The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ismail Jussa: Bila ya Mageuzi ya Kitaasisi Hakutakuwa na Maendeleo ya Kweli Zanzibar

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo anaieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalumu kwamba hajutii chama chake kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwani maridhiano yanahitajika kujenga taifa katika misingi ya umoja na maendeleo endelevu.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Moja kati ya matatizo sugu yanayoikabili Zanzibar ni suala la ubaguzi kwa misingi ya itikadi za kisisiasa, hususan katika eneo la nafasi za ajira na masomo zinazotangazwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ambapo vijana wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa upinzani, hususani kipindi kile Chama cha Wananchi (CUF) na sasa ACT-Wazalendo, hunyimwa fursa hizo hata kama wanasifa zinazotakiwa. 

Rais Hussein Mwinyi alivyochukua uongozi wa sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akidhamiria kurekebisha hili pamoja na kasoro nyengine kadhaa zinazozowakabili Wazanzibari walio wengi kijamii, kisiasa na kiuchumi. Ikiwa ni takribani miezi 10 tangu aapishwe kuwa Rais wa nane wa Zanzibar, The Chanzo imefanya mahojiano maalumu na Ismail Jussa, mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, chama mshirika katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na mjumbe mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupata tathmini yake ya hatua ambazo Dk Mwinyi amekuwa akizichukua kubadilisha maisha ya Wazanzibari.

Pamoja na mambo mengine, Jussa anaeleza kwamba juhudi za makusudi zinahitajika kufanya mageuzi makubwa ya kitaasisi visiwani humo kama kweli Serikali ya Dk Mwinyi imedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli Zanzibar na watu wake kwa ujumla. Endelea …

The Chanzo: Mheshimiwa Jussa karibu sana kwenye podcast hii ya The Chanzo.

Ismail Jussa: Asante sana, Khalifa [Said, mwandishi].

The Chanzo: Kitu cha kwanza ambacho ningependa kufahamu kutoka kwako ni, unaendeleaje kiafya kwa sababu tunafahamu kwa kipindi kirefu umekuwa ukijiuguza kutokana na kipigo kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama huko Zanzibar wakati wa uchaguzi na kupelekea kusafirishwa mpaka Nairobi, [Kenya] kwa ajili ya matibabu?

Ismail Jussa: Nashukuru ndugu yangu hali yangu imeimarika sana, ni afadhali sana kuliko nilivyokuwa, kwa hiyo namshukuru Mwenyezi Mungu. Bila shaka siwezi kusema nimepona kabisa kwa sababu bado sehemu zote mbili kwenye mguu bado nina chechemea chechemea, lakini nashukuru Mungu kwamba naweza kutembea nikienda ninapotaka bila shaka movements zangu zimeathirika kwa hiyo ile kasi ya kutembea au mwendo wangu si kama mwanzo. 

Na vilevile sitembei sawasawa lakini nashukuru Mungu kwamba angalau naweza kutembea kwa hiyo ni hatua kubwa sana namshukuru Mungu sivyo nilivokuwa. Na vilevile kwenye upande wa mkono ambao umetokana na athari kubwa ya kwenye bega pamoja na kwamba naweza kuunyanyua mkono lakini bado siwezi kunyanyua vitu vizito, na vilevile baadhi ya movements za mkono bado haziko sawa sawa kabisa kama nilivokuwa. 

Lakini sitegemei, kusema ukweli, kama inaweza kurudi kama nilivyokuwa kabla lakini nashukuru sana kwamba ukilinganisha na majeraha yalivyokuwa, maumivu yalivyokuwa na athari za kuvunjika zile, nashukuru kwamba kwa mtu ambaye nimetoka kutoka katika wheelchair [kiti cha magurudumu] mpaka kufika kutembea na magongo hadi leo naweza kutembea bila kushika gongo kwa hiyo ni hatua kubwa namshukuru Mungu.

The Chanzo: Hongera sana, hongera sana kwamba angalau sasa, lakini unaweza kufanya shughuli zako, za kibinadamu na za kisiasa? 

Ismail Jussa: Nashukuru katika hilo. Nafikiri mnaniona kwa sababu mimi kwa kawaida si mtu mtete ambaye nitabakia ndani tu. Kwa hiyo, mapema sana hata mtu wangu aliyekuwa akinifanyisha mazoezi kwa maana physiotherapy alikuwa akiniambia kwamba speed ambayo nilitumia kutoka kwenye kiti cha magurudumu, mpaka kutumia walker yenye miguu minne, hadi kutumia trachies zile na hatimaye kuweza kutumia gongo la mguu mmoja tu mpaka kuliacha ilichukua mchakato wote huo nazani ilichukua kama muda wa mwezi mmoja tu. Kwa hiyo, nashukuru imenisaidia na hivyo sasa nimo katika shughuli zetu za kisiasa pia nashiriki nashukuru Mungu.

The Chanzo: Sasa, sasa hivi ni takribani miezi kumi, tangu Rais Dr Hussein Mwinyi aapishwe kuwa Raisi wa nane wa Zanzibar na kuifanya sehemu hiyo ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na Serikali mpya. Nilikuwa nataka kufahamu tathmini yako, unaitazamaje hii miezi kumi ya utawala mpya Zanzibar? Nini haswa kimebadilika, hususani katika eneo la maisha ya Wazanzibar wa kawaida? 

Ismail Jusa: Kuna mambo yamebadilika kiasi na kuna mambo ambayo bado kusema ukweli hayajabadilika. Na kuna maeneo mengine, kwa mujibu wa mitazamo ya watu, pengine hali imekuwa hasi, au mbaya zaidi. Katika eneo moja ambalo limebadilika nadhani kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mara nyingine baada ya kipindi cha misukosuko mikubwa, kufuatia kufutwa kwa uchaguzi wa mwaka 2015, na hatimaye jinamizi lililotujia katika uchaguzi wa mwaka jana, wa 2020, ambao kwa hakika haukuwa uchaguzi, ulikuwa ni uchafuzi na maafa makubwa sana na kwa hakika umeacha athari nyingi sana Zanzibar. 

Kama mnavyojua kwamba watu kadhaa waliuawa takribani, watu 21, ilikuwa watu 17 kisiwani Pemba na watu wanne hapa kisiwani Unguja, waliuawa na vyombo vya ulinzi na usalama. Watu wengi wamejeruhiwa wengine wengi wanaendelea na ulemavu, mimi mmoja wapo, lakini na wengine wengi tu, kuna watu wanaendelea kuishi na risasi katika miili yao, kuna watu ambao wamepata vipigo, kuna watu waliowekwa vizuizini, akiwemo aliyekuwa, siye aliyekuwa mpaka sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa chama chetu cha ACT-Wazalendo Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui ambaye kwa sasa ni Waziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

Kuna watu ambao wameharibiwa mali zao, wameharibiwa nyumba zao kwa hivyo athari zilikuwa nyingi lakini hatimaye tulifanya maamuzi ya kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa hiyo, hiyo angalau ilituliza ile hali ya taharuki ambayo ilikuwepo Zanzibar na kiasi fulani unaweza kusema kwamba kuna hali ya utulivu wa aina fulani. Siwezi kusema ni hali ya amani moja kwa moja kwa sababu kwangu mimi tafsiri ya amani si tu kutokuwepo na varugu lakini na sababu zinazoweza kupelekwa vurugu pia zisiwepo. Kwa hivo hayo bado hayajakuwa addressed [kutatuliwa]. 

Lakini angalau kuna utulivu wa namna fulani watu wanafanya shughuli zao kwa hivyo katika eneo hilo angalau kuna hiyo nafuu. Lakini kiuchumi bado kabisa tunavozungumza. Kulikuwa na kampeni kubwa sana na tuliaminishwa kwamba Serikali hii imekuja kupambana na ufisadi na rushwa na Rais Hussein Mwinyi na hakika alitaka aonekane hivyo na kumechukuliwa hatua nyingi za, kwa mfano, kuwaondosha kazini watu mbalimbali, wengine walisimamishwa kazi, wengine wakabadilishwa kabisa, tukatangaziwa mambo mengi sana ya ubadhirifu na ufisadi uliofanyika lakini kinachosikitisha ni kwamba takribani tunakaribia mwaka mmoja sasa tangu Serikali hii ilipoingia madarakani mwezi Novemba wiki ya mwanzo mwaka jana [2020] hatujaona kesi hata moja ya watu hao ambao wametuhumiwa kwa ufisadi kufikishwa mahakamani, hakuna watu ambao wamechukuliwa hatua kwa maana ya hatua za kisheria. 

Tumeambiwa, kwa mfano, fedha nyingi sana zimefisidiwa, miradi inayogharimu mamilioni ya dola, kwa mfano, mradi ule wa Huduma za Miji katika Zanzibar, unaitwa Zanzibar Urban Service Project, unaambiwa takribani fedha dola za kimarekani milioni tisini na saba zimehujumiwa. Tumetajiwa miradi mingine mingi, kwa mfano, ule mradi wa kufuga samaki na viumbe wengine wa baharini ambao uligharimu mabilioni ya shilingi. Tumetajiwa mambo mengi tu lakini hakuna mtu hata mmoja ambaye amechukuliwa hatua hadi hivi sasa. 

Lakini kinyume chake kumekuwa na maneno mengi yanayoelezwa kwamba hata hivi sasa bado hakuna uwazi katika masuala ya zabuni za Serikali na watu wanalalamika wakiwemo wafanyakazi wa Serikali kwamba bado zabuni zimekuwa zikitolewa kwa misingi ya kujuana na ufisadi kwa maana hiyo bado unaendelea. Ni kama vile kumekuwa na cover up [kufunika] ya kutaka kuonesha kwamba ufisadi ulikuwa mkubwa katika Serikali iliyopita ili watu wazungumzie yale na wasizungumze haya ambayo yanaendelea hivi sasa. 

Lakini ukiachilia hayo, gharama za maisha zimeendelea kupanda. Vitu vimepanda bei sana. Bidhaa nyingi sana kuanzia vyakula, mafuta ya kupikia, bidhaa za ujenzi, vifaa mbalimbali ambavyo watu wanatumia, vimepanda sana na kimoja kinachozungumzwa sana ni kupanda kwa ushuru na kodi katika nchi yetu. Suala la ajira halijashughulikiwa kabisa. Vijana ambao hawana ajira wanaendelea kuongezeka mitaani. Kwa hiyo, kwa ujumla unaweza kusema kwamba bado hali ya maisha haijabadilika kiasi ambacho hata ile kauli mbiu iliyokuwa ikitumika katika kampeni za Dk Hussein Mwinyi ya uchumi wa bluu siku hizi imegeuzwa dhihaka katika Zanzibar.

Ni kawaida kuwasikia wananchi wa Zanzibar, kama kawaida yao watu wa pwani, mambo yakiwa magumu wakakwambia, “Ndo uchumi wa bluu huo.” Kwa hakika bado hakujaonekana mabadiliko ya maana katika nyanja za maisha Zanzibar.

The Chanzo: Asante sana, na hiyo kidogo inashangaza ukizingatia ukweli kwamba Dk Mwinyi ameingia madarakani akiwa na ari, kwa mfano, ya kupambana na ufisadi na masuala ya rushwa lakini pia kuboresha hali za maisha za watu. Labda kwa mtazamo wako, unadhani ni changamoto gani au changamoto zipi za msingi zinazoikabili Serikali ya Dk Mwinyi na ambayo unadhani kushindwa au kufanikiwa kwake katika kuzifanyia kazi hizo changamoto kunaweza kukaipa Serikali yake muelekeo tofauti? Kwa sababu, kama tunazungumza kwamba vita dhidi ya ufisadi bado ni lege lege, [kwamba] hakuna hatua zinazochukuliwa, unaona kuna changamoto zozote za msingi zinazoikabili Serikali ya Mwinyi ambazo wewe unadhani zinapaswa kufanyiwa kazi?

Ismail Jussa: Nadhani kuna mambo ya aina mbili, mimi ninavyoyatazama, la kwanza naona kwamba, na hili nimekuwa nalisema na sioni aibu kuendelea kulizungumza, mimi naona kwamba Dk Hussein Mwinyi alitamani sana kuwa Rais wa Zanzibar lakini hakujiandaa kuwa Rais wa Zanzibar na hakujiandaa kwa dhamana hii ya Urais. Na nalisema hilo kwa mtazamo wangu kwa mambo kadhaa. 

Kwanza, jinsi alivyounda Serikali yake. Mbali ya kuzungumzia labda kushirikisha watu kutoka chama cha ACT-Wazalendo ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini kutoka chama chake mwenyewe ukiangalia watu ambao amekuwa akiwateua katika safu yake ya mawaziri, katika safu yake ya makatibu wakuu, katika safu yake wakurugenzi mbalimbali, makamishna [na] mameneja, unaona kwamba hakujiandaa. 

Hana watu ambao labda ni timu labda aliyokuwa ameiandaa ambayo inaendana na hiyo dira ambayo alikuwa akituambia kwamba anayo ya kuendeleza Zanzibar. Kwa hiyo, matokeo yake tumekuwa na watu ambao uwezo wao ni mdogo, hakuna ubunifu, hakuna fikra mpya, imekuwa ni mambo yale yale kutoka chama kile kile katika sekta zilezile kwa mifumo ile Ile. 

Kwa hiyo, hakujabadilika, kikubwa kilichobadilika ni kile ambacho wazungu wanakiita rhetorics, yaani lugha za majukwaani. Tunataka tuaminishwe kwa maneno kwamba kuna mabadiliko lakini mabadiliko hasa hayaonekani katika uhalisia wake. Kwa hiyo, nasema hakujiandaa na si hakujiandaa katika kupanga timu au safu tu lakini vilevile natazama pia katika mipango ya Serikali. 

Unapokuja na mabadiliko ya Serikali ukawa na Serikali mpya pia chini ya Rais mpya hata kama chama ni kile kile ungetegemea kwamba ungepangwa utaratibu kwanza wakuendeleza mtazamo, yaani uoneshe kisawa sawa na sasa isiishie katika hotuba tu lakini iandikwe katika mpango maalumu ile dira ya tunataka kujenga Zanzibar ya aina gani? Na tunapozungumzia kujenga Zanzibar ya namna gani ungetegemea ifahamike na dira iwe wazi wazi iwe inaeleweka kabisa isiyo na maswali ambayo hayana majibu juu ya pengine unataka kujenga Zanzibar ya aina gani kiuchumi; unataka kujenga Zanzibar katika huduma za jamii, kama elimu, afya, maji safi na salama, umeme? 

Zanzibar ya aina gani katika maeneo ya huduma za kiuchumi kwa mfano barabara, bandari, viwanja vya ndege, unataka kujenga Zanzibar ya aina gani katika kuimarisha sekta zipi ambazo zitatoa ajira kwa watu na vipi vitakuwa vipaumbele vyako? Unataka kuijenga Zanzibar ya aina gani katika mifumo ya uongozi mwema, yaani good governance? Unataka kujenga Zanzibar ya aina gani katika masuala ya maadili ya kiinchi? Haya lazima yawe yanaeleweka katika mitazamo yako? Lakini yasiishie katika kusema tu badala yake hatua ya pili katika dira ungetegemea katika kujiandaa dira hiyo itafsiriwe katika sera za Serikali. Tungependelea kuona mabadiliko ya sera, mabadiliko ya sera baadae yahamishwe katika sheria za nchi. 

Kwa hivyo, ukishaendeleza dira uendeleze sera baadae uendeleze sheria ambazo zitatafsiri hizo sera katika sheria za nchi. Na baadae hayo yote yaonekane katika bajeti za nchi kwa sababu bajeti ndio mipango ya kila mwaka inayoonesha Serikali imeweka vipaumbele vyake gani kuvitekeleza katika kila mwaka. Sasa huoni huo mtiririko ninaoueleza katika mipango ya Serikali, unasikia hotuba tu kila wakati na lawama. Sasa unajiuliza kuna wakati ungelaumu ulipokuwa unafanya kampeni lakini sasa una mwaka mzima tungetegemea tusisikie lawama tuone unafanya nini wewe ambaye tumekupa au umejipa, maana hakupewa na wananchi lakini amejipa dhamana. Tunajua sote  mazingira ya uchaguzi lakini ndio yupo katika madaraka tungetegemea hayo tuyaone kwamba tunayatekeleza kivitendo. 

Lakini ukiacha hilo, jingine ambalo naliona kwamba lina upungufu mkubwa sana nadhani kwamba hata washauri hana ambao wamebobea wanaweza wakamsaidia. Na tumeshuhudia kwa tafsiri yangu mimi naona kwamba kama vile kumekuwa na udanganyifu mwingi sana kupelekwa. Kwa mfano, tumeshuhudia miradi mikubwa mikubwa ikitangaziwa kwamba itakujakuletwa kwa Zanzibar ambapo ukisikia gharama zake kwa mtu ambaye hata si mchumi kama mimi unajiuliza kwamba hivi kweli inaingia akilini kwamba mtu kuwekeza katika bandari ya uvuvi ya Mpiga Duri ambayo gharama zake zitakuwa tunaambiwa dola bilioni 6.3 wakati GDP ya Zanzibar yote, yaani pato la taifa la Zanzibar Unguja na Pemba ni dola bilioni 4? 

Sasa mtu atawekeza dola bilioni 6.3 atategemea apate faida gani katika Zanzibar? Ungetegemea kwa mtu wa kawaida kwamba wangemwambia kwamba hii haliingii akilini. Au, kwa mfano, tumeambiwa kwamba kunajengwa bandari mpya ya kibiashara na ya huduma itakayo saidia katika uchumi wa mafuta na gesi, kujenga kontena yard katika eneo la Manga Pwani, mpaka sasa hivi tumeambiwa baada ya miezi sita itawasilishwa feasibility study, kilichoshuhudiwa ni baadaye tumeambiwa kumewasilishwa master plan, hadi leo hakuna feasibility study

Lakini karibuni tumetangaziwa mradi ule wa kujenga jengo kubwa sana la ghorofa sabini ambalo litakuwa ni la pili kwa ukubwa Africa. Ambalo tumeambiwa litagharimu shilingi trilioni 3 za Kitanzania. Unajiuliza mtu anaweza kuwekeza mradi kama huu kwa Zanzibar kwa kutegemea nini? Kwa hivyo, inaonekana vile kwamba anatumainishwa na kuaminishwa kwamba mambo makubwa yanaweza yakafanyika lakini katika hali ya kawaida huuoni uhalisia wa mambo haya. Kwa hivyo, nasema hayo yako upande mmoja katika kujipanga lakini sioni kwamba alijiandaa na kujipanga ipasavyo katika kutekeleza kile ambacho anakiamini kinaweza kikafanywa na kingepaswa kufanyika kwa Zanzibar.

The Chanzo: Nataka kukuuliza kuhusiana na hicho ambacho umetoka kukigusia sasa hivi kwa sababu kusema ukweli kwa siku za hivi karibuni kitu kikubwa ambacho kimekuwa kinatawala vichwa vya habari kuhusiana na Zanzibar ni kuhusiana na huo ujenzi wa hiyo inayoitwa Domino Tower, pamoja na huu mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia kutenga visiwa 10 vidogo vidogo na kutangaza wawekezaji ambao wanapenda kuja kuvichukua kwa ajili ya kufanya masuala ya uwekezaji. Nilikuwa nataka kufahamu watu, wananchi wa kawaida, wa Zanzibar wanazizungumziaje hatua kama hizi hapa kwa sababu, kitu kikubwa ambacho tumekuwa tukikisikia ni sauti tu za viongozi na za watu wenye nafasi kwenye jamii, lakini maoni ya Wazanzibari wa kawaida ni yapi kuhusiana na hatua kama hii yakutaka kujenga hiyo Domino Tower, au Serikali kuita wawekezaji kuendesha hivi visiwa vidogo vidogo?

Ismail Jussa: Nitakwambia, Khalifa [kwamba] kuna mitazamo ya aina mbili ninayoisikia mimi ninapozungumza na watu mbalimbali. Kuna ambao ni wa kawaida binadamu wanakuwa na hamu ya kuona maendeleo kwa hivyo ninaposikia mambo kama hayo yanatajwa wako ambao wanaingia na tamaa ya kuamini kwamba yatafanyika na kwa hivyo wanayasubiri kwa hamu. 

Haidhuru wako miongoni mwao ambao wao wanaona kwamba tulitangaziwa mwaka mmoja uliopita kuhusu haya mabandari yale ambayo yatajengwa Mpiga Duri na Mangapwani mpaka saivi mwaka unakatika hatujaona chochote ungetegemea angalau kuna hatua zinaonekana lakini hadi saizi hakuna kizungumzwa katika vyombo vya habari hayatajwi tena. Kwa hiyo, yanatia mashaka huku wakijiaminisha.

Lakini wako ambao kundi la pili ambao ni wapembuzi wa mambo ambao wanaona kwamba hizi zimekuwa ni ndoto za alinacha na ni hadithi zile zile ambazo wamezisikia miaka nenda miaka rudi kutoka Serikali za [Chama cha Mapinduzi] CCM. Tulizisikia wakati wa utawala wa Dk Salmin Amour wakaja watu hapa matapeli wa kimataifa, nakumbuka mpaka ikasambaa katika magazeti kama ya Uingereza maarufu, na mpaka leo hata imeganda katika kichwa changu sisahau. 

Walikuja hapa watu  wawili mmoja akiitwa Patrick Patrick O’Sullivan mwingine akiitwa Tom Wells waliaminishwa kwamba wangekuja kuwekeza Zanzibar kwa wakati ule tuliambiwa kwamba ni dola bilioni nne. Watu wakajiuliza dola bilioni nne, kwa Zanzibar ya miaka ile ya tisini kweli mtu atawekeza unategemea nini? Kwa hiyvo, watu wanaona hadithi zile zile. Ni kama ambavyo alikuja Dk Shein akawadanganya watu kwamba ataigeuza Zanzibar kwamba itakuwa Dubai na leo imekuwa ni dhihaka kama ambavyo inafanyiwa dhihaka ya uchumi wa bluu hivi sasa na Wazanzibari. 

Kwa hivyo, watu wengine wanaona kwamba ni mwendelezo wa hadithi zile zile. Lakini ukiacha hayo, wako ambao wanaamini, na mimi nikiwa mmoja wapo, ambao wanahoji juu ya hata haya yanayotangazwa. Kwa mfano, kuna maswali mengi sana hivi sasa yanaulizwa kuhusu hii miradi inayotangazwa kwamba watu ambao wanataka kuja kuwekeza katika maeneo hayo, katika visiwa hivi ambavyo tumeambiwa kwamba mwenye nia, mwenye kuonesha hamu ya kutaka kuwekeza alete mapendekezo yake na kama ambavyo tulitangaziwa vilevile kwamba kuna mtu anataka kuchukua baadhi ya nyumba za Serikali na kuzifanyia uwekezaji awasilishe mapendekezo yake. 

Yako maneno ambayo bado tunayatizama kwa jicho la undani kabisa kuona kwamba yatakuwa ni kweli au pengine ni hadithi. Lakini, yako maneno yanayoaminishwa kwamba haya imekuwa ni kama vile geresha tu lakini kilichokuwepo ni kwamba tayari kuna watu maalumu ambao wameshachaguliwa wapewe hivyo visiwa au wapewe hayo majumba ya mji mkongwe na hicho kinachofanyika ni kiini macho tu cha kuaminishwa kwamba itakuwa inafanywa kwa uwazi lakini mchakato wenyewe haupo kwa uwazi kabisa. 

Kwa hivyo, inaaminika kuna watu maalumu ambao ndio waliotegemewa wapewe. Na hata kuna hisia kuna watu ambao wanamaslahi yao katika haya. Na ndio maana nikasema kwamba kuna maswali mengi sana kuhusu masuala ya kupigana vita na ufisadi na rushwa kwa sababu watu wangetegemea mambo kama haya yawekwe kwa uwazi kabisa. Katika jamii ambayo inakusudia kujenga utawala bora au uongozi mwema ungetegemea tutajiwe kwamba wangapi walitenda na wali-tender kwa kiasi gani na huyo ambaye alichaguliwa kwamba alichaguliwa kwa vigezo gani?

Sasa mambo kama haya huwa hatuambiwi na ndio maana yanazua maswali. Ni kama katika hilo jengo linaloambiwa la Domino Zanzibar ambalo mimi nilipoliona baadhi ya hao wawekezaji wanaotajwa kwa hakika nilijiuliza maswali mengi sana nikaona ni mwendelezo wa hadithi zile zile. Kwa hivyo, wako walioamini katika wananchi wa kawaida na wanaendelea kujipa tamaa lakini pia wako wengi wanaoona ni mwendelezo wa yale yale mambo yaliyokuwa yamesemwa nyuma na pengine watu kujitengenezea fursa za kujitajirisha wao wenyewe lakini si mambo ambayo yatakuwa na maslahi kwa wananchi wa Zanzibar. 

Na mimi binafsi sikufichi Khalifa, siamini chochote kwamba kinaweza kutoka katika mambo haya makubwa yanayotajwa kwamba tutayaona kwa sababu sioni kama kuna mambo ya msingi ambayo yanafanyika yatakayotufikisha huko. 

The Chanzo: Nataka kukuuliza kuhusu suala moja ambalo lilikuwa maarufu sana kipindi cha utawala wa Rais aliyepita wa Zanzibar [Dk Ally Shein] na hili linahusu suala la ubaguzi kwenye suala zima la ajira, kwa mfano, ambapo watu ambao walikuwa wanaaminiwa kuwa ni wanachama au wafuasi au wanaosadikiwa tu kuwa wafuasi wa upinzani walikuwa wanapata tabu sana kuweza kupata ajira za Serikali. Na hili tatizo lilikuwa kubwa sana kwa upande wa Pemba ambako kunajulikana kuwa ni ngome ya upinzani kipindi kile [Chama cha Wananchi] CUF na sasa ACT-Wazalendo na nakumbuka hili marehemu Maalim Seif Shariff [Hamad] aliwahi kulipigia kelele mara nyingi tu akizisihi mamlaka za Serikali ziache kufanya jambo hilo. Najua kwamba umefanya ziara Pemba, umeshiriki kwenye uchaguzi mdogo ule wa Konde ule wa ubunge na pengine ushawahi kukutana na makundi tofauti tofauti ya wananchi kule kisiwani Pemba au na wanachama wenu wa ACT-Wazalendo, hili tatizo chini ya uongozi wa Rais Mwinyi, limepungua kwa kiasi gani au bado hali ipo vilevile?

Ismail Jussa: Kwa kiasi kikubwa hali bado ipo ipo vilevile na kumefanyika majaribio na hiyo ndio shida mara nyingine ya wanasiasa wanaoshika nafasi za juu hizi ya kujaribu kuwaingiza wananchi wenye asili ya Pemba katika nafasi za madaraka. Lakini, kuingiza mawaziri kwa mfano kutoka Pemba au ukateua makatibu wakuu pengine wawili watatu kutoka Pemba au vilevile wakurugenzi, hakujasaidia ikiwa uajiri kwa jumla ambapo ndo unawagusa wananchi wengi wa kawaida, bado unaendeshwa kwa misingi ya ubaguzi na hilo ndio ambalo lipo hadi hivi tunapozungumza. 

Na ubaguzi huo hauwahusu wananchi wa Pemba ingawa wananchi wa Pemba ndio waathirika wakubwa zaidi, lakini kama ulivyosema kwa jumla wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa upinzani iwe unatoka Unguja au unatoka Pemba ni kazi ngumu sana kupata ajira. Na ndio maana nasema mambo haya hayawezi kumalizika kwa  rhetoric au kwa lugha za majukwaani au hotuba za majukwaani tu. 

Kama mambo haya yanataka kufanyiwa kazi lazima kuwe kuna institutional reforms, mageuzi ya kitaasisi, na vile vikwazo au taasisi ambazo zimekuwa zikitajwa kuhusika na kufanya ubaguzi huu uwe kama ni sehemu ya mwenendo wa Serikali kwa jumla zibadilishwe au hata zivunjwe kama hayo hayajafanyika si rahisi kutokea kwa mabadiliko haya. 

Na kimoja nikitaje mahususi kabisa sote tunajua kwamba Zanzibar kuna kitengo kinaitwa GSO ambacho kipo Ikulu ya Zanzibar. Hawa ni jamaa wa Usalama [wa Taifa] ambao wameweka kitengo maalumu ndio wanao pembua mara nyingi watu wanaoomba kazi katika sehemu mabalimbali na mara nyingi ungetemea ni jambo zuri kama ingekuwa ni kitu ambacho kingekuwa kinafanyika katika misingi ya kutazama watu labda wanamaadili ya kazi wanazoomba, wanavigezo na sifa zao, wana elimu inayo takiwa, wanauzoefu unaohitajika, hawana pengine muunganiko na watu wabaya na vitu kama hivyo. 

Lakini hayo sio yanayofanyika, mara nyingi kazi ya GSO  imekuwa ni kupekua kukutizama wewe unayeomba kazi hujawahi kuwa mwanachama au mfuasi wa chama cha upinzani, hujawahi kuonekana katika mikutano ya kisiasa ya chama cha upinzani, je, wazee wako awe baba au mama, mjomba au shangazi wanashabikia upande gani? Umezaliwa wapi? Una asili gani? Sasa haya hayasidii chochote katika kuingiza sio tu kuondosha ubaguzi hata kuingiza ufanisi katika kazi na utaalamu na weledi. 

Matokeo yake watu wengi wenye uwezo na sifa za kupewa kazi hawapewi wanapewa watu kwa sababu ni jamaa au watoto au ndugu wa mtu fulani. Kwa hivyo, nasema kama hatuja disband [vunja] kitengo hichi cha GSO, haya ninayoyazungumza mimi ndio mageuzi ya kitaasisi, tutaendelea kuimba tu kwamba tunaondosha ubaguzi lakini bado ubaguzi utaendelea kuwepo. 

Kwa hivyo, haya bado yanaendelea na vijana wengi tunakutana nao wanaendelea kulalamika kwamba masuala hayo bado yapo. Utakuta kuna nafasi nyingi ambazo hazijajazwa katika katika Serikali, katika utumishi wa umma pengine, kuna watu wanazo sifa lakini hazijazwi nafasi hizo haziajiriwi watu kwa sababu watu wanaotakikana ni wa jamii fulani kwa ndugu na jamaa au watoto wa watu fulani hawajapatikana, [na] wale waliopo wanasemekana wapo katika mrengo mbaya ambao hautakiwi katika Serikali. 

Kwa hivyo, hilo ni eneo moja ambalo bado halijafanyiwa kazi na hata kisiasa umetaja hapo katika chaguzi hizi tumeshuhudia katika chaguzi za Konde, chaguzi za Pandani na Kinuni hapa Unguja kwamba hata yale mambo ambayo yalipelekea maafa huko nyuma bado yangali yakitendwa. Tunashukuru kwamba hivi karibuni kupitia intervention iliyofanyika suala la Konde limefanyiwa intervention ingawa limefunikwa funikwa lakini limechukuliwa hatua. 

Lakini tungetegemea kuona mabadiliko ya mfumo wa kitaasisi ili ubaguzi huu wa kisiasa, wa ajira, wa fursa za kiuchumi usiendelee kabisa katika Zanzibar na tuwe na kweli jamii ya ambayo imeungana ambapo tunajenga nchi kwa umoja wetu. Bado huko hatujafika bado.

The Chanzo: Asante sana umezungumza mambo mengi sana ya msingi, na kitu kimoja ambacho nataka nikuulize kutokana na haya yote ambayo umeyazungumza, kama vile kutokuwepo kwa utayari kwa uongozi uliopo sasa Zanzibar kuweza kuleta mabadiliko ya kweli kisiwani humo, unazungumziaje sasa suala la chama chenu cha ACT-Wazalendo kuamua kuwa mshiriki kwenye Serikali hiyo? Nafahamu kwamba wewe ulitetea uamuzi wa ACT-Wazalendo kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Je, bado unaamini kwamba uamuzi huo ulikuwa sahihi na je, ni sahihi mpaka sasa na kama ni hivyo unakitenganisha vipi au utakitenganisha vipi chama chako cha ACT-Wazalendo na haya ambayo umeyazungumza kwa sasa kwa sababu ACT-Wazalendo ni chama mshirika wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inaongoza sasa hivi Zanzibar. Kwa hiyo, kwanza nataka kufahamu kama bado unaendelea kuamini kuwa ni uamuzi sahihi kuwepo serikalini na kama ni hivyo kwa nini? Kwa namna gani utakitenganisha chama chako na haya yanayotokea kw sasa Zanzibar?

Ismail Jussa: Asante. Umesema sahihi kabisa mimi nilikuwa ni miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa, tena nikiwa katika hali ngumu sana, nikiwa nimelala katika kitanda cha hospitali, hata kabla sijafanyiwa matibabu ya majeraha ambayo nilipata, lakini nikatoa kauli ya kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla haijaundwa na baada ya kuundwa nikiwa Nairobi pia nikatoa kauli ya kuunga mkono. 

Nikuhakikishie hadi hii leo bado naiunga mkono hatua ile na nina amini kwamba ilikuwa ni uamuzi sahihi na inapaswa kuendelea huko mbele. Mimi bahati nzuri Khalifa, nilikuwa ni mmoja mwa watu ambao walioasisi dhana hii ya maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2009-2010, na tulipo pigania suala lile tulikuwa tunaamini kabisa kwamba Zanzibar umefikia katika miaka zaidi ya hamsini ya migogoro ya kisiasa na haipaswi kuachwa kuendelea vile na tunapaswa kuachana na mfumo wa mmoja kutawala peke yake hata kama sisi tungeshinda kwa sababu kwa kufanya hivyo bado ungeitenga sehemu nyingine ya jamii na kwa jamii ambayo imegawanywa kwa muda mrefu hilo haliwezi kuwa ni suala lenye afya na katika uendeshaji wa nchi. 

Kwa hivyo, bado naliamini hilo na katika mazingira mahususi ya mwaka jana katika uchaguzi ilikuwa ndio njia pekee ya kujaribu kuwaleta pamoja Wazanzibari na kuondoa ile taharuki iliyokuwa imeikumba nchi wakati ule baada ya yote yale ambayo yalikuwa yamefanyika. Kwa sababu kama nafikiri mnakumbuka tulimaliza hatua zote mpaka barabarani tuliingia sisi wengine ndo tukayapata amabyo yametupata wala hatujutii. Kwa hivyo, bado tunaunga mkono suala la lile. 

Sasa suala la kusema kwamba tutajitenganisha vipi na haya ambayo yametokea nadhani kwanza tunajua uwakilishi wa ACT-Wazalendo ambao umetokana na matokea ya kupanga ya uchaguzi [na] sio matokea halisi umepelekea uwakilishi wetu kuwa mdogo sana. Lakini historia inaonesha hata uwe na uwakilishi mkubwa kama ambavyo ilikuwa mwaka 2010 mpaka mwaka 2015 kama hakuna utashi wa kweli wa kutaka kufanya kazi kwa pamoja bado hamuwezi kufika mbali. 

Kwa hivyo, kwa sasa kama mnavojua sisi tuliingia katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais mwezi Disemba mwaka jana [2020], ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu alipoapishwa Rais Hussein Mwinyi lakini mawaziri wetu wawili walikuja kujumuika katika Serikali mwezi wa tatu mwaka huu [2021], kwa hiyo hatuna muda mrefu sana. Lakini nataka nikuhakikishie kwamba waliokuwepo wanajitahidi kutoa mashirikiano ya dhati na kushauri, na kwa upande wa nafasi ya Makamu wa Kwanza kazi zake kubwa kwa mujibu wa Katiba [ya Zanzibar] ni kushauri, hilo linaendelea kufanyika. 

Mimi bado sitaki kuvunjika moyo kwani tutarudi kule kwetu tulikotoka nataka kuamini kwamba Rais Hussein Mwinyi ataona umuhimu wa michango, mawazo na fikra za namna gani ya kuipeleka Zanzibar mbele. Hivi sasa, kama chama, kuna baadhi ya maeneo ambayo tumejipanga kuyaandaa chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais ikiwa ni kufafanua yale ambayo Maalim Seif alimpelekea Rais Hussein Mwinyi wakati ule alipokuwa anakubali kujiunga na Serikali kama mambo ambayo tungependa afanyie kazi. 

Tunayachambua kwa kina na kupendekeza hatua gani zifanyike. Sasa, suala la yatatekelezwa kiasi gani hilo ni jukumu la Rais [Mwinyi] kwa sababu kama tunavyojua mifumo yetu bado tuna Executive President ambaye ndio mwenye madaraka makubwa sana wengine wote wanabakia kama washauri kwake. Kwa hivyo, tutafanya hivyo na naamini yakitekelezwa hayo mengi haya ambayo niliyazungumza mapema kama ni matatizo nadhani kwamba yanaweza kupatiwa ufumbuzi na nadhani lile la kwanza kabisa nililolisema la kwamba kwamba tunahitaji kuendeleza dira na baada ya dira tutengeneze sera na baada ya sera tutengeneze sheria na baadae bajeti za nchi ziwe zina akisi hayo. 

Haya nafikiri kwamba [Rais Mwinyi] akiamua kwamba nataka ushirikiano wa dhati na kukaribisha mawazo kutoka kila pembe basi mimi naamini Zanzibar ina watu wengi wenye vipaji na uwezo mkubwa. Sio tu kutoka ACT-Wazalendo, lakini hata kutoka katika makundi mengine mbalimbali ya kijamii wanaweza wakasaidia tukaipeleka mbele nchi yetu. Kwa hiyo, mimi bado naunga mkono suala hili. Tunajitenga kwa sasa kwa sababu kama nilivyosema kwamba sisi kazi yetu kubwa ni itakuwa ni kushauri lakini maamuzi anayo Rais mwenyewe lakini tutaendelea kutoa mchango wetu na mawazo yetu na fikra zetu. 

Sasa suala la kiasi gani yatachukuliwa ni la yule ambaye amepewa madaraka ya mamlaka katika nchi kwa maana ya Executive President ambaye tunae. Kwa hiyo, tutaendelea kusukuma bado tuna miaka minne kuelekea katika uchaguzi ujao tunayo nafasi kubwa sana kwenye mamlaka kuamua, kupokea mawazo na kuwashirikisha wengi zaidi ili tusonge mbele. Lakini ikiwa hawatataka kama ambavyo wamekuwa wakijisifu siku zote kwamba sera zinazotawala Serikali hii [ya Zanzibar] ni za CCM kwa hivyo, wakiona yameharibika wao ndio watakao beba dhamana kwa sababu ni sera zao kama wanavosema zinatawala. 

Ni pale tu ambapo watakubali kwa dhati kuchukua mawazo, fikra na sera kutoka kwa upande mwingine ndipo ambapo tutaweza kusema kwamba tutaungana kubeba jukumu hilo kwa pamoja kwamba likienda sawa ni letu sote na likiharibika litakuwa letu sote. Lakini kwa sasa maadamu wao wanajisifia kwamba ni sera zao na miongozo yao ndio inayoongoza kufanya kazi likiharibika litaendelea kuwa lao kama ambavyo likifanyika vizuri litakuwa lao. Lakini mpaka saivi halijafanyika vizuri.

The Chanzo: Sawa sawa labda kwa kumalizia tu, ni mambo gani mengine ambayo chama cha ACT-Wazalendo kinayapigania sasa hivi huko Zanzibar? Masuala gani ambayo mnayapigania huko Zanzibar nafahamu, kwa mfano, kwa ngazi ya kitaifa kuna suala la Katiba Mpya, masuala ya tume huru ya uchaguzi, na masuala mengine ya kisiasa. Lakini pengine kwa Zanzibar kuna mambo yeyote mahususi ambayo chama kinayapigania kabla ya uchaguzi unaokuja wa 2025?

Ismail Jussa: Sisi kuna mchanganyiko wa mambo kwa upande wa Zanzibar, Khalifa. Na kama nilivyosema kwamba tuna majukumu mawili [sisi] ACT-Wazalendo, yaani wajibu wetu unagawika katika namna mbili. Kwa upande mmoja sisi ni sehemu ya Serikali kwa upande wa Zanzibar lakini kama chama kitaifa sisi kwa upande wa [Tanzania] Bara hatumo kwenye Serikali kwa hivyo ni chama cha upinzani.

Na hili kwa watu wengi wanaliona kama ni jambo la ajabu lakini unapofuatilia siasa za kiulimwengu haya sio mambo ya ajabu. Serikali zozote au nchi zozote ambazo zina mfumo wa Serikali ambao una Serikali kuu na baadae una Serikali katika nchi washirika basi unayakuta hayo. Ni kama ambavyo ukienda Uingereza unaweza ukakuta vyama fulani ni chama cha upinzani katika Bunge la Uingereza, kwa mfano Scottish Nationalist Party ni chama kinachotawala Scotland lakini ni chama cha upinzani katika Bunge la Uingereza. Ni hivyo hivyo kama ambavyo ACT-Wazalendo unakuta, mifano kama hiyo ipo mingi. 

Kwa hivyo, kwa upande wa Zanzibar kuna mambo ambayo kama nilivyosema tunayafanyia kazi ambayo ni yale ambayo kiongozi wetu marehemu Maalim Seif Shariff Hamad aliyataka yasimamiwe na Serikali ya Umoja wa Kimataifa na hayo ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi. Kwa mfano, kuzungumzia vipi tutakuwa na marekebisho ya mfumo wa uchaguzi ambao utajumlisha masuala ya marekebisho ya sheria za uchaguzi, marekebisho ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar, marekebisho ya mifumo ya uandikishaji wapiga kura, ukataji wa majimbo ya uchaguzi na mambo kama hayo? 

Lakini upande mwingine tunazungumzia vilevile marekebisho ya vyombo vya dola hasa kwa yale ambayo yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Zanzibar, kwa mfano vikosi vya SMZ, uajiri wake, mafunzo yake, mafunzo yake ya kazi visitumike kisiasa kama ambavyo imekuwa ikifanyika hata hayo pia yamo katika ajenda ambazo tunazisimamia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

Kuna masuala, kwa mfano, yanayohusu vipi tunachukua hatua dhidi ya yaliyofanyika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020? Tunawapatiaje fidia watu ambao wameathirika? Kuna watu wamepoteza watu wao waliuawa. Kuna watu wameathirika kiafya wamepata ulemavu. Kuna watu ambao wameathirika katika mali zao. Lakini vile vile kuna masuala ya kuchukua hatua dhidi ya watendaji wa maovu yale, nini kinafanyika ili mambo yale yasiweze kujirejea? Kwa hiyo, haya yanahusu labda mifumo ya uchaguzi lakini vile vile unazungumzia masuala kwa ujumla, masuala yanayohusu mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji wa Serikali, tunaamini kuna mashirika mengi ya umma ambayo hayapaswi kuwepo ambayo yamekuwa yakiingizia hasara Serikali na nchi ambayo shughuli zake zinapaswa pengine kuachiwa sekta binafsi. 

Kuna mambo ambayo tunaamini ukubwa wa Serikali unaweza ukapunguzwa, kiasi gani tunaweza tukaingiza sera ambazo zitabadilisha maisha ya Wazanzibari kwa kuifanya kweli iwe kituo kikuu cha biashara na huduma za uchumi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki? Kwa hivyo, haya tunayafanyia Serikali kwa upande wa Zanzibar. Lakini kwa upande wa ngazi za kitaifa tunasikika na nafikiri mnatusikia na tunaendelea kuamini na kupigania kwa dhati kabisa suala la kuandikwa upya kwa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, kazi hii ilianza mwaka 2014 na inapaswa kukamilishwa na tukisema kukamilishwa hatuzumgumzii Rasimu ya Katiba Pendekezwa ambayo ilitengenezwa na wabunge wa CCM katika Bunge la Katiba baada ya kufanya hujuma kubwa dhidi ya Rasimu ya Katiba iliyotengenenezwa na Tume ya Katiba ya Warioba. Tunazungumzia kuifanyia kazi Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa na Warioba ambayo imetokana na maoni ya wananchi. 

Lakini kweli tunataka kuona kweli kuna mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uendeshaji wa nchi, tukitaka kuona uhuru zaidi wa vyombo vya habari, tunapaswa kuona uhuru zaidi wa wananchi, haki ya kutoa maoni na kusikilizwa, tunapaswa kuona tunaondokana na vizingiti vinavyowekwa katika shughuli za kisiasa, kwa mfano upigwaji marufuku wa shughuli za kisiasa, mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, [na] makongamano, viondolewe. Tunapaswa kuona mageuzi ya Jeshi la Polisi ambalo kwa sasa linaonekana kwamba limeshindwa kabisa kutekeleza kazi zake. Tunapaswa kuona marekebisho katika kazi zake kwa mfano usalama wa taifa unavyofanya kazi zake, tunapaswa kuona kwamba kwa ujumla sera za kiuchumi za nchi zinabadilishwa na kuwa na mfumo shirikishi zaidi. 

Kwa hiyo, hayo ni mambo ambayo tunayasimamia pia kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano. Ni mambo ambayo tunaamini tutayafanyia kazi. Kwa sasa hivi kama mnavyojua chama cha ACT-Wazalendo kimechukua uongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, yaani Tanzania Centre for Democray [TCD], na baadhi ya ajenda hizi tunajaribu kuzisukuma kupitia kipindi chetu hiki cha miezi sita ambacho tutakuwa tukiongoza TCD kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. 

The Chanzo: Brother Jussa, nashukuru sana kwa mazungumzo haya na kwa maoni yako mapana yaliyoshiba; kusema kweli siku zote ni faraja sana kwangu kuzungumza na wewe kwa sababu kuna busara na hekima najipatia. Sasa, watu wanasema unarudi lini Twitter, watu wanasema wameku-miss wanapenda kupata mitazamo yako kuhusiana na mambo yanayoendelea umewaacha. Kwa hiyo, ndo umeachana kabisa na matumizi ya Twitter ama ni vipi? 

Ismail Jussa: Hapana, nadhani, kama nilivyosema mapema kwamba kulikuwa na lazima kupitia hatua za kujiuguza kutokana na kadhia niliyopitia lakini kama ulivosema mwenyewe nimekuwa nikipita hatua kwa hatua nafikiri kwa sasa hivi nimeonekana katika majukwaa ya kisiasa, nimekuwa nikifanya vipindi vingi vya mahojiano na vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikinifanyia mahojiano. Kwa hivyo, mawazo yangu yanasikika. 

Ambacho bado sijafanya na nakusudia kukifanya karibuni kabisa na cha kukamilishwa ni kurejea katika matumizi ya akaunti zangu katika mitandao ya kijamii. Kwa sababu kama unavyojua sasa hivi vijana wengi wamezoea siasa kuziona katika mitandao ya kijamii. Kumekuwa na masuala hayo. Kuhusu matumizi yangu ya akaunti za zangu za Twitter, Facebook na Instagram ambayo nilikuwa nazo. Kwa hiyo, na huko niwahakikishie kwamba karibuni kabisa wataniona siku si nyingi kutokea leo [Septemba 9, 2021].

The Chanzo: Asante sana, brother Jussa kwa muda wako na nakutakia siku njema kusema kweli.

Ismail Jussa: Asante sana, Khalifa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts