Search
Close this search box.

Zanzibar Yafafanua Madai Ajira za Serikali Zinatolewa kwa Misingi ya Kivyama

Waziri mwenye dhamana ya kazi amewataka vijana waliopitia kadhia hiyo wafike ofisini kwake ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar Mudrik Ramadhan Soraga amewataka vijana wa Kizanzibari wanaodhani wamekosa ajira za Serikali baada ya kushindwa kuthibitisha uanachama wao kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamuone ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Wito huo umetolewa ikiwa ni takriban siku nane tangu The Chanzo ichapishe habari hapo Machi 16, 2023, ambapo baadhi ya Wazanzibari wamelalamikia kunyimwa fursa za ajira kwa sababu wao ni wafuasi wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo au wameshindwa kuthibitisha uanachama wao kwa chama tawala CCM.

Akizungumza na The Chanzo kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake hapo Machi 22, 2023, Soraga, ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Bububu (CCM), alisema kama kuna mtu yoyote – serikalini au kwenye sekta binafsi – anatoa ajira kwa misingi ya kivyama mtu huyo anavunja sheria za nchi.

“Kwanza niseme kwamba Sheria ya Kazi Na. 11 ya 2005, hakuna sehemu inasema kwamba muajiri asitoe ajira kwa mtu ambaye hana kadi ya CCM; hakuna takwa kama hilo,” Soraga alisema kwenye mahojiano hayo.

Soraga alisema kwamba hakuwa na taarifa hizo na kwamba ndiyo kwanza alikuwa anazisikia kutoka kwa mwandishi wa The Chanzo, akitoa wito kwa vijana wanaohisi wamefanyiwa hivyo wafike ofisini kwake ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

“Sisi kupitia kamisheni yetu ya kazi tunawajibu wa kusimamia Sheria ya Kazi na hakuna ubaguzi ambao unatakiwa ufanyike kwenye masuala ya kazi,” Soraga alisema kwenye mahojiano hayo.

“Hatupaswi kumbagua mtu kwa minajili ya shehia ambayo anatoka, chama ambacho anakiunga mkono, dini yake, kabila lake. Hayo hatuangalii [kwenye kuajiri mtu]. Sisi tunachoangalia ni uwezo wa mtu.

“Kwa hiyo, kama kuna muajiri, na kuna taarifa zipo, na ushahidi upo, mimi nitakuwa nipo tayari kupokea taarifa hizo na niwahakikishie kwamba nitazifanyia kazi kikamilifu kuhakikisha kwamba zile sheria ambazo zimewekwa kwa muajiri yule azifuate,” alisisitiza waziri huyo mwenye dhamana ya kazi.

Malalamiko ya muda mrefu

Malalamiko ya ajira za Serikali Zanzibar kutolewa kwa misingi ya vyama ni ya muda mrefu, yakiibuliwa na wafuasi wa vyama vya upinzani pamoja na viongozi wao pia.

Mnamo Januari 8, 2019, kwa mfano, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), hayati Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa kisiwani Pemba, alizungumzia kadhia hiyo, huku akiuita “ubaguzi” huo “kitu kisichokubalika.”

“Hivi sasa Zanzibar ili uajiriwe unalazimika kuwa mwanachama wa CCM vinginevyo utaendelea kusota na vyeti vyako nyumbani,” Maalim Seif, aliyefariki Februari 17, 2021, alikunukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema. 

SOMA ZAIDI: Kada wa CCM Zanzibar Apotea Kwa Miaka Miwili. Familia Yataka Majibu

“Kama utafanya tathmini, utakuta kundi kubwa la vijana waliomaliza masomo yao, wengine hata miaka mitatu au minne nyuma, wanaendelea kusota bila ya ajira,” aliongeza mwanasiasa huyo aliyehamia chama cha ACT-Wazalendo mnamo Machi 18, 2019.

Lakini akizungumza na The Chanzo kwenye mahojiano hayo maalum, Soraga aliwatoa hofu vijana wa Zanzibar, akiwaambia kwamba Serikali ya awamu ya nane chini ya Dk Hussein Mwinyi haitaruhusu hilo kutokea, akisema kwamba Serikali itasimamia sheria kama inavyosema.

“Kwanza niwatoe hofu, waondokane na dhana hiyo,” Soraga alieleza. “Sheria za nchi ziko wazi na sisi watendaji wa Serikali tupo kwa ajili ya kusimamia sheria, na kwa yoyote vile, yule ambaye pengine amepitia kadhia hiyo, kama nilivyosema, milango yangu iko wazi.”

“Waje tuonane, tuzungumze, lakini wasije kiushabiki, tuje kwa ushahidi, tuje na uhalisia wa jambo na tutalifanyia kazi,” aliongeza Soraga. 

“Ni jukumu letu la msingi kuhakikisha kwamba tunafuatilia yale yote yanayohusiana na utekelezaji wa  sheria na tukibaini kwamba muajiri anatumia vigezo hivyo basi, tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ambazo zimewekwa,” alisema.

Kazi mahotelini

Soraga alitumia fursa hiyo pia kutolea ufafanuzi malalamiko ya muda mrefu kuhusiana na vijana wa Kinzanzibari kukosa kazi mahotelini, ambapo alisema:

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

“Tulikuja tukagundua kwamba chanzo kikubwa ambacho kinasababisha vijana wetu wakose ajira katika mahoteli haya ni kwa sababu wale mameneja uajiri (Ma-HR) ambao wanakuwepo pale [hotelini] siyo Wazanzibari. 

“Unaweza ukakuta kwamba wengine wanatoka [Tanzania] Bara, wengine wanatoka Kenya, Uganda [na] kwenye nchi ambazo, kwa kweli, wamebobea kwenye masuala haya ya utalii.

“Kwa hiyo, hatua ambayo sisi tumeichukua kwanza, ni kutoa muongozo kwa mahoteli kwamba wahakikishe Ma-HR meneja wao wote wanakuwa ni Wazanzibari ili awepo Mzanzibari pale. Yeye sasa atakuwa na nafasi yakujua kuwa huyu kweli ni Mzanzibari au huyu si Mzanzibari. 

“Kwa hiyo, nadhani hilo tatizo sasa tutakuwa tumelipatia muarubaini wake na uzuri ni kwamba hoteli hizi sasa hivi zimeanza utekelezaji na utafiti wa haraka haraka utakuja kugundua kwamba sasa hivi zaidi ya asilimia 60 ya MaHR kwenye mahoteli yetu haya ni Wanzanzibari na wao ndiyo wamepewa sasa lile rungu la kuajiri.

“Lakini muajiri, kisheria, bado ana haki ya kuajiri mtu kutoka nje kutokana mahitaji yake na zile nafasi ambazo ni za kitaalamu sana ambapo mtaalamu wake pengine hapa Zanzibar atakuwa hayupo. 

“Kwa hiyo, kwenye hilo tumetoa kibali maalum kwa muajiri kuweza kuleta mtaalamu kutoka nje kwa masharti nafasi ile hakai zaidi ya miaka mitatu, aandae utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Mzanzibari, [ili] yeye atakapokamilisha ile miaka mitatu basi yule Mzanzibari aweze kuendelea kufanya ile kazi.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *