The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Richard Mabala: Je, Kupata Nafasi ya Shule Ni Kupata Nafasi ya Elimu?

Tusiangalie takwimu tu, tujue kwamba kila tarakimu ya mtoto aliyekosa fursa ya kujiendeleza kielimu ni mtoto mwenye ndoto yake.

subscribe to our newsletter!

Kabla ya kuongelea suala la watoto waliokosa nafasi ya shule za sekondari, naomba tutafakari kidogo kuhusu misemo miwili muhimu.  Msemo wa kwanza hutumika sana katika Serikali hii ya awamu ya tano.

Msemo wa kwanza ni ‘Maendeleo hayana chama.’ Ni kweli.  Neno maendeleo lina maana pana.  Linaweza kuhusu uboreshaji wa miundombinu, upanuzi wa huduma za afya, uimarishaji wa haki za binadamu mbele ya vyombo vya usalama, ujenzi wa madarasa nakadhalika.  Vyote hivi ni maendeleo, na haidhuru chama gani kinaviongelea au kuvipigania.

Lakini msemo huu unapaswa kwenda sambamba na msemo wa pili, uliokuwa ukitumiwa sana na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ‘Kupanga ni kuchagua.’

Ukishaanza kuchagua ndipo mawazo tofauti, itikadi tofauti zitaibuka.  Tuseme, kwa mfano, wakati huu wa Krismasi, kama baba, nataka kununua mbuzi kwa ajili ya kusherehekea na ndugu na jamaa zangu, nataka kuwanunulia wote nguo, nataka kutengeneza barabara ya kufika kwetu maana ni mbovu na wengine watashindwa kufika, nataka pia kuweka pesa pembeni kwa ajili ya ada za shule na nataka kununua kuku chotara wengi zaidi kwa ajili ya mradi wangu.

Wakati huu, natakiwa kulipia kadi ya bima ya afya, na bado nina mpango wa kupata usafiri, angalau kabodaboda.  Bila kusahau matumizi ya nyumbani ya kila siku. Vyote ni maendeleo, vyote ni muhimu, ningependa kufanya vyote lakini iwapo sina uwezo wa kutosha, itabidi nichague, na kuchagua kwangu kutategemea kitu gani naona ni muhimu zaidi.  Na bila shaka, mke wangu, na watoto pia wanaweza kuwa na mawazo yanayotofautiana na ya kwangu.  Sasa hapo, naweza kudai kwamba mimi ni kichwa hivyo sina haja ya mawazo ya wengine, au tunaweza kujadiliana ili tuweze kufikia muafaka juu ya vipaumbele vyetu.

Mawazo mbadala siyo usaliti

Hata kiwilaya na kitaifa hali ni ileile.  Ingawa maendeleo hayana chama, vipengele vya maendeleo vinaweza kuwa na chama kabisa, au hata kama havina vyama, angalau vina makundi ya watu wenye mawazo na chaguo mbadala.  Kila chaguo lina uzuri wake na ubaya wake, ndiyo maana anayeleta mawazo mbadala kuhusu vipengele vya maendeleo hatakiwi kuitwa msaliti.  Labda apendekeze kitu ambacho kitasabababisha maangamizi.  Lakini mimi nikiona kutengeneza barabara ya kufikia zahanati ndio maendeleo muhimu na mwenzangu akiona upatikanaji wa dawa ya kutosha kila wakati ni kipaumbele kikuu, hakuna anayeweza kumwita mwenzie msaliti.  Inabidi kukaa chini na kujadili.

Naam.  Kuna tofauti kubwa sana kati ya kuorodhesha na kupanga. Watu wanapenda sana kuorodhesha. Ni raha sana. Kwa mfano, tulipoanzisha mpango shirikishi wa jamii dhidi ya VVU na UKIMWI, kwenye ngazi ya kijiji, walikaa na kuorodhesha vitu vyote walivyoona ni muhimu, ikiwa ni pamoja na magari.  Karibu shilingi bilioni moja kijiji kimoja tu enzi zile.  Lakini tulipowaambia kwamba pesa zilizopo ni shilingi milioni ishirini, hapo ilibidi wakae na kutafakari, kipi muhimu, kipi kinawezekana, kipi kitakuwa na mafanikio zaidi, kipi wanaweza kuchangia wenyewe.   Ilibidi kupima maoni ya watu na makundi mbalimbali.  Mahitaji ya vijana yalikuwa tofauti na mahitaji ya viongozi, kipaumbele cha wanawake kiligongana na kile cha wanaume.  Na katika kukaa na kujadili utatuzi mpya ulipatikana pia na hata kama wote hawakukubaliana mia kwa mia na mpango huo, angalau walifikia muafaka na ari ya kutenda kufanikisha mpango ilikuwa juu sana.

Ndipo nakuja kwenye suala la watoto ambao ndoto yao ya kusoma sekondari inakatwa kutokana na uhaba wa madarasa.  Inawezekana wengi watachukuliwa katika uchaguzi wa pili kwa sababu wengi waliochaguliwa watakuwa wameshaamua bora shule binafsi kuliko za Serikali.  Lakini bado tatizo la upatikanaji wa nafasi ya kujiunga na shule ya sekondari ya Serikali upo.  Tusiangalie takwimu tu, tujue kwamba kila tarakimu ni mtoto mwenye ndoto yake.

Hata hivyo, haitoshi kuangalia shimo moja tu katika barabara wakati lami yake imeshaonesha kushindwa kuhimili magari.  Sijui kama, katika kuwapanga watoto katika shule, walizingatia kanuni za Wizara ya Elimu kuhusu idadi ya wanafunzi inayotakiwa katika darasa moja. Nina mashaka maana kila ukiongea na walimu utakuta kwamba mara nyingi darasa moja lina wanafunzi sabini na hata zaidi.  Hapa, ingawa wamepata nafasi ya shule, wamepata kweli nafasi ya elimu?  Vivyohivyo kwa idadi ya vitabu vilivyopo, idadi ya walimu, kuwepo kwa maabara na maktaba na kadhalika.  Mimi sidhani kama wazazi wote wanaokimbilia shule binafsi wanaangalia tu suala la lugha, wanataka watoto wao wakae katika mazingira bora ya elimu.

Lugha ya kufundishia inavyowachenga wanafunzi

Pamoja na hayo, tukiwa tunaongelea suala la elimu, siwezi kunyamazia suala la lugha.  Mwanangu amepata nafasi ya shule, heko Serikali.  Nikimwona amekaa darasani na wenzie, hata kama wamerundikana, moyo wangu unafurahi, najivunia. Lakini kumbe ingawa amekaa darasani, na ana hamu ya kusoma, anatoka kapa kila siku maana lugha ya kufundishia inamchenga moja kwa moja.  Anarudi kila siku akiwa hana raha maana haelewi, anajaribu kukariri lakini haelewi na anajiona anafeli tu kila siku.  Siku mojamoja anarudi anafurahi kwa sababu mwalimu aliamua kufundisha na hata kutoa mtihani kwa lugha wanayoielewa lakini bado naona ari yake inashuka siku hadi siku.  Ana nafasi ya shule lakini nafasi ya elimu kweli anayo?

Lakini bora mimi.  Angalau binti yangu anaweza kurudi kila jioni na tunakaa naye.  Tunajua anapambana kila siku na waovu wanaotaka kumharibia maisha yake lakini kaka yake anajitahidi kumsindikiza kila siku hadi kupita maeneo ya hatari na jioni na kumpokea pia akitoka shuleni. Kila siku!  Lakini jirani yangu analalamika sana maana mwanaye amepangwa shule ya mbali zaidi hivyo, ili atumie vizuri nafasi yake ya shule lazima apange chumba karibu na shule.  Nasikia shule nyingi sana zina ‘geto’ zao. Ingawa wanafunzi wanaziita eti bangaloo, kama vile wanakaa sawa na wanene wetu wenye mahekalu ya fahari.

Lakini ubunifu na utundu hauwezi kufunika hali halisi ya maisha yao pale, hali duni, hali hatarishi inayotishia elimu yao, ndoto zao na maisha yao.  Bado ni watoto, wanahitaji malezi na matunzo, wanakua na kuhitaji chakula cha kutosha lakini wazazi wanashindwa kutimiza mahitaji yao wakiwa mbali nao. Ndipo vishawishi na hata matumizi ya nguvu yanaingia na nafasi yao ya shule badala ya kujenga maisha yao huishia kuyabomoa.

Najua kwamba tukitaka kuongelea suala la elimu yapo mengi mengi mengi, mitaala inayoendana na hali halisi ya dunia ya leo, maandalizi ya walimu, hadhi ya walimu katika jamii na mazingira yao ya kazi, mazingira rafiki ya elimu ndani ya shule na kadhalika. Ndiyo maana wengi wamependekeza tuwe na mjadala mzito kuhusu mustakabali wa elimu nchi mwetu, mjadala utakaowashirikisha wadau wote bila kujali itikadi yao au rangi ya nguo zao. Mimi hapo juu nimetaja machache tu ambayo huonesha kwamba nafasi ya shule peke yake haitoshi kupata elimu.  Wizara yetu ya elimu imeainisha yenyewe viwango vya msingi kabisa ili elimu ipatikane.  Chini ya hapo, elimu inashindwa kupenya kwa watoto walio wengi.  Daima namkumbuka binti mmoja niliyekutana naye huko Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi kabla ya awamu hii.  Binti huyu alimaliza la saba tu na tayari ameanzisha biashara yake ya samaki.

Kaniambia: “Nikiwaangalia wenzangu walioenda sekondari, namshukuru Mungu sana kwamba sikuchaguliwa. Ningependa kupata elimu zaidi lakini unaona nilivyojiwekea misingi ya maisha. Wenzangu wengi walipata mimba kwenye mageto yao ili waende shule na hata wasioishia njiani wametoka na sifuri na bila stadi au ujuzi wa kuweza kujiendeleza kimaisha.  Naona wengi wamerudi nyuma.”

Na hapo narudi kwenye misemo ile miwili ya awali.  Maendeleo ya elimu hayana chama.  Kuna orodha ndefu ya vitu vinavyohitajika ili nafasi ya shule iwe kweli nafasi ya elimu.  Lakini katika hali halisi, kupanga ni kuchagua.  Tumewekea elimu kipaumbele kiasi gani mbele na vipaumbele vingine kibajeti, kimipango na kadhalika?  Maana bila bajeti mengine ni ndoto.  Na pili ndani ya elimu tumewekea kipaumbele mambo gani ili watoto wetu waendelee na taifa letu lifaidike na kuendelea kutokana na elimu yao?

Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu mbali mbali ikiwemo Mabala the Farmer na Hawa the Bus Driver. Anapatikana kupitia barua anuani yake ya pepe yake ambayo ni rmabala@yahoo.com au kupitia ukurasa wake wa Twitter @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative.

 

One Response

  1. Elimu si kipaumbele serikalini. Haina faida katika muda mfupi, pia, watawala wanatishika kwamba watu wengi wakielimika vizuri wataelewa maovu ya watawala. Zaidi, hata viongozi wenye nia nzuri wanakwamishwa na serikali kutokuwa na mipango inayooana vizuri
    .
    Rais anasema watu wazaane tu, atasomesha. Wakati hali halisi ni kwamba hawezi kusomesha inavyotakiwa. Matokeo yake tunazaana sana kupita uwezo wetu wa kusomesha.
    Hayo madarasa ya wanafunzi 70 miaka michache ijayo yataonekanqa kama anasa.Tutaona madarasa ya wanafunzi zaidi ya 100.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts