Assalam Alaykum, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Nakuamkia kwa heshima na taadhima, nikitumai umzima wa afya, wewe na familia yako. Nakuombea kila la kheri katika majukumu yako mengi na mazito ya kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa, nimeshawishika kuandika barua hii baada ya kuona yanayoendelea kuhusu mkataba kati ya nchi yetu kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia kampuni yao ya masuala ya kilojistiki iitwayo DP World.
Ni takribani mwezi wa pili sasa tangu mjadala wa bandari uibuke; mjadala ambao umeinua hisia nyingi kuanzia wanasiasa na wanazuoni mpaka wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa, nisingependa kurudia, kwenye barua hii, hoja zote na maneno yote ambayo yameshatolewa juu ya mkataba huu. Kwa mamlaka uliyonayo kwenye nchi yetu, natumai umeshasikia yote, na umeshayaona yote, hivyo hakuna jipya nitakalolileta kwako.
Lengo kuu la barua hii, kwa hiyo, ni kuanisha maeneo machache ambayo Serikali inaweza kuyaboresha kuhusiana na mjadala wa suala hili husika, hususan kwenye namna watendaji wa Serikali wanalitolea ufafanuzi suala hilo.
Diplomasia ya uchumi
Awali ya yote, hata hivyo, nikupongeze, Mheshimiwa Rais, kwa jitihada zako za kutumia diplomasia ya uchumi kama njia moja wapo ya kuifungulia Tanzania milango ya fursa. Kama ambavyo unafahamu, katika ulimwengu huu wa sasa, hamna nchi inayoweza kuishi kama kisiwa na ikafanikiwa, au hata kudumu.
Marekani, chini ya raisi mstaafu Donald Trump, walijaribu falsafa ya kujitenga na ulimwengu ila haikuweza kufanikiwa. Hivyo, naamini kabisa Tanzania, kwa uchanga wake wa kiumri na kiuchumi, inauhitaji ulimwengu kama ambavyo tunategema ulimwengu uihitaji Tanzania.
Pili, napongeza jitihada zako za kujaribu kuleta uwekezaji wa nje nchini Tanzania kupitia safari zako mbalimbali huko ulimwenguni. Mheshimiwa, ni dhahiri Tanzania inahitaji uwekezaji kutoka nje ambao utaleta fedha, ujuzi na uzoefu katika sekta mbalimbali za nchi yetu. Hilo hakuna mwenye akili atapinga na kama akipinga basi ni kwa maslahi yake binafsi.
SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?
Hili la DP World halina tofauti. Wengi tunaoitakia mema Tanzania tuna matumaini makubwa kwamba kampuni hii itakuja kuleta mageuzi katika suala la bandari na kuongeza ufanisi, pamoja na ujuzi na uzoefu binafsi, wa Watanzania.
Hofu yangu kubwa ni kwamba suala hili limeshakua la kisiasa. Kwa bahati mbaya, taarifa za kwanza za mkataba huu zilitokana na kuvuja kwa nyaraka ya Serikali ambayo bado haikua imewekwa wazi kwa Watanzania.
Napinga kwa nguvu zote kwa raia yoyote, awe mtumishi wa Serikali au mtu binafsi, kuvujisha nyaraka za Serikali. Ila hili limeshatokea, na kwa bahati mbaya, ikawapa nguvu wapinzani na wanaharakati kuusuka mjadala kwa namna ambavyo walitaka wao.
Natumai aliyevujisha taarifa ambayo hakua na mamlaka ya kuiweka wazi amechukuliwa hatua stahiki. Ila hili haliondoi ukweli kwamba kuvuja kwa mkataba huo kuliiweka Serikali kwenye mazingira ya kujitetea zaidi, hali inayoathiri uwezo wake wa kiushawishi.
Makosa ya kimkakati
Mheshimiwa, kosa la kimkakati lililofanyika, la kwanza, ni kutumia watu maarufu badala ya watu wenye ushawishi kujadili na kuwasilisha manufaa ya mkataba. Kwa bahati mbaya, umaarufu siyo sawa na ushawishi.
Watu maarufu waliotumika walikua na uwezo wa kuufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi ila hawakua na uwezo wa kumshawishi mtu yoyote. Mbadala yake ilikua nafuu zaidi kutumia watu wenye umaarufu kiasi ila ushawishi mkubwa.
Njia bora ingekua kutumia watu kadhaa wenye ushawishi na makundi fulani ndani ya nchi yetu kuliko kutumia watu maarufu ambao waliweza kuueneza ujumbe lakini walishindwa kumshawishi mtu yoyote.
Mheshimiwa, kosa la pili lilikua ni kuruhusu, au kukubali, kila mwanasiasa ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuzungumzia hili suala. Matokeo yake, kila mtu akawa anaongea lake na kukawa hakuna uratibu sahihi.
SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri
Hii ilipelekea hata wanaozungumzia mkataba kwa namna chanya kukinzana na kuacha wananchi wasijue washike lipi na waliache lipi, wamuamini nani na wasimuamini nani.
Serikali ilipaswa kuteua wazungumzaji wachache tu ndani yake na CCM na kuwaruhusu wao tu ndiyo wazungumzie juu ya mkataba. Ile nia ya kila mwanasiasa kutaka kutoa hoja juu ya mkataba ili aonekane na mamlaka kumesababisha mkanganyiko badala ya muafaka.
Mheshimiwa, tumeshuhudia namna watu kadhaa wametumia suala hili kupata huruma ya wananchi. Baadhi, ambao hata jamii ilikua haiwafahamu, walijitokeza hadharani na kudai maisha yao yametishiwa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na kwamba kuna maagizo ya kuwanyamazisha milele.
Binafsi siamini kama kuna maagizo yoyote, au mkakati wowote, ndani ya Serikali kufanya hayo ambao baadhi wamedai. Ila mazingira yaliyokuwepo yaliruhusu wananchi kuwaamini, hususani ukizingatia historia ya tulipotoka.
Kosa lililofanyika, ambalo ni la tatu kimkakati, ni kukamatwa kwa watu hawa, hali iliyoongeza hisia ya kwamba ni kweli kuna maagizo ya kuwanyamazisha. Ingependeza zaidi kama Jeshi la Polisi wangewaomba hawa watu wote wanaodai kutishiwa kwenda kutoa ushahidi kwa vyombo husika.
Serikali nayo ingetoka hadharani na kupinga vikali kwamba kuna mpango wowote wa kuwanyamazisha na kuwadhuru hawa watu ambao wengi wao suala la bandari limewapa fursa ya majina yao kujulikana mbele ya jamii.
Uratibu
Ushauri wangu, Mheshimiwa, ni kwanza utoe maagizo kwa wote wanaozungumzia suala la bandari ndani ya Serikali na CCM waache mara moja.
Chagua sauti chache ambazo unaamini zinabeba uzito ndani ya jamii ya Watanzania na hao tu washirikiane na Msemaji wa Serikali, Katibu Mkuu wa CCM, msemaji wa chama, Mwanasheria wa Serikali na waziri husika kulizungumzia hili suala.
Ujumbe uratibiwe ili kusiwepo na sintofahamu yoyote kwenye ujumbe na ufafanuzi unaotolewa. Naamini, kwenye mkataba huu, mazuri yapo, na naamini yakurekebishwa yatarekebishwa ili tupate mkataba ulio bora zaidi.
SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania
Ila pia kuna njia nzuri Mheshimiwa uliyopendekeza ambayo naamini ndiyo njia sahihi kwa hapa tulipofika na italeta muafaka. Ulipendekeza majina ya watu wanaoonekana wanafaa yaletwe kwako kwa ajili ya tathmini ili wajumuishwe kwenye kikosi kazi kitakachohusika na kujadili, kuchambua, na kukarabati mkataba.
Naamini, kwa hapa tulipofika, hiyo ndiyo njia pekee itakayoleta muafaka chanya katika jambo hili.
Mheshimiwa, mwisho, nimalizie kwa kusema mafanikio yako ni mafanikio ya nchi. Una sala za Watanzania milioni 60 wanaokuombea mema kwani wanaliombea mema taifa lao na vizazi vyao vya sasa na vya baadaye.
Tuendelee kuvumiliana pale ambapo tunapishana hoja. Naamini, ukiwaleta hata mafundi wawili pamoja, wajenge nyumba moja, bado watatofautiana katika njia sahihi ya ujenzi.
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa, japo dhamana na mamlaka ya kuijenga nyumba hii inayoitwa Tanzania iko mikononi mwako, naamini utaendelea kusikiliza maoni ya mafundi tofauti na kuazima ujuzi pale utakapoona inatufaa kama taifa.
Mungu Ibariki Tanzania. Mungu Ibariki Afrika.
Wasaalam!
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Hii dhana kuwa mkataba ulivuja haina ukweli wowote