The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha

Taasisi za elimu zisisitize kwenye ujenzi wa Stadi za Karne ya 21 kama ubunifu, fikra tunduizi na utatuzi wa matatizo.

subscribe to our newsletter!

Wakoloni wetu wa zamani – wa zamani tu au tuseme wakoloni wetu? – wana msemo katika lugha yao ya Kiingereza tunayoiabudu hadi leo hii usemamo, more is less, na bila shaka, kinyume chake kipo pia, ambacho ni less is more.

Ingawa misemo hii ilitumika kwanza katika tasnia ya usanifu wa majengo, ni muhimu tuitumie katika kuangalia mwelekeo wa elimu yetu. Naomba nianze na uzoefu wangu.

Nilipokuwa chuo kikuu, tulikuwa hatulazimishwi kuhudhuria mihadhara yoyote. Maprofesa walichagua mada zao ambazo ziliendana au hazikuendana na kozi zetu na sisi tulichagua tulizotaka kusikiliza.

Kwa namna hiyo, ingawa nilikuwa nasoma Kifaransa na Historia, nilihudhuria mihadhara ya siasa, sosholojia, Kiingereza, nakadhalika, na ukweli ni kwamba sikumaliza mihadhara yote ya profesa yeyote. Niliporidhika nimeelewa ninachotaka kuelewa baada ya mihadhara kadhaa, basi, niliacha.

Lakini si kwamba hatukuwa na wajibu wa kusoma. Kila wiki, kwa kila somo, ilibidi kutengeneza insha juu ya mada walizoamua maprofesa wetu wa karibu, kisha kujadiliana nao. Ila hakukuwa na maendeleo ya kila siku.

Hivyo tulikuwa na muda wa kusoma vitu vingine. Nilimsoma Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, nikiwa chuo pamoja na wenzangu wengi kwa kuwa wakati ule Tanzania ilikuwa inatamba kimataifa kwa watu wenye mrengo wa kushoto kutokana na misimamo yake.

Nilisoma sana siasa, historia nje ya kozi zangu, elimu jamii, na mengine mengi ambayo yamenisaidia sana hadi leo. Yaliweka elimu ya msingi nje ya masomo niliyoyasoma na kuyapenda pia. Aidha, niliweza kushiriki michezo kikamilifu, klabu mbalimbali na vuguvugu za kisiasa maana mimi ni kizazi cha mwaka 1968.

SOMA ZAIDI: Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe

Hiyo, kwangu mimi, ndiyo maana ya chuo kikuu. Chuo kikuu siyo shule ya sekondari, ni sehemu ya kupanua mawazo ya kila aina, kusoma vitabu vya kila aina na kushiriki mijadala ya kila aina.

Ndipo mtu anapotoka chuo kikuu anakuwa na fikra tunduizi na unyumbufu wa kuweza kufanya kazi ya kila aina, mtu anayejua mambo mengi na hasahasa anayejua jinsi ya kutafuta na kutathmini mambo mengine.

Sisemi kwamba nilifuzu sana katika hayo lakini najua niliyoyapitia chuoni yamenisaidia sana kutafuta hayo.

Aidha, nilipofika Tanzania na kupewa fursa na heshima kubwa ya kufundisha fasihi katika Kiingereza katika Shule ya Sekondari ya Milambo na baadaye Mzumbe, nilikuta si tu mitaala ya kuchokoza mijadala mizito na fikra tunduizi sana, bali muda wa kutosha wa kujisomea na kutafakari kwa kina.

Tena wanafunzi waliruhusiwa kuingia kwenye mitihani na vitabu vyao maana lengo halikuwa kukariri bali kuchambua.

Wanafunzi waliruhusiwa pia kufanya ‘kazi maalum’ za ubunifu, ambazo zilizalisha baadhi ya waandishi mashuhuri wa nchi yetu na pia za uchambuzi ambazo ziliwalazimisha wanafunzi wasome kwa upana zaidi nje ya vitabu vilivyopangwa kwenye muhtasari.

Na naamini wanafunzi waliiva kweli kutokana na nafasi hizi za kujisomea, kujadili, na kutafakari. Pungufu ya vipindi lilileta ongezeko la kutafakari na kuelewa wa kina – less is more, kumbuka, ambayo naweza kuitafsiri kama kupungezeka.

Mihadhara mingi, ya lazima

Sasa hali ya leo ikoje? Chuo kikuu kuna mihadhara kuanzia alfajiri, hadi usiku, na ole wako usihudhurie.

Tena kila mwanafunzi anapewa mihadhara juu ya somo lile finyu la mhadhiri wake. Atasoma na kufikiri saa ngapi? Kisha tunashangaa mtu anapotoka chuoni bila fikra tunduizi na bila unyumbufu wa kuweza kuajiriwa au kujiajiri.

Ongezeko la mihadhara = punguzo la fikra na uchambuzi – more is less, nilikugusia pale juu, hali ninayoweza kuitafsiri kama kuongepuka.

SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi

Tukishuka sekondari hali ni mbaya zaidi. Katika shule zinazosifiwa sana kwa matokeo mazuri ya NECTA, wanafunzi wanaamshwa saa tisa au saa kumi ili waanze masomo saa kumi na moja na nusu. Kisha usiku wanasoma hadi saa nne au saa tano na hatimaye kulala saa tano au saa sita.

Kwa vyovyote vile, wanafunzi hawa hawapati hata saa sita za usingizi wakati wataalamu wanasema vijalunga, au vijana chipukizi, wanatakiwa kulala kwa muda wa angalau saa saba na hata zaidi.

Ukiongea na wanafunzi na kuwauliza iwapo hawasinzii darasani, wengi wao watakujibu kwamba wanasinzia haswa, na hata wasipoishia kwenye usingizi, akili haipo maana uchovu unatawala!

Kwa vyovyote, more is less, kuongepuka. Kutokana na kukariri, ni kweli wanafaulu mitihani, lakini kwa gharama gani katika afya yao na hata maisha yao ya baadaye?

Sote tuliosoma masomo ya elimu au ya afya, tunajua kwamba mtoto na kijana anahitaji muda wa kutosha kujisomea, kuburudika na kupumzika, na hatimaye kulala vizuri.

Tunajua! Walimu wanajua! Hata wazazi tunajua! Sasa kwa nini hatusimami na kusema hapana? Lazima tukiri kwamba tumevuka mipaka. Tumezidi!

Serikali yapuuzwa

Wizara husika imesema. Tena imetoa maagizo kuhusu saa za kusoma na kupumzika, umuhimu wa mapumziko na burudani katika ukuaji wa mtoto, na umuhimu wa likizo pia, lakini shule, kwa kusikiliza shinikizo la wazazi wanaoangalia matokeo ya mitihani tu, zinapuuza, zinadharau, na hazisikilizi kabisa maagizo ya Serikali.

Tena hapo hatujahesabu pia kwamba hakuna muda wa michezo, na kujisomea mambo mengine, na kujadili, na kufurahia maisha, nakadhalika. Nikisikiliza maelezo ya wanafunzi wa siku hizi naona mara nyingine afadhali jela. Na tukishuka chini hata kwenye shule za msingi na chekechea mambo ni yaleyale.

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Hasa kwenye mwaka wa mtihani, darasa la nne na la saba, watoto wanakuwa waathirika wa mashindano kati ya shule na shule juu ya nani anaweza kupata matokeo mazuri zaidi. Hapa ninapokaa, watoto wa darasa la nne wanatakiwa kuwahi shuleni saa 12 na wanatoka darasani saa mbili za usiku!

Miaka tisa au kumi wanakuwa na siku ya ‘kazi’ ya saa 14. Si kwa sababu ya kuongeza elimu, la hasha! Ni kwa sababu ya mashindano ya shule. Najiuliza, huu ukichaa umetoka wapi?

Ukiwauliza walimu, “Je, hivi ndivyo mlivyofundishwa katika kusomea saikolojia ya elimu?” Hawana jibu zaidi ya kusema, “Ndiyo mpango wetu.” Na chekechea? Chekechea ni sehemu ya kujifunza maadili na stadi za msingi za maisha kwa kucheza, kusomewa hadithi, nakadhalika.

Lakini wapi! Wanapewa ‘homework,’ mitihani, wanakaa kama vile wako chuo kikuu. Au viitwe chuokichea?

Ajabu ni kwamba mtu akiibua suala na kupinga hali hii ya kuongepuka hadi kupukutika kwenye mitandao ya jamii au mikutano na warsha, wengi wanamuunga mkono, lakini katika hali halisi, msukumo wa mfumo tuliouzoea na unaotetewa na wehu wa kutaka watoto wao wafaulu mitihani tu badala ya kuelimika unatawala bado. Kama huniamini, jaribu kupinga mfumo huo katika mkutano wa shule.

Tufanye nini? 

Kwanza lazima sisi wazazi, walimu, wataalamu wa elimu, watunga mitaala na mitihani tuondokane na wazo kwamba more is more. Daima haiwezi kuwa more.

Tujue pia hasa siku hizi kwamba kinachotakiwa siyo tunajua nini na tunakumbuka nini bali tunachambuaje tunachoambiwa na tunatumiaje tunachokijua.

Ndiyo lengo la mitaala ya umahiri ambayo tumekuwa nayo bila kuitumia tangu mwaka 2005. Rasimu mpya ya sera ya elimu inatambua hivyo.

Baada ya kuanzisha mitaala inayosisitiza ujenzi wa umahiri, utaratibu wa upimaji haukubadilishwa kuendana na mabadiliko hayo. Vilevile, hakuna msisitizo kwenye ujenzi wa Stadi za Karne ya 21 kama ubunifu, fikra tunduizi, na utatuzi wa matatizo.

SOMA ZAIDI: Je, Kupata Nafasi ya Shule Ni Kupata Nafasi ya Elimu?

Hivyo basi, ni muhimu kuboresha mfumo wa upimaji kwa kutumia vigezo vinavyotambuliwa vya upimaji wa maendeleo ya kila siku ya mwanafunzi na tathmini ya mwisho ya kukamilisha ngazi husika kwa kuzingatia mtaala wa ujenzi wa umahiri na kukuza Stadi za Karne ya 21.

Naam! Watoto wetu kwa sasa wanatahinishwa badala ya kuelimishwa kisha tunashangaa kwamba hawawezi kushindana katika soko la ajira la humu ndani sembuse la dunia.

Turudi kwenye misingi ya elimu. Tujifunze kwa magwiji wa elimu duniani ambao hawaweki mitihani kabisa mwanzoni ingawa wanatathmini. Tuondoe mashindano kwa kuweka mtindo wa kufaulu/kushindwa ili tupime iwapo mtoto anaweza kupanda hadi darasa linalofuata.

Hii itaondoa mashindano kati ya shule na shule inayowageuza watoto kuwa waathirika wa matakwa ya watu wazima!

Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *