The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’

Mwandishi anamchora Kadiri, muhusika wake mkuu, kama baba anayeijali familia yake, muda wote akiwafikiria watoto wake.

subscribe to our newsletter!

Rafiki yangu M husema kuwa kusoma kitabu cha Kiswahili kina raha yake ambayo ni ngumu sana kwa watu ambao hawaijui lugha yetu kuisikia raha hiyo. Kuna namna yaani, unaposoma hadithi kwa lugha yako unahisi kama unaielewa kiundani, tofauti na usomapo kwa Kingereza, au lugha nyingine unayoifahamu. 

Mimi nakubaliana naye kwani Mali ya Maskini, riwaya iliyoandikwa na Zainab Burhani, na kuchapishwa na Longhorn Publishers mwaka 1981, imenipa raha isiyo kifani. Kinasimulia maisha ya Kadiri na familia yake – Imani mke wake, na watoto wao watatu, Ali, Zahara na Rukia.

Mali ya Maskini imenifanya niifikirie riwaya ya Mungu Hakopeshwi iliyoandikwa mwanamke mwengine mwenye jina hilohilo la Zainab, aitwaye Zainab Alwi Baharoon, ambayo, ikiandikwa kwa ustadi mkubwa, iliniachia simanzi kubwa nilipoisoma. 

Japokuwa Baharoon ameandika riwaya yake takribani miaka 30 baadaye, ni kama vile vitabu hivi vipo katika mazungumzo. Vyote vinaangazia familia za Waswahili, malezi, ujana, uwana, ndoa na utamaduni wa ukimya kwa namna tofauti na athari zake.

Mwanaume mwenye pesa zake anapotaka kumchumbia Zahara, kwenye Mali ya Maskini, binti huyo anaonekana kuwa na maamuzi zaidi kuhusu maisha yake mwenyewe kuliko mwenzake Layla, kwenye Mungu Hakopeshwi, ambaye hapewi nafasi ya uchaguzi. 

SOMA ZAIDI: ‘Mapenzi Bora’ ya Shaaban Robert Inavyochambua Maana Pana ya Dhana ‘Mapenzi’

Hata hivyo, katika simulizi zote mbili yupo mtu mmoja ambaye anaathiri uwezo wa mabinti hawa kufanya maamuzi au kutokufanya maamuzi kuhusu maisha yao wao wenyewe; na mtu huyo ni baba.

Waandishi hawa wanaonesha jinsi baba anaweza kujenga au kubomoa maisha ya watoto wake. Uwezo wa mtoto wa kike kuwa na sauti, siyo tu akiwa kwao lakini hata akienda kwa mumewe, hutokana na aina ya malezi, au uongozi wa baba katika familia. 

Kwenye Mali ya Maskini, Kadiri anachorwa kama baba anayeijali familia yake. Muda wote anawafikiria watoto wake. Anajitahidi kuwapa kila wanachokitaka, ikiwemo uhuru wa kuwa na mtu wampendaye.

Kadiri ana uwezo, japokuwa maisha yanayumba kidogo na hali yake ya kifedha inatetereka. Jambo hili linamtikisa kama mwanaume. Hata hivyo, anapotokea mwenye pesa kumzidi ambaye anataka kumuoa binti yake, Kadiri anakuwa mkali kidogo. 

Jambo linalopendeza ni kuwa Kadiri ana urafiki kwa binti yake, hujadiliana naye na kumpa nafasi ya kufanya maamuzi. Hata aliyetaka kumposa huyo tajiri alishangaa juu ya hilo.

SOMA ZAIDI: Tusome ‘Kielezo cha Fasili’ Tujue Jinsi ya Kusoma

“Mimi ni mzee kweli, lakini kuna wengine pia waliohusika; waliomzaa, waliomlea, waliomwangalia, wanaompenda na kumhesabu kuwa ni mtoto wao, ikiwa kwa damu, ikiwa kwa imani. Hao wote wana haki ya kuona kuwa furaha yake au msiba wake ni wao pia.” Kadiri, Ukurasa wa 96.

Msimamo huu ni wa tofauti kabisa na ule wa Ahmed kwenye Mungu Hakopeshwi. Hata katika kumwambia mkewe kuhusu posa ya binti yao, hakuna muungwana. Alikuwa anajifanyisha tu kuwa anajali shauri la mkewe lakini moyoni mwake haikuwa hivyo.

“Kwa hakika alikuwa anamchezea roho yake kwa vijiti tu, hana lolote analohitaji kwake ila kumpa taarifa tu kuwa mtoto wao ameposwa, basi! Hakutaka ushauri wala nasaha. Atakalo yeye ndio huwa…” Ukurasa wa 31.

Na tena mkewe alipotaka mtoto wao aulizwe kuhusu anachotaka, mumewe alimjibu “Aulizwe yeye kama nani?” (Uk. 32). Na ilipokuja kwa wana wao wa kiume, wanaume hawa wawili – Ahmed na Kadiri – walikuwa na msimamo tofauti. Ahmed anamuusia mwanae ya kwamba asiwekee mkazo elimu ya darasani kuliko kufanya biashara.

“Wewe ndiye mtoto wangu wa kiume, ndiye ninayekutegemea. Salah bado mdogo sana na waliokufuatia wote wanawake. Leo nikifa mimi najua nimeacha mtu madhubuti ambaye ataweza kuisimamia nyumba sawasawa.” Ahmed, Mungu Hakopeshwi, Ukurasa wa 14.

SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu

Hata hivyo, Kadiri alikuwa na msimamo tofauti katika jambo hili. Kijana wake Ali alipomfuata baba yake huyo, akimshirikisha uamuzi wake wa kuacha shule ili atafute kazi na kumsaidia baba yake, Kadiri alikataa. Yeye alimtaka mwanae wa kiume asome, akimaliza aajiriwe. 

Hata hivyo, baada ya kuona mwanae anakomalia suala hilo, akamshauri ajifunze ufundi kwa babake mdogo aitwaye Bakari. Alisisitiza kwamba kipato atakachokipata kitakuwa cha kumsaidia yeye mwenyewe, yaani Ali.

Inafikirisha, jinsi ambavyo jamii moja inaweza kuwa na baba aliye kama Kadiri lakini pia ikawa na baba mwengine afananaye na Ahmed. Inafikirisha zaidi kuona ni kwa jinsi gani malezi ya baba haswa yanaweza kumjenga mtoto. 

Mara nyingi tumezoea kuyaangazia malezi ya mama, lakini baba anayo nafasi kubwa sana ya kumjengea mtoto ujasiri, msimamo katika maisha na kuwa sauti itakayomwongoza. 

Inafurahisha kuona kwamba japokuwa vitabu hivi vimepishana kwa takribani miongo mitatu, ni kama vile kimoja ni kioo cha mwengine katika kuakisi nafasi ya baba kwenye familia na kwenye jamii kwa ujumla.


Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. Ester, unaandika vizuri sana. Nimependa upangiliaji wako wa maneno, tungo, vifungu vya maneno na hata moangilio wa mawazo yanayoweze kumjenge msomaji mantiki fuatilishi.

    Wasichofahamu wengi ni kuwa, licha ya Matumizi sahihi ya Lugha, kuna namna ya upangiliaji wa mawazo unaomfanya msomaji aendane na ajili na fikra za mwandishi hadi mwisho. Hatimaye spare hasa like alichokusudia mwandishi kimfikie msomaji.

    Binafsi nastafidi uandishi wako na nastaladhi utamu wa Lugha yako. Hakika unasaza kiu ya usomaji wangu.

    Shukran na ujaaliwe Ubora zaidi.

  2. Ester, unaandika vizuri sana. Nimependa upangiliaji wako wa maneno, tungo, vifungu vya maneno na hata moangilio wa mawazo yanayoweza kumjengea msomaji mantiki fuatilishi.

    Wasichofahamu wengi ni kuwa, licha ya Matumizi sahihi ya Lugha, kuna namna ya upangiliaji wa mawazo unaomfanya msomaji aendane na akili na fikra za mwandishi hadi mwisho. Hatimaye akinase hasa, kile alichokusudia mwandishi kimfikie msomaji wake.

    Binafsi nastafidi uandishi wako na nastaladhi utamu wa Lugha yako. Hakika unasaza kiu ya usomaji wangu.

    Shukran na ujaaliwe Ubora zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *