Dar es Salaam. Taharuki ilitokea mnamo Septemba 9, 2021, katika eneo la Msimbazi, Kariakoo, jijini Dar es salaam, baada ya mfanyabiashara mmoja mwenye duka katika eneo hilo maarufu nchini Tanzania kuanzisha mchakato wa kuzitoa meza za biashara zinazomilikiwa na wafanyabishara wadogo, maarufu kama machinga, kwa kile alichodai kwamba kinamzibia wateja.
Hatua hii haikuwafurahisha machinga waliokumbwa na kadhia hiyo ambao kwa kuungana na machinga wengine kutoka eneo hilo walianzisha mvutano mkali na mwenye duka huyo na watu wake kwa kurejesha meza zilizokuwa zikitolewa. Mwenye duka na watu wake wakitoa meza, machinga wanazirudisha. Meza za chuma zilikuwa zikirushwa kama maputo, hivyo kuhatarisha afya za wahusika.
Mvutano huu ambao ni sehemu tu ya mivutano mengi na ya siku nyingi inayowahusisha machinga na wenye maduka nchi zima uliokuwa unarushwa mubashara kupitia mitandao ya kijamii uliisha baada tu ya mmoja wa machinga kuamua kutumia mbinu ambayo mahasimu wake hawakuifikiria: aliamua kuvua nguo zake zote na kuzirejesha meza zote zilizotolewa na mwenye duka mahali zilipokuwa. Hakuna aliyemshika wala kumsumbua na hivyo kuifanya kazi yake kuwa rahisi sana.
The Chanzo ilimtafuta mtu huyu kutaka kupata upande wake na ule wa machinga wenzake baada ya kuongea na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Tanzania Ludovick Kiondo. Thomas Ben ndiyo jina lake, ameniambia. Nikamuuliza, kwa nini uliamua kutumia mbinu ya kuvua nguo kupambana na mahasimu wako badala ya njia nyingine?
Thomas Ben: Ni kweli nilikuwa uchi na nilikuwa najaribu kutafuta suluhu ya lile tatizo na kweli nilifanikiwa kwa namna moja au kwa namna nyingine.
The Chanzo: Kwani kulikuwa na nini hasa?
Thomas Ben: Ni kweli, ugomvi ulitokea baina ya machinga na mmiliki wa duka la Sunderland eneo la jengo la Simba mahali ambapo mwekezaji amewekeza. Chanzo ilikuwa baada ya mwekezaji kuondoa meza za machinga maeneo hayo kisha kuweka nyororo, yaani chain, kuzuia wafanya biashara [machinga] wasifanye biashara eneo lile.
Baada ya kufanikiwa kuweka zile nyororo ilichukua takribani siku tatu baada ya tukio la yeye kuweka zile nyororo na sisi wafanya biashara hatukuweza kufanya ndani ya siku tatu, baada ya kuona vipato vyetu vimezidi kupotea na tunashindwa kupata vipato vya kula watoto basi tulikusanyika wote kwa pamoja na tukaenda eneo la tukio na tukaweza kung’oa vile vyuma ambavyo ameviweka yule mmiliki wa lile jengo.
The Chanzo: Unadhani mbinu ya kuvua nguo ilisaidia?
Thomas Ben: Hatua niliyochukua mimi japo wengi hawakuiunga mkono lakini nafikiri kwenye harakati wanaharakati ni lazima wakuunge mkono. Napenda kutoa hali sintofahamu kwa nini niliweza kuvua nguo? Niliweza kuvua nguo ili kunusuru raia wasipate madhara kwenye ule ugomvi na kweli nilifanikiwa ule ugomvi kuutuliza.
The Chanzo: Ushawahi kukutana na huyo muwekezaji mkazungumza hili suala kwa njia ya amani?
Thomas Ben: Ilikuwa ndo njia moja wapo kubwa, lakini kutokana sikuweza kukutana nae na wala sikubahatika kukutana nae na yeye mwenyewe anasema kwamba yule bwana alikodiwa akaja akavua nguo. Lakini mimi nataka nithibitishe hili: mimi sikukodiwa na mtu kama wamachinga wanavonifahamu mimi. Mimi ni mwanaharakati na ni mfanyabiashara katika lile eneo nina zaidi ya miaka kumi na nne au kumi na tano. Siyo mgeni wa lile eneo yeye [mwenye duka] ndio atakuwa mgeni kwa sababu kwa mara ya kwanza amejaribu kuwekeza katika lile eneo.
The Chanzo: Baada ya lile tukio hujapata kesi au changamoto yeyote baada ya kile ulichokifanya?
Thomas Ben: Baada ya lile tukio sikupata kesi, sikupata changamoto ya aina yeyote ni mambo tu ya kibinadamu.
The Chanzo: Kuna suala la baadhi ya wafanya biashara wenye maduka kutoa bidhaa zao na kuzimwaga nje kama machinga. Je, lipo na unalizungumziaje?
Thomas Ben: Mimi kwa uzoefu niliokuwa nao, zaidi ya miaka kumi na tano, kumi na sita nipo barabarani nafikiri kipindi chote hicho mimi nikiwa kama mfanyabiashara tumeshirikiana na wenye maduka. Lakini sio kwa nidhamu hiyo ya kutoa biashara kwenye duka kwenda kumwaga chini.
Kwanza, aliyeongea vile [kwamba biashara za machinga siyo za kwao ni za wenye maduka] ni mwenyekiti wa wafanyabiashara wenye maduka, ametukosea sana na inatakiwa atuombe radhi. Amemdanganya Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu Hassan] hilo suala sio kweli. Ni amejaribu kuleta siasa zake kwamba aone namna gani sisi tuweze kutoka.
The Chanzo: Kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili yenu kufanya biashara lakini mara nyingi hamkubali kwenda, shida ni nini?
Thomas Ben: Cha kwanza kabisa maeneo yanakuwa sio rafiki. Ninapozungumzia sio rafiki haya maeneo kwanini yanakuwa sio rafiki, unaweza ukatengewa labda uende Machinga Complex [Ilala, Dar es Salaam], ukiangalia Machinga Complex ni sehemu ambayo hata wafanyabiashara wanaotaka Rwanda, Kenya, Burundi, Msumbiji [na] Afrika Mashariki yote nzima ni sehemu ambayo wale wafanya biashara wakubwa hawafiki kwenye maeneo hayo.
The Chanzo: Unaizungumziaje migogoro isiyoisha baina ya machinga na wafanya biashara wenye maduka?
Thomas Ben: Tatizo la machinga ni tatizo la nchi nzima, ili migogoro iishe kuna namna ya kukutana baina ya wafanyabiashara wadogo wadogo na wamiliki wenye maduka. Inawezekana wenye maduka na wao wana lao la moyoni, lakini wanashindwa kuyatoa yao ya moyoni. Na sisi tukawa na yetu ya moyoni lakini na sisi tukashindwa kutoa yetu ya moyoni.