Suala la hatima ya utolewaji wa mikopo ya asilimia 10 ya fedha za mapato ya Halmashauri za Serikali za Mitaa limekuwa na mjadala mkubwa sana hapa nchini kwetu kwa siku za hivi karibuni.
Historia ya azma ya Serikali kuyatazama makundi ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu ilianza rasmi mwaka 1993, pale Serikali ilipoanzisha Mfuko wa Fedha wa Maendeleo kwa Wanawake na Vijana.
Lengo kubwa lilikuwa ni kuweka mazingira wezeshi kwa makundi hayo kujiajiri na kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara, na uzalishaji wa bidhaa.
Katika kutimiza malengo haya, ndipo ulizaliwa mkakati wa kutoa mikopo yenye gharama na masharti nafuu kwa makundi hayo.
Katika kutekeleza hilo, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, ilifanyiwa marekebisho mwaka 2018 kwa kuweka masharti kwa kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ikiwa ni sehemu ya kuteleza azma hiyo ya Serikali.
Mnamo mwaka 2019, zilitungwa kanuni zilizoweka uwiano wa mgao wa fedha hizo kwa vijana (asilimia nne); wanawake (asilimia nne); na watu wenye ulemavu (asilimia mbili).
Manung’uniko
Tangu kuanza kutolewa kwake, hata hivyo, mikopo hiyo imekuwa ikigubikwa na changamoto, malalamiko, na manung’uniko mengi, hususani kuhusu utaratibu unaotumika kutolewa ambao umekuwa ukilalamikiwa kuwa na upendeleo kwa mrengo wa kisiasa.
Kwa mfano, kumekuwa na malalamiko kwamba chama kinachotawala Halmashauri na viongozi wa kisiasa, kama vile madiwani na wabunge, wamekuwa na nguvu ya nani anaweza kupata au kukosa mkopo huo.
Pia, kuwepo kwa vikundi hewa ambavyo vinaonekana vinapewa fedha bila kuwepo kwa utambulisho halisi.
SOMA ZAIDI: ‘Usumbufu Ni Mkubwa’: Wajasiriamali Waichambua Mikopo ya ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’
Vilevile, changamoto nyingine ambayo inatokana na utaratibu mbovu tulioutaja hapo juu, ni upotevu mkubwa wa mabilioni ya shilingi kwa kutorejeshwa kwa fedha hizo.
Aidha, baadhi ya Halmashauri zimelalamikiwa kutotenga kabisa fedha za mapato yanayokusanywa, kitu ambacho ni kinyume na sheria, kama nilivyosema hapo juu.
Kutokana na sababu hizi, malengo yaliyowekwa yanabaki kuwa ni ndoto za alinacha na kufanya fedha za umma zinazotengwa kuteketezwa na watu wachache kwa manufaa yako.
Changamoto kubwa iliyowashtua wengi na hata kuifanya Serikali kusitisha kwa muda utolewaji wa mikopo hiyo ni suala la ubadhirifu na upotefu wa fedha hizo.
Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo tumeweza kushuhudia ubadhirifu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya makundi haya kwa kiwango cha kutisha sana.
Ubadhirifu uliokithiri
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, mathalan, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliripoti kutorejeshwa kwa Shilingi Bilioni 88.42 zilizotolewa kama mkopo kwenye vikundi ambapo takribani Mamlaka 180 za Serikali za Mitaa zimeshindwa kurejesha mikopo ya Shilingi bilioni 88.42.
CAG pia alibaini kwamba vikundi 201 kwenye mamlaka nane za Serikali za Mitaa vilivyopewa mikopo ya Shilingi milioni 774.66 havikutekeleza miradi iliyoidhinishwa. Vikundi hivi viligawana fedha na hapakuwepo na ushahidi kama fedha zilitumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kuliripotiwa pia kutokuwepo kwa vikundi vilivyopewa mikopo ya Shilingi milioni 895.94, yaani uwepo wa vikundi hewa, ambapo CAG alishindwa kujiridhisha juu ya uwepo wa vikundi 48 vilivyopewa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 895.94.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata husika hawakufahamu lolote kuhusu vikundi hivyo!
CAG pia alionesha kwamba mikopo inayodaiwa kwenye vikundi vilivyositisha shughuli za biashara ni Shilingi bilioni 2.25 ambapo mamlaka tisa, zikiwemo Halmashauri za Temeke, Monduli, na Tandahimba zilitoa mikopo ambayo haikurejeshwa kwa vikundi vilivyositisha shughuli zao za biashara.
SOMA ZAIDI: Tamu, Chungu Bajeti ya TAMISEMI 2023/24
Pia, mamlaka 33 za Serikali za Mitaa hazikuchangia jumla ya Shilingi bilioni 5.06 kutoka kwenye mapato yao ya ndani kwa miaka mitatu mfululizo. CAG pia alionesha kwamba mikopo ya Shilingi milioni 147.26 imetolewa kwa watu wenye ajira rasmi.
Kwa mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilitoa Shilingi milioni 147.26 kwenye vikundi vitano vyenye wanachama wenye ajira rasmi kinyume na kanuni, hivyo kupelekea malengo ya mikopo hii kutofikiwa.
Kutokana na ukaguzi huu wa CAG, tunaweza kuona ni kwa kiasi gani fedha hizi za mikopo kwa makundi haya katika Halmashauri zetu ni kichaka cha uporaji wa fedha za umma.
Tunaona, pasi na shaka, kuwa upotevu wa fedha hizi unaongezeka kila mwaka na kupelekea hasara kubwa ndani ya nchi. Jumla ya Fedha zilizotolewa kwa utaratibu huu kwa miaka nne iliyopita ni Shilingi bilioni 396.
Kwa mwaka wa fedha unaokuja wa 2023/2024, jumla ya Shilingi trilioni 1.4 zinatarajiwa kukusanywa kama mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Shilingi bilioni 140 katika hizo zitapelekwa kwenye shimo hili la kutupa fedha za umma kama utaratibu huu wa usimamizi utaendelea.
Kumekuwa na baadhi ya mapendekezo kutoka serikalini na kwa baadhi ya wadau kwamba utaratibu wa kutoa fedha hizi ubadilishwe na kwamba benki za biashara zihusishwe.
Hata hivyo, ACT-Wazalendo tuna mashaka kwamba pendekezo hili litanufaisha zaidi mabenki kuliko kutatua changamoto zilizokusudiwa mfumo huu ulipoanzishwa kwani benki siyo rafiki wa mtu masikini.
Utaratibu m’badala
ACT-Wazalendo, kwa hiyo, tunapendekeza kuwa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu itolewe kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii ambapo fedha hizi zitakuwa ni mchango wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wananchi wenye sifa watakaoingia kwenye skimu husika.
Kwa mfano, katika mchango wa kila mwezi wa Shilingi 30,000 kwa Skimu ya Hifadhi ya Jamii, mwananchi atachangia Shilingi 20,000 na Mamlaka yake ya Serikali ya Mtaa itamchangia Shilingi 10,000.
Kwa mfumo huu tunaopendekeza, vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu watapata mikopo nafuu, bima ya afya kupitia fao la matibabu, na pensheni ya uzeeni watakapofika umri wa kustaafu.
SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni
Kwa pendekezo hili, tutakuwa tumedhibiti upotevu wa mabilioni ya fedha, tumechochea utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa wananchi wetu, kuongeza watu wenye bima ya afya nchini na kutoa mikopo nafuu inayolipika kwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu nchini kwetu.
Kwa kutumia makadirio ya makusanyo ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa katika mwaka ujao wa Fedha, yaani 2023/2024, jumla ya watu 1,167,000 watafaidika na skimu hii katika mwaka wa kwanza na akiba itakayokusanywa na Skimu ya Hifadhi ya Jamii itakuwa ni Shilingi bilioni 420.
Tukitekeleza mfumo huu kwa miaka mitano, ACT-Wazalendo tunaamini, tutakuwa tumejenga Skimu ya Hifadhi ya Jamii yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.1 yenye wanachama zaidi ya milioni tatu wenye fao la matibabu.
Mwanaisha Mndeme ni Waziri Kivuli wa Uwekezaji, Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii kutoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata kupitia mwanaisha.mndeme@yahoo.com au Twitter kama @Mwanaishamndeme. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na siyo lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.
One Response
Hongereni Chanzo kwa kutupasha Habari, Taaluma na weledi.