Dar es Salaam. Inaonekana ni kama vile utekelezaji wa mpango wa wasanii kuanza kulipwa mirabaha kwa kazi zao zinazotumika kwenye runinga, redio, mitandao na kumbi za starehe utachukua muda zaidi kuliko vile ilivyokuwa imeahidiwa awali, The Chanzo imebaini.
Mpango huo uliotangazwa kwa mbwembwe nyingi mnamo Juni 15, 2021, na Rais Samia Suluhu Hassan, na kupigiwa chapuo na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) mnamo Septemba 15, 2021, ulitegmewa kuanza Disemba 2021.
Lakini mpaka wakati wa kuandika habari hii, wasanii wameieleza The Chanzo kwamba hawajaanza kupokea mirabaha hiyo, huku wengi wakibainisha kwamba hawajui hata mchakato wenyewe umekwamia wapi.
“Binafsi bado sijalipwa mrabaha wowote,” Kala Jeremiah, msanii wa miondoko ya rap, ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano ya simu ya hivi karibuni. “Na sina uhakika kama mirabaha imeanza kukusanywa na kama itakuwa imeanza kukusanywa basi hiyo itakuwa ni habari njema.”
Wasanii wanafaike na kazi zao
Ahadi ya kuanza kulipa wasanii mirahaba ilijengwa kwenye misingi kwamba sanaa imekuwa ikikua kwa kasi nchini Tanzania na kutoa ajira kwa vijana wengi ambao vinginevyo wangekuwa bila kazi.
Lakini licha ya ukweli huu, kuna muafaka miongoni mwa wadau wa sanaa nchini kwamba mafao ya sanaa kwa wasanii hayaendani na kasi ya ukuaji wa sanaa yenyewe nchini.
Ni katika muktadha huu ambapo Serikali, kama sehemu ya kujaribu kutatua changamoto hii, imekuwa ikiahidi kuanza kutekeleza mpango wa wasanii, hususan wale wa muziki, kuanza kulipwa mirabaha inayotokana na matumizi ya kazi zao.
“Nataka kuaarifu vijana kuwa kuanzia Disemba [2021] wasanii wataanza kulipwa mirabaha yao kutokana na kazi zinazotumiwa kwenye runinga, redio na mitandaoni,” Rais Samia alisema wakati akiongea na vijana huko Mwanza mnamo Juni 15, 2021.
Rais Samia hakuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa kutoa ahadi hiyo.
Mnamo mwaka 2019, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe alisema kwamba Agosti 28, 2019, ndio itakuwa mwisho wa kazi za sanaa kutumika bila kulipia, akizungumzia zaidi redio, kumbi za starehe na vyombo vya usafiri.
COSOTA ilitangaza baada ya tamko hilo la Rais kuanza utekelezaji wa haraka wa agizo hilo, huku ikisema kwamba kwenye mirabaha itakayokuwa inakusanywa, msanii husika atapokea asilimia 70 huku COSOTA wakibaki na asilimia 30 itakayowawezesha wao kama chama kufuatilia makusanyo hayo
Ilikuwa ni hatua nzuri ambayo ingeiunganisha Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kama vile Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Ghana na Malawi ambayo yanatajwa kutekeleza mpango huo kwa wasanii wao.
Utekelezaji wakwama
Lakini kwa mujibu wa mazungumzo tuliyoyafanya na wasanii mbalimbali, hali inaonekana kuwa tofauti takriban mwezi na nusu tangu mpango huo utegemewe kufanya kazi.
“Hakuna utaratibu wowote [wa malipo], ni maneno tu,” anasema Ahmed Sadallah, maarufu kwa jina la kisanii Galatone. “Hakuna utaratibu wowote ambao umefanyika na hiyo mirabaha yenyewe watu hawajaanza kulipwa kwa sababu kuna wengine wanakubaliana na hiyo hali kwamba walipwe hiyo mirabaha lakini kuna wengine hawataki wanadai hiyo hali itaua mziki.”
Ni kweli. Siyo wasanii wote waliounga mkono wakati mpango huu unatangazwa. Baadhi ya wadau walibainisha kwamba kulazimisha utaratibu huo utumike Tanzania utapelekea runinga, redio na DJs wengine kupiga nyimbo za Ki-Nigeria, Ki-Afrika Kusini na nyenginezo ambazo hazina uhaba wa mashabiki nchini.
Hata hivyo, baadhi ya wasanii walioongea na The Chanzo wanaona huo ni utaratibu mzuri, na licha ya kwamba mpaka sasa haujaanza kufanya kazi, ipo siku utafanya kazi na wasanii watanufaika na kazi zao.
Moja kati ya wasanii hawa ni Frenk Felix anayejulikana kwa jina lake maarufu la Foby. Akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu, Foby anasema: “Mimi sijapata taarifa yoyote labda kwa [wasanii] wenzangu [wanaweza wakawa wameanza kulipwa]. Lakini nafikiri tutapata tu taarifa na ninafikiri labda kuna programu hazijakaa sawa.”
The Chanzo imejaribu kumtafuta waziri mwenye dhamana ya kusimamia sanaa nchini Mohamed Mchengerwa pamoja na COSOTA ili kufahamu nini kinaweza kuwa kimekwamisha utekelezaji wa mpango huu. Hata hivyo, juhudi zetu hazikuzaa matunda baada ya kushindwa kuwapata.
Wakazi, msanii wa miondoko ya rap, mwanaharakati na mwanasiasa, ameiambia The Chanzo kwamba amehuzunika kuona kwamba mpango huu haujaanza kufanya kazi lakini hajashangaa.
“Miezi sita ilikuwa ni michache sana kuanza utekelezaji wa mpango huo, tena nchi nzima,” anasema Wakazi, akiongelea mara ya kwanza ahadi hiyo ilitolewa Juni 2021. “Na haya mabadiliko ya mara kwa mara ya mawaziri yananipa hofu kwamba huu mchakato unaweza kusahaulika, ingawaje Katibu Mkuu [Wizara ya Sanaa, Dk Hassan Abbasi] amebakishwa.”
Urithi pekee wa msanii
Wakazi, ambaye aligombea ubunge kwenye jimbo la Ukonga kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia tiketi ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo, anaamini mfumo wa kulipa wasanii mirabaha haukwepeki kama kweli Tanzania imedhamiria kuimarisha sanaa yake na maslahi ya wasanii.
“Ulipaji wa mirabaha ni kitu sahihi cha kufanya,” Wakazi ameieleza The Chanzo. “Sanaa yetu kwa sasa haina thamani yoyote. Mirabaha itawahamasisha hata wasanii wa kimataifa kufanya kazi na sisi kwa kujua kwamba kuna kitu watapata.”
Ukizingatia ukweli kwamba pesa zinazotokana na mirabaha zinakuwa ni za kudumu, Wakazi anasema huo ndiyo urithi pekee ambao wasanii wa Tanzania wanaweza kujivunia.
“Bob Marley [gwiji la muziki wa reggae] amefariki mwaka 1982,” anasema Wakazi, “ila wajukuu zake hawawezi kukosa ada ya shule [kwani bado anaendelea kulipwa kwa kazi zake].”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.