Zanzibar. Juma Mohammed ni kijana mwenye umri wa miaka 27 ambaye kazi yake ni kutembeza watalii. Kazi hii Juma, mkazi wa Tomondo, Mkoa wa Mjini Magharibi, hapa Unguja, ameisomea kabisa, akiwa na Stashahada ya Utalii, na ndiyo kazi aliyokuwa akiifanya kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Mwaka 2020, hata hivyo, Juma na wenzake kadhaa ‘walipunguzwa’ kutoka kwenye kampuni waliyokuwa wakifanyia kazi.
Machi 25, 2020, Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye watu wapatao milioni 1.672 kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Taifa la Takwimu (NBS), ilitangaza kisa cha pili cha mtu aliyekutwa na kirusi ambacho husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). Ilikuwa ni mwanzo wa matukio ambayo yangeweka maisha ya Wazanzibari wengi, husasan wale wanaofanya kazi kwenye sekta ya utalii kama Juma, kwenye hati hati.
“[Kabla ya UVIKO-19] nilikuwa nalipwa Sh450,000 [kwa mwezi] mbali marupupu ya kufanya kazi muda wa ziada na wakati mwengine wageni wanakulipa pia nyongeza,” Juma anaiambia The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu. “Ila kwa sasa, nakaa hapa toka saa nne asubuhi mpaka saa 11 jioni, muda mwengine hakuna hata mtalii. Hapa unapata pesa kidogo sana ni Sh15,000 kwa masaa matatu kumtembeza [mtalii] mjini ambapo zamani ilikuwa ni Sh35,000.”
The Chanzo ilimkuta Juma maeneo ya Forodhani, Zanzibar, sehemu mashuhuri kwa wageni wanaotembelea kisiwa hicho kilichopo katika mwambao wa Bahari ya Hindi. Ni saa saba za mchana tayari na Juma, akiwa amelalalia mkoba wake kwenye kibaraza cha ufukwe, mpaka sasa hajapata mteja yoyote. Anasema leo, Septemba 14, 2021, ni siku ya nne hajapata kazi iliyoweza kumuingizia kipato chochote.
“Wakati mwingine napiga simu kule [nilikokuwa nafanya kazi] kuuliza kama kuna kazi ila [naambiwa] hali bado siyo nzuri,” Juma anasema kwa sauti inayoashiria kukata tamaa. “Kukosa fedha kwangu inaathiri familia yangu maana mimi ndio ninayetegemewa. Serikali ingeangalia jinsi ambavyo itaweza kutusaidia hata mikopo ili maisha yetu yaendelee.”
UVIKO-19 ilivyoathiri uchumi wa Zanzibar
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa Julai 29, 2021, hali ya uchumi wa Zanzibar iliathirika zaidi ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na kushuka kwa mapato yatokanayo na utalii ambapo uwiano wa vyumba vinavyokaliwa katika hoteli visiwani humo, occupancy rate, ulishuka mpaka kufikia takribani sifuri.
Hali hii ilichangia kushuka kwa Pato la Taifa la Zanzibar mpaka asilimia 1.3. Hii ni tofauti na kipindi cha nyuma, hususan kati ya mwaka 2017 na 2019, ambapo ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ulikua kwa wastani wa asilimia 7, kwa mujibu wa makisikio ya Wizara ya nchi, Afisi ya rais wa Zanzibar Fedha na Mipango.
Sekta ya utalii ni sekta muhimu sana kwa uchumi wa Zanzibar kwani inakadiriwa kuchangia asilimia 28 ya Pato la Taifa la Zanzibar na asilimia 60 ya fedha za bajeti ya Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar hutokana na mapato ya utalii, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya dunia ya hivi karibuni. Ripoti hiyo pia inaitaja sekta ya utalii kama muajiri mkubwa visiwani humo hivyo kudhoofika kwake kuna kuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa taifa na hali za maisha za watu kwa ujumla.
Shughuli kubwa za kiuchumi zinazohusiana na utalii ambazo zimeathiriwa zaidi na janga la UVIKO-19 kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Benki ya dunia ni pamoja na usafirishaji na uhifadhi; biashara ya jumla na reja reja; kilimo; masuala ya fedha na bima; na matumizi ya umma na masula ya kibajeti, huku makundi ya vijana na akina mama, hususani wale wanaofanya kazi kwenye sekta za kiuchumi zisizo rasmi, yakitajwa kuwa waathirika wakubwa.
Mmoja kati ya vijana hawa ni Diana Bahati, 24, ambaye kabla ya kuja kwa UVIKO-19 alikuwa akifanya kazi kama mtembeza watalii wa kampuni moja ya utalii mjini hapa lakini akalazimika kupunguzwa baada ya kampuni kuanza kukabiliana na athari za janga hilo ambalo Zanzibar inaendelea kupambana nalo.
‘Ilinibidi nihame Zanzibar’
“Nilipopewa taarifa [za kupunguzwa kazini] nikajua ni jambo la muda tu [kwa hiyo] nikaamua kubaki Zanzibar,” Diana, mama wa mtoto mmoja, anaiamba The Chanzo wakati wa mahojiano kwa njia ya simu kutokea kwao Gongo la Mboto, Dar es Salaam, yaliyofanyika Septemba 15, 2021.
“Ila baada ya miezi mitatu mambo yalikuwa mabaya zaidi maana hata kampuni nayo ikafungwa. Hapo nikaamua kuuza vitu vyangu na kurudi nyumbani kwa mama licha ya kuwa mimi ndo ninayetegemewa [kama mlezi] hapo [nyumbani].”
Diana anasema hali hii ilimsababishia kupata msongo wa mawazo kwani mambo ya kushughulikia yalikuwa mengi huku akiwa hana njia ya kujipatia kipato. Anafafanua: “Sikuwa na chanzo kingine cha kupata fedha hivyo kuanza upya ndo ulikuwa mtihani kubwa. Hakuna tena safari, [maana yake] hakuna tena kazi na majukumu bado ni yangu. Lakini nikaamua nifanye kitu kingine na kwa sasa najishughulisha na kutengeneza urembo wa shanga za mikononi na miguuni.”
Katikati ya barabara kuu iliyopo baina ya Forodhani na jumba la Beit-al-Ajaib, unaweza kuona watembeza watalii ambao wameshika vikaratasi vyao mikononi wakisubiri wageni wawageuze wateja endapo kama watapita kwenye eneo hilo. Hawa hawafanyi kazi na makampuni; wao ni watembeza watalii wa kujitegemea na wanatambulika kiserikali kwani wako na vitambulisho maalumu.
Miongoni mwao – wako kama saba hivi – namuona mmoja akiwa amevalia shati la bluu lenye vyumba vyenye mistari meusi, kiatu cha ngozi rangi ya kahawia na suruali ya jinzi ya mtindo wa zamani akiwa amevaa na miwani pia. Kheri Bakari Kheri, 62, ndiyo jina lake na ananiambia kwamba ameanza kufanya kazi hiyo tangu akiwa na umri wa miaka 19. Lakini sasa hali ni tofauti na zamani.
“Kazi zimekuwa ngumu [kwani] wageni hakuna,” Kheri, baba wa watoto watatu na mkazi wa Shangani, Mkoa wa Mjini Magharib, ananiambia nilipomuuliza kuhusu hali ya upatikanaji wa kazi. “Hata wageni wakija wengi wanakaa ndani hawataki kutoka kwenda kutembea kwa sababu ya [UVIKO-19] na hofu ya watu kutokuchanjwa inawaogopesha.”
Kheri anasema tangu Septemba ianze amepata kazi tatu tu za kutembeza watalii. Wakati mwanzo watalii walikuwa wanamlipa Sh50,000 kwa siku, sasa anapata Sh20,000 tu kwa siku na hio inategemea na mgeni .
Kwa ujumla, wafanyakazi wapatao 2,600 wa mahotelini walipunguzwa kazini ndani ya mwaka 2020 tu, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ndani na Mahotelini – Zanzibar (CHODAWU-Z) Adam Suleiman Simba. Simba anasema hali hii si tu inatishia maisha na familia za wafanyakazi hawa bali pia uhai wa chama chenyewe kwani chama hicho hujiendesha kwa michango ya wafanyakazi hawa ambao ni wanachama wake.
Wawekezaji hali tete
Lakini si Serikali na wafanyakazi tu waliothiriwa na athari zitokanazo na UVIKO-19. Tony Harold ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka kampuni ya Sindband inayojihusisha na utembezaji watalii katika maeneo mbali mbali ya kihistoria hapa Zanzibar. Harold anasema kwamba kati ya Machi 2020 mpaka Septemba 2021, imetoka kuwa na watembeza watalii 25 hadi kubaki na wawili. Pia, imetoka kuwa na madereva sita hadi dereva mmoja.
“Zamani, kwa siku au wiki tunaweza kuwa na wageni 35 hadi 15 kwa uchache ila sasa wakiwa wengi ni watano au watatu,” Harold anasimulia wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Septemba 15, 2021. “Hali ni mbaya zaidi kwani licha ya kuwa hakuna watalii bado tunalazimika kuendelea kulipa kodi. Ni kweli Serikali kuna kipindi ilipunguza [viwango vya kodi] ila suala la kupunguza liendelee hadi hali itakapo kaa sawa.”
Meneja wa Hoteli ya Shangani Florence Ruwa anasema kwamba hoteli hiyo kongwe visiwani hapa ililazimika kuwaachisha kazi wafanyakazi 20 na kubaki na saba tu. Anasema: “Kwa wiki yote hii tumeuza vyumba vitatu tu jambo ambalo si kawaida. Hakuna pesa na bado tunalazimika kulipa kodi kama kawaida.”
Katika jitihada za kuonesha namna hali ilivyo mbaya kwa wawekezaji, Msemaji wa Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) Fatma Ali Mohamed anasema kwamba mwaka 2019 jumuiya hiyo ilikuwa na wanachama 74 na kati ya hao 66 wameshindwa kuendelea na biashara kwa sababu ya athari zinazotokana na UVIKO-19.
Fatma anadhani Serikali kuwa na kigugumizi juu ya hali ya UVIKO-19 nchini Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kulisababisha kuchangia hali hii. Anafafanua: “Suala ya utoaji wa taarifa ni jambo muhimu sana kwenye utalii. Kwa kipindi kile [cha 2020] wageni walikosa taarifa ya hali ya [UVIKO-19] nchini hivyo kwao ikawa ni hofu na hapo ndipo biashara ya utalii iliposhuka na uchumi kuwa mgumu.”
Wamiliki wengi wa hoteli na kampuni za kitalii ambazo The Chanzo iliongea nao walilamikia suala la kodi ambazo wanapaswa walipe kwa mamlaka za Zanzibar. Benki ya Dunia inapendekeza kwenye ripoti yake hiyo ya Julai 29, 2021 kwamba mamlaka za Zanzibar ziache kuzielemea kampuni zilizopo Mji Mkongwe, Zanzibar na badala yake zifikirie kodi nyengine zitakazo tozwa kwa wageni pale wanapoingia nchini au kwa kila usiku watakotumia.
Nassor Abuu Abrahman ni mchambuzi wa masuala ya utalii Zanzibar kutoka Kawa Training College, kituo kinachojihusisha na utoaji wa mafunzo ya utalii, amesema kwamba Serikali haijaweza kutengeneza mfumo mbadala wa kuwasaidia wananchi ambao wameathirika kiuchumi moja kwa moja na athari za UVIKO-19.
“Kwa mfano suala la vijana ambao wanatembeza watalii wanatakiwa kulipa dola 100 [sawa na Sh230,000] kila mwaka na kuna vijana ambao wametoka vyuoni hawana kazi na hakuna kazi, wanawezaje kulipa pesa hio?,” anasema Nassor. “Hivyo, maisha yamesimamia. Serikali iangalie uwajibikaji wa kutatua changamoto kwenye sekta hii ili kupunguza athari.”
Hali inaanza kubadilika
Hata hivyo, kuna matumaini kwamba hali inaweza kubadilika na hivyo biashara kurudi katika hali yake ya zamani. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Tume ya Utalii Zanzibar zilizotolewa Julai 2021, hali ya utalii Zanzibar inaonekana kuimarika huku jumla ya watalii walioripotiwa kuingia visiwani humo kwa miezi saba ya kwanza ya 2021, yaani Janauri mpaka Julai, walifikia 218,512 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35.7.
Ongezeko hili linatokana, pamoja na mambo mengine, na kuongezeka kwa watalii kutoka nchini Urusi wanaokisiwa kuongezeka kwa asilimia 767, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Julai 2020 watalii 7,855 walioingia Zanzibar walitoka Urusi. Kati ya Januari na Julai 2021, watalii 68,169 wametoka Urusi, na kufanya nchi ya Urusi kuongoza kwa kuleta watalii wengi zaidi kwa miezi saba ya mwanzo ya mwaka huu ikichukua asilimia 31.2 ya soko lote la utalii.
Kwa mujibu wa Waziri wa Utalii na Mambo Kale Lela Muhamed Mussa, mabadiliko haya yanatokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Zanzibar katika za kuimarisha sekta ya utalii nchini humo, ikiwemo kuhimiza utalii wa ndani pamoja na kulenga masoko mengine yaliyopo ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
“Lakini pia tumeandaa mpango wa kuifufua [sekta ya utalii] Zanzibar kwa kuhakikisha kwamba tunachukua hatua ambazo zinakubalika duniani kote [za kukabiliana na UVIKO-19],” Lela aliwaambia waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena, Zanzibar, Septemba 24, 2021. Alikuwa akiwaeleza kuhusu Maonesho ya Biashara ya Kitalii yatakayofanyika Arusha, Octoba 2021. “Kama Serikali, tunahakikisha hatua hizi zinafuatwa kwenye maeneo yote ya nchi yetu ili wageni waweze kuona kwamba Zanzibar ni sehemu salama ya kutembelea.”
Lakini hatua hizi haziishi kwenye kudhibiti ueneaji wa ugonjwa hatari wa UVIKO-19 tu. Mnamo Septemba 24, 2021, kwa mfano, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi alitangaza mpango wa kuwapatia vitambulisho maalumu wafanyabiashara wadogo wadogo visiwani humo ikiwa ni sehemu ya kuwatambua ili iwe rahisi kuwasaidia. Hatua hii ilienda sambamba na kutangazwa kwa Shilingi bilioni 100 na Serikali ya Zanzibar zinazolenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo visiwani humo.
Rais Mwinyi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kamba Serikali itatoa Shilingi bilioni 50 na benki za kibiashara visiwani humo zitatoa Shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kiujasiriamali Zanzibar, hususani katika maeneo ya mikopo, mafunzo na masoko.
Najjat Omar ni mwandishi wa habari za kijamii kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.