The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Mapenzi Bora’ ya Shaaban Robert Inavyochambua Maana Pana ya Dhana ‘Mapenzi’

Katika utenzi huu, mwandishi anatukumbusha kwamba mapenzi bora hutupa akili ya namna ya kuenenda.

subscribe to our newsletter!

Nilipokuwa nasoma Shahada ya Uzamili ya Uandishi wa Habari nchini Canada, nilisoma somo moja ambalo sikuwahi kufahamu kuwa watu hulisoma; linaitwa Emotional Geographies kwa Kingereza. 

Ndani ya somo hilo, tulisoma kuhusu hisia mbalimbali – hasira, furaha, aibu, majonzi, upendo – na jinsi ambavyo hisia hizi hujenga msingi wa tuishivyo nyanja mbalimbali, ikiwemo familia, maisha ya akademia, michezo, mahusiano na viumbe vingine kama wanyama, makazi ya watu, sera ya nchi za uhamiaji, siasa, na kadhalika.

Mapenzi ni hisia yenye nguvu kubwa ya mabadiliko kwenye jamii, kuanzia ngazi ya mtu binafsi hata ngazi ya kitaifa na kimataifa. Yupo mwanamuziki aliouambia moyo – sukuma damu si vingine. 

Alitambua kuwa moyo unaweza kukusukuma ukafanya jambo jema, au jambo la hovyo kabisa kama usipojua jinsi ya kushirikiana nao. Kwa hakika, moyo wa mwanadamu ni kitu cha ajabu. Una ulimwengu wake wenyewe ambao kimsingi ndiyo ulimwengu halisi.

Nafikiri kama tusingekuwa na moyo, tusingekuwa wanadamu. Tungekuwa aina fulani ya akili bandia ndani ya miili ambao wanatekeleza ratiba ya kuwepo duniani kila siku – kuamka asubuhi, kwenda kwenye shughuli za siku, kurudi nyumbani, kula na kulala. 

SOMA ZAIDI: Tusome ‘Kielezo cha Fasili’ Tujue Jinsi ya Kusoma

Moyo wenyewe si lolote bila kuwa na hisia ndani yake. Bila huo moyo, tusingekuwa na nguvu ya kutusukuma kuyafikia malengo yetu, kujibidiisha kuwa bora zaidi kuliko jana, au kuwajali wengine na kujijali sisi wenyewe.

81. Mapenzi ni wokovu

Utiao roho nguvu,

Zikaenda kwa utuvu,

Safari ya utelezi.

82. Na safari ya maisha,

Kwa hali inavyotisha,

Kwenda ingali tuchosha,

Mungu bariki mapenzi.

Katika utenzi wa Mapenzi Bora, uliyochapishwa mara ya kwanza mwaka 1958, na kuchapishwa tena mwaka 2018 na Mkuki na Nyota, mwandishi Shaaban Robert ameandika maneno yanayohuisha. 

Kwa haraka haraka unaweza kudhani kuwa anaongelea mapenzi yale yanayofanya miili ichemke. Lakini mwandishi anayaangalia mapenzi kwa fikra pana sana. Anaanza kwa kuelezea mapenzi yake kwa uandishi. Anakiri jinsi anavyopenda kuandika. 

SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu

Japokuwa macho yameanza kufifia nuru, bado anaandika. Anazitamani siku alizokuwa na nguvu, siku za ujana. Lakini hana namna. Hawezi rudisha nyuma muda.

30. Maisha yetu mafupi,

Na sijui twenda wapi,

Mambo yatakuwa vipi,

Kama hima sifanyizi!

31. Tunaishi na kuhama,

Lazima nifanye hima,

Maana kifo daima,

Hutokea kama mwizi.

(uk. 5)

Anatumia muda kumwelezea mtu anayedai kuwa eti yeye hayapendi mapenzi. Ni lazima awe na kasoro fulani inayomfanya awaze hivyo. Aidha, amekunywa au amevuta kitu fulani kikamlevya, kikamfanya asiwe na akili zake timamu. Tena, anadadavua wasifu wa hayo mapenzi:

66. Ulimwengu kama huu,

Wenye mashaka makuu,

Kimbilio na nafuu,

Ni palipo na mapenzi.

67. Si kwamba nabahatisha,

Kweli tupu napitisha,

Hayana kitu maisha,

Kama hayana mapenzi.

(uk. 10)

Utenzi huu una jumla ya beti 690. Ndani yake, mwandishi anaongelea sana jinsi mapenzi ni kama ukombozi wa watu, nanga wanayoshikilia ili wasizamishwe na maji mazito yaliyo tabu mbalimbali za maisha. La sivyo, watu wengelemewa. Anaonesha jinsi ambavyo mapenzi si kitu ka kupuuzia tu. 

Unajua jambo la kushangaza ni kwamba japokuwa kila mwanadamu anayatamani mapenzi, aidha kupenda au kupendwa, lakini cha ajabu ni kwamba watu wengi kuonesha kwamba siyo kitu cha muhimu kwao. 

SOMA ZAIDI: ‘Utubora Mkulima’ na Funzo la Kuwekeza Nguvu Katika Kuipendezesha Nafsi Yako

Kwa mfano, mwandishi akiwa anaandika kuhusu mapenzi anaweza kuonekana kuwa anaandika mambo ya kupuuzwa tu. Utasikia, ah, anaandika mapenzi mapenzi tu. Au, mtu akiangalia filamu yenye hisia nyingi anaonekana kama ana kasoro fulani. Heri aangalie sinema za kupigana zaidi.

Anachoongelea mwandishi ni undani wa binadamu. Hali ya utulivu wa ndani na siyo mbwembwe za nje tu.

114. Kwa habari za mapenzi,

Nasema maneno wazi,

Si ubembe na upuzi,

Shauku na ubazazi.

115. Mimi nasema kiini,

Malkia wa moyoni,

Na johari ya Peponi,

Wakati wa maamuzi.

116. Mapenzi niyanenayo,

Ya saburi na makao,

Milele katika moyo,

Si mapenzi makumbizi.

117. Mapenzi ya kudumu,

Milele yaliyo tamu,

Moyoni mwa mwanadamu,

Husema kurasa hizi.

Tena si mapenzi tu ya mume na mke. Anasema, mapenzi tumpe Mungu naye atatupa fungu. Na si tu kumpenda Mungu, ila na binadamu mwenzako pia. Hamna haja ya kubaguana kwa sababu yoyote ile. Iwe kwa kabila, rangi au dini.

126. Ubaguzi ni husuda,

Wala hauna faida,

Unadhuru kila muda,

Katika kila kizazi.

127. Kuchukiana ni ila,

Madhara yenye sifa,

Yaliyofanya ni mila,

Yameona mapinduzi.

Na undani wa ubaguzi ni nini? Ni chuki. Ni ajabu sana kuwa moyo wa binadamu una uwezo wa kubeba hivi vyote – mapenzi na chuki, roho njema na roho ya korosho. Na kila siku anayo nafasi ya kufanya maamuzi ya kuyaishi mapenzi bora. Mwandishi anamwelezea mtu mwenye chuki kama mtu masikini, asiye na thamani (ubeti 146).

135. Chuki sipendi kuona,

Kitu hiki cha laana,

Ni sumu ya kuungana,

Kwa roho yake Mwenyezi.

136. Chuki uchafu wa moyo,

Ni hasara kuwa nayo,

Walia na wauiso,

Huikana kuwa mwenzi.

137. Penye mapenzi mapana,

Hasama huwa hapana,

Na tuhuma na fitina,

Kuja hapo haviwezi.

Mwandishi amechambua suala la watu kupenda sifa, wakidhani hayo ndiyo mapenzi. Si mnajua tena, mapambio yale tunayopenda kusikia. Na kuna watu hudhani kwamba kumpamba mtu ndiyo kumpenda, hata kama si kwa kumaanisha bali kwa kujionesha. Yeye mwenyewe anasema:

212. Mimi sida za dunia,

Sina haja kusikia,

Sababu zina hadaa,

Na wingi wa mapinduzi.

213. Ingawa kitu chema,

Sikio langu huuma,

Iwapo sifa yavuma,

Kuwa imara siwezi.

214. Siwezi kwa kuchukua,

Mara nyingi hulemea,

Na begani huchubua,

Mimi siwi mchukuzi.

Beti hili limefanya niwaze, ina maana uchawa si sehemu ya mapenzi?

240. Mapenzi yawe mwangaza,

Kwa wajuzi wa kuwaza,

Wajue la kutukuza,

Na lililo la upuzi.

Katika utenzi huu, Shaaban Robert anatukumbusha kwamba mapenzi bora hutupa akili ya namna ya kuenenda. Si udanganyifu. Mdomoni nakwambia nakupenda, lakini nafsini ninakuchukia. 

Ni maarifa yenye asili ya wema wa hali ya juu. Kimsingi, maisha yasingekuwa maisha bila mapenzi yaliyo bora. Mapenzi hutusaidia kuondokana na mashaka (ubeti 164); mapenzi ni nuru (ubeti 187) na mwangaza wa kuwaza (ubeti 240); mapenzi ni faraja (ubeti 192); na tena huleta maana ya kuishi (ubeti 275).

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *