Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amewapongeza ndugu wawili kutoka Tanzania Kili Paul na Neema kwa uwezo wao uliokosha mioyo ya watumiaji wengi wa intaneti duniani wa kuiga nyimbo nyingi mashuhuri za Kihindi.
Video za ndugu hao zikiwaonesha wakiimba nyimbo mbalimbali za wasanii mashuhuri kutoka nchini India zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hivi karibuni, hususan TikTok na Instagram na kuweza kujivutia mashabiki wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Akizungumza mnamo Jumapili ya Februari 27, 2022, kwenye kipindi chake cha redio cha kila mwezi kijulikanacho kama Mann Ki Baat, Waziri Mkuu Modi alielezea kufurahishwa na kile ndugu hao wanafanya.
“Nawapongeza Kili na Neema, ndugu wawili kutoka Tanzania ambao waliimba wimbo wetu wa taifa kusherehekea miaka 73 ya Siku ya Jamhuri ya India,” alisema Modi anayetumia kipindi hicho kuongea na wananchi wa India kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu nchi hiyo.
Social media is abuzz with the talent of Kili Paul and Neema Paul.
Their affection towards Indian culture is clearly visible. Lauded their creativity during #MannKiBaat today. pic.twitter.com/NfaEVBiwwP
— Narendra Modi (@narendramodi) February 27, 2022
Hatua ya Modi kuwapongeza ndugu hao inakuja siku chache baada ya kutunukiwa tuzo ya heshima na Balozi wa India nchini Tanzania Binaya Pradhan, hatua ambayo pia ilitambuliwa na Waziri Mkuu huyo wakati wa kipindi chake hicho cha redio.
“Upana na utofauti uliopo kwenye muziki wa India ni wenye kuvutia,” aliongeza Modi. “Kama Kili Paul na Neema Paul wanaweza kupelekea urithi wetu nchini Tanzania, kitu hicho pia kinaweza kufanywa na vijana wetu kupitia lugha na lahaja zao mbalimbali.”