Mtwara. Wakulima mkoani hapa wameelezea masikitiko yao juu ya ukosefu wa mvua za uhakika, hali wanayosema inatishia usalama wao wa chakula kwani wanahofia kwamba hali hiyo itaathiri mazao waliyopanda kama vile mchele na mahindi, mazao maarufu yanayotumika kwa chakula mkoani hapa.
Wataalamu wanabainisha kwamba kwa kawaida, mikoa ya Lindi na Mtwara huwa na wastani wa mvua wa milimita 950 mpaka milimita 1040. Hata hivyo, wastani huo umekuwa ukipungua kwa kadiri miaka inavyozidi kwenda.
Kwa mfano, msimu wa mvua wa mwaka 2021/2022 kwa mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zilinyesha kwa wastani wa milimita 691.5, ambao wenyewe ulikuwa mkubwa ukilinganisha na wastani wa mvua utakaopatikana msimu wa sasa wa 2022/2023.
Msimamizi wa Kituo cha Hali ya Hewa na Kilimo TARI-Naliendele, Mtwara, Omari Kahoki, ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba mpaka sasa mwenendo wa mvua umekuwa siyo wa kuridhisha.
Kahoki alisema kuwa Januari kulikuwa na mvua zenye milimita 143, Februari milimita 171, na mpaka kufikia Machi 18 mvua zilizonyesha hazizidi milimita 40.
“Sasa, ukiangalia kwa ujumla, [utaona] kwamba mvua zetu ziko chini ya wastani, yaani kwa miezi mitatu hii kuanzia Januari mpaka sasa [Machi] hazifiki hata milimita 300, na hata hivyo, unyeshaji wake umekuwa wa kuruka ruka sana, yaani siyo mfululizo kwamba leo, kesho na keshokutwa,” alisema mtaalamu huyo.
“Inaweza ikanyesha leo, ikakaa siku nne hivyo hivyo, ikakaa tena wiki moja, ikanyesha kidogo, unakuta kwamba hali iko hivyo,” aliongeza Kahoki.
SOMA ZAIDI: Wakulima Walalamikia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Serikali Yafafanua
Hali hii imewaathiri wakulima mikoani hapa ambao wengi wao wamezoea kwamba kipindi cha Disemba hadi Aprili kama kipindi cha mvua nyingi kwenye mikoa hii ya Lindi na Mtwara.
Wakulima hawa wadogo ambao hulima mazao ya mahindi, mpunga na mazao mengine ya chakula kwa ajili ya kujikimu na mazao ya korosho na ufuta kama mazao ya biashara, hutumia mvua hizo za Disemba hadi Januari kupandia mazao yao.
Wakulima hao hutumia mvua za Februari mpaka Aprili kwa ajili ya kukuza mazao hayo kuelekea kwenye mavuno ambayo huanza Aprili na kuendelea. Vilevile, mvua hizi za Februari mpaka Aprili husaidia kwenye kukuza zao la korosho.
Wakizungumza na The Chanzo kwa nyakati tofauti, wakulima mkoani hapa wamelalamika jinsi ukosefu wa mvua ulivyozuia mazao yao kustawi, hali ambayo inawatia wasiwasi kuhusu hatma ya maisha yao.
Mmoja kati ya wakulima hawa ni Hamisi Ismail, mkulima wa mazao mchanganyiko kutoka kijiji cha Nanguruwe, kata ya Nanguruwe halmshauri ya wilaya ya Mtwara, ambaye ameelezea kwamba uhaba wa mvua unamfanya awaze kama atavuna chochote.
Hakuna tija
“Mazao ambayo nimeyapanda ni mpunga, mahindi, karanga pamoja na muhogo, lakini hapa ninapozungumza, hakuna zao hata moja litakaloniletea tija kwa mwaka huu,” Ismail, 65, alisema wakati wa mahojiano na The Chanzo.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
Mkulima huyo anadai kwamba alilima shamba lenye ukubwa wa heka tano, akipanda mazao mchanganyiko kama ilivyo kawaida kwa wakulima wadogo.
“Hivi ninavyozungumza, mpunga ni nyasi tupu kiasi kwamba unaweza ukachukua kibiriti ukawasha, ukaungua,” alieleza mkulima huyo. “Hamna kitu.”
Bakari Chiungo ni mkulima kutoka kijiji hicho hicho cha Nanguruwe ambaye ameeleza kwamba amelima hekari nne za mahindi, mtama, ufuta, na karanga lakini yote yamekufa, na hategemei kuvuna chochote.
“Nina familia ya watu nane huku wawili wakiwa watoto wa shule ya msingi na sielewi hawa watoto watakula nini,” Chiungo, 55, alilalama.
“Hapa ninavyoongea, saa nne [watoto] walirudi nyumbani wakidai kwamba wana njaa,” aliongeza mzazi huyo. “Mvua zimeacha kunyesha muda mrefu, tulikuwa tunategemea watoto watakula mahindi, lakini mahindi sasa hivi hakuna, yamekufa yote. Sijui tunafanyaje!”
SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara
Naye Fatuma Lahi, bibi wa miaka 67, ameiambia The Chanzo kwamba kutokana na hali ya mazao yake ilivyo huko shambani, hatagemei kuvuna chochote. Lahi anasema alipanda mihogo na mahindi akitumaini kwamba ifikapo Aprili angeanza kuvuna lakini hali imekuwa tofauti.
“Hapa sijui na watoto wangu nitakula nini, sijui,” Lahi, bibi wa wajukuu watano wanaomtegemea, alisema kwenye mahojiano. “Sana sana nilitegemea muhogo na mahindi. Lakini kuanzia sasa, sina mahindi, na muhogo sijui kama utakuwa.”
Mazao stahimilivu
The Chanzo ilimuuliza Kahoki, katika mazingira kama haya, ni nini wakulima wanapaswa kufanya ili kukabiliana na hatari ya njaa, ambapo alisema kwamba kuanzia Machi 18, 2023, mvua inategemewa kunyesha maeneo tofauti tofauti ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kahoki pia alitoa wito kwa wataalamu wa kilimo kutumia muda huu kuwashauri wakulima kuhusiana na aina za mazao zinazoweza kufaa kupandwa kutegemeana na mvua hizo ambazo zinatarajiwa kunyesha mpaka mwezi Aprili.
“Kwa hiyo, sisi tunashauri kwanza [wakulima] wasiache kufuatilia taarifa za hali ya hewa ambazo zitawasisimua kutokana na kile ambacho wanataka kukifanya,” alisema Kahoki.
“Lakini, vilevile, kwa mvua hizi ambazo ni chache zinaelekea mwishoni kuelekea Aprili, kuna mazao ambayo wataalamu wa kilimo ndiyo wanajua zaidi yanahitaji mvua chache kwenye kukua kwake,” aliongeza.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) – Naliendele Dk Fortunus Kapinga ameshauri wakulima kulima mazao yanayohimili ukame, akitolea mfano mazao kama ya kunde na mtama.
“Kwa hali kama hii, mazao ambayo wakulima wanatakiwa kupanda ni yale ambayo ni ya muda mfupi, yale ambayo yanahitaji mvua kidogo,” alishauri Dk Kapinga. “Kwa mfano, kama kunde, choroko, na mtama yanahimili sana ukame.”
Omari MIkoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.