Dar es Salaam. Moja kati ya matatizo makubwa ambayo wadau wa haki za binadamu wamebainisha kuwa yanaukumba mfumo wa utoaji haki nchini Tanzania ni namna mfumo wa haki jinai wa taifa hilo la Afrika Mashariki ulivyotengenezwa kwa kuipa nguvu maradufu Serikali ya kuamua hatma ya mshukiwa huku Mahakama ikipokwa nguvu hiyo.
Pengine hakuna sauti muhimu nchini linapokuja suala la umuhimu wa kurekebisha mfumo wa haki jinai Tanzania zaidi ya Tito Magoti, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambaye pia alishawahi kuwa muhanga wa mfumo huo na kukumbana na madhila yake.
Kuweza kufahamu mambo mbalimbali yanayohusiana na mfumo wa haki jinai na namna za kuuboresha, mwandishi wetu Shafii Hamisi amefanya mazungumzo na Tito Magoti kama sehemu ya mfululizo wa podcast yetu iitwayo The Chanzo Podcast. Endelea …
The Chanzo: Mwananchi wa kawaida angependa kufahamu ni ipi, au ni zipi, changamoto kubwa ambazo zinaukabili mfumo wa haki jinai nchini Tanzania na labda ungeweza kwa kuanza kwa kutueleza kwa ufupi tunaposema haki jinai tunakuwa tunamaanisha nini?
Tito Magoti: Asante mwandishi, nafurahi kuzungumza na wewe leo. Tunapozungumzia haki jinai tunamaanisha taratibu za washitakiwa, ama washtumiwa, wa makosa fulani fulani ya jinai wanavyoshughulikiwa, ama wanavyodhibitiwa na sheria zetu. Mtu akikuzaba kofi apate haki yake na wewe upate haki yako.
Kama haki yake ni kuadhibiwa basi astahili kuadhibiwa na kama haki yako ni kupata tamko kwamba kweli ulizabwa kofi na kuona nafuu ya kwamba mtu anaadhibiwa basi ionekane hivyo. Ama kutibiwa kutokana na maumivu na kadhalika na kadhalika.
Sasa, kimfumo, [nchini Tanzania] tuna taasisi ambazo zinadhibiti masuala fulani fulani. Mfumo huo wa haki jinai [unaamua mambo kama vile] unapofanyiwa tukio la jinai unakwenda wapi? Utaenda polisi. Polisi wataenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwa niaba yako, kama ni Mahakama kuanzia ya wilaya yataenda mahakamani. Kwa hiyo, hapo umeona kuna polisi, kuna Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma [na] kuna Mahakama.
Kwa hiyo [hao], ni taasisi, ama ni wadau [wa haki jinai]. Lakini zaidi kuna wadau kama Magereza ambao wanahifadhi, wanakaa na watu ambao ni washukiwa wa makosa ya jinai. Lakini kadhalika wanakaa na wafungwa ambao wametamkwa kuwa wafungwa na wanastahiki kutumikia adhabu wakiwa magerezani.
Kwa hiyo, hao ni wadau wa haki jinai. Lakini sasa kwa Tanzania mambo ni mengi katika mfumo huu na kwa sababu shabaha ya mazungumzo haya ni kujaribu kuonesha changamoto ambazo pengine ni za kimfumo ambazo pia ni za kimsingi ambazo kama taifa tunafaa kuzimulika na kuzipatia majibu.
Sitajielekeza huko zaidi na nitapenda kuzungumzia masuala kama matatu au manne ambayo yakipata majibu yanaweza yakatuvusha, hata kutuondolea sintofahamu iliyopo katika mfumo wetu wa utoaji haki, hususani ya kijinai. Suala la kwanza ni upelelezi.
Upelelezi kwa sababu ni tatizo na kuona hata viongozi wa ngazi za juu, hata Mheshimiwa Rais marehemu [John] Magufuli katika moja ya hotuba yake katika Wiki ya Sheria alikiri kwamba upelelezi ni tatizo sugu. Simaanisha kwamba imekuwa ni tatizo kwa sababu Rais Magufuli alikiri lakini nataka kuonesha kwamba ni kilio ambacho hadi viongozi wamekiri kwamba kimewashinda.
Kwa hiyo, baada ya malalamiko yake Mheshimiwa Magufuli alisema kwamba tuwaombee wapelelezi na akaenda mbali zaidi akasema kwamba wapelelezi tuwaombee wanaweza wakalaaniwa na vitu vya namna hiyo. Kwa hiyo, unaona kwamba ni jambo kubwa la kitaifa ambalo limesikika kwa sauti za hali ya juu lakini bado limebaki kuwa vile vile.
Na upelelezi ni shida kwa sababu wapelelezi, kwa mujibu wa sheria zetu, wanaruhusiwa kumshtaki mtu yeyote kabla ya upelelezi haujakamilika. Na hili ni kwa makosa yote. Kwamba wakikushuku basi wanayo fursa ya kukupeleka hata jela kabla hawajakamilisha upelelezi.
Lakini pili upelelezi kuna makosa ambayo yana ukomo. Mtu akishtakiwa, kwa mfano, makosa ya kawaida, ikiwa ni pamoja pia na makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, sheria imeweka ukomo [wa] miaka mitatu katika upelelezi. Kwa maana kwamba ndani ya siku sitini, ambayo ni kama miezi miwili, mtu anaposhtakiwa kwa kosa kama hilo, yakiwemo pia makosa ya ubakaji, basi awe amesikilizwa, yaani kesi iwe imesikilizwa ikiwa haijaanza kusikilizwa inafutwa ama inaondolewa mahakamani.
Lakini kuna makosa ambayo hayana ukomo wa upelelezi. Siyo kesi nyingi sana kama uhujumu uchumi. Bwana James Lugemarila alitoka jela baada ya kukaa miaka minne, lakini miaka yote minne upelelezi wa kesi yake ulikuwa haujakamilika.
Kuna mifano mingi ya watu ambao wamekaa jela kwa kipindi hicho na wakaja kuachiwa baada ya upelelezi aidha kukamilika, kwa sababu huwa hatuambiwi kama umekamilika, [watakwambia] tumegundua huhusiki ama imekuaje. Kwa sababu huwa wanaachiwa kwa nolle prosequi, ambayo ni kanuni inayompa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuondoa shtaka mahakamani.
Kwa hiyo, tumekuwa tunaona kama mambo matatu kwenye upelelezi. Na imekuwa ni sugu, ni sugu sana katika mfumo wetu wa haki jinai kiasi kwamba imekuja kuleta maumivu mengi kuliko nafuu. Kwa sababu Mahakama zimekuwa hazina nafasi ya kutamka neno lolote, ama kuamuru chochote pale ambapo sheria haijaweka ukomo wa upelelezi.
The Chanzo: Umetolea mfano hapo huyo aliyeweza kukaa miaka minne mpaka kukamilika kwa upelelezi au akaja kutoka. Unadhani ni nini haswa ambacho kinapelekea mtu anakaa gerezani kwa miaka hiyo minne halafu baadae anakuja kuachiwa au pengine anakaa miaka kumi halafu anakuja kuachiwa, yaani ana kaa bila kutiwa hatiani halafu anakuja kuachiwa?
Tito Magoti: Ni ukoloni tu wala sio kitu kingine. Ni ukoloni tu kwa sababu viongozi wanaamua kwa niaba yetu. Kwa hiyo, kwa sababu ni maamuzi yao basi ni maamuzi yetu tunayamiliki ni kwamba kama taifa tunaona hiyo ni haki sawa sawa.
Kwa hiyo, ni ukoloni tu na sisi tumeamua kuishi humo kwenye ukoloni ambao mimi binafsi naupinga sana. Hakuna sababu ya kumkamata mtu kama haujakamilisha upelelezi. Hakuna sababu ya kumuweka mtu jela mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu kwamba upelelezi haujakamilika. Na hakuna sababu ya kuwa na Mahakama ambazo zinaangalia, yaani ambazo mambo haya yanafanyika mbele yake.
Kuna hakimu anaahirisha kesi mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne. Sasa huyo anailinda haki ya nani? Kwa hiyo, hakuna sababu ya maana ya kuwa na sheria za namna hii. Hakuna sababu yoyote. Mimi nikiitafuta siwezi kuipata kabisa.
The Chanzo: Je, kwa mujibu wa sheria, kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa kufahamu kwamba wewe ni mwanasheria, mtu wa kawaida angependa kufahamu sheria inaruhusu mtu kukamatwa kabla uchunguzi kukamilika?
Yaani ni mtuhumiwa akakamatwa, akafungiwa halafu uchunguzi ndio ukafuata na hiyo haitajalisha uchunguzi utachukua muda mrefu kiasi gani? Ama vyombo husika inabidi vifanye kwanza upelelezi halafu vikishajiridhisha na upelelezi ukiwa umekamilika ndiyo mshtakiwa akamatwe, ama huyo mtuhumiwa akakamatwe?
Tito Magoti: Hiyo ni hoja ya maana sana. Ni hoja ya maana sana kwa sababu hata sasa hivi bado kuna mabishano kwamba je, hii ni sahihi? Nasema ni sahihi kwa mujibu wa sheria zetu. Sheria yetu za mwenendo wa makosa ya jinai, sheria za uhujumu uchumi, ni sahihi, kwa mujibu wa hizo sheria na hili tukija kufikiri kama binadamu na watu ambao ni tuna upeo na ufahamu ni sahihi kwa mujibu wa Katiba.
Siyo sahihi. Siyo sahihi hususani unapomuweka mtu kizuizini kwa sababu unamfunga, kizuizi ni kizuizi tu yaani ni kifungo tu hata kama mtu haijatamkwa kwamba amefungwa. Kwa nini unizuie ndani wakati huo huo natuhumiwa tu? Kwa nini usinipe dhamana nisikilizwe ikithibitika basi nifungiwe ndani? Tukifikiria kama binadamu utagundua kwamba sio sawa sawa.
Yaani sio utamaduni mzuri ambao tunatakiwa kuufurahia ama kuuendekeza. Kwa nini tusirudi kwenye misingi ya haki za binadamu? Kwa sababu mimi ni mwanaharakati. Kwenye misingi ya haki za binadamu kanuni za kiulimwengu za haki za binadamu likiwemo Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, mikataba ya kimataifa kwenye mikataba ya haki za kisiasa na haki za kiraia, kuna mkataba ambao unazuia mateso kwa watu.
Hii [mikataba] yote imezuia mateso kwa watu. Imezuia haya mambo kwamba sio sawa sawa kumuweka mtu kizuizini bila kumshtaki na sio sawa sawa kumuweka mtu kizuizini kabla upelelezi haujakamilika. Kwa nini? Kwa sababu tunahitaji kulinda ile dhana ya kwamba huyu mtu hajatamkwa kuwa mhalifu. Sasa tunailinda vipi hii dhana wakati huyu mtu tunamfungia jela ama tunamkamata wakati upelelezi haujakamilika halafu tunakuja kumwachia baadaye?
Kwa hiyo, katika hivyo vipimo viwili, kipimo cha kwanza cha sheria zetu inaonekana ni sahihi katika macho ya hiyo sheria. Lakini katika kipimo cha haki [siyo sahihi]. Ndiyo maana tuna haki na sheria. [Hivi] ni vitu viwili tofauti. Katika vipimo vya haki, hiki kitu sio tu kwamba sio sawa lakini pia hakikubaliki na ndio maana katika mataifa yaliyokubali ustaarabu, kwa sababu sisi bahati mbaya ustaarabu wetu upo katika maandishi, mataifa ambayo yameweka vitendo na wanatekeleza yameondokana na hizi blaa blaa.
Polisi watimize wajibu wao wanapowaandikia watu kesi. Wanandaa mashtaka ya kubumba kwa kufahamu kwamba hawa watu watakwenda jela. Hawa watu watafungwa tumkomeshe huyu Shafii [Hamis, mwandishi], si ndio? Wakisema tukomeshe wanakukomesha. Kwa sababu wana huo uwezo wa kutumia sheria kukukomesha.
Kwa hiyo, katika macho ya haki haikubaliki hata kidogo na hata sasa hivi kuna mabadiliko ya sheria yamekuja ambayo kwa maoni yangu ni mepesi tu. Ni mabadiliko mepesi kwa sababu sheria imetamka kwamba usimshtaki mtu kabla upelelezi haujakamilika lakini ni kipimo gani ambacho Mahakama itatumia kujiridhisha kwamba upelelezi umekamilika? Ni kikao cha kwanza au ni kikao cha pili ama ni kikao cha tatu?
Nikiongelea kikao cha kwanza ni siku ambayo kesi inatajwa. Mtu anashtakiwa siku ya kwanza. Je, itaanza hapo hapo kwamba huyu mtu asikilizwe hapo hapo ama hatua zianze ama ni kikao cha pili? Kikija kikao cha pili ni siku 14 zinazofuata huyu mtu akiwa jela. Lakini pili sheria hii mpya inayoeleza kuzuia kushtaki kabla ya kupeleleza ni kwa baadhi ya makosa.
Hii sheria haijaelekeza ni nini kifanyike endapo litapelekwa shauri mahakamani kabla upelelezi haujakamilika. Marekebisho ya sheria pia hayajajibu hilo swali ambalo mimi nakuhakikishia ni kwamba sio sawa sawa kwa misingi ya haki na kwa misingi ya utawala wa sheria nzuri.
The Chanzo: Sawa sawa. Ninavyojaribu kuelewa ni kwamba hapa umesema kuna sheria lakini pia kuna haki za binadamu na kutokana na maelezo yako jinsi ulivyoelezea hapa naweza kuona kwamba hivi vitu viwili ni kama vinakinzana kwamba kwa mujibu wa sheria za Tanzania zinaruhusu mtu akamatwe kwanza halafu ndipo upelelezi ufuate, sivyo?
Lakini pia kwa haki za binadamu hiki kitu sio sawa. Unadhani shida ipo wapi hapa, kwa sababu mimi ninaamini Tanzania kama nchi ya kidemokrasia inazingatia pia haki za binadamu. Ninachotaka kujua ni kwamba kwa nini kuna hizi tofauti mbili hapa?
Tito Magoti: Nimekupata, nimekupata. Sina majibu lakini maoni yangu ni kwamba sisi tuna utamaduni wa kutokusikilizana ambao pia ni utamaduni wa kutokuheshimiana kwa sababu sio mara ya kwanza aidha sisi au mimi au watu wengine walioanza kuzungumza kabla yetu kuonesha kwamba sheria ya namna hiyo haiafikiani na matakwa ya haki na pia sio kweli kwamba watunga sera na wafanya maamuzi kwa maana ya viongozi hawajui hivi vitu.
Kwa hiyo, sisi shida yetu ni kwamba hatuheshimiani kama binadamu. Lakini shida ya pili ni kwamba hatushirikishwi kwenye kuamua haya mambo ambayo yanatuhusu kama binadamu. Nataka nikwambie mwandishi miaka mitano iliyopita nimeshuhudia ukamataji wa watu na kuwabambikia kesi katika kiwango ambacho hakijawahi kutokea kwenye historia ya hii nchi.
Na pengine ndiyo kipindi ambacho tumekuwa na makosa mengi sana yasiyokuwa na dhamana na tumekuwa na makosa mengi sana ya uhujumu uchumi. Yaani unakuwa na watu jela, yaani watu wenye wadhifa, wafanyabiashara, wataalamu mafungu na mafungu wapo jela.
Lakini baadhi yao ni watu ambao wamekuwa kwenye maamuzi na wangeweza kubadilisha haya mambo ili wasiyakute na mimi nimepata fursa ya kupata kuonana na hawa watu tukiwa jela wanakiri kwamba hivi vitu hawakuwa wanaviona tunavyoviona kama tukiwa jela walikuwa wanaviona kivingine. Sasa shida ni nini? Shida ni kwamba hatusikilizani na hatuheshimiani.
The Chanzo: Kutokana na hayo ambayo umeyasema kwamba kuna mambo ya kubambikiziana kesi, mambo ya kukamata kamata watu. Uliweza kuandika barua ya wazi kwa Rais Samia ukimueleza hatua gani za kuchukua ili kurekebisha mfumo wa haki jinai nchini. Nilitaka kufahamu kama endapo ulipata mrejesho wowote kutoka kwa mamlaka za nchi kufuatia wito ule?
Tito Magoti: Mamlaka ziliitikia na wameendelea kwa sehemu yao kufanya wanachoona wanaweza kufanya na siwezi kumiliki matokeo peke yangu kwa sababu hii lugha ya kwamba tupo kwenye mchakato, tupo kwenye mchakato wa kubadilisha hiki wameambiwa wengi sikuambiwa peke yangu.
Kwa hiyo, ninafikiri kwamba kuna mambo yanafanyika lakini bado kazi ni kubwa na tunahitaji kuendelea kupaza sauti. Kuna watu waliachiwa walifutiwa mashtaka. Kuna kesi zimeondolewa mahakamani. Kuna watu weondolewa makosa yasiyokuwa na dhamana wapo uraiani kwa sehemu.
Hiyo ilikuwa ni njema lakini kwangu mimi napenda kuona vitu ambavyo ni endelevu kwa maana kwamba hatua endelevu ni pamoja na kufuta sheria zote ambazo ni kandamizi. Kufuta, unajua kufuta?
Kufuta na kuondokana na sheria zote ambazo ni kandamizi na kuwa na sheria ambazo zinaoana na matakwa ya haki. Matakwa ya utu na haki. Huo ndiyo muafaka ambao tunahitaji kuuona na ndio mustakabali wa mtu yeyote anayejua haya masuala vizuri.
The Chanzo: Sawa sawa, na je, mpaka sasa unadhani ni kitu gani ambacho kimebadilika tangu uandike ile barua na kama labda pengine ungepata nafasi ya kuandika barua nyingine ni kipi ambacho ungekitoa kwenye barua yako ya mwanzo?
Tito Magoti: Kuna vitu vidogo vidogo vingi vimebadilika. Kwa mfano, kumekuwa na kupungua kwa matumizi ya mamlaka kwa baadhi ya watu. Kwa mfano, tulikuwa tuna sheria watu wanashtakiwa kwa maelekezo ya moja kwa moja imepungua kwa sehemu.
Lakini napoteza kujiamini sana kulizungumzia hili kwa sababu ninapoongea mzee wangu Freeman Mbowe [Mwenyekiti wa CHADEMA] yupo jela kwa maelekezo. Kwa hiyo, kuna vitu vimepungua vidogo vidogo lakini kuna vingine ivinaibuka.
Lakini pia tunaona idadi ya watu magerezani waliokuwa na kesi za uhujumu uchumi na kesi za kisiasa zimepungua japo bado kuna watu wetu, kuna washirika wetu wapo magerezani.
Tunaona pia hizi jitihada za kurekebisha sheria ambazo ni jitihada chanya na rai yetu kwamba tutaendelea kusikilizana na kuona mambo makubwa zaidi kama tukiamua kwa dhati kwamba tunayahitaji.
The Chanzo: Sawa sawa. Wakati tukielekea kumalizia malizia, ulikosoa namna ya Wiki ya Sheria inavyoadhimishwa nchini Tanzania kwenye andiko lako la hivi karibuni. Unadhani ni namna gani bora ya kuadhimisha wiki hii muhimu?
Tito Magoti: Hii ni kwa wanasheria na wadau wote wa sheria: tuache mazoea, tuache mazoea. Kwa sababu hatuwezi kuwa tunaadhimisha Wiki ya Sheria halafu tunaenda kujifungia Kisutu, [Dar es Salaam] tunaweka mabango pale kwamba tunatoa msaada wa kisheria kwa mtu gani wa kawaida mwenye ujasiri wa kwenda Kisutu.
Kwa sababu watu wanajua pale Kisutu. Watu wanakamatwa wanashtakiwa ni mahakama au uweke msaada wa kisheria pale viwanja vya Mahakama Kuu nani ataenda pale? Tuwafuate watu tondoke kwenye utamaduni twende kwenye vitendo tuwahudumie watu.
Tumewahi kuwa na Wiki ya Sheria [kwenye viwanja vya] Mnazi Mmoja, [Dar es Salaam] pale watu wanakuja. Lakini tubaini maeneo ambayo yanauhitaji wa huduma tupeleke huduma tusikae mjini tunagawana pesa, tunagawana nauli, hatumsaidii mtu yeyote. Na hii ni changamoto kwa Mahakama kuna watu wanahitaji msaada kweli kweli.
Twende magerezani kuna watu wanahitaji kuambiwa tu kwamba bwana wewe suala lako fanya hivi, anatoka jela. Wewe nipe namba ya ndugu yako nampigia akudhamini. Kuna watu wengi wanauhitaji. Tusifanye vitu ambavyo ni vya bei nafuu kwa sababu havitusaidii na tunazidanganya nafsi zetu kwa sababu Mungu hadhihakiwi na hadanganyiki.
The Chanzo: Sawa sawa. Tito, mwisho kabisa ukiwa kama mwanasheria, lakini vile vile mwanaharakati wa haki za binadamu, wewe unaitathimini vipi hali ya haki za binadamu kwa ujumla nchini Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kama kuna wito wowote ungependa kuutoa kwa wadau wa haki za binadamu nchini?
Tito Magoti: Mambo ni mengi lakini kwa ujumla namsihi sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan afungue milango ya mazungumzo na majadiliano. Yaani mimi nikitaka kujadiliana na wewe jambo fulani, mimi nikitaka kumpigia simu kiongozi fulani nisiogope yaani afungue hiyo milango.
Afungue anga la kisiasa kwa sababu mambo yetu mengi yanaathiriwa na siasa. Aruhusu watu kufanya shughuli zao, wawe ni watu wa vyama vya siasa wafanye shughuli zao, wawe ni watu wa biashara wafanye shughuli zao kwa uhuru, wawe ni vyombo vya habari wafanye shughuli zao kwa uhuru na kadhalika na kadhalika.
Kwa hiyo, anga la kisiasa likifunguliwa Mahakama itafunguka, Bunge litafunguka, kila kituo kitafunguka kwa sababu kufunga hili anga la kisiasa ndio kumekuja kufunga hivi vitu vingine vyote.
Kwa hiyo, ninamsihi sana mama yangu kama anaweza kufanya hivyo afanye kwa sababu kama hawezi bahati mbaya kwamba hali itaharibika zaidi na lawama zitaenda kwake na lawama zitaenda pia kwa watu wanaomuhusu na majirani zake na maumivu yatakuja kwetu kama taifa, lakini hatutaki kuona vitu vinatokea namna hiyo.
The Chanzo: Sawa sawa. Na unaitahimini vipi sasa hali ya haki za binadamu kwa ujumla nchini?
Tito Magoti: Tunasua sua tu.
The Chanzo: Tunasua sua ukimaanisha kwamba?
Tito Magoti: Tunafanya tathimini kwa kuangalia matukio. Kwa mfano, sasa hivi kuna visa vingi sana vimeripotiwa nchini vya ajabu kabisa lakini hatuoni mtu yeyote akichukuliwa hatua, hatuoni uwajibikaji. Tunaona kauli za wanasiasa tu. Tunaona kauli za viongozi majukwaani wanawalinzi lukuki lakini mtu anafariki, ananyongwa kituo cha polisi.
Tunasikia kwamba mkuu wa kituo cha polisi amesimamishwa kesho yake asubuhi tunasikia kwamba kuna mtu sijui amechomwa kisu na mapolisi akiwa mikononi mwao bado tuna mkuu wa polisi yule yule.
Sasa ni binadamu gani ambaye yupo salama na hiyo hali ya haki za binadamu ipoje kama sio kusua sua? Ni kusua sua. Tunapozungumza muafaka kwenye mambo ya msingi kama elimu, hatuna muafaka kwenye huduma za kijamii, watu hawana nishati ya umeme sasa hivi watu wanahangaika.
Wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kwa kutumia nishati hii wanahangaika tunaathiriwa wote kwa ujumla tunasua sua. Wanasiasa, nitajie mwanasiasa gani ambaye anatembea peke yake sasa hivi, hayupo. Nimezungumza kuhusu Mzee Freeman Mbowe yupo jela sasa hivi siku ya 204 leo.
Nitajie chama cha CHADEMA kinaionaje hali ya kisiasa nchini hapo Mwenyekiti wao yupo jela. Nyinyi waandishi wa habari kuna waandishi wenzenu wamefungiwa hawaruhusiwi kutangaza matangazo yao kama kawaida magazeti, televisheni za mitandaoni. Sasa nitajie ni chombo gani cha habari yenye utashi wa kumuhoji mtu kama unavyonihoji mimi hapa sasa hivi na nikazungumza?
Wamebaki watu wachache tu tena ni watu sio taasisi. Ni watu wachache ambao wanaamua kuasi dhidi ya sheria ambazo ni za hovyo. Kwa hiyo, hali yetu ni mbaya tunasua sua tunahitaji kujisahihisha hususani kwenye kulinda haki ya kuishi, haki ya kuishi. Kuna vijana watano wamepotea tangu mwezi Disemba nafikiri, watano wako wapi?
Hatuoni uwajibikaji. Tutamueleza nani? Hayupo wa kumuuliza wewe ukiambiwa kama mwandishi embu tufanyie utafiti, uchunguzi hawa watu wapo wapi, unaweza ukawa na sehemu pa kuanzia lakini hautajiamini kwenda. Wewe unaweza kumuhoji [Mkuu wa Jeshi la Polisi] IGP kwamba hawa watu wako wapi? Huwezi. Unaweza kumuhoji Waziri wa Mambo ya Ndani? Huwezi. Tunasua sua tu, tunasua sua.
Mahojiano na uhariri wa sauti yamefanywa na Shafii Hamisi anayepatikana kupitia shafii@thechanzo.com. Mahojiano haya yamebadilishwa kutoka sauti kwenda kwenye maneno na Lukelo Francis anayepatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.