The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Hayatibu Ugonjwa Wowote’: Zanzibar Yatahadharisha Unywaji wa Maji ya Chemchemi Pemba

Serikali imewaonya wananchi kwamba unywaji wa maji hayo unaweza kupelekea kupata magonjwa mbalimbali, ikiwemo yale ya kuharisha.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amewasihi wananchi visiwani humo kuacha kunywa maji ya chemchemi iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi huko Micheweni, kisiwani Pemba, akisema hakuna ushahidi wa kisayansi kwamba maji hayo yanatibu ugonjwa wowote ule.

Kwenye taarifa yake ya Aprili 5, 2023, Mazrui amewaonya watu dhidi ya kunywa maji hayo, akisema kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wa kisayansi uliofanywa kwenye maji hayo, wanywaji wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, ikiwemo yale ya kuharisha na kutapika.

Hatua hiyo inakuja baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku za hivi karibuni zikidai kwamba maji yatokanayo na chemchemi hiyo iliyopo katika shehia ya Msuka Mashariki, wilaya ya Micheweni, Kaskazini Pemba yanatibu magonjwa mbalimbali.

Imeripotiwa kwamba kufuatia taarifa hizo, mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi wamekuwa wakifurika kisiwani Pemba kuchukua maji hayo kwenye madumu, ndoo, chupa na vyombo vingine mbalimbali.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Yafafanua Madai Ajira za Serikali Zinatolewa kwa Misingi ya Kivyama

Lakini Mazrui amesema kwenye taarifa yake hapo Jumatano kwamba kutokana na uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ya Zanzibar kwenye sampuli zilizochukuliwa kwenye maji hayo umeonesha kwamba badala ya maji hayo kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa, yanatishia kuwapa wanywaji wake magonjwa.

Kwa mfano, uchunguzi huo umebaini uwepo wa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya kuharisha (bacteria wa E. coli) wa idadi kubwa kati ya 220 na 1,800 kwa kila lita moja ya maji hayo. Kwa kawaida, maji ya kunywa hayatakiwi kuwa na kimelea hata kimoja.

Pia, uchunguzi huo umebaini uwepo wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa kuharisha aina ya ‘Coliforms’ zaidi ya 1,800 kwa kila lita. Kwa kawaida, vimelea hivi vinahitajika viwemo kwenye maji ya kunywa lakini isiwe zaidi ya watatu kwa kila lita mia moja.

Uchunguzi pia umebaini uwepo wa Chloride kwa kiwango kikubwa cha kiasi cha upimo wa kuanzia 1,490 miligramu kwa kila lita hadi 2,059 miligramu. Kiwango cha Chloride kinachokubalika ni kipimo kisichozidi 250 miligramu kwa kila lita moja.

Uchunguzi pia umebaini kuwa maji hayo yana kiwango kikubwa cha chumvi chumvi (salinity), 2.827 hadi 3.827 psu, huku kiwango kinachokubalika kuwepo kwenye maji ya kunywa ni sifuri, yaani 0 psu.

SOMA ZAIDI: Undani Kuhusu Mmiliki wa Asilimia 35 ya Kampuni ya Dnata Zanzibar

“Matokeo haya yanatuthibitishia kwamba maji haya yamechafuliwa na kinyesi cha viumbe hai na pia kuna kiwango kikubwa cha kemikali ambazo siyo salama katika mwili wa binadamu,” Mazrui alisema kwenye taarifa yake.

“Kwa maana hiyo, maji haya siyo salama kwa kunywa na kama tukiendelea kuyatumia yanaweza kuathiri afya zetu na kupelekea matatizo mbalimbali ya kiafya,” aliongeza.

Maradhi yanayoweza kupatikana kutokana na kunywa maji hayo ni pamoja na magonjwa ya kuharisha, ikiwemo kipindupindu, kutapika, na kupoteza maji mengi mwilini.

Pia, mtumiaji wa maji hayo yupo katika hatari ya kupata maumivu makali ya tumbo na baadaye anaweza kupata vidonda vya tumbo, Mazrui ametahadharisha.

“Taarifa kwamba maji haya yanatibu magonjwa mbalimbali hazina ukweli wowote na hivyo nawasihi wananchi wazipuuzie taarifa hizi,” Mazrui alisema. “Mwananchi yoyote mwenye matatizo ya kiafya afike katika kituo cha afya, au hospitali iliyokaribu, kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts