The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tusome ‘Kielezo cha Fasili’ Tujue Jinsi ya Kusoma

Kikiandikwa na nguli Shaaban Robert, ‘Kielezo cha Fasili’ kinamsaidia msomaji kujua jinsi ya kusoma habari, kuielewa na kuielezea kwa maneno yake mwenyewe.

subscribe to our newsletter!

Binti yangu, J, anapenda sana kusoma vitabu vya hadithi. Shule anayosoma imeweka utaratibu wa kuwaruhusu wanafunzi kuchukua kitabu kimoja siku ya Jumatano na kwenda nacho nyumbani.

Wakimaliza kusoma hadithi hiyo, wanapaswa kutumia kitabu maalumu chenye maswali yaleyale kwa kila kitabu wasomacho – Mwandishi wa kitabu anaitwa nani? Mchoraji wa kielelezo kilicho juu ya jalada anaitwa nani? Hadithi hii inahusu nini? Umefurahia nini kuhusu hadithi hii? Hujafurahia nini? – Haya ni baadhi ya maswali wanayopaswa kujibu. 

Wakimaliza, wanapewa ukurasa mzima wa kuchora mchoro wowote walioupenda katika kitabu hicho na kisha kuupaka rangi. Zoezi la mwisho humfurahisha sana Picasso wangu mdogo.

Zoezi hili lote ni zuri kwa watoto, na kwa watu wanaojifunza kusoma utu uzimani. Lakini, tupo wengi sana ambao bado tunahitaji mazoezi mengi ya jinsi hii bila hata kufahamu kuwa tunao uhitaji huo. 

Katika kumjenga mwandishi, kuna vitabu vingi sana, haswa vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambavyo lengo lake ni kumfanya mwandishi awe bora zaidi katika fani yake. 

Baadhi ya vitabu hivyo ni kama On Writing: A Memoir of the Craft kilichoandikwa na Stephen King, On Writing Well: The Classic Guide to Writing Nonfiction kilichoandikwa na William Zinsser na The Elements of Style kilichoandikwa na waandishi wawili – E. B. White na William Strunk Jr.

SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu

Lakini ni nadra sana kuona kitabu ambacho kimeandikwa kwa ajili ya msomaji, yaani, kitabu ambacho kinakufundisha jinsi ya kusoma. Simaanishi jinsi ya kutamka silabi zikawa neno, na neno yakawa maneno, na maneno yakaunda sentensi. La hasha! 

Namaanisha, vitabu vinavyokupa mbinu zinazoweza kukusaidia kusoma ili kupata maana iliyojificha katika tungo fulani. Mtu anaweza kudhani anajua kusoma vizuri, lakini mara nyingine ukimuuliza kidogo kuhusu yale aliyosoma, anabaki kubabaika.

Kama ilivyo kwa fani nyingine, huwezi kuwa mbobevu kama hufanyii kazi kipaji chako. Fundi seremala haamki tu siku moja akawa fundi bora bila kutumia msasa, msumeno na nyenzo nyingine mara kwa mara kabla hajachonga samani zilizo na ubora wa juu. 

Vilevile, daktari bingwa hapewi nafasi hiyo bila ya kuwa ametumia masaa mengi kusoma, kufanya upasuaji, kujadiliana na wataalamu wengine, na kadhalika. Hali kadhalika, mwandishi anahitaji muda wa kutosha kuwa karibu sana na vitabu pamoja na kalamu kabla yeye mwenyewe hajaitwa ‘mwandishi nguli.’

Japokuwa msomaji hatafuti kuitwa nguli, lakini anaweza kuwa msomaji bora zaidi kama akifahamu mbinu mbalimbali anazoweza kutumia kuyaelewa kwa undani zaidi matini, au tungo, yoyote anayosoma. 

SOMA ZAIDI: ‘Utubora Mkulima’ na Funzo la Kuwekeza Nguvu Katika Kuipendezesha Nafsi Yako

Kama kuna yeyote anayehitaji kitabu cha jinsi hiyo kama nyenzo ya kumfanya awe msomaji mzuri zaidi, basi Kielezo cha Fasili, kilichoandikwa na Shaaban Robert na kuchapishwa na Mkuki na Nyota mwaka 2015, chapa ya kwanza ikipigwa mwaka 1971 na Neslson, ndicho kitabu hiko! 

Kitabu hiki, chenye kurasa 82, kinamsaidia msomaji kujua jinsi ya kusoma habari, kuielewa na kuielezea kwa maneno yake mwenyewe. Mwandishi anafafanua katika utangulizi wake kuwa fasili ni maelezo ya fikra na maono katika karaa, aghalabu ya mashairi, kwa usemi mwepesi wa mjazo. 

Fasili ni pale ambapo mtu unaelezea maana ya neno kwa lugha yake asili. Si maelezo ya neno kwa neno tu, bali tafakuri ya maana halisi aliyolenga kuwasilisha mwandishi. Faida yake, anasema Shaaban Robert ni kuwa, “Twapata kuwa watu wa fikra; siyo kasuku wa kukariri na uigaji.” (uk. xiv).

Anaanza na mashairi mafupimafupi, yenye maelezo yanaoakisi ufupi huo. Kisha anahamia kwenye mashairi marefu. Mwisho, anaweka mashairi ambayo hayana maelezo kabisa. 

Bila shaka anaamini kwamba sasa msomaji anaweza kutafuta njia yake yeye mwenyewe, bila kuhitaji msaada wowote kwani tayari amepewa mifano mingi ya kutosha.

SOMA ZAIDI: ‘Kusadikika’ ya Shaaban Robert na Nasaha Njema za Maisha

Mwanzoni, anatoa mwongozo kwa msomaji. Jumla ya ‘maonyo’ sita ya kumwongoza na kisha tahadhari tatu. Anasema katika onyo mojawapo kuwa: usijaribu kuandika neno moja mpaka umefahamu barabara maana na kusudi ya karaa – ambayo ni fungu la maneno lenye aya zaidi ya moja. Isome kwa uangalifu mara nyingi mpaka uwe umelipata hili, au liwe limekuzama vema katika akili.

Kwa wasomaji wanaopenda kusoma kwa kina, na wale wanaopenda kujijengea nyenzo za kufikiri kwa undani na kuelezea mambo kwa undani vilevile, Kielezo cha Fasili ni kitabu ambacho wapaswa kuwa nacho na kukisoma maramara. 

Hiki si kitabu cha kawaida, ni nyenzo ya kukufanya uwe msomaji bora zaidi.

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *