Niger, taifa la Afrika Magharibi lililopo kwenye mtanziko mkubwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo, lina akiba kubwa ya madini kama vile kobalti, almasi, platinamu, na urani.
Kwa mujibu wa Shirika la Nyuklia Duniani, taifa hilo lenye watu milioni 25 lilizalisha tani 2,248 za urani mnamo 2021, huku sehemu kubwa ya madini hayo ikichukuliwa na Ufaransa.
Tangu mwaka 1968, kampuni ya Ufaransa iitwayo Orano, imekuwa ikichimba urani nchini Niger, ambayo ilipata uhuru wake kutoka Ufaransa hapo mwaka 1960, na kuipeleka kwenye taifa hilo la Ulaya ambako inatumika, pamoja na mambo mengine, kuzalisha asilimia 70 ya umeme unaotumika nchini humo.
Wakati urani ya Niger inatumika kuzalisha umeme huko Ufaransa, nchini Niger inaripotiwa kwamba ni asilimia 16 tu ya wananchi wanatumia umeme, huku asilimia 90 ya umeme huo ukitajwa kutoka Nigeria, ambayo inapakana nayo. Nchi nyingine zinazopakana na Niger ni kama vile Mali, Chad, na Burkina Faso.
Inaripotiwa kwamba, kampuni hiyo ya Orano ilinunua machimbo hayo ya urani kwa bei ya kutupwa, kama ambavyo ‘wawekezaji’ wengi tu wa nchi za Magharibi wanavyojipatia ulaji kwenye mataifa masikini, baada ya kuwalainisha watawala wa mataifa hayo kwa ‘misaada’ na ‘mikopo.’
Orano, kupitia migodi hiyo, inadaiwa kukusanya faida zaidi ya bajeti nzima ya Serikali ya Niger, taifa ambalo ripoti zinaonesha zaidi ya wananchi wake milioni 10 wanaishi kwenye hali iliyopitiliza ya utegemezi.
Unyang’anyi
Unyang’anyi huu wa rasilimali za Niger, kwa kiwango kikubwa, umekuwa ukiwezeshwa na mfumo wa sarafu uliorithiwa tangu nyakati za ukoloni, ule wa Faranga, au CFA. Ni utaratibu ambao hata Ufaransa yenyewe imeacha kutumia na badala yake inatumia Euro.
Hata hivyo, nchi 14 barani Afrika zinaendelea kutumia Faranga inayodhibitiwa na Ufaransa, na ambayo inatajwa kuwa kikwazo cha maendeleo. Nusu ya akiba yote ya CFA inawekwa Ufaransa. Hii maana yake ni kwamba Ufaransa ndiyo inaamua thamani ya CFA. Sera hiyo ya ukoloni wa Kifaransa barani Afrika inajulikana kama Francafrique.
SOMA ZAIDI: Mnyukano wa Mafahali Wawili Unavyowatesa Raia wa Sudan
Mwaka 2015, Idriss Déby, akiwa Rais wa Chad, alisema kutegemea CFA maendeleo ya Afrika yanakwama, akisema umefika wakati wa mataifa ya Afrika “kukata kamba hii ya kikoloni.” Déby alitawala Chad kwa miaka 30 mpaka alipouliwa mwaka 2021. Chad ingali imo katika CFA, huku Burkina Faso na Mali zikiwa nchi pekee zilizoweka kuikata kamba hiyo.
Kwa kifupi, huo ndiyo ukoloni mambo leo. Ni vizuri tukaongeza kuwa mfumo huu wa kinyonyaji usingeendelea kuwepo bila ya kuungwa mkono na watawala wa Kiafrika wanaofaidika nao. Kwa hiyo, haishangazi sana kuona wananchi wengi nchini Niger wakiupokea kwa bashasha uamuzi wa Jeshi la Niger kuipindua Serikali ya kiraia nchini humo.
Ukinzani
Kama ambavyo tumesoma kwenye vyombo vya habari, dunia imeyapinga vikali mapinduzi hayo ya kijeshi, ambayo ni ya nane barani Afrika katika muda mfupi kuanzia Januari 2020 hadi Julai 2023. Mapinduzi kama hayo yametokea pia nchini Mali, Chad, Guinea, Burkina Faso, na Sudan.
Ukinzani dhidi ya uamuzi huo wa Jeshi la Niger, uliofanyika mnamo Julai 26, 2023, majira ya saa tisa alfajiri, umekuwa mkubwa sana kiasi ya kwamba baadhi ya mataifa, hususan yale yanayounda Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), yakiongwa na Nigeria, yalifikiria kuivamia Niger kijeshi kurudisha utawala wa kiraia nchini humo.
Uvamizi huo, hata hivyo, umeshindwa kufanyika kwani Baraza la Seneti la Nigeria lilikataa ombi la Serikali ya Nigeria kutuma vikosi vyake nchini Niger, likiielekeza ijikite kutatua matatizo ya ndani yanayowakabili Wanigeria, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?
Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wa mambo wanadokeza kwamba hatua ya kushindwa kwa Rais aliyepinduliwa, Mohammed Bazoum, kurudi madarakani, na kuendelea kwa utawala wa kijeshi chini ya Abdourahamane Tchiani, kunaashiria pia kuyeyuka kwa ushawishi wa Ufaransa – Francafrique – nchini Niger na kuibuka ushawishi wa Marekani – Amerafrique.
Ushawishi wa Marekani
Wadadisi wanaitaja ziara ya Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Victoria Nuland, nchini na Niger, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Moussa Salaou Barmou, afisa wa kijeshi na mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi, kama hatua muhimu ya kubadilisha upepo wa ushawishi.
Ni muhimu kufahamu kwamba huyu Barmou ni mnufaika wa mafunzo ya kijeshi yaliyotolewa na Jeshi la Marekani ambayo ina vikosi vyake ndani ya Niger. Kwenye mazungumzo yake na Barmou, inaripotiwa kwamba Nuland alionesha wasiwasi mkubwa kuwa Niger inaonekana kuikataa Ufaransa na kuikaribisha Urusi.
Ikumbukwe kwamba tayari Warusi wana majeshi yao nchini Mali, Afrika ya Kati, na Burkina Faso. Sasa, Niger nayo inaelekea kuwakaribisha wanajeshi hao ambao wengi huja kupitia kikundi cha kimamluki cha Wagner.
SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika
Inaripotiwa kwamba Jenerali Barmou akamwambia Nuland jambo hilo halizuiliki na liko nje ya uwezo wake, hasa kwa vile ECOWAS imepania kuishambulia Niger. Barmou pia akamwambia Nuland aangalie mabango ya waandamanaji mitaani.
Kwa mujibu wa jarida Le Figaro la Ufaransa, ndipo Nuland akaahidi kuwa yeye atasaidia kuzuia mashambulizi ya ECOWAS, naye Barmou azuie vikosi vya Wagner visiingie. Badala yake waruhusu majeshi ya Marekani yabaki Niger, hata kama Wafaransa wakiondoka.
Inasemekana Wafaransa wamechukizwa sana na jinsi Marekani walivyowasaliti na jinsi walivyofanya mbinu ya kuchukua nafasi yao huko Niger. Matokeo yake tunaona sera ya Francafrique inaanza kutoweka huko Niger na badala yake inaimarishwa sera ya Amerafrique.
Suala la Marekani kudaiwa kuwasaliti rafiki zao Ufaransa huko Niger halishangazi hata kidogo, kwani, kama wasemavyo wenyewe, wao hawana rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu bali wana maslahi ya kudumu!
Nizar Visram ni mchambuzi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.