwe na wakati na mahangaiko tuanze kutafsiri tutumie lugha yetu moja kwa moja watoto waelewe. Mimi sababu yangu siyo kwa sababu labda hawawezi kuelewa Kiingereza, hapana. 

Nadhani kwamba ni ile kwa sababu tunajifunza mambo ambayo ni ya Kitanzania zaidi, ndiyo maana kunakuwa na historia ya kawaida lakini kutakuwa na historia ya Tanzania na maadili. Kwa hivyo, yale mambo ya Kitanzania ambayo yapo kwa lugha ya Kiswahili moja kwa moja tuwe tunajifunza kwa Kiswahili, hakuna sababu ya kwenda kutafsiri. 

Pili, Maadili. Maadili ni hivyo hivyo. Maadili ni ya Kitanzania, kwa hiyo maadili ya Kitanzania, tunavyotafuta maadili ya Kitanzania tukianza kutafuta maadili ya Wamakonde hatuna sababu twende kule kwa wamakonde au Wamaasai tuanze kupambana kutafsiri kwenda kwenye lugha ya Kiingereza.

Kwa hiyo, tukasema wajifunze moja kwa moja lugha hii. Nadhani hiyo ndiyo mantiki yake. Sidhani eti labda waelewe zaidi, hiyo mimi kwangu sioni kama ni sababu. Sababu ya msingi ni kwamba kwa sababu ni mambo ya ndani ya Watanzania yapo tayari kwenye lugha yao, wajifunze kwa lugha hiyo kuliko Fizikia [au] Kemia ambayo ni ya ulimwengu mzima. 

The Chanzo: Lakini na kilimo, tuna kilimo [kama somo kwenye sera]?

Kitila Mkumbo: Ni hoja nyingine. Lakini kilimo pia ni cha ulimwengu wote. Tukianza kuizungumzia mbolea ni ya ulimwengu mzima, hamna kipya katika hilo. Aina ya mbolea haitakuwa Tanzania, itajulikana duniani kote. Mazao tunayolima kama ni mahindi, kama ni mchele, kama ni maparachichi ni ya ulimwenguni kote. Kwa hiyo, hakuna chochote cha Kitanzania pekee kwenye kilimo.

The Chanzo: Lakini si tunaandika somo ambalo linaakisi uhalisia wa Kitanzania? 

Kitila Mkumbo: Uhalisia ni kwamba watakapokuwa wanajifunza kahawa ni kama ilivyo Burundi, kama ilivyo Kenya. Sioni sababu kwa nini kilimo ni tamaduni ya Kitanzania ambayo ni sayansi kabisa. 

The Chanzo: Sawa sawa, na tukibaki kwenye hili suala la lugha ya kufundishia … 

Kitila Mkumbo: Najua utakaa muda mrefu sana hapo. 

The Chanzo: Moja kati ya hoja ambayo munaitoa ni kwamba hatuwezi kufundisha Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiingereza ni ya kidunia, soko la ajira, vijana wetu tutawapunguzia wigo wa kupata ajira. Na mimi nikisikia hizi hoja huwa nawaza kama nilivyouliza swali langu la mwanzo, yaani hizi hoja zinakuwa zinajengwa na taarifa gani? Mimi ninavyoona ni kwamba kiingereza kutotumika kama lugha ya kufundishia haimaanishi kwamba isifundishwe kama somo.

Kitila Mkumbo: Hoja iko hivi, watu wanaopigia chapuo Kiswahili wanaitumia sana hiyo hoja. [Kuna] mambo mawili ya msingi. Moja, unajifunza lugha kwa kuitumia. Kwa hivyo, utakapotoa Kiingereza kwamba hukifundishi kama lugha ya kufundishia, hakuna nguvu ya kuitumia. Kuitumia kwenda wapi? 

Kwa hiyo, hata Mwalimu [Julius] Nyerere aliwahi kuisema, nadhani unaifahamu hiyo, ni kwamba mtakapoacha kutumia Kiingereza kitapotea. Kwa hiyo, hoja [ya] kwamba mbona Sweden wapi hawatumii Kiingereza ni mazingira tofauti kabisa. Lakini ya pili ni ukweli kwamba unapoandaa mitaala ya elimu, pamoja na mambo mengine, unazingatia sana matakwa ya wazazi. 

Wadau wa elimu ni wawili wakubwa: Serikali [na] wazazi. Serikali, kwa niaba ya wananchi wote, lakini wazazi kwa niaba ya watoto wao. Kwa hiyo, huwezi kuondoa watoto [au] wazazi kwenye mnyororo wa elimu. Na wazazi Watanzania, tumeshafanya utafiti inajulikana, zaidi ya asilimia 70 ukiwahoji wanataka watoto wao wafundishwe kwa Kiingereza. 

The Chanzo: Kwa nini wanataka hivyo? 

Kitila Mkumbo: Bila shaka wanaamini kwamba watoto wao wakifundishwa kwa Kiingereza watakuwa wanaongeza wigo wa kwenda sehemu mbalimbali na nini na kadhalika kadhalika. 

The Chanzo: Na unaamini hivyo?

Kitila Mkumbo: Wanaamini hivyo.

The Chanzo: Wewe, kama mtaalamu, unaamini hivyo?

Kitila Mkumbo: Kuhusu nini?

The Chanzo: Hicho, kwamba ukisoma Kiingereza, yaani lugha ya kufundishia ikiwa Kiingereza, ndiyo wigo wa watu, vijana, utaongezeka, sijui soko la dunia. Na wewe unaamini hivyo? 

Kitila Mkumbo: [Maoni yangu] siyo muhimu. Muhimu hapo ni kwamba wakitumia watajifunza wataajiriwa kwa Kiingereza. Mimi kwangu hiyo hoja siyo hoja ya msingi. Lakini wazazi maoni yao lazima yazingatiwe. 

The Chanzo: Na unajua profesa kwa nini wazazi wanaamini hivyo? 

Kitila Mkumbo: Kwa nini?

The Chanzo: Kwa sababu ya watu kama nyinyi, kwa sababu mnakipigia propaganda Kiingereza. 

Kitila Mkumbo: Kwa sababu wazazi hawana akili?

The Chanzo: Hapana, kwa sababu mnakipigia propaganda Kiingereza.

Kitila Mkumbo: Mbona nyie mnakipigia Kiswahili [propaganda], kwa nini wasiamini Kiswahili? Kwa sababu mnakipigia kiswahili watu wengi. Kwa nini wasiamini Kiswahili? Wewe unadhani kwa nini waniamini mimi kuliko wewe? Hapana bwana!

Nadhani hapa ni hoja. 

Hoja ya msingi kabisa ni kwamba mimi kwangu hatuna sababu ya kukitupa Kiingereza na nimesema juzi bungeni, Kiingereza kiliacha kuwa lugha ya wakoloni siku nyingi. Waingereza wako milioni 67 tu. Kwa hiyo, Mimi nadhani hapa tujadili Watanzania wazimudu lugha mbili hizi [za Kiswahili na Kiingereza]. 

Kwa sababu hata Kiswahili pia tumeanza kuwa na changamoto. Kiswahili cha Watanzania ni Kiswahili cha kawaida, cha mawasiliano, hii ya kulia ugali, kwenda sokoni, yaani mawasiliano ya kawaida haya. 

Inapokuja kwenye Kiswahili rasmi, tumeanza kuzidiwa na Wakenya. Ndiyo maana, tulifanya usaili hapa kutafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kiswahili [ya] Afrika Mashariki, alishinda Mkenya. Yaani tumeanza kuwa na changamoto hata kwenye lugha rasmi ya Kiswahili, imeanza kuwa changamoto. 

The Chanzo: Siyo kwa sababu tunakipa kipaumbele Kiingereza? 

Kitila Mkumbo: Hapana, siyo kweli. Hata huu usaili tulifanya kwa Kiswahili. Kwa hiyo, nadhani hoja ya msingi hapa [ni kwamba] Watanzania wajifunze lugha. Moja ya udhaifu ambao, kama taifa, lazima tukubali tuna udhaifu wa lugha. Kuanzia lugha yetu wenyewe ya Kiswahili. 

Lakini tuna udhaifu mkubwa zaidi wa kutokutaka kujua lugha za watu wengine. Tupo kama Wamarekani ambao wenyewe wanajifunza Kiingereza tu. Sasa Wamarekani na sisi ni tofauti. Wenyewe bahati nzuri lugha yao ni Kiingereza. Kwa hiyo, hata ukibaki na Kiingereza haikusumbui sana. 

Sisi Watanzania hatuna chaguo. Watoto wetu lazima wajue, hawa [watoto wetu], Kiswahili, wajue Kiingereza na lugha zingine, ikiwemo Kifaransa. Na mini natamani kwamba-. Kuna hoja watu wa lugha [wanasema] kwamba Kiingereza siyo lugha ya pili lakini inapaswa kuwa, inabidi Kiingereza kiwe lugha ya pili. 

Mimi nilipo hapa nyumbani, mimi ni Mnyiramba [na] mke wangu Mchaga. Watoto wangu hawa ni Wanyiramba kwa cheo tu kwa sababu ya kabila la baba yao. Hawajui Kinyiramba hawa. Wanajua Kiswahili [na] wanajua Kiingereza. Sasa utasemaje kwa huyu mtoto Kiingereza siyo lugha yake ya pili? 

Hapana. Huyu kaongea lugha yake ya pili. Lugha ya kwanza Kiswahili, Kiingereza lugha ya pili. Kwa hiyo, tuifanye hivyo iwe hivyo. Tuipe hiyo sifa. Kisha tukiwa na lugha mbili zipo huyu mtoto wangu huyu unayemuoana hapa atakuwa huru. 

Atatumia Kiswahili, atatumia Kiingereza. Hakuna shida. Na tusifanye Kiingereza yaani iwe suala kubwa, ni lugha waikamate basi. 

The Chanzo: Lakini profesa, kung’ang’ania kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia hakutupeleki pahala. 

Kitila Mkumbo: Shida yenu nyie [mnaotetea Kiswahili] mnadhani kwamba kwa kuacha Kiingereza mambo yatakuwa rahisi. 

The Chanzo: Hapana, hatukiachi. 

Kitila Mkumbo: Suala ni kwamba, kwanza Kiswahili kuna kazi ya kufanya. Kwanza kuna miundombinu ya kufanya ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia. Muundombinu wa kwanza ni wa kisaikolojia ili hawa wazazi wote wa Tanzania uwabadilishe kisaikolojia na waelewe kwamba tutakuwa tunasoma kwa Kiswahili na bado wanapata elimu. 

Hiyo ni kazi ya kufanya. Ya pili itabidi tufanye kazi ya kubadilisha dhana zetu ziwe kwa Kiswahili. Hiyo ni kazi pia haitakuwa rahisi. Kwa hiyo, je, tunataka kufanya hayo yote wakati tayari tunashughulikia matatizo yote ya Tanzania ya elimu ambayo ni makubwa? Kuna ubaya gani ukaendelea kuboresha kufundishia Kiingereza watu wakaelewa, wakaendelea kuitumia? 

Mimi nimetoa hoja hiyo lakini yote haya yanawezekana. Lakini kwa sasa nadhani na kwenye wadau tuliokaa nao pale Dodona [kujadili rasimu ya elimu] wengi waliona, walisema ni sawa sera ilivyokaa. 

The Chanzo: Sawa sawa, kama wadau wanasema hivyo mimi ni nani wa kupinga? Labda pengine unadhani kuna namna yoyote ambayo Serikali inaweza ikaiboresha hii rasimu ya sera kwa mtazamo wako? 

Kitila Mkumbo: Yapo mambo ya kuboresha. Kwa mfano, Serikali, rasimu, inasema kwamba elimu ya awali siyo sehemu ya elimu ya lazima. Kosa kubwa kabisa hilo kwa sababu sasa hivi duniani kote tumeshakubaliana, sisi watalaam wa elimu, kwamba msingi wa elimu ni huu wa chini. Ukishakosea hapa, huko mbele utapambana.

Mahojiano haya yametolewa kutoka sauti kwenda maneno na mwandishi wa The Chanzo kutoka Mtwara, Omari Mikoma. Kama una maoni, tuandikie kupitia: editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *