Mimi naitwa Wema Hassan Hamis, mama wa watoto wawili, nilizaliwa Arusha mnamo mwaka 1979, ambaye kwa sasa naishi mkoani Dodoma. Kwa baba yangu na mama yangu sisi tumezaliwa watoto wawili.
Mimi mpaka nakua nilikuwa mzima, kwa maana kwamba nilikuwa natembea vizuri tu. Ila nilipofikisha umri wa miaka mitatu, ghafla nikajikuta siwezi kutembea tena. Kwa hiyo, sijui chanzo cha mimi kutokutembea ni nini. Maana wengine walikuwa wakisema niliugua ugojwa wa polio uliosababisha mimi kuwa hivi niliyo.
Kuna wengine walikuwa wakisema kwamba mama yangu mdogo sijui alinifanya nini kwenye mguu. Chakushangaza polio yangu mimi iko tofauti na polio ile ambayo mimi ninaifahamu. Unajua mimi ninavyoijua polio mtu ukimfinya hasikii chochote lakini polio yangu mimi hata ukinigusa tu nahisi, hata ukinifinya mimi nasikia kabisa maumivu.
Sasa polio yangu hii sijui ni ya aina gani. Sijajua. Kwa hiyo, historia yangu siwezi kuisema sana. Polio yangu mimi ni polio kama wanavyodai wao? Kiukweli, pamoja na kuugua ugonjwa huu toka utoto hadi nakua mtu mzima ninayejitambua, nimeshuhudia baba yangu mzazi ndiye alikuwa akinihangaikia sana kupona hili tatizo. Nilikuwa namuona anahangaika sana Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Safari ya kupata elimu
Ilipofika mwaka 1990, baba yangu alinipeleka kujiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Amani iliyopo hapa Dodoma. Ilipofika mwaka 1996, nilifanikiwa kuhitimu elimu ya darasa la saba. Kwa bahati mbaya sikufanikiwa kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari.
Wakati baba yangu anahangaika kunitafutia ada ya kujiunga na elimu ya masomo ya sekondari, kwa bahati mbaya, nikajikuta nimeingia kwenye mahusiano na kijana mmoja ambaye alikuwa ni jirani yetu. Hivyo, nikajikuta napata ujauzito nikiwa na umri wa miaka 16 baada tu ya kumaliza darasa saba. Aliyenipa ujauzito huo alikuwa na umri wa miaka 17.
Unajua kuingia kwenye mahusiano katika umri mdogo nadhani ni mambo ya utoto tu. Nilijikuta nimeingia kwenye mahusiano na siwezi kusema kwamba nilishawishiwa. Hapana. Au nilibakwa, hapana. Yaani, nilijikuta nimeingia kwenye mahusiano. Nakumbuka nilivyoingia kwenye mahusiano nilikutana na yule mwanaume siku moja tu basi nikapata mimba.
Nilienda kumueleza kwamba nina mimba yako lakini aliukataa ujauzito. Yeye pia alikuwa ni mdogo, kama nilivyosema, alikuwa na umri wa miaka 17 tu na vile vile alikuwa bado yuko kwao. Na yeye kwa wakati huo alikuwa akielelewa na mama yake mdogo.
Mama yake mdogo baada ya kugundua jambo hilo ilikuwa ni changamoto kwa sababu alisema yeye mwanae bado ni mdogo na hawezi kumpa mtu ujauzito. Tulikuwa ni majirani tu. Kwa hiyo, nikawa nimezaa mtoto wangu wa kwanza. Kwa hiyo, kuendelea na sekondari ikawa imeishia pale.
Elimu ya ufundi
Pamoja na kupitia changamoto hiyo baba yangu hakunikatia tamaa kwani aliamua kunipeleka kusoma ufundi katika chuo cha ushonaji cha kanisa kilichokuwa kinaitwa CCT hapa Dodoma, sikumbuki vizuri ilikuwa ni mwaka gani.
Na baada ya kutoka pale nikafanikiwa kupata ufadhili wakanipeleka mkoani Morogoro kwenda kusoma chuo cha ufundi Kihonda, kusomea masomo ya ushonaji pia. Ushonaji, hata hivyo, haikuwa fani yangu. Nilienda kusoma tu basi kwa sababu baba yangu alikuwa hataki nikae nyumbani.
Mimi nilikuwa napenda sana kusuka japo sikwenda kusomea ususi lakini huwa nafanya kazi za ususi. Pamoja na kusomea ufundi, nimesomea pia masuala ya hoteli katika chuo kinachoitwa Maisha Mapya kilichopo hapa Kigamboni, Dodoma, ni muda kidogo.
Baada ya kumaliza nikafanya kazi kwenye hoteli inaitwa Kidia Vision, nikawa nafanya hapa naacha hapa. Si unajua tena mtu mwenye ulemavu kuhudumia. Pia, nikafanya kazi za baa. Nikaona umri unaenda masuala ya baa siyo vizuri. Nikaona ni bora niingie kwenye biashara.
Bahati nzuri nikakutana na dada mmoja anafahamika kwa jina la Aneti yeye ana matatizo ya kutosikia, yaani ni kiziwi, akatupatia elimu ya ujasirimali. Kwa hiyo, baada ya kufundishwa masuala hayo, mimi nikaamua kuwekeza kwenye biashara ya usindikaji pilipili.
Ndiyo nikaanzia biashara hapo. Huku nikiwa natengeneza pilipili nikaamua kujiongeza nikaanza kutengeneza bisi, karanga za kukaanga na kusindika.
Changamoto ya biashara
Shida ilikuwa inakuja kwenye wanunuzi wenyewe. Halafu pia, shida nyingine kutembeza ni lazima sasa hivi biashara umfuate mteja alipo. Sasa mimi biashara yangu ni ya kukaa ili mteja anifate. Kama unavyojua, mteja ni lazima umpelekee biashara.
Kuna mdogo wangu ambaye alikuwa akifanyakazi mahali fulani yeye mara nyingi alikuwa akinisaidia kusambaza bidhaa zangu. Alikuwa akichukua pilipili ananisambazia mahali kule anapofanyia kazi na mwisho wa siku anakusanya pesa ananipatia.
Nimeona kuna soko linajengwa hivi sasa la Machinga Complex hapa Dodoma nitashukuru sana nikipata nafasi ya kwenda kufanya biashara pale.
Changamoto ambayo niliipata na mtoto wangu wa kwanza aliyekataliwa na baba yake ni kutokuwa karibu na baba yake. Lakini siyo changamoto ya kusema labda nashindwa kumlea mtoto wangu wa kwanza.
Huyu mtoto nimemsomesha mwenyewe kuanzia elimu ya awali mpaka sekondari. Mimi mwenyewe nilikuwa nalipa ada. Kwa sababu mtoto wangu mimi wa kwanza hakufanikiwa kufalu lakini niliweza kumlipia ada kama mama. Nilisimama peke yangu bila msaada wa mtu yeyote.
Kwa hiyo, kuwa mlemavu siyo kushindwa. Ulemavu ni kupambana na siyo mlemavu tu kwa sababu nimelemaa niende kuomba omba. Hapana. Walemavu hatutakiwi kuwa hivyo. Kwa sababu tuna akili timamu tunatakiwa tusimame.
Kama tukifanikiwa kuzaa lazima tuweze kuwalea watoto wetu kwa sababu tuna akili timamu. Na ndiyo maana mimi ninahangaika kufanya hiki na kile sitaki mimi kuwa omba omba.
Manyanyaso
Naomba niseme mimi kama mimi walemavu wanawake wanapitia manyanyaso mengi. Ukishapewa mimba, mzigo unakuwa ni wa kwako. Yaani wewe ndiye utakayepambana. Na siwezi kusema kwamba ni watu wote. Kuna wengine wenye miguu yao wanapewa mimba na wanakimbiwa na wenzi wao.
Lakini tatizo ni kubwa zaidi hasa kwa wanawake wenye ulemavu. Wewe mlemavu leo umepewa mimba, wewe ndiye uhangaike jinsi ya kulea mimba mpaka utakapojifungua yule mtoto mpaka hapo atakapokua.
Kwa hiyo, hiyo ni changamoto kubwa sana kwa watu hasa wenye ulemavu. Wengi waliopo ni watu tunaozalia nyumbani, hatuna msaada na wababa waliotupa mimba.
Watu wanapaswa kujua mwanamke mwenye ulemavu ni kama mwanamke mwingine kwa sababu hata yeye anatamani kuwa na mwanaume. Lakini wao wanatuchukulia kama watu wa msaada. Wanasema nikimchukua huyu nikienda nikifanya nae hivi, yaani wanatuchukulia kama watu rahisi rahisi.
Wanajua yule mwenye ulemavu yaani kama ni mzigo ukimchukua unaenda unamfanyia hivi anaridhika. Lakini siyo kweli. Sisi ni wanawake kama wanawake wengine. Tunastahili kuheshimiwa. Tunastahili kupendwa na tunastahili kulindwa.
Unakuta mwanamke mwingine mwenye ulemavu mwanaume anakuja anamchukua, yaani anamuambia kwamba tukutane sehemu fulani anaenda na huyo mwanamke. Nahisi anakuwa hakupendi anakuwa amekutamani. Kwa hiyo, anataka mahusiano.
Na mwingine unakuta anasema ukiwa na mwanamke mwenye ulemavu wale ni ‘watamu’. Kwa hiyo, kila mtu anatamani kujaribu. Sawa anakuambia labda tukutane sehemu fulani, yaani unaenda naye siyo kwamba unaongozana naye kama mtu ambaye ana miguu yake.
Yeye anakuambia tukutane chumba namba fulani sasa wakati wa kutoka unakuta anatangulia mwanaume na wewe ndiyo utafuata. Lakini hiyo siyo haki. Kama unampenda kweli ongozana naye jinsi alivyo. Umempenda, umeamua kumpenda, mpende hivyo hivyo alivyo, ongozana naye.
Kufunga ndoa
Nimebahatika kufunga ndoa mwaka huu wa 2022. Kwa sasa, namshukuru Mungu nimebahatika kumpata mume ambaye ananipenda sana. Na nimebahatika kufunga naye ndoa na kuzaa naye mtoto mmoja.
Jamii iendelee kupewa elimu. Jamii inaamini kwamba watu wenye ulemavu ni watu wa msaada tu. Zipo baadhi ya jamii zinaamini kwamba wanawake wenye ulemavu hawastahili kuolewa.
Walemavu na sisi ni binadamu. Tunamahitaji. Tunatamani na sisi kuolewa. Tunatamani na sisi tupate furaha. Tunatamani na sisi tupate amani na sisi tuishi kama wanavyoishi watu wengine.
Wito kwa Serikali
Kwa upande wa Serikali, ninaiomba iweze kuwafikiria watu wenye ulemavu kwenye huu mkopo wa asilimia mbili kutoka halmashauri. Watufikirie. Ninasema kwa niaba ya walemavu wengine japo mimi sina changamoto sana hizo.
Kwa sababu asilimia kubwa ya watu wenye ulemavu wanalalamika asilimia hizo mbili. Wanavyodai ni kwamba hela zipo lakini unapokwenda huko kufuatilia hizo asilimia mbili wanasumbuliwa.
Basi wafanye watu wenye ulemavu hizo asilimia mbili wapewe kwa wakati. Hakuna mtu muoga kama mtu mwenye ulemavu kwenye masuala ya marejesho, yaani wako makini sana, hasa wanawake wako vizuri kwenye marejesho.
Kwa hiyo, mimi naomba wawape sana kipaumbele wanawake wenye ulemavu. Wapewe hiyo mikopo.
Wema Hassan Hamis amesimulia hadithi hii kwa mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma Jackline Kuwanda. Unaweza kumfikia Jackline kupitia jackline@thechanzo.com.