Dar es Salaam. Wadau wa ardhi nchini Tanzania wameitaka Serikali kuheshimu maamuzi ya Mahakama ili kuepusha kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi, ambayo mara nyingi huathiri ustawi wa wananchi na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa hapo Disemba 20, 2022, na Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji Tanzania (PINGO’s), Jukwaa la Ardhi Tanzania, HakiArdhi na Shirika la Msaada wa Kiraia na Kisheria (CILAO) wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini hapa.
Mashirika hayo yanayojishughulisha na matumizi ya ardhi yalitoa wito huo kufuatia uwepo wa baadhi ya kesi za migogoro ya ardhi ambazo wananchi walishinda mahakamani lakini Serikali imeshindwa kutekeleza maamuzi hayo na kuwaacha wananchi bila haki.
Moja kati ya kesi iliyotajwa na wadau hao ni ile ya kijiji cha Mabwegere, wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro, ambapo kijji hicho kilifungua shauri namba 23 la mwaka 2006 dhidi ya wakulima 33 katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
SOMA ZAIDI: Namna Ukosefu wa Ardhi ya Kutumia Unavyogeuka Kuwa Janga Kilosa
Kijiji hicho kilishindwa kesi hiyo na kukata rufaa namba 53 ya mwaka 2010. Lakini Mahakama ya Rufaa Tanzania mnamo mwaka 2010 iliamuru mipaka iliyohamishwa ya kijiji cha Mabwegere irejeshwe ilipokuwa na pia mipaka hiyo iheshimiwe.
Lakini badala ya kutekeleza amri ya Mahakama ya Rufaa, Serikali ilichukua hatua ya kukifuta kijiji hicho!
Kesi nyingine ni ile inayohusisha wawakilishi 17 wa wafugaji wa kijiji cha Vilimavitatu, wilaya ya Babati Vivijini, mkoa wa Manyara.
Wafugaji hao walishinda rufaa namba 16 ya mwaka 2013 katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania dhidi ya halmashauri ya kijiji hicho na Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii Burunge (JUHIBU).
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali Haitekelezi Maamuzi Yanayotolewa na Mahakama?
Pamoja na ushindi huo, Serikali za wilaya na mkoa zimekataa kuheshimu uamuzi huo wa Mahakama waliopewa wafugaji hao kisheria, wadau hao wa ardhi waliwaambia waandishi wa habari.
Kuingilia uhuru wa Mahakama
Edward Porokwa ni Mkurugenzi wa PINGO’s ambaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba kitendo cha Serikali kushindwa kutekeleza maamuzi ya Mahakama ni sawa na kuingilia uhuru wa mhimili huo wa dola.
“Suala la Serikali Kuu kuingilia mhimili wa dola, kidogo, nafikiri inapingana na utaratibu uliopo ambapo Mahakama zetu zinapaswa kuwa huria,” alisema Porokwa.
“Kulingana na Katiba yetu [ya nchi], Mahakama ni chombo huru [na] hakipaswi kuingiliwa na dola na [Mahakama] ina heshima zake,” alisema Porokwa ambaye shirika lake hutetea wafugaji wa asili Tanzania.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula alikataa kuongea na The Chanzo kuhusu shutuma hizo, akimuelekeza mwandishi aongee na majaji waliotoa maamuzi hayo.
Dk Mabula pia aligoma kuelezea mikakati ambayo Serikali inachukua kupunguza migogoro ya ardhi nchini, hususan ile inayohusisha Serikali na wananchi.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara
Porokwa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Serikali kushindwa kutekeleza maamuzi ya Mahakama pia ni kuzuia wananchi wasipate hazi zao, kwani Mahakama ndiyo chombo kikuu cha utoaji wa haki nchini kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Unapoilazimisha [Mahakama] kutenda kwa muelekeo ambao wewe unataka, kidogo inakuwa inapingana na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Porokwa.
“Na inatutisha sisi vilevile kwamba haki inaweza isitendeke kama mhimili wa Mahakama hautakuwa huria,” aliongeza mdau huyo.
Ukamati haramu wa mifugo
Bernard Baha ambaye ni Mratibu wa Jukwaa la Ardhi Tanzania alisema kwamba kutokana na tathmini yao, wamebaini uwepo wa ukamataji wa mifugo na kupigwa minada kama mali isiyo na mwenyewe.
Hali hii imeripotiwa zaidi kwenye migogoro ya ardhi inayohusisha wakulima/wafugaji na mamlaka za hifadhi.
Akitaja baadhi ya maeneo hayo, Baha aliitaja Mbarali, eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Loliondo na wilaya ya Longido mkoani Arusha.
SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo wa Kile Kinachoendelea Ngorongoro
Kwa mfano, Baha alisema kwamba mnamo Julai 23, 2022, jumla ya mifugo 1,448 ya wilaya ya Longido katika mkoa wa Arusha, ilipigwa mnada kwa amri ya Mahakama ya wilaya ya Siha kwa madai kwamba mifugo hiyo iliingia kwenye mashamba na haina wenye nayo.
Mnamo Novemba 22, 2022, pia, askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha waliwakamata ng’ombe 172 katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na kupigwa mnada licha ya mmiliki wake kujitokeza.
Na Disemba 14, 2022, jumla ya ng’ombe 1,772 za wafugaji katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha waliuzwa katika mnada wa hadhara kwa amri ya Mahakama kwa madai kuwa mifugo hiyo haina wenye nayo.
“Tunaitaka Serikali kusitisha mazoezi yote yanayofanywa na askari na wahifadhi ya kuwakamata kwa dhuluma wafugaji na kutaifisha mifugo yao,” alisema Baha.
“Kuendelea kufanya hivyo ni kuongeza umaskini na mateso kwa wananchi wasiokuwa na hatia.”
Baha pia aliitaka Serikali iwafidie wafugaji ambao mifugo yao imepigwa mnada kwa hila, akisema mifugo hiyo ndiyo tegemeo kubwa siyo tu kwa uchumi wao bali kama chakula cha familia.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.